AN-NUUR
Na.159 Rabi' Awal 1419, Julai 24 - 30, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Maoni yetu

Umakini wa Wabunge unatia wasiwasi

Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Ali Ameir akijibu hoja za Wabunge Bungeni hivi karibuni alidai kwamba hakuna haja ya kuundwa Tume kuchunguza suala la Mwembechai.

Aidha, alidai kwamba mtoto Chuki Athumani ambaye alipigwa risasi na Polisi na sasa kapooza alikuwa na makaratasi ya uchochezi na kwamba alihusika na vurugu zile kwa kutumiwa.

Mhe. Ali Ameir baada ya kuyasema hayo akawataka wale ambao wanamtetea mtoto huyo na kuwashutumu Polisi waliompiga risasi na wale waliomkosesha matibabu; kwamba wahoji na ni walimtumia mtoto huyo na kumpa makaratasi ya uchochezi.

Zaidi ya hayo Mhe. Ali Ameir alidai kwamba mama mzazi wa Chuki Athumani amesema kwamba Chuki hayupo tayari kurudi tena shuleni alikokuwa na akahoji kwanini hataki kurudi.

Kundi kubwa la Wabunge lilikuwa limepiga kimya wakati Mhe. Ali Ameir akitoa maelezo haya. Hata hivyo wapo baadhi yao ambao walikuwa wakipiga makofi.

Pengine ilikuwa waulizwe Wabunge hawa waliokuwa wakipiga makofi; ni lipi walilokuwa wakilishangilia au kulipongeza? Kwamba Waziri katoa majibu sahihi ya hoja za Wabunge! Anachosema ni cha kweli! au kupongeza kitendo cha Polisi kumpiga risasi mtoto Chuki Athumani kwa hilo dai la kukutwa na karatasi za uchochezi!

Wabunge walitaka kujua ni nani aliamrisha kuua watu, na kwanini mtoto yule alipigwa risasi akanyimwa matibabu na kuendelea kufungwa pingu hata baada ya kutolewa maelekezo kwamba watoto waachiwe.

Kujibu hoja hizo Mhe. Waziri anadai kwamba upo ushahidi kuonyesha kwamba mtoto huyo alihusika na vurugu kwa kukutwa na karatasi za uchochezi.

Swali ni je!, Polisi walimkamata na karatasi hizo ndio wakampiga risasi au walimpaiga risasi ndio wakagundua kwamba ana makaratasi ya uchochezi! Na je; hukumu ya Mtu ambaye kakamatwa na karatasi za uchochezi ni kupigwa risasi!

Kama kweli alikuwa na makaratasi ya uchochezi; mbona hakufunguliwa shitaka lolote juu ya uchochezi na mbona Mhe. Waziri hakuyatoa kama ushahidi!

Ni jambo la kusikitisha na kutia huzuni kwamba kauli ya Waziri ilipita bila kuhojiwa. Lakini inatia huzuni zaidi kwamba hata waheshimiwa Wabunge waliridhia hali hiyo na ikaingia kwenye rekodi za Bunge la Jamhuri ya Tanzania.

Hii imetupa wasiwasi juu ya umakini wa Bunge letu na usahihi wa taarifa mbalimbali zinazotolewa na Waheshimiwa Mawaziri na kukubaliwa na Bunge.

Lililo wazi Serikali au pengine tuseme baadhi ya viongozi wa Serikali wamekiuka Katiba ya nchi; Sheria na hata zile sheria za Kimataifa kwa kuua raia pasi na haki, kuvamia Msikiti, kuwatesa akina mama, watoto na wazee pasi na kosa lolote.

Baada ya kosa hilo wahusika hawataki kukiri kosa, lakini baya zaidi unajengwa mshikamano katika Serikali na chama Tawala kutetea uovu huo. Na hapo ndipo inapoibuka dhana kwamba Serikali ipo dhidi ya Waislamu.

Zipo propaganda zinazoendeshwa mitaani hivi sasa kwamba viongozi wa ngazi za juu wa chama Tawala na Serikali hawahusiki na kuuliwa Waislamu wala kudhalilishwa kwa watoto, wazee na akina mama. Lakini wao ndio waliowapa madaraka wahusika na tukio hili. Mbona hatuoni wakiwachukulia hatua kama hawaafikiani na yale waliyowafanyia Waislamu!

Mbona hatusikii kauli zao wenyewe wakikana kuhusika, watu wengine baki ndio wanaochukua ‘tenda’ ya kuwasafisha wakati wenyewe wapo. Yaliyotokea wanayajua na madai ya Waislamu kwamba wanataka wahusika wafikishwe mahakamani wanayajua pia! Mbona kimya; kimya hiki tafsiri yake nini!

Na kwanini kauli za kuwaosha zitolewe katika hafla za Waislamu na Waislamu, badala ya watu wa Serikali au chama Tawala katika vikao rasmi vya Chama na Serikali!

Waislamu tumeuliwa kinyume cha sheria, misikiti yetu imenajisiwa. Wazee wetu wameteswa, watoto wetu wametiwa vilema, mama zetu wamedhalilishwa. Haki na sheria za nchi zinadai wahusika wakamatwe wafikishwe mahakamani.
Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Maoni yetu: Umakini wa Wabunge unatia wasiwasi 

AGIZO LA MANISPAA KUPEWA MAJINA YA WANAFUNZI WA KIKATOLIKI 
Na Mwandishi wetu, Morogoro 

Madai ya Ali Ameir kuhusu Chuki yakanushwa 
Na Mwandishi wetu 

AN-NUUR  kwenye Internet 

Mwanamuziki Nyota CAT STEVENS asimulia alivyosilimu 

Watakiwa kuacha kuwatuma watoto mitaani 
Na. Kassim Juma 

Kijana wa Kibarbaig aliyejitolea kupigania dini yake 
Na. Ali Njuki 
 
MAKALA: Zanzibar na tamasha la filamu
Na Said Mzee

'Waislamu wenye sisa kali'
Na. Ustaadh A. S. Fundi 

MAKALA: Maisha ya ndoa kwa Muislamu - 2
Ustaadh Khamis Suleyman Nassoro, Usangi, Mwanga - Kilimanjaro

Pongezi hizi za nini?

Mjibuni Mwinjilisti Kusupa msitukane 
Na Paskal Msemakweli

BARUA YA WAZI KWA WABUNGE

Vigogo wahusishwa na madawa ya kulevya Z'bar
Na Mwandishi Wetu

Da’awa Handeni yashika kasi
Na Ibn Muhammad

Kongamano la vijana wa Kiislamu Masjid Nuur Dar
Na Mwandishi Wetu

Mafunzo ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)

Habari za Madrasa 

Masomo 

Chakula na Lishe 
 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita