AN-NUUR
Na.159 Rabi' Awal 1419, Julai 24 - 30, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 

Waislamu acheni ushirikina 

Mjibuni Mwinjilisti Kusupa msitukane 

Na Paskal Msemakweli 

NIMESOMA maoni ya Mhariri, barua za wasomaji na wachangiaji wa mada iliyoanzishwa na Mwandishi Mohamed Said ambao wengi wamejiita Ustaadhi na vyeo vingine vya dini ya Kiislamu ambavyo mimi sivijui kwakuwa si Mwislamu. Hata hivyo nashangaa ni kwanini wote wanamshambulia Mwinjilisti Kusupa tena kwa matusi na hasira huku wakiacha kabisa kuijadili mada yenyewe ya Tewa Said Tewa kufukuzwa Uwaziri kwa sababu ya Uislamu.

Makala ya Mwinjilisti Kusupa iliandikwa katika lugha nzuri ya kujibu hoja sasa matusi ya nini? Au kwakuwa yeye ni Mkristo na gazeti lenu ni kwa ajili ya Waislamu tu? Kwa kweli mmeonyesha chuki na ubaguzi ambao hauna mfano wake hapa nchini. Sisi tunaoitakia mema nchi hii tunasema kwamba Waislamu acheni ushirikina. Je mnajua mshirikina ni mtu wa namna gani? Ni yule ambaye mtoto wake anaumwa kwashakoo au maradhi ya utapiamlo yanayotokana na lishe duni lakini anamlaumu jirani yake kwamba ndiye anayemloga mwanawe ndiyo maana hana afya. 

Madai ya kusingizia Wakristo kwamba ndiyo waliosababisha Waislamu kunyimwa elimu ni madai ya kishirikina ambayo ni sawa na kumsingizia mtu uchawi na hatimaye kumwadhibu kwa kosa ambalo mtu hakulifanya. Kanisa na madhehebu ya Kikristo havikuwa na mkataba wa kuwaendeleza Waislamu kielimu wala kanisa halikuwakataza Waislamu nao wasijenge shule zao na kusomesha watu wake. Madhehebu ya Kikristo ndiyo yaliyoathirika zaidi na sera za Rais Nyerere za kutaifisha mashule ili kutoa elimu (kusomesha) watu wote. Je enzi za shule zote za msingi na za sekondari zilipomilikiwa na serikali mna uhakika kweli kwamba mtoto wa Kiislamu alipata alama 100 za kufaulu akaachwa kwa sababu ya Uislamu wake na badala yake akatwaliwa mtoto wa Kikristo aliyefeli kwasababu tu ya Ukristo wake? Je mnao ushahidi wa kufanyika mambo hayo au manachoangalia ni idadi tu kwamba Wakristo wengi kwenye shule za sekondari na vyuo vya elimu ya juu basi mnahukumu kwamba Waislamu tumeonelewa kwa sababu ya Uislamu wetu? 

Zaidi ya yote imekuwa kawaida kwenu kutoa takwimu ambazo si za kweli. Kwa mfano mnaposema nchi hii Waislamu ndiyo wengi, wako asilimia 60%. Je, ni nani aliyefanya sensa ya kupita nyumba kwa nyumba na kuuliza watu dini zao hadi ninyi mkajua kwamba Waislamu ndiyo walio wengi nchi hii? 

Kama kweli Waislamu ndiyo wengi katika nchi hii ni kwanini basi hamkumchagua Mwislamu mwenzenu Ibrahim Haruna Lipumba kwenye uchaguzi wa 1995 ili awe rais? Maana sera zake zililenga kuwapendelea Waislamu! 

Serikali ya Mkapa haistahili lawama kwa sababu alisema mapema kwenye kampeni kwamba akishinda Urais atalivalia njuga tatizo la mihadhara ya kashifa. Jambo ambalo amelitimiza kwa kuidhibiti mihadhara ya Mwembechai na sehemu zingine sasa mnachomlaumu ni nini! Rais hana mkataba wa kuwapendelea Waislamu. Badala yake yeye anasimamia haki za watu wote hata wale walioamua kuabudu jiwe na kusema jiwe ndiye Mungu wangu. 

Ninyi mliokazana kusema Yesu siyo Mungu mnatarajia msaada gani kwa rais hata muombe kuonana naye? Kama dini yenu inasema Allah ndiye Mungu mimi dini yangu haisemi hivyo bali inasema Yahwe ndiye mungu pekee. Sasa nitakapoandika kwenye baskeli yangu Allah siyo Mungu, au Muhammad siyo Mtume Je, huo si uchokozi? 

Katika dini yangu kuna amri kumi kutoka kwa Mungu wangu, amri ya kwanza inanikataza kuabudu miungu wengine miongoni mwa hao miungu wengine ni Allah. Je kwakuwa kitabu changu kinasema hivyo, nidiriki kuwaambia Waislamu waache kumkiri Allah bali wamkiri Mungu Yahwe ninayemtambua mimi kwa kuwa tu kitabu changu kinasema hivyo? Eleweni wazi kwamba kusema Yesu siyo Mungu huo ni uchokozi wala siyo uhubiri. Kama kuna mhubiri wa kweli aliyetumwa na Allah basi ahubiri mema ya Allah na siyo kuchokoza watu wa dini zingine zisizomtambua Allah. Kuna ajabu nyingine kwenu mnaojidai kupigania haki za Waislamu, mmekazana kuukosoa Ukristo na kuushambulia Ukatoliki wakati katika Tanzania kuna dini nyingi tu Wahindu, Wabahai,Wabudha na nyinginezo, wote hawa hawamjui Allah, wana miungu yao mbona hamuwachokozi kwa kukanusha Miungu yao kuwa siyo Miungu bali Mungu ni Allah tu? Ama mnaogopa mikong’oto toka kwa Waumini hao kwa kuwa wao siyo wavumilivu kama walivyo Wakristo? Tafadhali jitahidini kuwa Waungwana. Visingizio vya kwamba Waislamu tunaonewa wakati ninyi ndio mnaotaka kuonea wengine hiyo ni janja ya nyani ya kula hindi bichi ambayo Serikali imekwishang’amua. 

Nampongeza Yusufu Makamba kwa ujasiri wake na msimamo usiotetereka maana pamoja na kumsomea itikafu bado anaishi na Mungu anamlinda na mimi nazidi kumuombea mema kwa Mungu wangu. 

Kuhusu madai yenu ya Waislamu kudhulumiwa mbona hamtoi mifano hai kutoka Zanzibar ambako Serikali inafunga watu na yamekuwako mauaji tangu miaka ya sitini! Au kwakuwa mauaji yanafanywa kati ya Waislamu kwa Waislamu basi kwenu ni halali? Sasa tumegundua kwamba kumbe msichokitaka ninyi ni Wakristo, si kweli kwamba mnataka haki za Waislamu. Maana Zanzibar tokea enzi za Masultani haikuwahi kutawaliwa na Mkristo, hata baada ya mapinduzi aliyetawala ni Sheikh, lakini si Wazanizbari wote wenye digrii, si Wapemba wote waliofika Chuo Kikuu wala si Waislamu wote wenye madaraka wako wanaotawaliwa kama walivyo Waislamu wa bara. Sasa tuelezeni ni nani aliyewahujumu Wapemba wasiwe na elimu? Huko kuna mambo ya ajabu ya Visima kuwekwa vinyesi, na shule pia kutupiwa vinyesi ili watoto wasisome. Mambo hayo yanafanywa na Waislamu dhidi ya Waislamu wenzao hakuna Paroko aliyeamuru mabaya hayo yafanyike wala hakuna Askofu Pengo wa kutoa maagizo hayo sasa ni kwanini yawepo maovu kama hayo? 

Tuelezeni ni kwanini Zanzibar haina maendeleo wakati hakuna mkoloni aliyewatoza kodi Wazanzibari na kuitwaa kodi hiyo kuwajengea Wakristo mashule! 

Tuelezeni ni kwanini Waislamu wa huko hawakusoma na ni nani aliyewanyima elimu wakati hakuna kanisa wala kiongozi yeyote wa serikali aliye Mkristo? 

Ndiyo maana nasema baadhi ya madai yenu ni sawa na madai ya mshirikina ambaye siku zote anaona matatizo yake binafsi yanasababishwa na watu wengine. 

Ilivyo ni kwamba elimu siyo Pilau ambayo mtu anawezakupakuliwa kwenye sahani kiasi kwamba mtu anaweza kuigawa kwa upendeleo akampa mwingine ama kumnyima yule anayemchukia, au kumpa kidogo, bali elimu ni mtokeo ya mpango wa Taifa na juhudi za mtu binafsi. 

Katika nchi yetu serikali ilitaifisha mashule na mahospitali ili kutoa huduma hizo kwa watu wote. Katika hili kufaulu kwa mwanafunzi hadi Chuo Kikuu kulitegemea uwezo wa binafsi wa mwanafunzi pasipo kujali dini yake au kabila lake, Sasa mnapodai Mwislamu kunyimwa elimu mnatumia vigezo gani au mlitaka mtu apewe digrii kwa kuwa tu anaitwa Abdallah? Elimu ya Chuo Kikuu haianzii pele Mlimani bali inaanzia kwenye darasa la chekechea (Nursery School). Sasa tuelezeni ni Jumuia ngapi za Kiislamu zenye shuleza Chekechea ikilinganishwa na makanisa? Nijuavyo mimi kwa makanisa hiyo ni sera, kila Kanisa lina darasa la chekechea ambalo lina waalimu waliosomea kwa kazi hiyo na ndio wanaomuwezesha mtoto wa Kikristo kuingia darasa la kwanza huku akiwa anajua kusoma na kuandika tofauti na watoto wengine ambao huanza darasa la kwanza wakiwa mbumbumbu na kwa maana hiyo huanza shule na msingi mbovu wa kutokujua. 

Hadi sasa shule za seminari hasa seminari za Wakatoliki (mnaowachukia bila sababu) ndizo zinazoongoza kwa kufaulu kuanzia mitihani ya kidato cha nne hadi mitihani ya kidato cha sita kwenda Chuo Kikuu kutokana na ufundishaji mzuri na hali ya nidhamu iliyojengwa kwenye mazingira ya shule hizo sasa ninyi msichokitaka ni nini au mnataka makanisa yaache kusomesha watu wake ili kuwaridhisha ninyi! Makanisa hayana choyo kwa sasa hivi ambapo serikali haisomeshi wanafunzi nje ya nchi, makanisa yamekazana kuwadhamini watu wake wasome nje,. Je, ninyi ni nani aliyewakataza kuwasomesha Waislamu nje ya Tanzania? 

Namaliza kwa kusema iangalieni Somalia pamoja na kwamba ni nchi ya Waislamu watupu lakini kuchinjana kwao imekuwa kama kazi kwahiyo hata Wakristo wakifutika kabisa katika nchi hii bado huo hautakuwa ndiyo mwisho wa matatizo ya Waislamu.Nadhani yule Sheikh alikuwa sahihi alipowaambia kwamba Mwenyezi Mungu hakuiumba hii dunia kwa ajili ya Waislamu tu, siku ile ya ufunguzi wa msikiti wa Mwembechai. 

Leo hii mnayaelekeza mashambulizi yenu kwa Wakristo mara kwa Pengo, mara kwa Paroko mara kwa Mwinjilisti Kusupa mara kwa huyu, lakini nawaambia hata baada ya hao kutoweka mtabakia ninyi peke yenu katika nchi hii, bado mtawageukia Waislamu wenzenu, na mara mtakapowamaliza hao, mtageukiana wenyewe kwa wenyewe. Nadhani makala ya Mwinjilisti Kusupa ilikuwa na mantiki aliposema Ibilisi hana rafiki. Ninyi hamjajitambua kwamba shetani anafanya kazi ndani ya mioyo yenu ndiyo maana mnejaa chuki, uchungu na hamu ya kupiga nakuchokoza watu wengine walio nje ya dini yenu. 

Pale Mwembechai siku ya vurugu kuna maduka ya Waislamu wenzenu yaliporwa na mali za ndugu zenu Waislamu kuharibiwa mbona hamtetei haki yao? Ni haki gani hiyo ya kuchokoza wengine, mnayoipigania ninyi? 

Kumbukeni kwamba hata watu waovu hujiona wanayo haki ya kufanya maovu. Mwizi huona anayo haki ya kuchukua cha mtu mwingine. Mharibifu huona anayo haki ya kuharibu mali ya mwingine, vivyo hivyo mchokozi hujiona anayo haki ya kuchokoza. Hivyo haki mnayoipigania ninyi ni hatari tupu. 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Maoni yetu: Umakini wa Wabunge unatia wasiwasi 

AGIZO LA MANISPAA KUPEWA MAJINA YA WANAFUNZI WA KIKATOLIKI 
Na Mwandishi wetu, Morogoro 

Madai ya Ali Ameir kuhusu Chuki yakanushwa 
Na Mwandishi wetu 

AN-NUUR  kwenye Internet 

Mwanamuziki Nyota CAT STEVENS asimulia alivyosilimu 

Watakiwa kuacha kuwatuma watoto mitaani 
Na. Kassim Juma 

Kijana wa Kibarbaig aliyejitolea kupigania dini yake 
Na. Ali Njuki 
 
MAKALA: Zanzibar na tamasha la filamu
Na Said Mzee

'Waislamu wenye sisa kali'
Na. Ustaadh A. S. Fundi 

MAKALA: Maisha ya ndoa kwa Muislamu - 2
Ustaadh Khamis Suleyman Nassoro, Usangi, Mwanga - Kilimanjaro

Pongezi hizi za nini?

Mjibuni Mwinjilisti Kusupa msitukane 
Na Paskal Msemakweli

BARUA YA WAZI KWA WABUNGE

Vigogo wahusishwa na madawa ya kulevya Z'bar
Na Mwandishi Wetu

Da’awa Handeni yashika kasi
Na Ibn Muhammad

Kongamano la vijana wa Kiislamu Masjid Nuur Dar
Na Mwandishi Wetu

Mafunzo ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)

Habari za Madrasa 

Masomo 

Chakula na Lishe 
  

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita