Home  History
Politics
Relevant articles Education
Links to other sites Hot links
Comments
e-mail usearth Sign the GuestBook

Kamati ya Kupigania Haki za Waislamu Tanzania:

Barua kwa Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Wananchi wa Tanzania kuwaomba waibane Serikali juu ya kadhia ya Mwembechai

Utangulizi

Mara baada ya mauaji ya kinyama yaliyofanywa na polisi katika eneo la Mwembechai tarehe 13 Februari, 1998, Kamati yetu iliitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza ukweli wa mambo yalivyotokea. Tulifanya hivyo kwa sababu hadi wakati huo, taarifa zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi wa mamlaka mbalimbali za nchi zilikuwa hazielezi ukweli wote. Na kwa bahati mbaya taarifa hizo zikawa zinafikishwa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari na hivyo kupotosha ukweli wa mambo. Ndio maana katika mkutano ule tuliiomba serikali yetu, ili kuondosha utata uliokuwepo, iunde tume huru ya kuchunguza tukio la Mwembechai na yale yaliyopelekea kutokea kwa tukio hilo.

Kwa bahati mbaya hadi leo tume hiyo bado haijaundwa. Mbali ya kutoundwa kwa tume, taarifa zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu serikalini, viongozi ambao awali walidai kuujua ukweli wa mambo na hivyo kuikataa haja ya kuundwa tume, ziliendelea kuwakanganya wananchi. Kwa kipindi kisichozidi mwezi na nusu, viongozi hao waliodai kuujua ukweli wa mambo walitoa sababu nne tofauti, na zenye kupingana. Hali hiyo ilitosha kuwa ni ushahidi wa haja na umuhimu wa kuundwa tume ya kuchunguza ukweli wa tukio na hasa yale yaliyopelekea kuzuka kwake.

Waheshimiwa wabunge, hiyo ndio hali iliyopelekea Kamati yetu kutoa waraka wa kurasa 13 ambao ulieleza kwa kina chanzo cha tukio lile na yale yaliyotokea. Waraka huo uliosainiwa na Sheikh Ponda Issa Ponda, Katibu wa Kamati yetu, ulisambazwa kwenu waheshimiwa wabunge, wanasheria, wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na taasisi mbalimbali za nchi ikiwemo inayoshughulikia usalama wa taifa letu. Tulikuleteeni waraka ule Waheshimiwa wabunge ili kukujulisheni ukweli wa mambo na hivyo kukupeni fursa ya kuuchambua ukweli wa tukio hilo kwa kupima maelezo ya pande zote.
 
 
Shukrani

Hatuna budi Waheshimiwa wabunge kutanguliza shukrani zetu kwenu na hususan Mheshimiwa Kitwana Kondo, Mheshimiwa Ibrahim Msabaha, na Mheshimiwa Spika wa Bunge aliyewaruhusu kuzungumza juu ya kadhia ya Mwembechai, na ukatili wa polisi uliowadhalilisha akina mama na uliomtia kilema kijana Chuki Athumani. Aidha Waheshimiwa wabunge tunaomba kutoa shukrani za dhati kwa mbunge na waziri, Mheshimiwa Kingunge Ngombale Mwiru pamoja na baadhi ya wabunge kwa jinsi alivyojitokeza na kumtembelea mtoto Chuki Athumani alipokuwa mahabusu Hospitali ya Muhimbili alikofungwa pingu kitandani licha ya kilema cha kupooza mwili, alichopewa na polisi waliompiga risasi.

Waheshimiwa wabunge, Kamati yetu na wanachi wote waliolaani mauaji yaliyofanywa na polisi Mwembechai tulifarijika sana kuona Jumuiya ya wanafunzi wa taaluma ya siasa, Utawala na Sayansi ya Jamii wakishirikiana na jopo la wasomi maarufu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliona umuhimu wa kukutana ili kujadili kadhia ya Mwembechai, ukatili wa polisi na uvunjwaji wa haki za binadamu ulioandamana na kadhia hiyo. Tunakiri kufarijika vilevile na juhudi za Mwislamu mmoja aitwae Abu Aziz aliyempelekea Mwanasheria Mkuu wa Serikali yetu waraka wa kurasa 53 kuhusu suala la Mwembechai. Waraka huo ambao nakala yake pia ulitumwa kwenu, ofisi ya Rais, mabalozi na kwenye taasisi na jumuiya mbalimbali nchini, ulituongezea tamaa kuwa huenda wahusika na wenye majukumu ya kusimamia haki nchini watauona ukweli wa mambo kutokana na uchambuzi wa kina uliofafanua dhulma iliyotendwa na polisi Mwembechai dhidi ya haki za raia zilizoainishwa katika katiba ya nchi yetu.
 

Matumizi Mabaya ya Bajeti

Waheshimiwa wabunge, wananchi tunafahamu kuwa moja ya majukumu yenu ni kuchambua na kuidhinisha kasma ya bajeti kwa ajili ya matumizi ya wizara na taasisi mbalimbali za serikali, na mnafanya kwa niaba yetu. Na kwa sababu ya idhini mliyoipata kutoka kwa wananchi, mnayo haki na wajibu wa kuhoji matumizi mabaya au yale yanayokwenda kinyume na makusudio ya idhini yenu.

Ni dhahiri, Waheshimiwa wabunge, kuwa kitendo cha wizara ya Mambo ya Ndani kuwaacha polisi wawapige risasi raia na kuwauwa kwa makusudi ni matumizi mabaya ya idhini yenu katika kupitisha bajeti ya wizara hiyo mwaka uliopita (1997/98). Hatuamini kwamba mliipa idhini serikali kutumia kodi za wananchi kununulia risasi jeshi la polisi ili liwauwe raia kwa kuwalenga shabaha kama wanyama. Na hivyo ndivyo walivyofanya pale Mwembechai tarehe 13 Februari, 1998.

Mbali ya mauaji hayo wizara ya Mambo ya Ndani ilitumia pesa mlizoidhinisha mwaka jana kuwalipa posho askari ili wauzingire na waugeuze msikiti wa Mwembechai kuwa ni lindo la polisi, na wakadiriki hata kuzifuja pesa za wananchi kwa kuzungukazunguka na helikopta eneo la msikiti huo. Ilizitumia pesa hizo pia kwa kuwatesa raia waliovamiwa na kukamatwa kwa nguvu pasipo na kosa lolote, wengine wakiwa wamelala majumbani kwao, bila hata kufuata taratibu za kisheria kama vile kuwa na "Arrest Warrant" au "search warrant." Wananchi zaidi ya 200 walikumbwa na ukamatwaji huo wa kinyama ndiyo maana wengi kati ya hao wameachiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka kwa kutokuwepo na shitaka la kujibu.

Wengi wa watuhumiwa, wake kwa waume, watoto na vikongwe waliwekwa mahabusu kwa zaidi ya miezi minne na kupewa mateso ya kila aina. Waliwekwa katika hali mbaya na kupatwa na magonjwa, walinyimwa matibabu wanayostahili, kisha walinyanyaswa kwa matusi na masimango kinyume na haki zao za Kibinadamu.

Waheshimiwa wabunge, mahabusu mmoja Mohamed Omari alifia mikononi mwao. Wengi wengine wametoka wakiwa katika hali mbaya kiafya. Mtoto Chuki Athumani aliendelea kufungwa pingu kiasi cha kuwa taabu kumhudumia huku akiwa katika hali mbaya kiafya baada ya kupigwa risasi na polisi.

Familia za mahabusu hao zimeteseka pia kwa kukosa huduma na msaada wa wale ambao walikuwa wasimamizi na viongozi wa familia hizo, kutokana na kuwekwa mahabusu kinyume cha sheria.

Ni mateso makubwa kwa binadamu kuona binadamu mwenziwe anaonewa kwa kunyimwa haki yake ya kimsingi kama Mwanadamu. Ni jambo la mateso na huzuni kubwa vile vile kwa wananchi waliohuru katika nchi yao kuona wananchi wenzao wakinyanyaswa na kudhulumiwa haki zao kama raia.
 

Kulaani na Kudhibiti Madhalimu

Waheshimiwa wabunge, tumewaandikieni barua hii kwa kuzingatia mambo mengi likiwemo hili la kuidhinisha na kusimamia matumizi ya serikali na kutetea haki za raia. Mkiwa wananchi mlio Bungeni, mnalo jukumu la kitaifa la kuona kuwa taifa letu katika masuala tuliyoyataja haliwi taifa la madhalim na wabaguzi wa haki za binadamu kwa kisingizio chochote kile kama ilivyokuwa katika nchi ya Afrika Kusini zama za utawala wa makaburu. Ndiyo maana mnapo tunga na kuzipitisha sheria mbalimbali huzingatia yale yaliyotamkwa kwenye Katiba yetu ya nchi ambayo inalinda ubinadamu wetu na kusimamia haki za raia, pasipo ubaguzi.

Hivyo mnayo haki na uwezo wa kulaani na kudhibiti madhalim wa haki za binadamu na raia nchini.

Hadi leo, Wizara ya Mambo ya Ndani haijawakamata na kuwafikisha mbele ya vyombo vya Sheria wale polisi waliouwa wananchi kwa kuwapiga risasi tarehe 13/2/98 Mwembechai. Bado haijawakamata na kuwafikisha mbele ya Sheria wale waliotoa amri kwa polisi kuwauwa wananchi wale. Bado haijachukua hatua yoyote dhidi ya malamiko ya wananchi waliopata mateso wakati wakiwa mahabusu. Haijawachukulia hatua yoyote wale polisi waliompiga risasi mtoto Chuki Athumani na kumsababishia kilema cha kupooza mwili. Hawajachukua hatua yoyote ya kuchunguza kifo cha mtuhumiwa Mohamed Omari aliyefia mahabusu.
 

Maombi Yetu

Kutokana na haya, Waheshimiwa wabunge tunakuombeni:

(i) Mchukue hatua za kulaani utendaji mbovu uliojitokeza Wizara ya Mambo ya Ndani kuhusu suala la Mwembechai kwa kushindwa hadi sasa kuchukua hatua dhidi ya wauaji na waliodhulumu haki za raia kwa kuwatesa, kuwatia kilema na kuwaweka ndani kinyume cha Sheria.

(ii) Tunakuombeni muibane Serikali iwaondoshe watendaji wabovu katika Wizara hiyo hususan viongozi wa Wizara na watendaji wake wakuu kwa kuachia polisi wauwaji na watesaji kuwa huru hadi leo.

(iii) Tunawaomba muibane serikali ihakikishe kuwa polisi waliouwa Mwembechai na wale waliowatesa watuhumiwa wanafikishwa mbele ya Sheria.

(iv) Tunakuombeni Waheshimiwa wabunge muibane Serikali mpaka tume ya kuchunguza kifo cha mtuhumiwa Mohamed Omari aliyefia Mahabusu inaundwa kama taratibu za kisheria (Inquest) zinzvyotaka.

(v) Waheshimiwa tunawaomba muiambie Serikali iunde tume huru ya kuchunguza sababu zinazopelekea Waislamu kupuuzwa na kunyimwa haki zao za kimsingi kama binadamu na raia katika nchi yao.

Tupo tayari kushirikiana na tume hiyo kupata ukweli wote ili nchi yetu iepukane na dhulma zinazotaka kuota mizizi dhidi ya wananchi kwa misingi ya kibaguzi.

Tunakuombeni Msiidhinishe bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya mwaka huu (1998/99) mpaka Serikali ikupeni majibu sahihi.

Vinginevyo itakuwa mmeshirikishwa katika kuwapa nyenzo wauwaji na kuhalalisha dhulma kwa kwa raia nchini.

Tuanakutakieni heri,

 
(Abdul Sattar)
KAIMU Katibu
Kamati ya Kupigania Haki za
Waislamu Tanzania.

Dar es Salaam, 9 Julai, 1998.

Home  History
Politics
Relevant articles Education
Links to other sites Hot links
Comments
e-mail usearth Sign the GuestBook