AN-NUUR
Na.159 Rabi' Awal 1419, Julai 24 - 30, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 Agizo la Manispaa kupewa majina ya wanafunzi wa Kikatoliki:

Wasiwasi wazidi kutanda Moro

  • Waalimu wakiri kuwepo kwa zoezi hilo 
  • Wazazi wahoji ni la nini.
  • Wananchi wasema kuna 'ushirika' baina 
  • ya serikali na Kanisa Katoliki

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Agizo la Ofisi ya Elimu ya Manispaa ya Morogoro linalowaagiza walimu wakuu wa Shule za Msingi watume majina ya wanafunzi Wakatoliki wa darasa la saba, limeendelea kuibua wasiwasi na hisia tofauti miongoni mwa wananchi nchini.

Wananchi wengi wamekuwa wakihoji ni kwanini ofisi hiyo ya elimu iagize majina ya wanafunzi wa dhehebu moja. Nini lengo na kwanini agizo hilo litolewe katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wa darasa la saba wanakaribia kufanya mitihani yao ya mwisho.

Mzazi mmoja mwenye mtoto anayesoma Shule ya Msingi Mtawala alisema lau kama agizo au ombi hilo lingetoka kwa padri au askofu kusingekuwa na sababu ya kuwa na wasiwasi; lakini akasema kwamba inapokuwa ni ofisi ya elimu ambayo huhudumia wanafunzi wote bila kujali dini zao, inajenga dhana mbaya.

Mzazi mwingine ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini alishtuka kuiona nakala ya barua hiyo ambayo nakala zake zimesambazwa karibu maeneo yote mjini hapa.

Mzazi huyo ambaye mtoto wake anasoma Shule ya Msingi Misufini amesema kwamba japo mtoto wake anafanya vizuri sana katika masomo lakini ashaanza kuwa na wasiwasi.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba zoezi hili si mara ya kwanza kufanyika, bali hufanyika kila mwaka inapofika nyakati kama hizi.

Waalimu Wakuu wengi waliohojiwa na gazeti hili walikataa majina yao na hata shule zao kutajwa gazetini walikiri kuwepo kwa agizo hilo lakini wakadai kwamba hawajui majina hayo yanaagizwa kwa lengo gani.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Mlimani (Forest juu) alidai kutokujua jambo hilo na akashtuka sana alipooneshwa nakala ya barua hiyo.

Hata hivyo mwalimu mkuu wa shule nyingine iliyopo katika Manispaa hii alimwonyesha Mwandishi wa habari hizi barua hiyo ndani ya faili(file) lake.

Alipoulizwa kwamba majina hayo yametakiwa kwa lengo gani alijibu kwamba hajui na yeye alichofanya ni kutekeleza agizo la mwajiri wake.

Baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba katika shule za msingi Msamvu, Mafiga, Mtawala, Misufini na Mlimani waliohojiwa juu ya jambo hili walikiri kuwepo kwa zoezi hilo.

Katika baadhi ya shule wamesema Mwalimu amekuwa akiita majina na kuuliza dini ya kila mmoja ambapo wale wakatoliki majina yao yamekuwa yakiandikwa.

Baadhi ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka jana ambao walihojiwa na mwandishi wa habari hizi walikiri kwamba waliwahi kufanyiwa zoezi hilo.

Kutokana na hali ya mtafaruku ambayo inaendelea katika Manispaa ya Morogoro juhudi za kuwaona wahusika kuzungumzia suala hili zimekuwa zikikwama kwa namna moja au nyingine.

Katika miaka ya hivi karibuni kimetolewa kitabu ambacho kimeeleza kwamba yapo mahusiano ya Karibu sana baina ya Kanisa Katoliki na Serikali ambayo hufanya matendo, msimamo na uamuzi wa Viongozi wa Serikali ufanane na mwelekeo wa Kanisa.

Ni hivi karibuni pia Baraza kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu limehoji kuwepo kwa habari kwamba Kanisa hilo lina Tume ya Majeshi ya Vita.

Kutokana na hali hiyo Wananchi wamefikia kudai kwamba upo ushirika usioeleweka baina ya Serikali na Kanisa hilo.
 

Juu 
 

YALIYOMO
 
 

TAHARIRI 

Maoni yetu: Umakini wa Wabunge unatia wasiwasi 

AGIZO LA MANISPAA KUPEWA MAJINA YA WANAFUNZI WA KIKATOLIKI 
Na Mwandishi wetu, Morogoro 

Madai ya Ali Ameir kuhusu Chuki yakanushwa 
Na Mwandishi wetu 

AN-NUUR  kwenye Internet 

Mwanamuziki Nyota CAT STEVENS asimulia alivyosilimu 

Watakiwa kuacha kuwatuma watoto mitaani 
Na. Kassim Juma 

Kijana wa Kibarbaig aliyejitolea kupigania dini yake 
Na. Ali Njuki 
 
MAKALA: Zanzibar na tamasha la filamu
Na Said Mzee

'Waislamu wenye sisa kali'
Na. Ustaadh A. S. Fundi 

MAKALA: Maisha ya ndoa kwa Muislamu - 2
Ustaadh Khamis Suleyman Nassoro, Usangi, Mwanga - Kilimanjaro

Pongezi hizi za nini?

Mjibuni Mwinjilisti Kusupa msitukane 
Na Paskal Msemakweli

BARUA YA WAZI KWA WABUNGE

Vigogo wahusishwa na madawa ya kulevya Z'bar
Na Mwandishi Wetu

Da’awa Handeni yashika kasi
Na Ibn Muhammad

Kongamano la vijana wa Kiislamu Masjid Nuur Dar
Na Mwandishi Wetu

Mafunzo ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)

Habari za Madrasa 

Masomo 

Chakula na Lishe 
 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita