AN-NUUR
Na.161 Rabiul Thani 1419, Agosti 7-13, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Chakula na lishe
Ulazima wa kuchemsha maji ya bomba yaliyotiwa dawa 

Na Mujahiid Mwinyimvua 

MARA nyingi yanapojitokekza maradhi ya kipindupindu na yale ya homa ya matumbo (typhoid fever) viongozi wa kisiasa huwahamasisha wananchi kuchemsha maji ya kunywa.  

Kuhusu zoezi hilo baadhi ya wananchi hujiuliza maswali, moja ya maswali hayo ni hili: Wataalamu na wafanya kazi wa mamlaka mbali mbali za maji hutuambia kuwa, maji yanayosambazwa kwenye mabomba kwa baadhi ya miji kama vile Dar es Salaam, Tanga na Morogoro yanatiwa dawa ya kuua vijidudu vinavyoambukiza maradhi, kwanini tena tunaambiwa tuyachemshe maji ya aina hiyo? 

Swali hili la wananchi lina mantiki hivyo basi linahitaji majibu ya kisayansi, vinginevyo wananchi wanaweza kuupuzia wito huo muhimu wa viongozi wetu. 

Tatizo linakuwa kubwa zaidi juu ya hoja ya hapo juu kwa vile, viongozi wengi wa kisiasa huwa hawatoi maelezo ya kina ni kwa sababu gani maji yaliyotiwa dawa yanahitaji kuchemshwa. Makala yetu ya wiki hii inalenga katika kujibu swali la wananchi tuliloliona hapo juu. 

Maji ya bomba yanayosambazwa katika miji yetu hapa Tanzania yanatoka katika vyanzo mbali mbali kama vile mito, maziwa, mabwawa, chemchem, visima n.k. Mamlaka za maji safi na maji taka katika miji yetu mbali mbali zinajitahidi kuyasafisha na kuyatia dawa maji hayo. 

Wananchi waliopata bahati ya kutembelea mitambo ya kusafisha maji ya kunywa wanajua kazi ngumu na gharama kubwa inayoipata serikali yetu (au serikali nyingine) katika swala zima la kusafisha na kusambaza maji ya kunywa. 

Hata hivyo, mara kadhaa maji yanayosambazwa kwenye mabomba huwa si safi wala si salama. Hii haina maana kuwa maji hayo yanasambazwa bila ya kusafisha au kutiwa dawa. Maji yanasafishwa na pia yanatiwa dawa, lakini kuna kasoro za kiufundi na sababu za kiuchumi zinazofanya maji yaliyosafishwa na kutiwa dawa yamfikie mteja (mtumiaji) hali ya kuwa si safi wala si salama. 

Kwa maneno mengine, mara nyingi katika baadhi ya miji yetu maji huwa safi na salama pale katika mitambo. Lakini yanachafuka wakati wa kuyasafirisha kwa watumiaji. Kasoro hiyo inachangiwa na sababu nyingi, baadhi yake ni hizi. 

Uchakavu wa mabomba 

Mabomba mengi yanayosambaza maji katika miji yetu ni ya zamani, mengine yaliwekwa enzi ya Wakoloni. Mabomba mabovu huingiza uchafu katika maji hasa kama nguvu (pressure) ya maji katika mabomba ni ndogo. Ufumbuzi wa kasoro hii ni kuweka mabomba mapya. Lakini kikwazo ni uwezo mdogo wa kifedha wa serikali! Kwa hoja hii lazima wananchi wachemshe maji hata kama maji hayo yalitiwa dawa katika mitambo (au matanki ya kuhifadhia maji), la sivyo wananchi tutakwisha kwa magonjwa kama vile kipindupindu na homa ya matumbo. 

Kupasuka kwa mabomba 

Mara nyingi mabomba ya wananchi (mitaani) hupasuka kwa sababu mbali mbali, mojawapo ni kupasuliwa na magari au watoto. Bomba linapopasuka huwa ni sababu ya maji safi na salama kuchanganyika na uchafu, hasa kama nguvu ya maji katika bomba ni ndogo. Hali inakuwa mbaya zaidi kwa maeneo ambayo uchafu hutandaa katika maeneo yanayopita bomba. 

Jambo la kufanya ni kuwa wananchi tuyaweke mazingira yetu katika hali ya usafi na pia mabomba lazima yachimbiwe kina cha kutosha. 

Vijidudu vilivyojeruhiwa 

Kwa kawaida wataalamu wa maji safi (maji ya kunywa) huwa wanachunguza ubora wa maji. Katika kazi hiyo huwa wanapima pamoja na vitu vingine, vijidudu vilivyo hai katika maji. Kama hawakuviona vijidudu hivyo, hujua kwamba maji yamesafishwa vizuri. Hivyo huyaruhusu kusambazwa kwa wananchi. 

Hata hivyo, maji hayo yanaweza kuwa na vijidudu kabla ya kumfikia mnywaji na hapa sasa sababu yake siyo uchafu wala uchakavu wa mabomba. Sababu yake hapa ni vijidudu vilivyojeruhiwa, kwa Kiingereza vinaitwa injured/stressed microorganisms. 

Vijidudu vilivyojeruhiwa (kuzimia) huwa na uwezo wa kufufuka vinapopata mazingira mazuri kama ya kuwepo dawa kiasi kidogo katika maji. Hoja hii ni ngumu kidogo kwa watu ambao si wataalamu wa sayansi ya vijidudu (microbiology). Hata hivyo, jambo la kuzingatia kwa watumiaji wa maji ni kuwa, mara nyingi wataalamu wa maji hawavichunguzi hivi vijidudu v ilivyojeruhiwa. Kwa hiyo vikipata uhai huwa ni hatari kwa afya ya watumiaji wa maji. 

Kwa kuzingatia falsafa hii ya vijidudu vilivyojeruhiwa ninawaomba wataalamu wa maji kuvichunguza v ijidudu hivi wakati wanapopima ubora wa maji. Kwa hakika ninajua ugumu na gharama ya kuvichunguza vijidudu hivyo, lakini afya ni bora kuliko mali, ndiyo maana katika baadhi ya nchi vijidudu hivyo huwa ni lazima kuvichunguza unapopima ubora wa maji. 

Kwa vile makala hii imelenga kutoa mwanga kwa wananchi juu ya ulazima wa kuchemsha maji yaliyotiwa dawa, ninadhani kwamba haitakuwa jambo zuri kuzidi kueleza vitu ambavyo ni vya kitaaluma zaidi. Kwa maneno mengine, sababu tulizoziona hapo juu ambazo zinachangia kuyachafua maji yaliyotiwa dawa, zinatosha kujibu swali la wananchi kuwa kwa nini maji ya bomba yaliyotiwa dawa yachemshwe hasa katika nchi zetu zenye matatizo ya uchumi na teknolojia duni. 
 

Sufa (Cress) Hurfun 

Amesema Abuu Hanifa Dinawarriyu, "Hivi ni chembe ambazo hufanywa dawa, nazo ni sufa (thufaau)". Chembe ambazo mmea wake unaitwa Hurfun na kwa jina jengine watu wengi wanaziita (Haba Rashaad); na amesema Abuu Ubeidin kuwa hio Thufaau ndio Alihurfun, ambazo imekuja hadithi kutoka kwa Mtume (S.A.W.). 

Hadithi inayoashiria juu yake ni ile iliyopokelewa na Abuu Ubeid na wengineo kutokana na hadithi ya Ibni Abass (R.A.) kutoka kwa Mtume (S.A.W.) kuwa yeye amesema "Ni zipi dawa mbili zenye uchungu? Jibu lake ni sufa na swabri (shubiri)." Hadithi hii ameipokea Abuu Daud katika kitabu cha Marasiil. 

Nguvu ya sufa ni ujoto na ukavu katika daraja la tatu nayo inatia joto, inalainisha tumbo, inatoa wadudu wa minyoo waitwao chembe chembe za mumunye (Round worms), inaondosha uvimbe ulioko kwenye wengu, inaponyesha mapele yenye majeraha na mabaka na inazidisha hamu ya maingiliano ya mume na mke. 

Sufa ikichanganywa na asali safi na kufungwa penmye uvimbe katika wengu huponyesha. Ikinywewa huondosha sumu ya vidudu vitambaavyo vyenye sumu kama nyoka, nge n.k. Ikipikwa pamoja na lina huondosha taka taka zilizoko kwenye kifua; ikifukizwa ndani ya nyumba hukimbiza vidudu vyote vyenye sumu. Ikichanganywa pamoja na unga wa ngano na siki ya zabibu na kufungwa penye maumivu makali ya mishipa ya nyuma ya mapaja (sciatic nerve), na mshipa wa kiuno (cavity of the hip) huponyesha, na pia huondosha uvimbe wenye joto mwisho wake. 

Ikifungwa pamoja na maji safi inaivisha majipu na inaponyesha maradhi ya ulegevu wa viungo vyote, inazidisha hamu ya chakula, inaponyesha pumu na uzito wa kuvuta pumzi (breathlessness). Pindi ikinywewa au kupenyezwa kwenye mishipa (kudunga sindano) inasafisha mianzi ya mapafu na kutoa malenda mazito mazito yaliyomo humo na pia inafungua hedhi. 

Ikisagwa, uzito wa kiasi wa dirham tano (swa na vijiko vidogo 10) na kunywewa na maji ya moto, hufungua choo, huondosha gesi tumboni na huondosha maumivu makali wakati wa kwenda haja kubwa yanayosababishwa na baridi, na huponyesha maumivu ya kichwa kinachotokana na baridi na mabalagham; huponyesha mabalalagha na huondosha mabaka meupe ikipakwa na siki ya zabibu. 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI  

Waislamu hawatokubali kusingiziwa mambo 
Na Mwandishi wetu 

Serikali ya Sudan yadhamiria kuleta amani ya kudumu 
Na Mwandishi Wetu 

Mwalimu alaumiwa kuwashawishi watoto waingie ulokole 
Na Badru Kimwaga 

Wanawake Arusha watakiwa kutafuta elimu 
Na Habiba Swedi, Arusha 

Tamsa Tanga yapata viongozi wapya 
Na Masoud Mohamed 

Mjue Dr. Abuu Ameena Philips: Mwanaharakati aliyewasilimisha askari 3000 wa Amerika 

Duniani kwa ufupi 

Barua ya Ofisa Elimu ina agenda nyuma yake 
Na Mussa Ally Morogoro 

Nabii Isa Mwana wa Maryamu ni Yesu huyo huyo!! 

Kuanzishwa ‘Islamic Club’ ni ajenda ya siri inayoweza kuhatarisha amani Tanzania 

Agenda ya siri 
Na. Hassan Kimangale 

Hatua ya Rais kutengua uteuzi wa Parole ni ya kizalendo 
Na J. R. Msuya 

Serikali iwahurumie raia wake 
Na BADRU KIMWAGA  

Wanawake  Waislamu  Wilayani Masasi waanzisha Jumuiya 
Na Yousouf  S. Kayungilo, Masasi 

Kuhifadhika kwa mwanamke ni kuhifadhika kwa jamii 
Na Zuhra Tajiri 

Waislamu  wekezeni kwenye kheri -Mwinyi 
Na Mwandishi Wetu, Tanga 

Biashara ya ufuska yavamia Z’bar Polisi uchwara’ wanufaika 
Na Rajab Rajab 

Asimamishwa uongozi kwa kutoa fat’wa ya Hitma 
Na Nadhiru Ishengoma Wetu , Kahama 

Aqswa waazimia kufuata Qur’an na Sunna 
Na Mwandishi Wetu 

Mafunzo ya Quran  

Barua za wasomaji  

Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)  

Masomo  

Chakula na Lishe  
  

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita