AN-NUUR
Na.161 Rabiul Thani 1419, Agosti 7-13, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Serikali iwahurumie raia wake 
 
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu na Utamaduni ilitangaza ongezeko la gharama za ada kwa shule zake zitakazoanza mwakani. Je,ongezeko hili linapokelewaje na wananchi hasa wale wenye kipato cha chini. Mwandishi BADRU KIMWAGA  

WAKATI ilipotangazwa kuongezeka kwa gharama za masomo kwa shule za serikali, kila Mtanzania alitambua kuwa huenda dhumuni la serikali ni kuwatenga watoto wa kilalahoi kuendelea kuwa kizani, huku watoto wa vigogo kuendelea kupanuka kielimu kutokana na kuweza kumudu gharama hizo. 

Waziri wa Elimu na Utamaduni, Profesa Juma Kapuya alitangaza mwishoni mwa wiki iliyopita bungeni wakati wa hotuba ya Wizara yake kuwa, serikali kuanzia mwakani imeongeza gharama za Ada kwa wastani wa asilimia kumi na tano, bila kujua kama bajeti hiyo na utekelezaji huo unawakandamiza watoto wa walio wengi ambao wanastahili kupata elimu kama ilivyo ada na haki yao kielimu. 

Upandaji huo wa gharama huenda ukawafanya wazazi wengi, ambao kabla ya upandaji huu, walikuwa hawawezi kumudu kulipia gharama za awali kwa watoto wao, jambo lililopelekea watoto hao kushinda majumbani na mitaani wakizurura, kuendelea kuwatupa watoto wao kielimu na huenda baada ya miaka mitano ijayo vijana wengi watakuwa mambumbumbu kwa ujinga. 

Gharama hizi ni kubwa na haziwiani na kipato cha wazazi wa daraja la tatu ambao mshahara wao hauzidi shilingi 30,000 kwa mwezi huku fedha hizo, zigawe katika kodi ya nyumba, nauli, chakula na matibabu, mavazi na gharama za masomo kwa watoto. 

Serikali sina shaka inatambua kuwa ilipokuwa inaomba kura kwa wananchi, yenyewe ilitangaza kuwa ikiingia madarakani itakazania kukwamua hali za huduma za jamii, elimu ikiwa mojawapo. Lakini ajabu ndio kwanza inakwaza. 

Ina maana gharama za awali hazikuwa zinakidhi haja ya mashule hayo hadi kufikia kuongeza gharama hizo toka shule za msingi hadi shule za sekondari? Au serikali ina agenda ya siri juu ya watoto kupata elimu? Kama sio, kwanini sasa inazidi kumpa mzigo mzazi katika hali hii iliyo ngumu kiuchumi, ambapo wengi wao hushindwa kujua watakula nini kutokana na kutokuwa na kipato kizuri huku wakiwa hawana ajira? 

Sidhani kama ongezeko hilo la gharama za masomo, lilifanyiwa uchunguzi kabla ya kupelekwa bungeni ili kupitishwa na mwakani kuanza kutumika, ikiwa imefanyiwa uchunguzi, basi uchunguzi huo haukuwa wa kitaalamu. 

Na nani katika hali hii ngumu atakayeweza kuwasomesha watoto wake wanne au kumi,kwa gharama hizi huku kipato chake kikiwa hafifu? Au mzazi yupi ambaye hutegemea kukaanga samaki kuweza kuwapeleka watoto wake shuleni, huku akikabiliwa na matumizi mengi kuliko fedha alizo nazo? 

Kwa hiyo, watoto wa walalahoi wataendelea kujazana mitaani wakiwa mambumbumbu, huku watoto wa wakubwa na matajiri wakiendelea kusoma hadi vyuo vikuu, kutokana na kuweza kumudu gharama zake. Serikali kwa yakini ingekaa na kufanya tathmini ili kuweza kujua licha ya gharama za awali kuwa nafuu, watoto wangapi wa wachovu waliokuwa wanarudishwa majumbani kwa kushindwa kulipa ada na gharama nyingine? 

Ikiwa gharama za kumuandikisha mtoto mmoja, kumlipia ada na michango ya ujenzi na mingine katika shule za msingi huwa kubwa na mzigo kwa wazazi wa daraja la tatu, je, hivi sasa hao hao wanaweza kumudu gharama hizi mpya? Nini maana ya ukweli na uwazi, kwanini isitangazwe wazi kuwa wanaotakiwa kusoma ni watoto wa wanene tu? 

Ukichukua gharama hizi kupanda tangu shule za msingi hadi sekondari ina maana kuwa watoto wa wazazi wasio na uwezo, uwezekano wa kusoma kuanzia mwakani utakuwa mdogo au haupo kabisa na kuishia kushinda mitaani wakijishughulisha na kazi za biashara au kujitumbukiza katika vitendo viovu na vya kihalifu. 

Serikali kupitia Wizara yake imesema kuwa mwakani UPE itakuwa kiasi cha shilingi 2,000 badala ya 1,000 iliyokuwa inatozwa, shilingi 40,000 badala ya 30,000 kwa shule za sekondari za kutwa na 70,000 badala ya 45,000 kwa shule za bweni, inaonyesha kwamba ikichanganya na michango ya shule na gharama nyingine, ili mtoto aweze kusoma shule ya msingi au sekondari basi itamgharimu mzazi si chini ya shilingi kati ya 20,000 kwa shule za msingi na 150,000 kwa shule za sekondari, mzazi gani wa kipato cha chini atakayeweza kumudu gharama kama sio matajiri? 

Uwiano gani huu unaoimbwa majukwaani kuwa watu wote ni sawa na wenye kuhitaji mahitaji yote muhimu, kama elimu? Hapa si kufumbiana fumbo tu na mwerevu aling’amue kama tunavyoelezwa na waswahili! 

Mshahara wa wazazi wengi wa kima cha chini ni 50,000/- huku wengine ambao waliokumbwa na zoezi la kupunguza wafanyakazi makazini mwao wanajishughulisha na kazi za kujitafutia riziki zao za kila siku ‘kimawengemawenge’, sasa kwa mtaji huu kweli watasomesha watoto wao na kumudu hali ngumu ya uchumi inayowakumba wengi nchini, hasa watu waishio vijijini? 

Pengine serikali ingefikiria upya suala hili ili watoto wa walalahoi wasome na pia kuwapunguzia mzigo mzito unaowabana, mzazi wa kipato cha chini, akigeuka VAT, huku gharama za matibabu, mara elimu, au sijui kodi ya nini, kweli atakuwa na furaha ya kuwa mwananchi, kwa kuelewa kuwa wako wengine wanaosomesha watoto Ulaya, matibabu yao Ulaya na kila kitu nje ya nchi, huku wakikandamizwa wao, sio kujenga chuki na vinyongo mioyoni? Mimi sichochei, lakini serikali haioni? 

Muungano wa vyama vya Wafanyakazi nchini (TFTU) na vingine vinavyojihusisha na wafanyakazi vimekuwa vikiipigia kelele serikali iongeze mshahara wa wafanyakazi, kima cha chini kisiwe chini ya shilingi 200,000, lakini serikali imekuwa "kiziwi", huenda wangelikubali ombi hili kidogo kama sio sana ingewasaidia wazazi wenye kipato cha chini kuweza kumudu hali ngumu ya uchumi na kugharamia baadhi ya huduma za jamii, lakini kwa hali hii inazidi sio kuwawia vigumu bali kuwafanya wazidi kutengwa ndani ya jamii na wao kama binadamu hujenga chuki. 

Hata matukio mengine yanayotokea nchini kama fujo za Mwembechai, Arumeru, sijui wapi, zote hutokea sababu ya serikali kutojali masilahi ya wananchi wenye vipato vya chini na kujijali binafsi na zinapotokea uonyeshaji wa kuchoka kwa wananchi, lawama hutupiwa wapinzani kwa mtazamo wa kisiasa badala ya kuona hali halisi wanayoipandikiza. 

Wananchi wengi hudhani serikali imewatupa, wakifanya biashara hukamatwa, wanavunjiwa vibanda, nyumba zao, wanapandishiwa kodi, gharama za matibabu, mara elimu na katika kuonyesha chuki na kilio chao ndio hufanya yale yanayoweza kuhatarisha amani, lakini kwa hekima na uvumilivu walio nao wananchi, wamekuwa wakilia kimoyomoyo bila kuonyesha dhahiri. Lakini hali hii nayo ina mwisho wake. 

Serikali haioni uchungu kuwa na vijana wengi wa mitaani wasio na elimu ambao kutokana na kushindwa kuwa na elimu hujitumbukiza katika. 

Sina shaka serikali italiona hili na kuchukua tahadhari mapema kuweka hali sawa na kuwapunguzia gharama wazazi wenye kipato cha chini ambao kula yao ni shida seuze kuchangia gharama nyingine za huduma muhimu kama hiyo ya elimu? 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI  

Waislamu hawatokubali kusingiziwa mambo 
Na Mwandishi wetu 

Serikali ya Sudan yadhamiria kuleta amani ya kudumu 
Na Mwandishi Wetu 

Mwalimu alaumiwa kuwashawishi watoto waingie ulokole 
Na Badru Kimwaga 

Wanawake Arusha watakiwa kutafuta elimu 
Na Habiba Swedi, Arusha 

Tamsa Tanga yapata viongozi wapya 
Na Masoud Mohamed 

Mjue Dr. Abuu Ameena Philips: Mwanaharakati aliyewasilimisha askari 3000 wa Amerika 

Duniani kwa ufupi 

Barua ya Ofisa Elimu ina agenda nyuma yake 
Na Mussa Ally Morogoro 

Nabii Isa Mwana wa Maryamu ni Yesu huyo huyo!! 

Kuanzishwa ‘Islamic Club’ ni ajenda ya siri inayoweza kuhatarisha amani Tanzania 

Agenda ya siri 
Na. Hassan Kimangale 

Hatua ya Rais kutengua uteuzi wa Parole ni ya kizalendo 
Na J. R. Msuya 

Serikali iwahurumie raia wake 
Na BADRU KIMWAGA  

Wanawake  Waislamu  Wilayani Masasi waanzisha Jumuiya 
Na Yousouf  S. Kayungilo, Masasi 

Kuhifadhika kwa mwanamke ni kuhifadhika kwa jamii 
Na Zuhra Tajiri 

Waislamu  wekezeni kwenye kheri -Mwinyi 
Na Mwandishi Wetu, Tanga 

Biashara ya ufuska yavamia Z’bar Polisi uchwara’ wanufaika 
Na Rajab Rajab 

Asimamishwa uongozi kwa kutoa fat’wa ya Hitma 
Na Nadhiru Ishengoma Wetu , Kahama 

Aqswa waazimia kufuata Qur’an na Sunna 
Na Mwandishi Wetu 

Mafunzo ya Quran  

Barua za wasomaji  

Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)  

Masomo  

Chakula na Lishe  
  

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita