|
|
|
Na J. R. Msuya NAPENDA nichangie makala ya Bw. Edmund Kapinga aliyotoa katika gazeti la Rai 16 –22 Julai, 1998 juu ya hatua aliyoichukua Rais kutengua bodi ya Parole na kuagiza ziundwe nyingine kwa kuzingatia uwiano katika jamii. Kwa ujumla, Bw. Kapinga anamlaumu Rais kufuatia hatua yake hiyo kwa kile anachokiita kuendekeza udini. Bw. Kapinga anabainisha hofu yake hii pale anaposema kuwa hali hii inaleta wasiwasi kuwa huenda baadaye Waislamu wakadai tena uwiano wa kidini uangaliwe na hii ikasababisha vurugu pindi uteuzi mwingine ukitokea. Labda swali dogo tu kwa Bw. Kapinga, ana ushahidi gani kuwa uteuzi au teuzi zitakazofuata katika nafasi mbalimbali zitajaza Wakristo tu? Na nani atakayekuwa mwendawazimu adai kuangaliwa uwiano pale ambapo uadilifu na usawa utafuatwa. Hii inanitisha kuwa huenda maana ya ‘udini’ kwa Bw. Kapinga ni tofauti na ile tunayoifikiria. Endapo shirika la serikali linalojaza watu wa kabila moja tu huambiwa kuwa lina ukabila, iweje taasisi ya serikali inayojaza Wakristo watupu isiwe na udini? Kama Afrika Kusini ililaumiwa kwa ubaguzi wa rangi kutokana na watu weupe kugawana vyeo na kuwa wenyewe vipi leo Wakristo wakihodhi madaraka kwenye mashirika na vyombo vya dola isiwe ni ubaguzi wa kidini? Bw. Kapinga anatuambia kwamba zile Parole hazina sura ya udini bali zimezingatia sifa na uzoefu, uwezo na utaalamu. Huenda Bw. Kapinga, ama kwa makusudi au kwa kutokujua analosema anawafanya Watanzania wote kuwa ni wajinga, vipofu au viziwi. Huenda angetusaidia sana endapo angetuambia kuwa uzoefu na uwezo huo unapatikana kwa Wakristo tu wakiongozwa na viongozi wao wa kanisa. Askofu, uzoefu wa sheria, wafungwa na Parole kaupata wapi! Hoja ya Bw. Kapinga kuwa uteuzi ulifanywa na Waziri Ali Ameir Mohamed na hivyo uteuzi huo ni halali na hauna sura ya udini ni hoja kiwete. Kwanza kwa kuwa Waziri Ameir sio Mungu ambaye ameepukana na upungufu. Ameonyesha kumsifu Waziri huyo hasa kutokana na msimamo wake ambao unafanana na wake yeye (Kapinga). Hata hivyo, anashindwa kuelewa kuwa Waziri huyu ni yule ambaye amekuwa akitoa kauli ambazo ama anashindwa kuzithibitisha au kuzitolea maelezo. Ni vema Bw. Kapinga akatuambia kama anajua zile balozi nne alizotaja Waziri Ameir kuwa ana ushahidi kuwa zilihusika na vurugu za Mwembechai. Je vile vyama vya upinzani alivyovituhumu Waziri kwa hili hili suala la Mwembechai Kapinga anavijua? Je, sio huyu huyu Waziri aliyedai bungeni kuwa sababu ya mtoto mdogo Chuki kupigwa risasi ni kwa vile alikutwa na nyaraka za uchochezi, lakini akashindwa kuelezea kuwa ilikuwaje polisi wagundue kuwa huyo Bw. Mdogo alibeba nyaraka za uchochezi wakati wao walikuwa mita kadhaa wakati wanamlenga risasi? Huenda Bw. Kapinga anamsifu au kumvika kilemba cha ukoka Bw. Ameir kwa vile amefanya kile anachotaka yeye kifanyike, vinginevyo mtu mwenye mapenzi na nchi yake, ambaye ni mcha Mungu kweli angehoji kwa nini huyu Waziri asijiuzulu kwa kuchafua na kutia doa jeusi serikali yetu ya ukweli na uwazi. Ni bahati mbaya kwamba ukweli na uwazi umegeuzwa kuwa ubabe na uwongo na baadhi ya viongozi wa serikali kama kina Ameir. Shutuma za Bw. Kapinga kwa Rais kwamba kitendo chake cha kutengua bodi za Parole si kwa maslahi ya wananchi wa nchi hii, hakina msingi bali ni hisia za ushabiki, ubinafsi na chuki za kidini. Bw. Kapinga amejaribu kutetea shutuma zake hizo kwamba utenguzi wa Parole hauna uhusiano na maslahi ya wananchi eti kwa kuwa hamna kamati iliyofanya utafiti na kuthibitisha kuwa yale yalikuwa ni madai ya wananchi au watu wachache wa Dar es Salaam. Hata hivyo, anasahau kuwa ameanza makala yake kwa kubainisha kuwa uamuzi wa Rais kutengua Parole hizo kulifuatia malalamiko ya Mabaraza ya Kiislamu. Kwa kauli hiyo, anataka tuamini kwamba mabaraza ya Waislamu ni kwa ajili ya watu wa Dar es Salaam tu! Aidha, huenda Bw. Kapinga anataka tuelewe kuwa magazeti kadhaa kama Mtanzania, Majira n.k. ambayo yaliona kasoro hizi na kuzikemea katika tahariri zao au makala nyingine ni mabaraza ya Kiislamu! Vile vile Bw. Kapinga anashangaa ni vipi Rais aingilie kati suala la Parole wakati amekuwa akipuuza malalamiko halisi ya wananchi kama mabadiliko ya katiba n.k.. Kwa kutumia kigezo chake cha kuthibitisha labda ni kamati zipi zilizoundwa kuratibu maoni ya wananchi wote ili kujua kama kweli anayoyataja kuwa maoni halisi ya wananchi ni ya kweli. Hapa Bw. Kapinga anaonyesha ukereketwa ambao huenda akiambiwa aue ili kuonyesha mapenzi kwa dini yake atafanya hivyo. Ama kuhusu takwimu alizotoa Bw. Kapinga ambapo anadai kuwepo dini kubwa tatu na kila moja ikiwa na waumini ambao ni takribani asilimia 30 ni namna nyingine ya kujichanganya na hii haiwezi kuondoa dhambi ya kundi moja kati ya hayo ya kuhodhi nafasi muhimu katika vyombo vya serikali na vile vinavyohusika na utoaji wa maamuzi muhimu. Ikiwa kundi au dini moja lina waumini ambao ni asilimia 30 na itokee nafasi zote muhimu zihodhiwe na dini hii basi hii ina maana kuna uporaji wa haki za wengi unaofanywa na wachache na hii haileti matarajio ya amani na utulivu huku tuendako maana asilimia 70 iliyobaki itaamau kujichukulia haki yao. Hii imetokea sehemu nyingi duniani, Rwanda, Burundi na Afrika Kusini ni mifano michache tu. Kwa hiyo, Bw. Kapinga kama ni raia na Mcha Mungu Mwema angeona ukweli huu badala ya kupiga propaganda. Ama nukta ya Bw. Kapinga kuwa uteuzi pamoja na kuangalia sifa umeangalia pia nafasi zao kiutendaji serikalini ni porojo ambayo hata mtu ambaye hajaenda ngumbaru anaweza kuiponda. Bila shaka angetueleza nafasi walizonazo serikalini Mapadri na Maaskofu walioteuliwa katika bodi za Parole ingeweza ikaleta mantiki. Nahitimisha kwa kumpongeza Rais kwa hatua yake ya kijasiri na kizalendo. Ni matarajio yangu kuwa hii ni hatua ya awali tu katika kurekebisha mifumo mibaya ya utawala ili watu wote wachangie maendeleo ya nchi bila kujali dini. Kuendelea na dhana kuwa watu wa dini moja tu ndio wenye uwezo ni hatari.Na tunategemea Rais wetu kupitia vyombo vyake kutupa maelezo juu ya wale wanaoorodhesha majina ya wanafunzi Wakatoliki kila inapokaribia mitihani kama ilivyodhirika kule Morogoro. |
Waislamu hawatokubali kusingiziwa
mambo
Serikali ya Sudan yadhamiria kuleta
amani ya kudumu
Mwalimu alaumiwa kuwashawishi watoto
waingie ulokole
Wanawake Arusha watakiwa
kutafuta elimu
Tamsa Tanga yapata viongozi
wapya
Mjue Dr. Abuu Ameena Philips: Mwanaharakati aliyewasilimisha askari 3000 wa Amerika Barua ya Ofisa Elimu ina agenda nyuma
yake
Nabii Isa Mwana wa Maryamu ni Yesu huyo huyo!! Kuanzishwa ‘Islamic Club’ ni ajenda ya siri inayoweza kuhatarisha amani Tanzania Agenda ya siri
Hatua ya Rais kutengua uteuzi wa
Parole ni ya kizalendo
Serikali iwahurumie raia wake
Wanawake Waislamu Wilayani
Masasi waanzisha Jumuiya
Kuhifadhika kwa mwanamke ni kuhifadhika
kwa jamii
Waislamu wekezeni kwenye
kheri -Mwinyi
Biashara ya ufuska yavamia
Z’bar Polisi uchwara’ wanufaika
Asimamishwa uongozi kwa kutoa
fat’wa ya Hitma
Aqswa waazimia kufuata Qur’an
na Sunna
Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)
|