AN-NUUR
Na.161 Rabiul Thani 1419, Agosti 7-13, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
BARUA

Vifungu vya sheria vinavyohalalisha zinaa vifutwe 

Ndugu Mhariri 

Maoni juu ya yatokanayo na nakala ya barua ya Bi. Halima Mussa wa Iringa na ushauri alioshariwa katika kipindi cha Mwangaza 

Nimebahatika kusikia kipindi cha Mwangaza siku ya Jumapili Julai 26, mwaka huu kuanzia ilipokuwa inasomwa nakala ya barua ya Bi. Halima Mussa wa Iringa aliyeishi na Ndugu Polikap kwa muda wa miaka 18 na kuzaa naye watoto kama mume na mke, hadi kujihisi kuwa ni mume na mke. 

Msimamizi wa kipindi hicho alisisitiza kwa mwanasheria aliyekuwepo katika kipindi hicho, kuwa matatizo yaliyompata Bi. Halima yanawapata wanawake wengi sana. Na kumtaka mwanasheria atoe msaada wa ushauri wa kisheria utakaomsaidia Bi. Halima na wanawake wengine wenye matatizo kama hayo. Na mwanasheria alishauri kama ninavyokumbuka hivi ifuatavyo: 

Baada ya barua yake Bi. Halima Mussa kwa Paroko ya kupinga ndoa ya ndugu Polikap na aliyekusudia kumuoa, aende Baraza la Usuluhishi la Ustawi wa Jamii la Wilaya hiyo wanayoishi, huko watamwita Polikap na kumuhoji na kumlazimisha baadhi ya mambo kisha aende mahakamani kufungua madai ya takala huko mahakamani ndipo atakapopata, haki ya masurufu ya watoto na mali waliyochuma naye huyo Polikap, na adai mali ya kuanzia maisha, yote atayapata huko mahakamani kisha akatoa nasaha na kusisitiza sana kwa huyo Paroko asiikubali ndoa naye. 

Na akatoa hoja kuwa Maparoko hairuhusiwi kuwafungisha ndoa zaidi ya moja waumini wao! Wakati huyo Polikap alishakuwa katika baina yake na Bi. Halima Mussa. 

Maoni yangu juu ya chanzo cha matatizo aina hii: 

Chanzo na mtaji mkubwa wa matatizo haya ni ongezeko la wimbi la watoto wanaoitwa wa mitaani ni Sheria ya ndoa kuhalalisha zinaa. 

Kwa hiyo, njia nyepesi ya kinga ya matatizo haya ninawaomba wasimamizi wa mapendekezo ya kurekebisha Fungu la 72, linaloruhusu kuzini na mke au mume wa mtu, na kupewa fidia hiyo iliyeziniwa mkewe au mumewe. 

Kwa kweli hii fidia labda kwa wale wasiokuwa na dini kabisa, lakini kwa wenye dini mke au mume akizini inakuwa nikinyaa kabisa na ni hatari kubwa inayoweza kupelekea kifo au vifo kwa hatua atakazozichukua mtendewa au kwa magonjwa ya hiyo zinaa. 

Na ni msingi mkubwa wa kuvunjika kwa ndoa nyingi na watoto kuingia mitaani. Na fungu la 160, hili lifutwe kabisa na lisahauliwe nahata masikioni lisisikike kwa vizazi vijavyo, kwa kuhalilisha zinaa iliyodumu kwa miaka miwili, kwani fungu hili ndiyo mtaji mkubwa wa matatizo yanayomsibu Bi. Halima Mussa na hao wanawake wengi wengine. 

Fungu hili linapingana na matakwa ya Mwenyezi Mungu. Na ni kumkosoa Mwenyezi Mungu aliposema: "Usiue, Usizini, Usiibe" n.k. Kutoka 20:12-17 Kumbukumbu 5:16-21. Mathayo 5:27-28. Luka 18:20. Qur’an 17:32, Qur’an 24:2-3. 

Mtu akiua au akiiba sheria zetu zinamtia hatiani, lakini akizini (ukiondoa kubaka) inayoonekana ni halali. Je, Mungu aliyekataza kakosea? Huu ni ujeuri mkubwa mbele ya Mwenyezi Mungu, ambaye tunamuomba kwa wimbo wa Taifa na dua ya kuliombea Bunge! 

Na juu ya kumsihi kiongozi wa dini au muumini wa dini kuitambua ndoa inayotajwa na hilo fungu la 160, ni jambo gumu sana maana kwenye dini, hiyo ndiyo zinaa, siyo ndoa. Na kwa kuwa zinaa ni uasi, katika dini kuna kitu kinaitwa, toba au kuungama, ni kutokana kuacha kabisa uasi huo kutafuta msamaha kwa Mungu, sasa ikiwa sheria yeyote inamlazimisha kiongozi au muumini wa dini kuutambua uasi! Itakuwa umemvunjia haki ya kikatiba Ibara ya 19. 

Sasa tuingie kuchuma na kumiliki mali kwa mume na mke 

Kwa kweli kufanya kazi ya kuchuma na kumiliki ulichokichuma ni haki na wajibu wa mume na mke. Ndiyo maana tokea kale katika Agano la Kale, utakuta mama Sarai alimiliki hata mjakazi wake akampa mumewe Ibrahim awe mkewe. Mwanzo 16:3. Kwa hiyo, hadi leo naomba visomwe vifungu hivi Qur’an4:32, Qur’an 3:195. 

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 Ibara ya 22-23. Sheria ya ndoa 1971, fungu la 56. Ukishasoma utafahamu wazi kuwa kila mwanamume na mwanamke anawajibika kuchuma na kumiliki alichochuma, hivyo basi, kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu amemuumba mwanamume kuwa na maguvu mengi ya kazi ngumu, ndiyo maana sheria ya Mwenyezi Mungu inamtaka ale kwa jasho lake. (Mwanzo 3:19) 

Na chakula cha mke na watoto kuwa juu yake. (Qur’an 2:233) na anachokichuma mke halazimishwi kumlisha mume wala watoto, ila anayo khiari ya kufanya hivyo, anacholazimika yeye kwa Mungu ni kuhiji na kutoa zaka na sadaka. 

Lakini hivi leo kuna kudhulumiana mali eti kwa sababu ya ndoa, siku za nyuma wakidhulumiwa sana wanawake, haswa wa vijijini, kwa kufanya kazi za uzalishaji mali bila mikataba ya mali. 

Aliyoisema Mwenyezi Mungu katika Qur’an 2:282 na sheria ya ndoa 1971, fungu la 58 matokeo yake ndoa ikivunjika mke huondoka patupu. 

Hii ni dhulma kubwa yapaswa kupigwa vita, na vimeibuka vikundi vya kina mama vyenye kuendesha kampeni kubwa ya kuwadhulumu wanaume, na wanaume wengi wanadhulumiwa, mwanamke hata asiyejishughulisha na uzalishaji wa mali, au amechuma mali, lakini akitumia kwa maslahi yake bila ya kuchangia kwa mume chochote, ndoa yake ikivunjika wanasimama kidedea kuwa mali ya mume iuzwe agaiwe huyu aliyekuwa mke, hata sheria ya ndoa ya 1971 fungu la 114 kifungu cha (2) (b) kinachoeleza kugawa mali ya ushirika wa mume na mke, wao hawakitaki wanadai kinamdhulumu mwanamke! 

Hii ni kwa sababu ya utamu wa dhulma walioonja umewanogea. Pia dhulma hii yapaswa ikomeshwe kabisa kuikataa Ibara hiyo kwa sababu za kijinsia ni kukiuka katiba ya Jamhuri Ibara ya 13 kifungu (1) – (5). 

Kwa uchache wa maoni yangu napenda nishauri mambo matatu: 

Juhudi ziongezwe za kuelimisha umma wa Watanzania haki na wajibu wao ili dhulma zipungue au zitokomee. 

Wakati wa kupendekeza sheria washirikishwe kimaoni au kiushauri wana dini. 

Serikali na vikundi vyote vinavyotangaza na kusambaza kondom, viwasaidie wana dini kupinga na kukataza zinaa. 

Saidi Jadi Omar, 
Mbagala Kibonde Maji, 
S.L.P. 77635, 
DAR ES SALAAM. 
 

Luteni kila kitu kina mwisho 

Ndugu Mhariri, 

NIFIKISHIE salaamu zangu kupitia gazeti lako nipate kujibu shutuma za Bw. Makamba dhidi ya Itkafu za Waislamu Mwembechai: Dar Leo No. 599 JulaI 27/7/98 ambalo lilimnukuu akijipa ushindi dhidi ya itikafu hizo. Awali ya yote Luteni anapaswa kuelewa kwamba Mungu hafanyi kazi zake kwa jazba wala Mungu hajaribiwi wala hashindwi na lolote. 

Wala usidhani Mwenyezi Mungu ameghafilika na (haya) wanayoyafanya madhalimu. Hakika Yeye anawaakhirisha tu mpaka siku ambayo macho (yao) yatakodoka (yatoke nje kwa khofu 14:42. 

Imekuwa kawaida ya Bw. Luteni kujipa ushindi pindi anapowafanyia madhila Waislamu rejea kipindi cha Redio Tanzania katika Hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja na Redio tarehe 03/04/1994 Jumapili ya Pasaka akiwa mgeni rasmi katika Ibada ya Pasaka Morogoro Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT). 

Baada ya madhila yaliyowapata Waislamu ya kupigwa mabomu msikitini na wengine kuumizwa Askari kuingia msikitini na viatu kama kawaida yao wanapovamia misikiti. Alitamba mbele ya Askofu Sendoro kwa kunukuu aya za biblia - Warumi Kumi na tatu: Itikeni mamlaka inayowazidi nguvu na waliopewa mamlaka wamepewa upanga: (hata ya shetani)? akaifananisha na Qur’ani 4-59. Akasema: Enyi mlioamini mtii Mwenyezi Mungu na mtume wake na wenye mamlaka. Aliendelea na mhadhara. Baba Askofu ukisoma Mathayo 23 Inasema maneno ya makuhani hawa mafarisayo muyasikilize kwa sababu hawa wameketi katika kiti cha Mussa akamalizika aya hiyo kwa kusema! 

Mchungaji akishamaliza kusali akatengeneza bustani yake akafuge nguruwe, akafuge kuku wale wanaosema nguruwe ni haramu ni sawa kwa kitabu chenu maana nina marafiki zangu wengine Biblia hii hununua kwenye bookshop, wengine husoma miaka saba sasa Mwafanana? Ndiyo yeye anaenda kwa....anachukua Mstari mmoja anasoma kwamba Walawi 11.7 Nguruwe yuapaswa makwato hacheui kwa hiyo msimle, lakini kuna agano la kale. Kuna agano jipya linasema kila kiingiacho sio najisi isipokuwa kinachotoka (vifijo na vigelegele na vicheko. Ukisoma ukichukua neno moja tu, ukatafsiri basi utaleta matatizo. Mwisho Makamba alisema sisi ni serkali tulitangaza tukasema, tumepiga marufuku mihadhara ya dini, watu wengine hawakuelewa wakasema serikali imekataza mihadhara ya dini, sio kweli hivi Injili hii baba Askofu si lazima itangazwe sasa unaitangazia hum humu. Maana hawa ukitoka bango lao linasema tumepokea na tumemkiri Yesu wote hawa. Jamani kila mtu ana bango lake. Bango la hawa wakina Tesi limeandikwa hapa mimi nimemkiri Yesu. Sasa ukieneza Injili humu utapata tabu wako watu wako kule Magubike. Wako kwifipa, wako Bilo, wako Kilosa kwa mpepo wanaawangoja. Sasa wewe serikali ukisema msihubiri hawa watalisikia lini nendeni tu watu watatu, pale sokoni funga kipaza sauti anzeni tu kuimba. Bw. Makamba akaanza kuimba kama kawaida yake "Bwana Yesu yuko wapi mpenzi wangu Rafiki (vicheko na vifijo) njia gani amekwenda nitamwonaje mimi watu watakuja: Mwisho wa kumnukuu: 

Uchambuzi: Mungu anasema: Basi usimuombe Mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa - watakaoadhibiwa: 26:213. 

Luteni imekuwa kawaida yake kuchanganya Ibada ya Mungu pamoja na wale waliomfanyia Mungu Washirika kama ulivyofanya hapo Morogoro, na huko Uwanja wa Taifa na au ukashiriki kuimba pamoja na Bonkhe. 

Kumbuka Ndugu Luteni Bwana Mrema ambaye ulimkanyaga katika mkutano wako alikuwa na nafasi kubwa. Alikua ni Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Ndani, alifanya mengi dhidi ya Uislamu na Waislamu. Waislamu walimuomba Mola wao nae alitamba kwamba itkafu zinamnenepesha. Vipi leo; yuko wapi? 

Pamoja na kwamba unajigamba kwamba mwanajeshi hashindwi. Rejea Historia; walikuwepo waliotamba; leo wako wapi? 

Abuu Hafsa, 
Dar es Salaam. 
 

Kadinali usiseme yasiyo kweli 

Ndugu Mhariri 

Hotuba ya Kadinali Pengo iliyotoka katika gazeti la Msemakweli la tarehe 5-11/7/98 yenye kichwa cha maneno "Jiepusheni na Wendawazimu" ni kielelezo wazi kuonyesha namna kiongozi huyu alivyokosa uvumilivu katika kukabiliana na mambo mbalimbali yanayousumbua moyo wake. 

Pamoja na kwamba katika hotuba yake amejipigia ngoma na kucheza mwenyewe kwa kujifanya yeye ni mtu wa busara na hekima na kuwaona wenzake ni wendawazimu na watu wa jazba, hotuba yake ilitawaliwa na lugha ya jazba. 

Kuwaita watu wendawazimu kwa sababu tu wanatumia haki yao ya kikatiba kutoa mawazo yao sidhani kuwa ni lugha ya kiuchungaji. 

Yapo maneno mengi bwana Kadinali Pengo angeyatumia kama hakukusudia kutukana. 

Pia katika hotuba yake Kadinali Pengo alidanganya pale aliposema kwamba vurugu za Mwembechai, wakorofi walianzisha mihadhara, wakatokea Wakristo wakajibu, na polisi walipofika walishindwa kumtambua mwendawazimu ni yupi......" Kadinali Pengo anapaswa kuwaeleza watu ukweli tu chanzo cha vurugu za Mwembechai hazikuhusiana na Wakristo kwenda kwenye mhadhara na kubwa zaidi ni kwamba siku ya vurugu hapakuwa na mhadhara. 

Kadinali Pengo pia hakusema ukweli pale alipotamka kwamba yeye hajibizani na wendawazimu kwa sababu ya kulinda amani na wakati hotuba yake yote ilikuwa ni majibu na tena ya jazba. 

Japo Pengo anajisifu kuwa amechaguliwa kuwa Kadinali kwa sababu nchi hii ina imani thabiti, ingempasa pia kujua kuwa taifa la Tanzania halinufaiki vyovyote kwa yeye kuchaguliwa ama kutochaguliwa kuwa Kadinali mbali ya Wakatoliki wenzie. 

Ndugu Pengo angejaribu kuiga lugha nzuri za maaskofu na wachungaji wenzie kama akina Mchungaji Kusupa, Father Mkwera, Mchungaji Kakobe na Mchungaji Sambano. Vinginevyo, mimi sina muda wa kutumia lugha chafu katika kujibizana naye kwani namuogopa Mungu. Pia simuombi aombe msamaha wala akanushe aliyoyasema kwani anajua afanyalo. Na kwa wale wanaouliza nini maana ya muhadhara ya kashfa huu ndio mfano wa wazi. 

Ibin Masoud Mohammed, 
S.L. Posta 65404, 
Dar es Salaam. 

1. Salaam Aleykum, 
Umati wa Islamu, 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI  

Waislamu hawatokubali kusingiziwa mambo 
Na Mwandishi wetu 

Serikali ya Sudan yadhamiria kuleta amani ya kudumu 
Na Mwandishi Wetu 

Mwalimu alaumiwa kuwashawishi watoto waingie ulokole 
Na Badru Kimwaga 

Wanawake Arusha watakiwa kutafuta elimu 
Na Habiba Swedi, Arusha 

Tamsa Tanga yapata viongozi wapya 
Na Masoud Mohamed 

Mjue Dr. Abuu Ameena Philips: Mwanaharakati aliyewasilimisha askari 3000 wa Amerika 

Duniani kwa ufupi 

Barua ya Ofisa Elimu ina agenda nyuma yake 
Na Mussa Ally Morogoro 

Nabii Isa Mwana wa Maryamu ni Yesu huyo huyo!! 

Kuanzishwa ‘Islamic Club’ ni ajenda ya siri inayoweza kuhatarisha amani Tanzania 

Agenda ya siri 
Na. Hassan Kimangale 

Hatua ya Rais kutengua uteuzi wa Parole ni ya kizalendo 
Na J. R. Msuya 

Serikali iwahurumie raia wake 
Na BADRU KIMWAGA  

Wanawake  Waislamu  Wilayani Masasi waanzisha Jumuiya 
Na Yousouf  S. Kayungilo, Masasi 

Kuhifadhika kwa mwanamke ni kuhifadhika kwa jamii 
Na Zuhra Tajiri 

Waislamu  wekezeni kwenye kheri -Mwinyi 
Na Mwandishi Wetu, Tanga 

Biashara ya ufuska yavamia Z’bar Polisi uchwara’ wanufaika 
Na Rajab Rajab 

Asimamishwa uongozi kwa kutoa fat’wa ya Hitma 
Na Nadhiru Ishengoma Wetu , Kahama 

Aqswa waazimia kufuata Qur’an na Sunna 
Na Mwandishi Wetu 

Mafunzo ya Quran  

Barua za wasomaji  

Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)  

Masomo  

Chakula na Lishe  
  

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita