AN-NUUR
Na.161 Rabiul Thani 1419, Agosti 7-13, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Kuhifadhika kwa mwanamke ni kuhifadhika kwa jamii

Na Zuhra Tajiri 

Mwanamke kama mama na mlezi wa jamii anahitaji sana kupewa heshima yake pamoja na hifadhi bora ili kuinusuru jamii kutokana na kuangamia. Hii, kama nitakavyoelezea, inatokana na ukweli kwamba kuhifadhika kwa mwanamke ndiko kuhifadhika kwa jamii na kufisidika kwa mwanamke ndiko kwa hakika kufisidika kwa jamii yote. 

Unaweza kuthibitisha kauli yangu hii ukitaka, kwa kuangalia kwa undani sana mchango wa mwanamke asiye na hifadhi katika maovu takribani yote ambayo yameenea katika jamii na kwamba laiti mwanamke huyu angehifadhika na walau kusema "hapana" basi hali isingalikuwa hivi ilivyo. 

Kufanikiwa kwa "starehe" zote zijulikanazo ni kwa mchango wa mwanamke huyu asiye na hifadhi. Kwa mfano hakuna pombe itakayonywewa katika baa na nyumba za "starehe" bila kuwa na mwanamke kama mshiriki na walevi wakaburudika, hakuna dansi au disko litakalochezwa na kufana bila kuwa na mwanamke kuwa mshiriki, tena wakati mwingine uambiwe "....vimwana wataingia bure", kuashiria tu kuwa mwanamke ni muhimu mno katika kufanikisha jambo hilo na kuwa hatakiwi kukosekana kabisa. 

Vikundi vya kupiga muziki navyo, tangu vile vya dansi hadi vya taarabu, bali na hata vile vya ngoma za kienyeji, mwanamke hatokosekana humo na mara nyingi yeye ndiye anakuwa muimbaji "anayekonga" roho za wasikilizaji au mnenguaji anayekamilisha "furaha" ya watazamaji. 

Wamiliki wa vilabu vya pombe nao kwa kuzingatia umuhimu wa mwanamke huyu ninayemzungumzia wana sifa zao katika kuajiri wahudumu wa vilabu vyao. Miongoni mwa sifa hizo ni kama vile; "awe mwanamke, umri usizidi miaka 25, mchangamfu, sura nzuri, mweupe au maji ya kunde n.k." na kamwe hutokuta anatafutwa mwenye sifa ya "mwenye mavazi ya stara". 

Nenda katika hoteli kubwa kubwa, zile ziitwazo za kitalii na uone maovu yafanyikayo humo, tembelea fukwe za bahari kandokando ya hoteli hizo na ikiwa utaweza kuondoa haya japo kidogo ushuhudie ufuska unaofanyika hadharani. Ni ukweli ulio wazi kuwa laiti mwanamke asingeshiriki katika mambo hayo basi mahoteli na fukwe hizo vingekosa kabisa watu wa kuzuru huko. 

Maovu mengine ambayo yanasababishwa na mwanamke huyu ni kama vile mauaji yatokeayo kwa watu kugombea mwanamke huyuhuyu ambaye kwa kutohifadhika kwake anahesabika kuwa ni mwanamke huru kwa kila mwanamume. 

Maovu ya kamari na wizi mbalimbali yanashamiri kwa kukithiri kwa matamanio ya kufanya "starehe", mwanamke akiwa ndiye mlengwa katika kutimiza "starehe" hizo. 

Mchango wa "changudoa" na jamii yake katika kuziandama na kuzivuruga ndoa halali pamoja na athari ya watoto waitwao wa mitaani ambao sehemu kubwa ni wale wasiotokana na ndoa ni zao pia la kutohifadhika kwa mwanamke. Bali pia nathubutu kusema kuwa kwa nini "wakimwi" wasiongezeke wakati hatua hazijachukuliwa za kumhifadhi mwanamke? 

Uislamu kama mfumo wa maisha uliotimilia una jawabu kwa tatizo hili kwa kumuwekea mwanamke hifadhi ya kuaminika. Kwanza unamfundisha mwanamke amjue Muumba wake (elimu) na ajijue yeye mwenyewe kuwa ni kiumbe wa Allah SWT anyaepaswa kuishi maisha yake yote kwa mujibu wa maelekezo ya Muumba wake huyo. 

Katika maelekezo hayo ameamriwa kuvaa mavazi ya stara, anakatazwa kulegeza sauti na kurembua macho itokeapo dharura ya kuongea na mwanamume asiye maharimu wake, anakatazwa pia kutoka nyumbani kwake bila dharura ya msingi na kwenda akibahashika ovyo majiani. Uislamu pia unamfundisha kusema "hapana" dhidi ya kauli yote au tendo lolote ovu, na si "hapana" isiyo na sababu bali "hapana" kwa ajili ya Allah SWT. Hifadhi nyingine kwa mwanamke na jamii nzima ni ile ya kuifanya ndoa kuwa ni jambo la sheria na la kiucha Mungu. Mtume amelisisitiza jambo la ndoa kwa kauli nyingi, hizi mbili zikiwa miongoni mwa hizo; (Ndoa ni katika mwenendo wangu basi atakaejitenga na mwenendo wangu huu si katika walio wangu), na nyingine ni ile isemayo kuwa; (Mwanamke huhifadhika kwa mambo mawili, kwanza mume na pili kaburi). 

Kwa umuhimu wa hilo ikawa Uislamu umetoa hata ruhusa kwa mwanamume kuoa mke zaidi ya mmoja hadi wanne ili kama kuna "surplus" ya wanawake wema katika mujtamaa wapate hifadhi zao katika ndoa-Alhamdulillaah. Lengo la yote haya ni ili jamii ipate kuhifadhika na fitna inayoweza kusababishwa na mwanamke kuwa "huria" kufanya chochote na vyovyote atakavyo. Mifano ya nchi chache tu inaweza kukupa mwanga wa hili ninalolizungumzia hasa zile nchi zinazofahamika kuwa ni nchi za Kiislamu ingawa nyingi ya hizo hazijasimamisha hasa utawala wa Kiislamu. Nchi kama vile Sudan na baadhi ya zile za mashariki ya kati (middle east) zinaweza kutumika kama mfano hasa unapolinganisha maovu na mema baina ya nchi hizo na zile za Ulaya magharibi au hata Tanzania ukitaka. Chukulia kwa mfano suala la ukimwi, watoto wa mitaani, maovu ya kamari na ufuska katika makasino pamoja na idadi ya makasino hayo halafu upate msaada wa kujua idadi ya mambo hayo katika nchi za Kiislamu nilizozitaja ukilinganisha na idadi yake katika nchi za Ulaya. Japo haiwezi kusemwa kuwa nchi za Kiislamu zimenusurika kabisa na maovu hayo lakini ni kwa desimali ndogo sana ikilinganishwa na zile za Wazungu "walioendelea na kustaarabika". Hii ni dalili ya wazi tu kuwa ikiwa mafundisho ya Uislamu yatafuatwa vilivyo mahali popote pale na hasa katika suala hili la kumhifadhi mwanamke basi watu wa mahali hapo watapata ahueni sana kutokana na mchafuko wa kijamii uliopo leo. 

Wanaharakati wa ukombozi wa mwanamke wasibahatishebahatishe tu, Uislamu unalo jawabu madhubuti na la kudumu. Kumpigania mwanamke kwa maana ya kuwa huria kuwa, na kufanya vyovyote bila mpaka ni kumvua stara yake na kuivua stara ya mwanamke ni kuivua stara ya jamii nzima. 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI  

Waislamu hawatokubali kusingiziwa mambo 
Na Mwandishi wetu 

Serikali ya Sudan yadhamiria kuleta amani ya kudumu 
Na Mwandishi Wetu 

Mwalimu alaumiwa kuwashawishi watoto waingie ulokole 
Na Badru Kimwaga 

Wanawake Arusha watakiwa kutafuta elimu 
Na Habiba Swedi, Arusha 

Tamsa Tanga yapata viongozi wapya 
Na Masoud Mohamed 

Mjue Dr. Abuu Ameena Philips: Mwanaharakati aliyewasilimisha askari 3000 wa Amerika 

Duniani kwa ufupi 

Barua ya Ofisa Elimu ina agenda nyuma yake 
Na Mussa Ally Morogoro 

Nabii Isa Mwana wa Maryamu ni Yesu huyo huyo!! 

Kuanzishwa ‘Islamic Club’ ni ajenda ya siri inayoweza kuhatarisha amani Tanzania 

Agenda ya siri 
Na. Hassan Kimangale 

Hatua ya Rais kutengua uteuzi wa Parole ni ya kizalendo 
Na J. R. Msuya 

Serikali iwahurumie raia wake 
Na BADRU KIMWAGA  

Wanawake  Waislamu  Wilayani Masasi waanzisha Jumuiya 
Na Yousouf  S. Kayungilo, Masasi 

Kuhifadhika kwa mwanamke ni kuhifadhika kwa jamii 
Na Zuhra Tajiri 

Waislamu  wekezeni kwenye kheri -Mwinyi 
Na Mwandishi Wetu, Tanga 

Biashara ya ufuska yavamia Z’bar Polisi uchwara’ wanufaika 
Na Rajab Rajab 

Asimamishwa uongozi kwa kutoa fat’wa ya Hitma 
Na Nadhiru Ishengoma Wetu , Kahama 

Aqswa waazimia kufuata Qur’an na Sunna 
Na Mwandishi Wetu 

Mafunzo ya Quran  

Barua za wasomaji  

Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)  

Masomo  

Chakula na Lishe  
  

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita