AN-NUUR
Na.161 Rabiul Thani 1419, Agosti 7-13, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Wakati Bunge likihitimisha shughuli zake; Othman Matata asema:   
  • Waislamu hawatokubali kusingiziwa mambo Hatua zichukuliwe, vinginevyo ‘Tunakwenda Mahakama ya Kimataifa’ 
  • Mhe. Maghimbi asema Ameir aadhibiwe kama Mrema 
Na Mwandishi Wetu 

Wakati Bunge la Bajeti likihitimisha shughuli zake; imeelezwa kwamba Waislamu hawatokubali kusingiziwa mambo ili kuhalalisha dhulma dhidi yao. 

Aidha imeelezwa kwamba habari zinazowahusu Waislamu zimekuwa zikipotoshwa na hata kuwasingizia mambo Waislamu ili kupata sababu ya kuwafanyia hujuma. 

Akiongea na gazeti hili jana Agosti 6; Mwanaharakati mashuhuri Ustadh Othman Matata amesema kwamba Waislamu wakiwa raia sawa na raia wengine katika nchi hii hawawezi kukaa kimya huku wakidhulumiwa, bali wataendelea kuvichagiza vyombo husika kama Bunge virekebishe hali hii na ikishindikana watalazimika kulichukua jambo hili katika vyombo vya Jumuiya ya Kimataifa. 

Akitoa mfano Ustadh Matata alisema kwamba suala la Mwembechai ambapo baadhi ya Waislamu waliuliwa na polisi haliwezi kuisha bila ya wahusika kufikishwa mahakamani. 

Aidha, alisema kwamba tukio la Mwembechai limekuwa ni sehemu tu ya vielelezo vya uonevu na uvunjaji wa Haki za binadamu inaofanywa nchini hapa dhidi ya Waislamu. 

Ustadh Matata ambaye ni mtaalam wa sheria amesema kwamba anashangazwa na hali iliyojitokeza Bungeni ambapo taarifa zisizo sahihi zilitolewa bila ya hatua zozote kuchukuliwa. Akifafanua alisema kwamba hivi karibuni. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Ali Ameir aliliambia Bunge kwamba mwanafunzi Chuki Athumani aliyepigwa risasi na polisi alikuwa na makaratasi ya uchochezi. 

Mbali ya mwanafunzi huyo kukanusha; Ustadh Matata amesema; kuwa kwamba mwanafunzi huyo hakufunguliwa kesi inayotaja kosa la kukutwa na makaratasi ya uchochezi ni ushahidi kwamba aliyoyasema Mhe. Waziri Ali Ameir si sahihi. Ustadhi ambaye wakati akiongea alikuwa na nakala za mashitaka (charge sheet) za watuhumiwa wote wa Mwembechai, alisema kitendo hiki ni cha dhulma. Alisema, Mhe. Ali Ameir kwa nafasi yake kama Waziri wa Serikali hakusema kweli Bungeni. Na ni dhulma kwa sababu amesema mambo yasiyo sahihi juu ya watu ambao hawana fursa ya kuingia Bungeni kukanusha hayo wanayosingiziwa. Kwamba kamsingizia kwa kujua kwamba hawezi kuingia Bungeni kujitetea. 

Lakini linaloshangaza; anasema Ustadh Matata ni jinsi suala hili lilivyopita Bungeni.Kwanza anasema Wabunge wangetakiwa wamhoji Mhe. Waziri, kipi kilitangulia. Kumpiga mtoto huyo risasi ndio akakutwa na makaratasi ya uchochezi au kakutwa kwanza na makaratasi hayo ndio akapigwa risasi. Na je hiyo ndiyo hukumu kwa mujibu wa sheria? 

Lingine ambalo amelitaja Ustadh Othman Matata kama mfano wa mambo yaliyoelezwaBungeni na si sahihi ni suala la kulindwa kwa msikiti wa Membechai na madai kwamba Mama Chuki amesema kwamba mwanawe hataki kurudi kusoma tena Alharamain. 

Kwa mujibu wa maelezo ya Ustadh Matata msikiti bado unalindwa na Mama Chuki amekanusha kutoa maelezo hayo. Ustadh Matata amesema kwamba anashangazwa na utendaji kazi wa Mhe. Waziri kwani hata katika suala la Parole alishindwa kuona kosa hata baada ya Rais kuingilia kati na kuzivunja "Parole" zake. 

Akihitimisha kutoa maoni yake Ustadh Matata ambaye alisema anafanya hivyo kama mwananchi na kwa kutumia haki yake ya kikatiba alisema dhulma haiwezi kuachwa iendelee. Kwahiyo akasisitiza kwamba waliohusika na mauaji pale Mwembechai wafikishwe Mahakamani. Na Tume iundwe kujua kwanini na nini chanzo cha dhulma wanayofanyiwa Waislamu; athari zake kwa Taifa letu sasa na baadae na namna ya kuliondoa tatizo hilo. 

Akiongea na mwandishi wa habari hizi kutokea Dodoma jana usiku, kiongozi wa upinzani bungeni Mhe. Fatma Maghimbi amesema kwamba kanuni za Bunge zinatoa adhabu kwa Mbunge kusimamishwa lau itagundulika kwamba kaongopa. Na kosa hilo huwa zito zaidi inapokuwa anayeongopa ni Waziri katika serikali, ambapo katika nchi zilizoendelea hulazimika kujiuzulu. 

Kwa mantiki hiyo, Mhe. Maghimbi amesema kwamba, kama alivyoadhibiwa Bw. Augustino Mrema, Mhe. Ali Ameir naye aadhibiwe kama ni kweli kaongopa. 

Kuacha kutolewa adhabu kwa Mhe. Ali Ameir , amesema Mhe. Fatma Maghimbi ni kujenga jamii ya ‘Animal farm’ ambapo baadhi ya watu huhesabiwa kuwa wa hadhi ya juu zaidi ya wengine. 

Wakati huo huo, Mama yake Chuki Athumani amedai kwamba kufuatia kauli ya Mhe. Waziri Ali Ameir Bungeni anaogopa kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani kufuatilia masuala ya mwanawe. Alisema siku polisi walipomfungua mwanae pingu na serikali kumfutia mashitaka walimwambia akiwa na tatizo lolote kuhusu mwanawe afike Wizarani au awaarifu kwa simu kwa namba ambayo alipewa. Lakini anasema toka itoke kauli inayodai kwamb mwanawe kakutwa na makaratasi ya uchochezi anaogopa kwenda. 

Juhudi za kumpata Mhe. Waziri Ali Ameir kuzungumzia suala hili hazikuweza kufanikiwa. Bw.. Mwakilembe ambaye alijitambulisha kama Msaidizi wa Mhe. Waziri aliliambia AN-NUUR kwa njia ya simu toka Dodoma kwamba Mhe. Waziri asingeweza kupatikana kutokana na shughuli alizokuwa nazo. 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI  

Waislamu hawatokubali kusingiziwa mambo 
Na Mwandishi wetu 

Serikali ya Sudan yadhamiria kuleta amani ya kudumu 
Na Mwandishi Wetu 

Mwalimu alaumiwa kuwashawishi watoto waingie ulokole 
Na Badru Kimwaga 

Wanawake Arusha watakiwa kutafuta elimu 
Na Habiba Swedi, Arusha 

Tamsa Tanga yapata viongozi wapya 
Na Masoud Mohamed 

Mjue Dr. Abuu Ameena Philips: Mwanaharakati aliyewasilimisha askari 3000 wa Amerika 

Duniani kwa ufupi 

Barua ya Ofisa Elimu ina agenda nyuma yake 
Na Mussa Ally Morogoro 

Nabii Isa Mwana wa Maryamu ni Yesu huyo huyo!! 

Kuanzishwa ‘Islamic Club’ ni ajenda ya siri inayoweza kuhatarisha amani Tanzania 

Agenda ya siri 
Na. Hassan Kimangale 

Hatua ya Rais kutengua uteuzi wa Parole ni ya kizalendo 
Na J. R. Msuya 

Serikali iwahurumie raia wake 
Na BADRU KIMWAGA  

Wanawake  Waislamu  Wilayani Masasi waanzisha Jumuiya 
Na Yousouf  S. Kayungilo, Masasi 

Kuhifadhika kwa mwanamke ni kuhifadhika kwa jamii 
Na Zuhra Tajiri 

Waislamu  wekezeni kwenye kheri -Mwinyi 
Na Mwandishi Wetu, Tanga 

Biashara ya ufuska yavamia Z’bar Polisi uchwara’ wanufaika 
Na Rajab Rajab 

Asimamishwa uongozi kwa kutoa fat’wa ya Hitma 
Na Nadhiru Ishengoma Wetu , Kahama 

Aqswa waazimia kufuata Qur’an na Sunna 
Na Mwandishi Wetu 

Mafunzo ya Quran  

Barua za wasomaji  

Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)  

Masomo  

Chakula na Lishe  
  

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita