AN-NUUR
Na.161 Rabiul Thani 1419, Agosti 7-13, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Kuanzishwa ‘Islamic Club’ ni ajenda ya siri inayoweza kuhatarisha amani Tanzania
  

Mada hii imetafsiriwa na Abu Halima Sachangwa kutoka katika gazeti la Sunday Observer la tarehe 5 Julai, 1998. Linalochapishwa Tanzania kila Jumapili. 

KATIKA Tanzania, watumishi wa serikali wa ngazi za juu za Rais, Waziri Mkuu huhesabika kikatiba kama ni walinzi wa sera za taifa katika maisha yao bila ya kujali kwamba bado wako kazini au wamestaafu. 

Hii ndio maana baada ya kustaafu, waheshimiwa hawa wa taifa hupewa huduma maalum kama vile ulinzi, makazi yanayotambulika kiserikali, usafiri wa kiserikali, na hata huduma ya kifedha ya kuwatosheleza wao na familia zao katika maisha yao yote. 

Moja kati ya sera kuu za kitaifa za Tanzania, tangu uhuru, ni ile inayohakikisha kwamba nchi inabakia kutokuwa ya kidini, ambayo kikatiba inalinda haki ya watu ya kuabudu na kuamini dini waipendayo. Ni msingi huu imara wa kijamii na kisiasa ulioiwezesha Tanzania kubakia "kisiwa cha Amani" ndani ya bara linalokabiliwa na misuguano na migongano ya hatari ya kila aina. 

Hata hivyo, ikichochewa na viongozi wenye ushabiki wa kidini, hasa tangu serikali ya awamu ya pili ilipoanza kuwa madarakani, Watanzania wamekuwa wakishuhudia nchi yao waipendayo ikitumbukizwa taratibu katika hali ambayo hatimaye itafikia katika migongano ya hatari ya kidini kama ile inayotokea huko Algeria, Afghanistan, Sudan na sehemu nyinginezo. Vurugu za kidini kama zilizotokea katika eneo la Mwembechai mjini Dar es Salaam miezi michache iliyopita ni moja tu ya mifano ya hali hizo zinazowezekana kutokea. 

Uchunguzi wa karibu unaotiwa vigezo na tukio la hivi karibuni la kuanzishwa kwa kikundi cha kidini kwa jina la "Dar es Salaam Islamic Club" (DIC) chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Pili, Rais Ali Hassan Mwinyi, umeonyesha ugunduzi unaoashiria hali ya uvunjwaji amani nchini. 

Kwa kutumia nafasi ya kuwepo kwa ushabiki wa kidini ndani ya uongozi wa serikali ya Tanzania, nchi za Kiislamu, zikiwa chini ya Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC ) zimekuwa zikitumia misaada kama chambo cha kuivuta Tanzania kuwa ndani ya wanachama wa OIC. Lengo hili lilitimia kwa uchache kabla serikali ya Awamu ya Pili haijaisha. Ingawaje Tanzania inadai ilishavunja lengo lile, inaaminika kuwa uongozi wa OIC bado unaihesabu Tanzania kama mwanachama wake kama ilivyokwisha kusainiwa na viongozi wa Tanzania wanaoaminika kuwa ni wa Awamu ya Pili. 

Walichokuwa wakishuhudia Watanzania wasiohusika - yaani wasio Waislamu - ni vita vya msalaba (crusades) vya kashfa, tangu mwanzo wa Serikali ya Awamu ya Pili, na kwa mujibu wa wachunguzi wa mambo vita hivyo vya mahubiri ya kashfa ni baadhi tu ya mbinu za OIC katika kuanzisha serikali kamili ya Kiislamu Tanzania. Chini ya stratejia hizi, baadhi ya vikundi vya kidini vilivyosajiliwa nchini, vinavyopewa fedha na vikundi wanachama vya OIC vya humu nchini, vimekuwa vikitekeleza matashi ya OIC nchini kwa misingi ya "Jihad"(vita vitakatifu). Haya yalipelekea kwenye migongano mibaya ya kidini kama ile ya misikiti ya "Kwa Mtoro" na "Mwembechai" mjini Dar es Salaam. 

Inajulikana kwamba katika Uislamu, kifo katika "Jihad" kinahesabika kama ni "tiketi ya moja kwa moja" ya peponi, na ndio kutokea upinzani mkubwa uliotolewa na Wahubiri wa Kashfa wa Kiislamu katika matukiombali mbali yaliyofikia kilele katika vurugu mbaya za msikiti wa Mwembechai. 

Kuanzishwa kwa "Dar es Salaam Islamic Club", kwa mujibu wa wachunguzi, ni kubadilisha gea kuelekea kwenye hatua ya juu zaidi ya kutekeleza stratejia za OIC ndani ya Tanzania. Inaaminika kwamba ofisi ya Dar es Salaam Islamic Club, ikiongozwa na Ali Hassan Mwinyi, itatumika kama makao makuu ya muda ya OIC hapa Tanzania. 

Ni jinsi gani jumuiya hii iliyoundwa kwa nia mbaya, ya Dar es Salaam Islamic Club, ilipitishwa kwa kupewa usajili, bado ni kitendawili kwa wachunguzi wa ndani na nje ya nchi. Lakini dodoso za kitendawili hiki zilikuwa ni rahisi kung’amuliwa hasa pale walioalikwa katika uzinduzi wa DIC walipojulikana. Hawa walikuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani (ambaye ndiye msajili wa vikundi), Bwana Ali Ameir; Makamu wa Rais, Dr. Omari Ali Juma, na waheshimiwa wengine wa Kiislamu kutoka serikalini, jeshini, sekta za umma na sekta binafsi.. 

Kinyume cha suala zima ni ukweli kwamba maandalizi ya sherehe za uzinduzi wa DIC yalifanyika katika wakati ambao kampeni kali zilikuwa zikifanywa na serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani na Chama Tawala - Chama Cha Mapinduzi kuyafungia baadhi ya makanisa, ikiwa ni pamoja na lile kanisa maarufu la Mchungaji Kakobe (Full Gospel Bible Ministry) lililopo Dar es Salaam likiwa na matawi katika mikoa mingi. 

"Hivi hii ndio njia nzuri ya kutekeleza uhuru wa dini na kudumisha amani na uimara katika nchi hii, uliokuwepo kwa muda mrefu?" Wachunguzi wa mambo wamekuwa wakiuliza. 

Kwa nini Ali Hassan Mwinyi, ambaye hadhi yake inalindwa na kuchangiwa na walipa kodi wa Tanzania wa imani tofauti, amechagua kufanya mambo yanayoonekana kuwa na madhara kwa nchi, bado ni kitendawili kwa Watanzania wengi na wageni pia. 

Akiongozwa na ushabiki wa kidini na huku akifanya mambo yake nyuma ya mgongo wa "uhuru wa kuabudu", Ali Hassan Mwinyi anaonekana na wachunguzi wa mambo kama mtu ambaye siku zote ameshindwa kuelewa ni kipi kinatangulia kati ya kufanya kazi kwa manufaa ya taifa na kuendekeza matashi ya Uarabu wa Kiislamu. Hili la Uarabu wa Kiislamu ndio lililomchukua zaidi, kwa mujibu wa wachunguzi wa mambo, ambalo linapelekea katika maangamizo ya taifa. 

Ajenda ya Siri 

Tangu mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambayo yaliung’oa utawala wa muda mrefu wa Kisultani kule Visiwani, mataifa ya Kiarabu hayajaisamehe Tanzania kwa kitendo hicho. 

Kidini, mataifa ya Kiarabu kwa ushabiki mkubwa yamekuwa yakiifanya Tanzania kama ndugu wa karibu, lakini tukirudi katika masuala ya kiuchumi na kisiasa, Tanzania inafanywa ni miongoni mwa maadui wa Uarabu, ya pili baada ya Israel. 

Yakiwa na shauku ya kurejesha matakwa yao ya kuikamata Tanzania kisiasa na kiuchumi mataifa ya Kiarabu yamekuwa yakitumia nafasi ya hali ya kutokuona mbali waliyonayo baadhi ya viongozi wa Tanzania ambayo inasababishwa na ushabiki wa kidini. 

Walipokwishagundua muda muafaka wa vitendo wakati wa serikali ya Awamu ya Pili, Waarabu hawajaacha kutumia uwezo wao wa kidiplomasia na kifedha kuhakikisha kwamba sio tu wanairudisha Zanzibar peke yake katika utawala wao kisiasa na kiuchumi, bali hatimaye waikamate Tanzania yote. 

Kihistoria, kwa zaidi ya karne sita Waarabu wamekuwa wakileta madhara nchini Tanzania, na kwa uhakika, katika Afrika yote ya Weusi, ambapo walijishughulisha na kukamata na kuuza watumwa na pembe za ndovu. Ukatili wao wa hali ya juu kwa wenyeji wa Kiafrika kwa kipindi chote hicho umo katika mamia ya vitabu vya historia ulimwenguni kote. 

Lugha ya Kiswahili iliibuka wakati wa kipindi cha biashara ya utumwa wakati watumwa waliokamatwa kutoka sehemu mbali mbali za nchi walipokusanywa pamoja katika kambi za watumwa katika mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi wakisubiri kuuzwa. Kama njia ya kujaribu kuwasiliana wao kwa wao, maneno ya Kiarabu, taratibu yalitengeneza njia ya mawasiliano ya kuelewana miongoni mwa watu waliitwa watu wa "Swahel" (yaani watu wa Pwani). Lugha hii ilipokuwa ndipo ikasambaa hadi vijijini ambako baadaye iliendelezwa na vikundi vya kidini kuenea katika nchi nzima. 

Majina kama "Kitwana" (yaani Mtumwa), "Mwinyi" (yaani Mswaga Watumwa)_ na "Mwinyimkuu" (yaani Mkuu wa Waswaga Watumwa) ni baadhi ya maneno yaliyobakia yaliyotokana na utumwa wa Waarabu katika Tanzania. Je, Watanzania wako tayari kufungua milango tena kwa utumwa-mamboleo unaotaka kuletwa kupitia ushabiki wa kidini? 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI  

Waislamu hawatokubali kusingiziwa mambo 
Na Mwandishi wetu 

Serikali ya Sudan yadhamiria kuleta amani ya kudumu 
Na Mwandishi Wetu 

Mwalimu alaumiwa kuwashawishi watoto waingie ulokole 
Na Badru Kimwaga 

Wanawake Arusha watakiwa kutafuta elimu 
Na Habiba Swedi, Arusha 

Tamsa Tanga yapata viongozi wapya 
Na Masoud Mohamed 

Mjue Dr. Abuu Ameena Philips: Mwanaharakati aliyewasilimisha askari 3000 wa Amerika 

Duniani kwa ufupi 

Barua ya Ofisa Elimu ina agenda nyuma yake 
Na Mussa Ally Morogoro 

Nabii Isa Mwana wa Maryamu ni Yesu huyo huyo!! 

Kuanzishwa ‘Islamic Club’ ni ajenda ya siri inayoweza kuhatarisha amani Tanzania 

Agenda ya siri 
Na. Hassan Kimangale 

Hatua ya Rais kutengua uteuzi wa Parole ni ya kizalendo 
Na J. R. Msuya 

Serikali iwahurumie raia wake 
Na BADRU KIMWAGA  

Wanawake  Waislamu  Wilayani Masasi waanzisha Jumuiya 
Na Yousouf  S. Kayungilo, Masasi 

Kuhifadhika kwa mwanamke ni kuhifadhika kwa jamii 
Na Zuhra Tajiri 

Waislamu  wekezeni kwenye kheri -Mwinyi 
Na Mwandishi Wetu, Tanga 

Biashara ya ufuska yavamia Z’bar Polisi uchwara’ wanufaika 
Na Rajab Rajab 

Asimamishwa uongozi kwa kutoa fat’wa ya Hitma 
Na Nadhiru Ishengoma Wetu , Kahama 

Aqswa waazimia kufuata Qur’an na Sunna 
Na Mwandishi Wetu 

Mafunzo ya Quran  

Barua za wasomaji  

Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)  

Masomo  

Chakula na Lishe  
  

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita