|
Na. 057 Jumatano Julai 19 - 25, 2000 |
|
|
|
|
|
Wazalendo wafaidi ardhi Zimbabwe HARARE, Zimbabwe MWISHONI mwa wiki iliyopita wazalendo wa Zimbabwe wasio na ardhi walianza kugawiwa ardhi chini ya usimamizi wa serikali. Akitangaza kuanza kwa zoezi hilo, Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo alisema kuwa idadi ya mashamba 160 yatagawanywa kwa wazalendo kuanzia Jumamosi ya tarehe kumi na tano ya mwezi huu. Aliyasema hayo katika mazishi ya mmoja wa askari wazalendo wa vita vya ukombozi, aliyezikwa Ijumaa iliyopita. Bwana Mugabe aliita siku hiyo ya ugawaji mashamba ni sikukuu," kesho ni kesho" aliongeza. Serikali imetwaa baadhi ya mashamba ya wazungu kwa lengo la kuwagawia wazawa wasio na ardhi kwa ajili ya mustakabali wa wazalendo. Mgogoro wa ardhi nchini humo uliibuka mnamo mwezi Februari mwaka huu pale askari wa zamani wa jeshi la ukombozi walipovamia mashamba ya wazungu. Wapiganaji hao walidai kuwa wanafanya hivyo kwa sababu lengo la ukombozi lilikuwa ni kupata ardhi yao iliyoporwa na wakoloni, lakini toka uhuru umepatikana lengo lililokuwa limekusudiwa halijafikiwa. Katika kuadhimisha miaka ishirini ya uhuru wa nchi hiyo April mwaka huu, Rais Mubage aliunga mkono msimamo huo wa maveterani hao kwa kusema kuwa hawawezi kuwakataza kupora mashamba kwa sababu kile walichokipigania miongo miwili iliyopita hakijapatikana. "Wakongwe wa vita vya ukombozi wananafasi muhimu katika maamuzi ya mustakabali wa nchi hii", alisema Rais huyo. Rais Mugabe vile vile alipotembelea Namibia mwezi Juni mwaka huu alizitaka nchi za Namibia na Afrika Kusini ziige mfano wa nchi yake kwa kuchukua mashamba ya wazungu na kuwagawia wazalendo wasio na ardhi. Hata hivyo, Namibia haikuafiki mpango huo moja kwa moja kwa kusema kuwa mazingira ya Zimbabwe ni tofauti na nchi hiyo kufanya zoezi hilo. Nchini Afrika Kusini maveterani walimwita Waziri wa Ardhi afafanue juu ya wao kupatiwa ardhi, ambapo serikali ilitoa taarifa kuwa ardhi ya kuwagawia wazalendo ipo na ekari kadhaa zimetengwa kwa ajili ya zoezi hilo. Huko Kenya, fikra hizo zilipigwa teke na Rais Daniel Arap Moi kwa kusema kuwa haafiki mpango huo wa kunyang'anya mashamba ya wazungu. Aliongeza kuwa cha muhimu ni wazalendo watafutiwe ajira na si kupora mashamba ya walowezi hao wa kikoloni. Nchi za magharibi zikiongozwa na Uingereza na Marekani hazikuunga mkono mpango huo wa kiongozi huyo wa Zimbabwe. Mara kadhaa nchi hizo zilitoa tishio kuwa endapo mgogoro huo hautatatuliwa kwa maelezo wanayotaka, basi wangesitisha mikopo na ruzuku kwa nchi hiyo. Hatimaye mapema Julai mwaka huu chama cha wakulima wa kizungu chini ya Rais Tim Henwood kilipeleka taarifa serikalini kuwa watatoa mashamba kadhaa ili yagawiwe kwa wazalendo wenye tatizo la ardhi. Zimbabwe ipo Afrika ya Kati, ilipata uhuru mnamo
mwaka 1980 toka kwa utawala wa kikoloni wa Kiingereza kwa kutumia njia
ya mtutu wa bunduki.
BEIJING, China RUSSIA na China zimelaani mpango wa Marekani wa kuwa na mfumo mmoja wa makombora ulimwenguni. Hayo yamo katika taarifa ya pamoja waliyoitoa Marais wa China na Russia hapo jana katika mkutano wa pamoja kufuatia kumalizika ziara ya Rais Vladimir Putin wa Russia. Viongozi hao wamesema, wanapinga na kulaani mpango huo wa Marekani ambao una lengo la kufaidisha taifa hilo la magharibi ili kuzipiku nchi nyingine kinyuklia. Marekani imezitolea mwito nchi hizo zijiunge katika mpango huo ili kujilinda na mataifa ambayo imedai kuwa hayaaminiki. Mataifa yaliyotajwa kuwa hayaaminiki ni Korea ya Kaskazini, Iran na Iraq. Bwana Putin alikuwa na ziara ya siku mbili nchini China, ambayo ilianza juzi, alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuendeleza uhusiano wa kibalozi na kuzidisha ushirikiano wa kibiashara na kiteknolojia. Maofisa wa pande hizo mbili walitia saini na kubadilishana makabrasha ya mikataba kadhaa ya ushirikiano ikiwemo ule wa mabenki na teknolojia ya nishati. China na Russia zimekuwa zikilaumiwa na nchi za Magharibi kwa ukiukwaji wa haki za binadamu. Madai hayo yamepingwa vikali na wakongwe hao wa Ukomonisti kuwa huko ni kuingilia masuala ya ndani ya nchi zao. Russia imeivamia Jamhuri ya Kiislamu ya Chechnya ili kuitawala kwa mabavu na China inalaumiwa kwa suala la Tibet na Taiwan. Bwana Putin leo anatarajia kuanza ziara nyingine huko Korea ya Kaskazini kabla ya kwenda Japan siku ya Ijumaa kuhudhuria mkutano wa mataifa nane yenye viwanda vingi ulimwenguni, yajulikanayo kama G8. Rais wa China Bwana Jiang Zemin na Putin kwa pamoja wametia saini na wameitaka Jumuiya ya kimataifa kupinga mpango huo wa Marekani.
MANILA, Philipines SERIKALI ya Philipines wiki hii imeendelea kubanwa na Waislamu ili watekeleze masharti kadhaa na kukamilisha haki zao. Wiki hii serikali hiyo imelipa dola milioni sitini na tano na imetakiwa kutekeleza masharti mengine ambayo imesema imeyapokea na inayafanyia kazi. Waislamu hao wakiongozwa na kikundi cha Abu-Sayaf wanadai haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kutekeleza sheria za Kiislamu kwa mujibu wa kitabu chao kikuu cha Qur'an. Rais wa Philipines Bwana Joseph Estrada alisema wiki hii kuwa anahofia kuchukua hatua yoyote kwani huenda athari kubwa inaweza kutokea kutokana kubanwa na Waislamu hao kimbinu na kiufundi.
KHARTOUM, Sudan SERIKALI ya Sudan inaandikisha kwa wingi zaidi askari wa kujitolea kuanzia wiki hii. Zoezi hilo linafuatia Eritrea kuwasaidia waasi wa SPLA waliofanya shambulio wiki hii mashariki mwa Sudan, alifafanua Gavana wa jimbo hilo Bwana Ibrahim Mohamed Hamid. Imeelezwa kuwa Eritrea imechukua hatua hiyo ya kuwasaidia waasi kwa sababu Sudan ilikuwa upande wa Ethiopia wakati wa vita vya hivi karibuni kati ya nchi hizo. Sudan imeamua kuongeza askari kujiunga na jeshi
ili kukabiliana na waasi wa SPLA ambao wamevunja mapatano ya kusimamisha
mapigano ya silaha.
DAMASCUS, Syria MSIMAMO dhidi ya udhalimu wa Israel uko pale pale hadi iachie ardhi za Syria, imeelezwa wiki hii. Akifafanua msimamo huo, Rais wa Syria Bwana Bashar el Asad amesema kuwa nchi yake ipo tayari kufanya mazungumzo ya amani na Israel. Aliongeza kuwa hali hiyo itafanyika endapo Israel itarudisha ardhi zote za Syria zilizoziteka na hasa milima ya Golan. Kiongozi huyo ambaye ataiongoza Syria kwa kipindi cha miaka saba ijayo amesisitiza kuwa "lazima Marekani itoe shinikizo kwa Israel iachie ardhi hizo". Israel iliiteka ardhi za Syria na nchi nyingine
za mashariki ya kati katika vita vya mwaka 1967.
|
YALIYOMO
Tahariri
Cheyo kuendeleza ‘mfumo Kristo’ Rushwa katika kura za maoni: 'CCM isitafute mchawi' CUF yakanusha propaganda za waraka Wanachama wa CUF kortini Kilwa KINYANG’ANYIRO CHA UBUNGE: CCM Temeke wamtaka Bazaar 'Wanafunzi Lindi wamshughulikia Mkuu wa Shule aliyewazuia kuswali' Milioni moja zachangwa kujenga madrasa USHAURI NASAHA
MAKALA
MAKALA
MIPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
MAKALA
Burudani/Muziki
LISHE
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza
hapa
Au
Andika barua kwa: nasaha1420@yahoo.com
|
|
|
|