|
Na. 057 Jumatano Julai 19 - 25, 2000 |
|
|
|
|
|
Kushindwa kujitegemea ni laana Na Mwinjilisti Kamara Kusupa NABII Yeremia anasema amelaaniwa mtu yule amtegemeaye binaadamu na hasa yule amfanyaye mwanadamu mwenzake kuwa ndio kinga yake maishani huku moyoni mwaka amemwacha Mungu. Tanzania ni taifa lililotangaza sera ya kujitegemea tangu 1967, naam, huo ulikuwa ni msimamo mwema na msimamo wa Kimungu kwasababu tangu awali Mungu hakumuumba mtu ili amtegemee mwingine na kumfanya binaadamu mwenzake awe ndiye mkirimaji mkuu na mwenye wajibu na maisha yake. Mungu kama Muumba na mzazi wa mataifa yote ya dunia hakupanga kwamba taifa moja litegemee taifa jingine. Pia Mungu hakupanga taifa moja lijifanye kuwa Mungu wa mataifa mengine hadi liabudiwe, na litumainiwe mia kwa mia kwa mambo yote yanayohusu maisha ya watu kitaifa. Kwa ajili hiyo, leo hii ukikuta taifa lisilojali heshima yake yaani lisilojali national sovereignity yake, na badala yake limejitoa mia kwa mia kama wakala, au kibaraka wa taifa jingine lenye nguvu kuliko hilo taifa tegemezi, basi jua wazi kwamba kinachofanyika hapo ni uzinzi, na uasherati mtupu sawa tu na ule wa Sodoma na Gomora na kwahiyo, taifa hilo tegemezi linaishi katika kilindi cha laana ya Mungu. Mara nyingi mataifa yenye uchumi dhaifu, na maendeleo duni, na yasiyo na nguvu za kijeshi ndiyo huanguka katika mtego huu wa kutegemea mataifa mengine. Aidha, viongozi wengine kwa hulka tu ya mapungufu mengi yaliyo katika mioyo yao, huamua kujisalimisha mbele ya madola yenye nguvu kwa matumaini ya kwamba wakipata upendeleo wa viongozi wenzao wa madola yenye nguvu basi kuna uwezekano wa kulindwa na kuhifadhiwa madarakani hata kama wananchi watakuwa hawautaki utawala wake. Kiongozi wa nchi asiyejiamini kwamba anapendwa na watu wake au haamini kwamba anakubaliwa na wananchi wake lakini wakati huo huo madaraka anayapenda huyo akijua kwamba kuna dola kubwa (Taifa kubwa) na yenye nguvu inaweza kumlinda na kudumisha utawala wake, basi ni lazima atajisalimisha kama mateka na kwahiyo kipindi chote cha utawala wake ataishi kwa kulinda nchini mwake maslahi ya dola nyingine yaani hiyo dola yenye nguvu na siyo kulinda maslahi ya hao watu wake anaowatawala. Mtawala wa jinsi hiyo ni lazima atawaona hao "superiors" wake, kuwa sawa na Mungu. Chochote watakachomwamuru kufanya atakifanya. Hata hivyo taifa lenye kiongozi wa namna hiyo lina hasara tupu kwasababu litaishi kwenye laana ya Mungu kwa wakati wote wa utawala wa huyo kiongozi bomu. Utegemezi ni maradhi, chanzo chake ni muhusika kukosa roho ya Mungu na kutokuendana katika maagizo ya Mungu. Vinginevyo mtu yeyote anayemcha Mungu kidhati, ni lazima awe anajiamini na hawezi kuwa mwoga wa jambo lolote hapa duniani. Hata pale anapokabiliwa na vitisho vinavyozidi ufahamu wake ama uwezo wake wa kufikiri na kuhimili, bado atamkimbilia Mungu awe jawabu lake badala ya kumkimbilia binaadamu mwenzake. Kwa kifupi tabia ya utegemezi inatokana na mtu kumwasi Mungu. Tanzania ni taifa lililotangaza sera nzuri ya kijitegemea lakini kinyume chake sasa limegeuka kuwa taifa tegemezi hata kwa mambo madogo ambayo yangeweza kufanywa na wataalamu wake, wasomi wake, na wananchi wake kulikoni? Je nini kilichoisibu nchi hii hata ishindwe kujitegemea? Kuna neno gani gumu la kuzuia Tanzania isijitegemee mia kwa mia badala yake ikawa kila mwaka asilimia themanini ya bajeti yake ni lazima ichangiwe au itoke kwa wafadhili? Je, ni kweli Tanzania hatuwezi kuishi pasipo kufadhiliwa? Ni wazi kwamba kuna ulegevu mahala fulani lakini watu wameshindwa kuunena wazi wazi ulegevu huo kwa hofu ya kueleweka vibaya. Sababu kubwa ya kuunyamazia ulegevu ni huo utamaduni wa miaka mingi wa kuogopa kuonekana kama mpinzani dhidi ya hao walioko madarakani. Kwa ajili hiyo mtu pekee anayeweza kuendesha upinzani wa kweli. Usiokuwa na chuki, hila, wala uwongo, yaani upinzani wa kuwaambia waziwazi watawala juu ya maovu yao ili wajirekebishe ni yule tu mwenye msukumo wa Mungu moyoni mwake. Kuua uhuru wa wana taaluma? Anayestahili kujibu shitaka la kwanini Tanzania kamataifa imeshindwa kujitegemea ni chama tawala cha CCM. Tanzania mbali na mali asili nyingine ni taifa ambalo lina rasilimali ya bongo za watu wake na maarifa ya wananchi wake. Humo humo ndani ya CCM kuna wasomi wa kutosha, kuna wataalamu wa kutosha, na kuna wenye uzoefu wa kutosha. Sasa swali linafuatia nini "role" ya Bachelors, Masters, na PhD zilizoko ndani ya CCM? Digrii za wasomi ndani ya CCM zimewekwa kando na kinachofanya kazi sasa ni ushabiki tu. Mtu msomi anapoingia CCMau anapopewa kazi chini ya utawala wa CCM hapewi uhuru wa kitaaluma hana uhuru wa kutumia taaluma yake vilivyo na huo ujuzi wake wa kazi. Badala ya kuyasoma matatizo ya jamii na kuyatolea ufumbuzi, anachokifanya msomi na mwana taaluma ni kuisoma akili ya mkubwa wake na kujua kile ambacho mkubwa anakitaka kisha msomi huyo anaishia kushauri au kufanya kama atakavyo bosi wake ili tu yeye msomi huyo mambo yake binafsi yafanikiwe. Wasomi ndani ya CCM wanatimiza ile methali ya mtimizie kafiri ili upate mradi wako. Hicho ndicho walichokosea viongozi wa CCMyaani wamezoea kusikia yale wanayotaka wao kusikia na kushauriwa sawa kabisa na matakwa yao na siyo kushauriwa sawa na inavyotakiwa. Msomi ambaye yuko radhi kuona mambo yanaharibika lakini hayuko tayari kuchukua msimamo wa kitaaluma kwa hofu tu kwamba asije kumuudhi bosi wake na mambo yakamharibikia yeye binafsi basi msomi huyo hana faida kwa jamii ni afadhali ya ng'ombe ambaye hakuwahi kwenda shule kuliko mwenye masters au PhD lakini hawezi kuchukua misimamo inayofanana na taaluma yake, na badala yake ati akaishi ndani ya hofu ya kwamba "usimuudhi mchinja mbwa kichaa kisije kikakurudia". Kwasababu ya dhambi hiyo ya wasomi kuweka kando taaluma zao ndiyo maana uchumi wa nchi umekufa mbele ya mabingwa wa uchumi, Elimu katika nchi hii nayo imekufa kifo cha mende mbele ya wenye Bachelors in Education, Masters, na PhD in education. Wenye taaluma ya elimu wamekuwa sawa na mtu anayeangalia jahazi linazama lakini hana uwezo wa kuliokoa. Mtandao wa afya nao umekufa mbele ya wataalam wa afya, mfumo wa tiba umekufa mbele ya mabingwa wa tiba. Siku hizi Hospializa rufaa kama Muhimbili si mahala pa kuponea tena bali pamegeuka mahala pakufia. Siku hizi maternity si mahala pa kuzalia wajawazito bali zimegeuka mahala pa vichanga kufia na wakati mwingine mahali bora pa biashara ya kununua watoto ama kubadilisha watoto na hasa watoto wa kiume. Kilimo nacho kimekufa mbele ya wataalamu na maafisa kilimo. Wakati wakulima wako vijijini, maafisa na wataalamu wa kilimo wako mijini tena maofisini. Kwamba wanafanya nini maofisini, hiyo ni siri yao. Lililo baya kupita yote ni kwamba wataalamu wa nchi hii na hasa wale walio karibu na utawala wameridhika kabisa na hali hii ya kuhuzunisha, hali ya laana kama ilivyo sasa kwa nchi hii. Vinginevyo kama wangekuwa wanakerwa na hali hii ya kuhuzunisha, wao wataalamu wa fani zote ndio wangekuwa mstari wa mbele kuupinga utawala uliotufikisha hapa tulipo. Lakini kimyume chake, wasomi wameridhika kupanda ndege kila mwaka kwenda Paris Club kuhudhuria vikao na wafadhili pasipo kujali kwamba katika uhalisi wa mambo wamejiweka kwenye nafasi ya Ombaomba na hawana tofauti na yule ombaomba anayepanda treni kutoka bara na kuja Dar es Salaam kunyoosha kopo lake ili asaidiwe. Kama iko tofauti basi itakuwa ni ile kwamba ombaomba anayekwenda Paris anapanda ndege na ana digrii kichwani na yule anayekuja Dares Salaam kutoka bara anapanda garimoshi, na hana digrii. Wapiga debe wanakazana kwamba utawala wa Mkapa umeiongezea Tanzania heshima mbele ya jumuiya ya kimataifa, hawa ni waongo wa kutupwa. Labda wana chuki zao dhidi ya utawala (uliopita) wa Rais Mwinyi na kwahiyo wanataka kuleta hoja zisizo na msingi wala zisizoweza kupimwa kwa kipimo chochote cha ndani ili tu watu waone kwamba na utawala wa Mkapa nao ni bora, kumbe uhalisi wa mambo ni kwmaba hakuna taifa lolote linaloweza kujiongezea heshima mbele ya jumuia ya kimataifa pasipo kujitegemea. Taifa omba omba haliwezi kuheshimika hata kidogo. Taifa lililobarikiwa kuwa na rasilimali lukuki lakini papo hapo likawa na ujinga wa kutokujua jinsi ya kutumia utajiri wake wa asili kwa manufaa ya wananchi wake haliwezi kujigamba kwamba linajiongezea heshima kama kuna watu wanaliheshimu taifa la aina hiyo watakuwa wanalivika kilemba cha ukoka. Wanalipa heshima ya kejeli tu kutokana na kujua kwamba taifa hilo limeshindwa kutumia rasilimali zake kwa aajili ya manufaa ya wananchi wake na kwahiyo hatua inayofuatia baada ya kushindwa huko ni wageni kuzivamia rasilimali hizo na kujinufaisha. Kwa sasa hivi wageni wajao Tanzania kuchuma wanayo haki ya kufurahi kwasababu wanapewa uhuru ambao hawawezi kuupata nchi nyingine yoyote ya dunia hii, hata nchi ile ambayo haina mwenyewe. Katika Tanzania mgeni yeyote ajaye kwa jina la mwekezaji, kwanza anayo nafasi kubwa ya kuonana na viongozi wa nchi hata kuliko wapiga kura. Mgeni ajaye Tanzania kamamwekezaji hata kama atakuwa Tapeli wa kutupwa atapokelewa, atapewa heshima zote za dola, na pia atapewa leseni na mahali pa kuendeshea shughuli zake kirahisi wakati mzawa anaweza kuyasotea hayo miaka na miaka bila kufanikiwa. Katika Tanzania mgeni anapata mikopo toka Benki kirahisi kuliko mwenye nchi. Katika Tanzania mgeni ajaye kwa jina la mwekezaji anapata likizo ya kodi wao wanaiita "tax holiday" ya miaka mitano. Hii maana yake ni kwamba mgeni anayo haki ya kufanya shughuli zake za kibiashara pasipo kulipa kodi wala kulipia ushuru vitu aviingizavyo kwa muda wa miaka mitano. Je, ni nchi gani nyingine ya dunia iliyowalegezea wageni kiasi hicho? Maana ieleweke wazi kwamba mgeni wa kuja hata angekuwa tajiri kiasi gani, haji ili kugawa utajiri wake isipokuwa kuchuma na kujiongezea katika hicho alicho nacho. Sasa mantiki ya misamaha ya kodi kwa wageni na mikopo ni nini? Wageni wanapokutana na ulaini wa namna hiyo ambao hata katika nchi zao hawaupati ndipo wanapovumisha sifa za bandia kwamba Tanzania inaheshimika sana kimataifa. Neno lililo wazi ni kwamba mambo yote haya yanafanyika chini ya msukumo wa rushwa na hiyo siyo rushwa ya wadogo ni rushwa ya watawala ndiyo inayotuponza. |
YALIYOMO
Tahariri
Cheyo kuendeleza ‘mfumo Kristo’ Rushwa katika kura za maoni: 'CCM isitafute mchawi' CUF yakanusha propaganda za waraka Wanachama wa CUF kortini Kilwa KINYANG’ANYIRO CHA UBUNGE: CCM Temeke wamtaka Bazaar 'Wanafunzi Lindi wamshughulikia Mkuu wa Shule aliyewazuia kuswali' Milioni moja zachangwa kujenga madrasa USHAURI NASAHA
MAKALA
MAKALA
MIPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
MAKALA
Burudani/Muziki
LISHE
|
|
|
|
|