|
MASHAIRI
Huyu ndiye afaaye
Kwa jina lake Muumba, naingia kwenye fani,
Jamali ametuomba, ushauri tumpeni,
Kuna Mkapa, Lipumba, kuraye ampe nani,
Kura mpe afaaye, kuongoza Tanzania.
Anza ubeti wa tatu, kwa makini kuchungua,
Zisome herufi tatu, za kwanza kutangulia,
Kwenda chini mara tatu, jinale utalijua,
Kura mpe afaaye, kuongoza Tanzania.
Lakini yaonekana, sifa zao wazijua,
Ila kusaidiana, yupi anayetufaa,
Pia ni muhimu sana, mmoja kumchagua,
Huyu mtu anafaa, Jamali tumchague.
La kwanza kuzingatia, mikutano hudhuria,
Inaweza saidia,wagombea kuwajua,
Pengine utaamua, yupi anayekufaa,
Huyu mtu anafaa, mimi ninavyomjua.
La pili kuzingatia, uwezowe mgombea,
Ili uchumi kukua, awe aliyebobea,
Punde itapowadia, siku ya kuwachagua,
Mchague huyu bwana, nchi ataikomboa.
Ungezingatia pia, ahadi walizotoa,
Mmoja alituambia, dhiki itatapakaa,
Bado hazijatimia, za mwingine alotoa,
Mchague huyu bwana, ni mkweli nakwambia.
Angalia za jamii, huduma zimepungua,
Yeyote bila bidii, hili ataligundua,
Elewa ndugu Jamali, watu sasa watambua,
Sina shaka ushajua, yupi wa kumpa kura.
Zuberi Dibwine,
S.L.P. 18112,
Dar es Salaam.
Lipumba sasa acheza
Nimemuona kwa macho, Lipumba sasa acheza,
Kwa yangu mawili macho, Lipumba ngoma acheza,
Sasa hana wasi nacho, KIDUMU afanya pweza,
Lipumba sasa acheza, ngoma kwenye mikutano.
Kazi keshaimaliza, Lipumba sasa acheza,
Angojea kuwaliza,KIDUMU wanaombeza,
Mpira keshatuliza, golini kaelekeza,
Lipumba sasa acheza,ngoma kwenye mikutano.
Sasa anasawazisha, hitilafu ndogo ndogo,
Kazikubwa imekwisha, kesha imaliza gogo,
Sasa meno aonesha, akili kejeli gogo,
Lipumba sasa acheza, ngoma kwenye mikutano.
Lipumba sasa atisha, KIDUMU wamuonapo,
PRESHA awapandisha, sasa wamekuwa popo,
Kwa watu furaha tosha, Lipumba wamuonapo,
Lipumba sasa acheza, ngoma kwenye mikutano.
Lipu letu tumaini, mwaka huu chaguzini,
Wote tumeshasaini, wacha awe na imani,
Asifurahi kwa nini, na sisi tuko nyumani,
Lipumba sasa acheza, ngoma kwenye mikutano.
Pale Kidongo Chekundu, jukwaani kachezea,
Kumbe Lipumba mtundu, asili kaizoea,
Lipumba sasa acheza, ngoma kwenye mikutano.
Lipu cheza lulu yetu, walausiwe na shaka,
Wewe ndo chagua letu, ngangari tunatamka,
Cheza cheza ngoma zetu, ya jadi kuyakumbuka,
Lipumba sasa acheza, ngoma kwenye mikutano.
Kwa heri baba Lipumba, Shemdoe nakuaga,
Nitashiriki kuimba, hata nawe kujimwaga,
Tuweze warimbarimba, KIDUMU waweze aga,
Lipumba sasa acheza, ngoma kwenye
mikutano.
Almasi H. Shemdoe,
“Tunda la Matumaini”,
Dar es Salaam.
Wito tujiandikisheni
Leo ni Jumamosi, saa tatu metimia,
Nilikaa nikahisi, nilonayo kuwambia,
Haki hii kwetu sisi, ni muhimu kutambua,
Shime tujiandikishe, wakati ukifikia.
Hii ndiyo haki yetu, ndugu zangu tambueni,
Tusije kuacha katu, nafasi kuja zihini,
Ni haki ya kila mtu, kila raia nchini,
Shimetujiandikishe, wakati ukifikia.
Kujiandikisha kwako, kutaleta manufaa,
Kwani hiyo haki yako,kuchagua anofaa,
Vita kutoka vicheko, pale atakapofaa,
Shime tujiandikishe, wakati ukifikia.
Sio kama nawatisha, tashindwa kuchagua,
Fujo msije kuzusha, ni vyema hilo kujua,
Kasheshe kujaizusha, si jambo jema tambua,
Shime tujiandikishe, wakati ukifikia.
Wale waliofikia, kumi na nane miaka,
Na wale walozidia,wasije wakajiweka,
Shime kwenda itikia,wakati utapofika,
Shimetujiandikishe, wakati ukifikia.
Mimi nina toa wito, kwa waliotimilia,
Msije kwenda watoto, au msio raia,
Tapata vitumbo joto, msije baki kulia,
Shime tujiandikishe, wakati ukifikia.
Msiogope vitisho,vyovyote mtavyopewa,
Wala msitoke jasho, kibanoni mkitiwa,
Ni lazima muwe macho, haki zenu kuchukuwa,
Shime tujiandikishe, wakati ukifikia.
Imefikasaa sita, nakimbiliajikoni,
Hapa ndio nina sita, naweka kalamu chini,
Bila ya kusitasita, tungo hizi zitoeni,
Wakati utapofika, shime tuandikisheni.
H.S.B. Ummul Jamilah,
Dares Salaam.
Hoja hupingwa kwa hoja
Imetangazwa nchini, kwamba hii mpya sana,
Kila mtu kibaini, mambo yaenda mrama,
Kusema ni ahueni,kuliko kuyafichama,
Hakuna atomkhini, uwe ukweli daima.
Wengine wakiuweka, ukweli uwe bayana,
Huonekana mashaka, pia hawana maana,
Hupingwa bila mpaka, hata kama wanonena,
Ni mambo yenye fanaka, na baraka za kufana.
Hoja zao ni nzito, zenye kupimika vyema,
Siyo hoja za kitoto,zilojaa lelemama,
Zina nikali mvuto, huwezi kuzisukuma,
Nyingi zinatoa wito, maisha ya hali njema.
Lakini wasema ovyo, haziwapi usalama,
Kila vile wakaavyo, hoja zawachomachoma,
Zawasuta kwa ambavyo, wanavyojali dhuluma,
Na ni hivyo watakavyo, kuzidi nasi kukoma.
Sasa wanaadhirika, bila hoja walalama,
Hawanapo pa kushika, hauwatui mtima,
Wamebaki kupayuka, hawajui wanosema,
Mizee inaumbuka, ulaji unawahama.
Wamekua kichekesho, pumzi wanazohema,
Mapafu yana miwasho, kwa haraka wanapuma,
Wanaona ndiyo mwisho, maisha yanayoyoma,
Kumbe kidogo mipasho, Roho juu mesimama.
Na linopasua mbavu, misuli ikiwatuna,
Hujitanua kwa nguvu, eti wataka kunena,
Huishia upumbavu,wajinga wana maana,
Tawashindaje werevu, wenye data kila kona.
Hawajui pinga hoja, kazi yao kutukana,
Wanavifanya viroja,vituko tunawaona,
Heshima zinawavuja, zawazengea laana,
Watakamambo kufuja, kwa sababu ziso kina.
Hawana pa kukamata, wameshashikwa na homa,
Sasa wanaenda tata, miguu inatetema,
Uzewe umewapata, hawawezi kujituma,
Lakini bado wateta, kuuleta uhasama.
Hoja hupingwa kwa hoja,si ovyo ovyo kusema,
Bure wanajikongoja, hawataki kuungama,
Wanafukuza wateja, soko lao wamegoma,
Wataruka wakitoja, wajishushia heshima.
Sihaba,
Safarini Pemba.
TOT karibuni CUF
Watani zangu sikia, yalotupata ni tabu,
Hotuba tulisikia, Radioni kihutubu,
Taarifa kutwambia, kafariki Mahabubu,
Mwenzetu ndugu yetu, Mwalimu Kei Nyerere.
Tangu tu ameondoka, hajapata kupumua,
Mwalimu katutoka, alikwenda tibiwa,
Na watu wataondoka, mwili hapa kuletewa,
Mwenzetu ndugu yetu, Mwalimu Kei Nyerere.
Akatangaza Rais, msiba mwezi mmoja,
Radio upepe upesi, nyimbo tu moja kwa moja,
Hata kwenye mabasi, muziki kuwa kiroja,
Mwenzetu Ndugu yetu, Mwalimu Kei Nyerere.
Kikundi cha kwanza TOTI, lete wimbo wa majonzi,
Wakaja wa Mlingoti, wakaimbaza kuenzi,
Pia wacheza ngongoti, kisha jeshi la ulinzi,
Mwenzetu ndugu yetu, Mwalimu Kei
Nyerere.
Mkasema mlosema, Mapunda mwenzio Komba,
Na watu walitetema, kwa jinsi mlivyoimba,
Walidhani lelemama, polisi itawakumba,
Ndugu yetu mwenzetu, Mwalimu Kei Nyerere.
Mlonena mdomoni, watutumeyasikia,
Mwasema mpo gizani, hamna pa kushikia,
Ushauri nao kwa nani, atakaye tusikia,
Ndugu yetu mwenzetu, Mwalimu Kei Nyerere.
Mengi mmelalama, ndiyo ukweli wa mambo,
Funga virago kuhama, funga kabati na vyombo,
Kumbuka alivyosema, BwanaMhashamu Pengo,
Ndugu yetu mwenzetu, Mwalimu Kei, Nyerere.
Kama mmeona giza, kuhama mwangoja nini?
Nyerere aliagiza, nurunjema upinzani,
CCM imeoza,watu wote wa zamani,
Nduguyetu mwenzetu, Mwalimu Kei Nyerere.
Tawi lengu lipo Mwenge, kadiufanye chagua,
Uje kafu tuijenge, kwa njia ya mtandao,
HAKI yetutuikinge, kwa mbwembwe na minenguo,
Ndugu yetu mwenzetu, Mwalimu Kei Nyerere.
Said M. Buweta (Fundi),
S.L.P. 33726/22010
Mwenge,
Dar es Salaam.
Mtoto hamjamjuwa? (Jibu)
Bismillah naanza, kwa jina lililo kuu,
Kula mchele na panza, ufurahi Kijukuu,
Nikupe jibulo kwanza, mimi sitaki makuu,
“Mtoto huyo NASAHA, mwaka mmoja tayari.”
Mwaka mmoja kafika, mtoto huyo NASAHA,
Anasema nakucheka, kwa mbwembwe naze furaha,
Huku akiruka ruka, Mbeya, Tanga na Kibaha,
Moto huyo NASAHA, mwaka mmoja tayari.
Na hucheka ki!ki! ki! ki! mara moja mebaini,
Katikati kila wiki, JUMATANO namba wani,
Halafu hadanganyiki, na si mwongo mdomoni,
Mtoto huyo NASAHA, mwaka mmoja tayari.
Si wa kiume wala kike, mtambueni malenga,
Mwana wa aina yake, wengine ni wa kuchonga,
Mia mbili ada yake, akili atakujenga,
Mtoto huyo NASAHA, mwaka mmoja tayari.
Shemdoe na Halima, Kijukuu anatamba,
Halafu atatusema,akirudi livu shamba,
Ndipo tutapochutama, kama tumemwona simba,
Mtoto huyo NASAHA, mwaka mmoja tayari.
Said M. Buweta (FUNDI),
S.L.P. 22010, 33726,
Mwenge, Dar es Salaam.
|
YALIYOMO
Tahariri
Tume, PCB na vyama vya siasa
mmekiona mliochoandaliwa Oktoba?
Cheyo
kuendeleza ‘mfumo Kristo’
Rushwa
katika kura za maoni: 'CCM isitafute mchawi'
CUF
yakanusha propaganda za waraka
Wanachama
wa CUF kortini Kilwa
Waumini
waapa kulinda Msikiti
KINYANG’ANYIRO
CHA UBUNGE: CCM Temeke wamtaka Bazaar
'Wanafunzi
Lindi wamshughulikia Mkuu wa Shule aliyewazuia kuswali'
Milioni
moja zachangwa kujenga madrasa
Hata
na mimi sijala
USHAURI NASAHA
Jinamizi
la ukewenza
MAKALA
Kushindwa
kujitegemea ni laana
MAKALA
UDP,
TLP wathibitisha hisia za Waislamu kuwa Uislamu ni kero Tanzania
MIPASHO NASAHA
Mwanasiasa
wa kisasa
Kalamu ya Mwandishi
Mamluki
wa mageuzi
MAKALA
Mrema
na Cheyo wajihadhari wasije wakatumiwa kuwavuruga wananchi
MAKALA
Viongozi
wa vyama vya siasa na udini nchini Tanzania
Mandela
ni mfano wa kuigwa
Burudani/Muziki
Cat
Stevens: Historia kwa Ufupi
Habari
za Kimataifa
LISHE
Yanayoweza
kumdhuru mtoto tumboni
MASHAIRI
MICHEZO
Jenerali Ulimwengu amgonga nyundo
Mkapa
Hassan Affif aitabiria Simba
Ubingwa
|