NASAHA
Na. 057 Jumatano  Julai 19 - 25, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
HABARI 

Wanachama wa CUF kortini Kilwa 

Na Mwandishi Wetu 

WANACHAMA watano wa Chama cha Wananchi (CUF) akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho wilayani Kilwa, Bw. Suleiman Bungara, wanashikiliwa na polisi baada ya kutokea mtafaruku baina ya wanachama hao wa CUF na wale wa Chama tawala CCM.

Akiongea na gazeti hili Naibu Mkurugenzi wa haki za binadmu wa CUF Bw. Ernest Lyanga amesema Mtafaruku huo uliopelekea wanachama hao kurushiana mawe uliotokea Julai 11, wakati wakitekeleza 'harambee' ya kufukia shimo lililopo karibu na eneo la soko la samaki wabichi Kilwa Kivinje iliyoitishwa na Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Wilfred Ligubi. 

Ameeleza kwamba wakati wa Harambee hiyo ikiendelea mnamo majira ya saa tano asubuhi kundi watu aliodai ni la wakereketwa wa CCM likiwa limevalia mashati ya kijani na suruali nyeusi lilianza kuimba nyimbo za kuisifu CCM, serikali na Rais Mkapa mbele ya Mkuu wa Wilaya. Hatua hiyo ilipelekea kuonekana kuwa shughuli yote ilikuwa ikitekelezwa na wanachama wa CCM. 

Kufuatia hatua hiyo ameeleza Bw. Lyanga wanachama wa CUF nao wakaanza kuimba nyimbo za kukisifu chama chao na viongozi wao ambao zilikuwa na vijembe dhidi ya CCM jambo ambalo haliwakupendeza wakereketwa wa CCM na hivyo wakaanza kurushiana mawe. 

Amesema wakati tukio hilo likiendelea Polisi walifika eneo hilo na kuwakamata baadhi ya wanachama wa CUF na viongozi wao waliokuwepo kwenye harambee hiyo. 

Kwa mujibu wa maelezo ya Bw. Lyanga Miongoni mwa waliokamatwa na polisi ambao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Julai 19, ni pamoja na Mohamed Said Salim ambaye ni Mkurugenzi Uenezi wa wilaya, Jaffar Arubaini Mwenyekiti wa serikali ya Kitongoji na Rehema Ndambachia. 

Bw. Ernest Lyanga amesema, inashangaza kuona wanachama wa chama chake wilayani Kilwa wamekamatwa na polisi na wale wa CCM wameachwa wakati wote walihusika kwenye tafrani hiyo ya kurushiana mawe ambayo ilisababishwa na wakereketwa na CCM. 

"Naelekea Kilwa na nitakutana na Mkuu wa Wilaya kwani yeye alikuwepo eneo la tukio na ndiye aliyewaita polisi...", alisema Bw. Lyanga. 

Jitihada za gazeti hili kumpata Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Lindi Bw. Peter Nyoosha kuzungumzia suala hili hazikuweza kufanikiwa baada ya kukosekana kwa mawasiliano ya simu. 
Juu


Waumini waapa kulinda Msikiti

Na Mwandishi Wetu 

WAUMINI wa Msikiti wa Tahiyyatul Temeke wameapa kuulinda Msikiti wao kwa nguvu zote.

Hali hiyo imetokana na dalili kwamba kuna uwezekano wa dola kuvamia Msikiti Ijumaa kufutia hatua ya BAKWATA kuutaka kwa nguvu. 

Hayo yamo katika barua ya BAKWATA wilaya ya Temeke ya kuutaka uongozi uliopo kuukabidhi kwa 'wenyewe' ambao ni waasisi ifikapo siku ya Ijumaa ya keshokutwa mwezi huu muda wa alasiri. 

Barua hiyo iliyosainiwa na Katibu wa Wilaya yenye kumbukumbu nambari BWT/SER/5/024/2000 imeviarifu vyombo vya dola viwepo siku hiyo kwa ajili ya usalama na ulinzi. 

"...Mtatakiwa kufanya hivyo siku ya Ijumaa Julai 21, 2000 alasiri msikitini mbele ya uongozi wa BAKWATA wilaya na kata 14 Temeke, na Afisa wa serikali wa Mtaa wa Yombo Kisiwani", imeeleza sehemu ya barua hiyo. 

Aidha, barua hiyo imemtaka Mkuu wa wilaya ya Temeke kutoa msaada wa ulinzi; "Tunaomba msaada wa usalama siku hiyo". 

Nakala ya barua hiyo imetumwa kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD) kwa ajili ya kupatiwa ulinzi: "Tunaomba ulinzi siku hiyo". 

BAKWATA imekuwa ikilaumiwa na Waislamu kuwa imekuwa ikianzisha fitna katika misikiti na hatimaye kuwachonganisha na serikali ambayo hutumia nguvu za dola na kusababisha adha kubwa kwa Waislamu ikiwemo kuwaweka jela Masheikh mara kwa mara na mauaji kama ya Mwembechai. 

Viongozi wa Msikiti huo waliopo madarakani ni Sheikh Rashid Chibwana Maulid, Sultan Ally Malenda, Hamis Muharami Ramadhan, Said H. Msumi na Juma Bakari Mchuchuli. 

Wakiongea na Mwandishi katika ofisi za NASAHA wamewataka Waislamu wajitokeze siku hiyo ili kuuhami Msikiti huo. 

"Tunatoa wito kwa Waislamu na jumuiya kuungana na waumini wenzao kuja kuuhami msikiti dhidi ya madhalimu siku hiyo", alisema mmoja wa viongozi hao. 

Msikiti wa Tahiyyatul uliopo Yombo Kisiwani, kwa mujibu wa barua ya Barazsa Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania (BARAZA KUU) haupo chini ya mamlaka ya BAKWATA. 

"Hivyo basi kuanzia tarehe hiyo (12/05/2000) Msikiti huu hauko tena kwenye mamlaka ya BAKWATA", imeeleza sehemu ya barua hiyo yenye nambari REF/BK/MOS/77/2000 kwenda kwa Katibu wa BAKWATA mkoa. 

Katika barua yake hiyo BARAZA KUUU lilieleza kuwa barua ya kusimamisha uongozi na kutaka ukabidhiwe kwa waasisi haina kazi tena. 

Nakala yake ilipelekwa kwa mkuu wa mkoa ikimuarifu kuwa "Tafadhali migogoro ya misikitini ziachieni jumuiya na taasisi za kidini zishughulikie zenyewe". 

Barua hiyo iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa BARAZA KUU, Sheikh Omar M. Samatta ilimuarifu pia kamanda wa polisi wilaya ya Temeke (OCD) Kwa taarifa: "Tafadhali migogoro ya misikiti ziachieni jumuiya na taasisi za kidini zishughulikie zenyewe". 

Juu


KINYANG'ANYIRO CHA UBUNGE
CCM Temeke wamtaka Bazaar 
  • Wasema hawataki watoa rushwa 
Na Mwandishi wetu 

WAKATI vugu vugu la kutoa fomu za uchaguzi ndio limeanza, wananchi kadhaa wamesikika wakielezea hisia zao kuhusu wagombea. Huko katika jimbo la Kawe, watu wamepokea kwa hisia tofauti kwamba Mbunge wao Adamjee anachukua fomu. Wananchi wa Kigamboni nao wanaongelea mno uamuzi wa mbunge wao, Kitwana Kondo, kuchukua fomu.

Kibao kinaelekea kuwa na dalili ya kugeuka katika jimbo la Temeke. Wananchi kadhaa walioongea na mwandishi wa habari hizi walikuwa na hisia za kutaka mabadiliko, wengi wao wakidai kwamba jimbo lao limekuwa na mkosi wa kupata watu ambao wamejaaliwa taaluma ya "kutelekeza" watu wao. 

Wananchi wengi walikuwa na hisia kwamba sasa hivi wanajaribu kuwatafuta watu ambao wana dalili za kujali wananchi, tena wawe ni wale ambao hawatakiletea chama chao, yaani CCM, kashfa ambazo zinavuma sasa hivi. Mwandishi aliwaomba baadhi yao wamwambie mfano wa watu ambao wanadhani huwasaidia watu kwa kiasi kikubwa, na hawataweza kutaka uongozi kwa rushwa. Jina la Farid Bazaar lilionekana kung'ara miongoni mwa watu walioulizwa. 

"Yeye ni mfanya biashara za halali na aliyetosheka. Hawezi kununua ubunge kwa rushwa, kwani tayari ana biashara zake zinazompatia kipato. Sio kama wengine wanatoa rushwa ili wapate nafasi ya kupata mapajero ya bure. Tunataka kumtumia ujumbe achukue fomu za kugombea ubunge kupitia chama chetu". Alisema Mzee mmoja aliyejitambulisha kama Mzee Mwakatobe. 

Pamoja na wasemaji wengine alikuwapo mwalimu mmoja wa shule ya msingi ya Temeke ambaye alieleza kwamba kutakiwa kwa Faridi kugombea ubunge kunatokana na moyo wake wa kujitolea katika huduma za jamii. "Kwa mfano pale kwenye shule yetu, ametupa misaada mingi sana, na ana uchungu mkubwa akiona vijana wanasoma katika mazingira magumu na yanayohatarisha maslahi yao na afya zao". Aliongeza mwalimu huyo, ambaye hakupenda jina lake litajwe. 

Juhudi za kumpata bwana Faridi ofisini na nyumbani kwake hazikuzaa matunda, lakini habari za watu walio karibu naye zinasema kwamba wananchi wengi wanamtaka agombee ubunge, lakini yeye anaonekana kutokulitilia ombi lao maanani. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Tume, PCB na vyama vya siasa mmekiona mliochoandaliwa Oktoba?

Cheyo kuendeleza  ‘mfumo Kristo’

Rushwa katika kura za maoni: 'CCM isitafute mchawi'

CUF yakanusha propaganda za waraka

Wanachama wa  CUF kortini  Kilwa

Waumini waapa kulinda Msikiti

KINYANG’ANYIRO CHA UBUNGE: CCM Temeke wamtaka Bazaar

'Wanafunzi Lindi wamshughulikia Mkuu wa Shule aliyewazuia kuswali'

Milioni moja zachangwa kujenga madrasa

Hata na mimi sijala

USHAURI NASAHA
Jinamizi la ukewenza

MAKALA
Kushindwa kujitegemea ni laana

MAKALA
UDP, TLP wathibitisha hisia za Waislamu kuwa Uislamu ni kero Tanzania

MIPASHO NASAHA
Mwanasiasa wa kisasa

Kalamu ya Mwandishi
Mamluki wa mageuzi

MAKALA
Mrema na Cheyo wajihadhari wasije wakatumiwa kuwavuruga wananchi

MAKALA
Viongozi wa vyama vya siasa na udini nchini Tanzania

Mandela ni mfano wa kuigwa

Burudani/Muziki
Cat Stevens: Historia kwa Ufupi

Habari za Kimataifa

LISHE
Yanayoweza kumdhuru mtoto tumboni

MASHAIRI

MICHEZO

  • Jenerali Ulimwengu amgonga nyundo Mkapa
  • Hassan Affif aitabiria Simba Ubingwa

  •  


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita