|
Na. 057 Jumatano Julai 19 - 25, 2000 |
|
|
|
|
|
Jinamizi la ukewenza Na Khadija M. Idd
KUNA kanuni inayoaminiwa na baadhi ya watu inayosema kwamba uongo ukirudiwa rudiwa mara nyingi huaminika na kuonekana kuwa ni ukweli. Na hii basi ndiyo kanuni inayotumiwa na wanapropaganda wengi, na miongoni mwa mambo yaliyofanyiwa hivi ni suala zima la ukewenza. Vyombo vya habari, pamoja na utamaduni wa Kimagharibi vinafanyakazi sana kueneza uongo na propaganda nyingi kuhusu ukewenza. Hadithi nyingi za watoto zimetungwa zikieleza ubaya wa ukewenza na ubaya wa mama wa kambo. Kutokana na hali hii mtoto anakua huku akijua kwamba ukewenza ni mbaya hivyo naye anaanza kuchukia mama wa kambo na ukewenza. Vyombo vya habari pia vimeeleza ubaya wa ukewenza hata kama ubaya huo ni wa mtu binafsi au ni tatizo la jamii nzima. Kwa mfano mwanamke ambaye ni mchoyo na uchoyo wake huu unamuathiri mtoto wa mke mwenzie. Hapa uchoyo ni tabia yake binafsi, ambaye hata mtu aliye peke yake katika ndoa anaweza kuwa nao. Lakini kwa maslahi ya kueneza uongo, vyombo vya habari vitahusisha tabia hii ya kutesa watoto wa mke mwenzake kama ubaya wa ukewenza. Vilevile jamii nzima ya Tanzania inasumbuliwa na umaskini ambao hutokana na mambo mengi, mojawapo likiwa ni mgawanyo mbovu wa huduma za jamii. Mgawanyo huu hufanya watu wa mijini hususan waliosoma na wanaofanya kazi wafaidike na huduma za elimu, matibabu, maji, umeme n.k. Huku kundi kubwa la wanajamii likiachwa maskini na lisilopata huduma hizo. Kwa maslahi yao basi, wanapropaganda hawa huweza kunega hoja kwamba familia zenye mlo zaidi ya mmoja eti zinashindwa kuwapatia watu wake mahitaji muhimu. Hivyo ili waweze kupata huduma hizo, wanajamii wanashauriwa kuwa na mke mmoja na watoto wachache. Lakini, wale ambao wana mke mmoja na pengine hata mtoto hawana na bado ni maskini wa kutupwa wanaambiwaje? Wafuate ushauri wa waziri mkuu wa kutooa au ule wa walokole wa Uganda wa kujitanguliza mbinguni kwa kupitia motoni? Wanapropaganda hawa hawauoni umaskini, ubinafsi, unyanyasaji unaosababishwa na mfumo mbovu bali huona umaskini na kukosa elimu ulioko katika nyumba zenye zaidi ya mke mmoja. Hawaoni chanzo cha umaskini huu bali huona matokeo yake na huyatumia kama kigezo. Kutokana na hali hii kila mtu katika jamii huona ukewenza kwa namna yake tofauti. Uoni huo basi hufanya wanawake wengi na wanaume wachukie mitala. Kwa mfanojamii sasa inauona ukewenza kama njia ya kumkomoa mke wa kwanza, wanamuona mke wa kwanza kama "amepatikana", na "bora akomeshwe" kwa maana"alizidi kujidai". Humuona kuwa mvivu, mbaya kwa sura na tabia, ameshindwa kazi n.k. Kwani kama isingekuwa hivyo mume wake asingeoa mwingine. Wako wanaoyasema haya waziwazi ili mke wa kwanza asikie, wako wanaofinyana macho na kuoneshana ishara. Lakini haya yote mwanamke huyu wa kwanza anayaona na kuyasikia na huweza kufanya jambo lolote kuonyesha hisia zakejuu ya haya yote. Hili linapotokea anaonekana mwenye wivu, anakuza mambo, mfa maji n.k. chuki yake juu ya mitala huongezeka. Mwanamke huyu wa kwanza pia anamuona mume kama ni wake peke yake na kila alichonacho ni vyao wawili na watoto wao. Atakayeolewa baadaye anaonekana kama kibaka,dhuluma na kila aina ya ubaya. Vilevile uzoefu wa maisha yake, kwa mfano iwapo ameishi katika familia yenye ukewenza ambayo haikuwa na hali iliyo shwari na labda ndoa haikudumu; humfanya achukie ukewenza, vyombo vya habari na mtazamo wa jamii kwa ujumla humfanya mama huyu auone ukewenza kama jahanam. Jamii pia humuona mwanamume aliyeoa kama aliyekuwa anateswa na kuzeeshwa na mke wa kwanza na sasa huona afadhali apumzike apate wa kufariji na kumfurahisha. Kwa wngine watamuona mwanamume huyu msaliti, asiye na shukrani, asiyekumbuka alikotoka n.k. Mke wa pili huonekana ni "super",ni mzuri wa kila kitu, husifiwa kwa kila alichonacho. Wako pia wanaofurahia ili amkomoe mke aliyetangulia,wako pia wanaomuona kama mchawi, muuaji wa mwanake mwenzie hana huruma n.k. Yeye mwenyewe hujiona mali mpya, chuma, bora, mzuri kwa sura na tabia na anayependwa na mumewe kuliko aliyetangulia, kwani kama huyo wa kwanza angelikuwa mzuri asingeliolewa yeye. Haya yote huchangia watu kuuchukia ukewenza. Ukiacha upande huu; kwa wanaume wanaooa, nao wana mchango wao ambao unasababisha wanawake kuchukia ukewenza. Wako wale ambao huoa si kwa vile Mwenyezi Mungu ameamrisha bali ili kumtia adabu mke wake kwanza ambaye labda ni mvivu, au hawezi kufanya kazi zake haraka. Wanaume hawa huwafanya wanawake kama zana ya kufanyia kazi au mtoto wa shule ambaye akikosea huti wa bakora. Bakora ya mke wake mume huyu ni kumuoolea mke wa pili. Ukiangalia kwa makini hapa utaona tayari kudonda na mume huyu anaongeza msumari wa moto. Jamii imeshaelezwa mengi juu ya ubaya wa ukewenza na anapoutumia ukewenza kama bakora, mambo huwa mabaya zaidi. Talaka inapotolewa, wanapropaganda hupata sababu ya "msingi"ya kuthibitisha kwa nini ukwewenza ni mbaya. Wako wanawake waliowahi kulalamika wengine kupitia vyombo vya habari kwamba mume ana kimada, amemjengea nyumba,ametoa "outing" n.k. Au wanaume kuonekana katika mazingira ya kutatanisha na saa za kutatanisha na kuwa pamoja na mwanamke ambaye baadaye huja kumuoa. Katika hali kama hii haitegemewi wanawake hawa kuishi kwa wema na kwa kupatana,labda mke mkubwa asijue yaliyotokea nyuma. Baadhi ya wanaume pia huwasimanga na kuwatukana au kuwapa maudhi na mateso wake zao huku wakiwapa kila huduma vimada au wachumba zao. Wanapokuwa wameshaoa, wanaume wengine pia huendeleza ubaguzi wa waziwazi kwa mke wake mkubwa na hata watoto. Na mke huyo anapolalamika ,anaambiwa kama huwezi fungasha uondoke, "kwani na wewe ni mwanamke?" Mwanamke huyu ashukuru tu iwapo haya yatasemwa na mumewe peke yake, lakini mara nyingi ndugu wa mume, majirani na wambea wanakuwa ndio wa kwanza kuyasema haya. Mwanamke huyu ataupendaje ukewenza? Na jewalendugu na majirani wanaoshuhudia haya wataupenda ukewenza? Wanaume wengi hujiuliza kwa nini wanawake wanachukia ukewenza, na wengine hujiuliza kwanini wanaume wengi hawaoi mke zaidi ya mmoja. Kabla hatujawalaumu kwa kuwaona wanaharamisha aliyohalalisha Mwenyezi Mungu, tujue vita inayoelekezwa katika jamii ya Kiislam, vita ambayo imeathiri sehemu kubwa ya jamii hata wenyewe kwa wenyewe tukawa ndio chachu ya kutodumu kwa ndoa za zaidi ya mke mmoja. Maneno na macho yetu yameathiriwa kwa kiasi kikubwa hata inafikia mahali tunatoa kauli ambazo zinaharibu familia, macho yetu yanasengenya na kumfunga kitanzi aliyeolewa na mume mwenye mke zaidi ya mmoja. Kwa kweli kilio na masikitiko ya wanawake walionyanya kutokana na ukewenza na propaganda za makafiri hazijaangukia patupu bali zimegusa akili za watu wengi. Pamoja na hayo hapo juu, wanaume katika jamii ya Kiislam, wanaojiandaa kuoa mke wa pili au zaidi waelewe kwamba wakati wa Mtume mambo yalikuwa rahisi kuliko sasa,wakati ule suala la ukewenza ilikuwa ni kupunguza kutoka wengi mpaka kubakiza wanne. Mazingira yale yalikuwa tayari ya ukewenza, kwa Waislam na wasio Waislam, sisi leo maadui wana sera tofauti na zetu, na hapo ndipo suala hili linapokuwa gumu. Hutumika kama kigezo cha kuuharibu Uislam na kwa sababu wanakuja na jicho la upole tunawasikiliza na pengine tunawaunga mkono bila kujua. Wanaume wawaelewe wanawake na waelewe kwa nini
wengi wanachukia ukewenza. Kwa ujumla kuna ulazima wa kufanya jihadi kuondoa
yale yaliyowekwa na makafiri nyoyoni mwa wake wa kwanza na wale wanaofuatia
hususan wale waliopitisha miaka mingi katika shule zenye mfumo wa kikafiri
kubariki chuki juu ya ukewenza haijatoka hewani wala nyoyoni mwa wanawake.
Haya yote yanayotendeka humfanya mwanamke anapoulizwa juu ya mumewe kutekeleza
jambo hili,aitike mara mbili kabla ya kuuliza kwa uchovu mwingi, kama mtu
aliyepandisha mlima mkali, "umesemaje" ili tu aonekane hajasikia. Kwa hakika
hilo ni jinamizi la ukewenza.
|
YALIYOMO
Tahariri
Cheyo kuendeleza ‘mfumo Kristo’ Rushwa katika kura za maoni: 'CCM isitafute mchawi' CUF yakanusha propaganda za waraka Wanachama wa CUF kortini Kilwa KINYANG’ANYIRO CHA UBUNGE: CCM Temeke wamtaka Bazaar 'Wanafunzi Lindi wamshughulikia Mkuu wa Shule aliyewazuia kuswali' Milioni moja zachangwa kujenga madrasa USHAURI NASAHA
MAKALA
MAKALA
MIPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
MAKALA
Burudani/Muziki
LISHE
|
|
|
|
|