|
Na. 057 Jumatano Julai 19 - 25, 2000 |
|
|
|
|
|
Cat Stevens: Historia kwa Ufupi Cat Stevens Avunja Ukimya Wake Utangulizi: Cat Stevens au Yusuf Islam alikuwa mmoja wa wasanii maarufu kabisa duniani katika miaka ya '70. Vibao kadhaa alivyotoa pamoja na maonyesho ya muziki aliyofanya wakati huo vilimfanya awe nyota. Pamoja na mafanikio aliyopata Yusuf Islam aliacha kupiga na kuimba muziki wa Pop mara aliposilimu mnamo mwaka 1977. Miongoni mwa vibao alivyopiga katika miaka ya umaarufu wake ni pamoja na "Tea For the Tillerman", "I Love My Dog" na "Matthew & Son". Hatimaye baada ya miaka ya ukimya Yusuf Islam amejitokeza na kuhojiwa na mwandishi Andrew Dansby mnamo mwezi Juni mwaka 2000. Makala hii, pamoja na kuchapisha mahojiana hayo, inazungumzia kwa ufupi maisha ya Yusuf Islam na mafanikio na matatizo aliyoyapata toka aingie Uislamu. Vilevile makala inataja nyimbo zake alizotoa baada ya kuacha muziki wa Pop ambazo ameziimba bila ya gita. Endelea Mwamko na ubadilishaji wa dini siyo jambo geni. Toka Martin Luther hadi Muhammad Ali, kwa njia moja au nyingine wamesaidia kuunda jamii yenye mchanganyiko wa watu wenye njia tofauti za maisha na kuvumiliana. Lakini ilishangaza sana mara mtunzi na muimbaji maarufu wa muziki wa Pop Cat Stevens alipoamua kuachana na maisha ya unyota wa muziki na kuwa Yusuf Islam, uamuzi wake huu ulipokelewa kwa kejeli na dharau karibu toka kila pembe ya Uingereza. Kwa zaidi ya miaka kumi sasa, jina la Yusuf Islam limekuwa likipakwa matope kwa "kuunga mkono" fatwa ya Ayatollah dhidi ya Salman Rushdie kwa kuandika kitabu cha Aya za Kishetani. Kama ilivyo ada, muda unapokwenda mbele hatimaye hupambanua juu ya ukweli wa mambo. Lakini ukorofi haukukosekana kwani kiasi cha wahuni 10,000 walilazimisha kuondolewa kwa wimbo wake wenye kuashiria amani "Peace Train" toka katika albam yake ya In My Tribe. Nyimbo zake zilipigwa marufuku katika Radio za Uingereza na imani yake ya dini kufanyiwa dhihaka. Katika wakati wote huo, Yusuf Islam alifanya kazi zake za kutoa misaada ya kibinadamu kimyakimya huko London. Akatoa albam kadhaa za nyimbo za dini ambazo zilipata mauzo mazuri kimataifa lakini zikapuuziwa katika Marekani. Hata hivyo hii ni karne mpya na Yusuf Islam amerudi katika ulingo wa habari. Kampuni maarufu ya kurekodi muziki ya universal ina mpango wa kutoa katalogi tofauti za muziki wake baadaye mwaka huu. Nayo VH1 ina mpango wa kutoa makala ya televisheni itakayoitwa "Behind the Music." Na ni hivi majuzi tu amekamilisha ziara yake nchini Marekani ambayo aliitumia kuongea na watu ili kuondoa uvumi na uzushi uliodumu kwa zaidi ya muongo mmoja. Mahojiano yake ni kama ifuatavyo: Dansby: Je ilikuwepo sababu maalum ya ziara yako nchini Marekani ambapo uliongea na watu mbalimbali? Yusuf: Sababu yangu ya kuzuru Marekani ni katika jitihada ya kuungana tena na mashabiki na wapenzi wangu, yaani wale ambao walidhani niliwapa mgongo na ambao walistahili kupata melezo. Kuna watu wengi ambao walitaka nitembelee jumuiya zao na nimefurahi kubadilishana nao mawazo na bila shaka nimependezwa na ukarimu wao mkubwa. Dansby: Kubadili kwako dini ni jambo la kawaida lakini baadhi ya watu waliamua kuukosoa sana uamuzi wako. Je unadhani ni kwanini ulikuwepo uelewa mdogo wa jambo hili? Yusuf: Wakati nilipoipokea na kuikubali dini ya Kiislamu watu wengi hawakuelewa. Kwa wapenzi wa muziki wangu ilionekana kwamba kuingia kwangu Uislamu ilikuwa ndiyo sababu hasa iliyopeleka mimi kuachana na shughuli za muziki hivyo watu wengi walikasirika. Na kama utasikiliza muziki wangu na maneno yake kama "Peace Train" na "On The Road to Find Out," inaonyesha wazi azma yangu ya kupata muelekeo wa njia sahihi ya maisha ya kiroho. Dansby: Suala la fatwa ya Rushdie limeonekana kuchukuliwa kwamba ni kweli ulitaka Rushdie auawe, licha ya kwamba hakuna mtu aliyeweza kutoa uthibitisho juu ya hilo. Je ni vipi uvumi huu ulianza? Yusuf: Nasikitika kwamba hili limetokea kuwa swali la kwanza ambalo watu wanataka nilijibu. Ukweli sihusiki na suala zaidi ya kile kilichozushwa na vyombo vya habari. Bila makosa yoyote niliingizwa katika lawama. Hivyo baada ya miaka mingi, nafurahi sana kwamba hatimaye nimepata fursa ya kuueleza umma na wapenzi wangu sehemu yangu ya suala hili kwa kutumia maneno yangu mwenyewe. Katika hotuba niliyotoa hapo kabla mnamo mwaka 1989 niliulizwa swali kuhusiana na kashfa kulingana na sharia ya Kiislamu nami nikakariri mtazamo wa kisheria juu ya suala hili. Licha ya elimu ndogo ya dini niliyokuwa nayo wakati huo, nilitoa msimamo unaotokana na tafsiri yenye ushahidi wa kihistoria katika Qur'an yenyewe. Siku iliyofuata vichwa vya habari vya magazeti vikasomeka, "Cat asema, muueni Rushdie." Nikachukiwa lakini ningefanyaje? Nilikuwa bado mgeni katika Uislamu. Kama utamuuliza mwanafunzi wa Biblia kunukuu adhabu ya kisheria toka katika Biblia dhidi ya mtu anayefanya kosa la kukufuru, basi hatakuwa mkweli iwapo hatanukuu Mambo ya Walawi 24:16. Dansby: Ukosoaji na lawama dhidi yako vilifanywa kwa nguvu sana. Albamu zilifungiwa na baadhi ya nyimbo kutolewa katika albamu. Yusuf: Kwa miaka kadhaa baada ya hapo, nimekuwa nikichukuliwa kama mtu anayeweza kuthubutu kutoa kauli hiyo na kufanya vitendo hivyo. Ukweli ni kwamba nimekuwa nikishikilia kwa nguvu msimamo wa kutetea haki za kibinadamu. Nimekuwa nikisimama kidete kuondoa ugomvi na vita pamoja na mambo yanayopelekea kuanza kwa hayo. Mtu anapaswa kutazama muziki na nyimbo zangu na shughuli zote za misaada ya kibinadamu ambazo nimekuwa nikizifanya tangu niache shughuli za muziki na hata kabla ya hapo. Nikikariri moja ya maneno ya nyimbo zangu, "kwa nini tuendeleze chuki? Kwanini tusiishi kwenye neema?" Lakini inaonekana baadhi baadhi ya watu walikuwa na lengo la kunichafulia jina, walijaribu kunitia mtegoni na kisha kunipaka matope kwa kuripoti yale niliyoyasema kinyume na makusudio yake halisi. Hili ni jambo lililoniuma sana. Ama juu ya kufungiwa muziki na rekodi zangu, inaonekana 'uhuru wa kutoa mawazo' kwa upande wangu haukuwa huru kama wa wengine- isipokuwa pale tu kile nilichokisema kilipopotoshwa kwa makusudi. Iwapo mtu yeyote angenifuata na kuniuliza kuhusu ukweli wa mambo--basi yote hay u mimi kwamba nilikuwa nikiishi Tehran na kuwa ombaomba mitaani hali ya kwamba sikupata kuondoka nyumbani kwangu Uingereza wakati huo, na mpaka leo hii sijapata kukanyaga Iran. Inaendelea toleo lijalo Nyongeza Cat Stevens alizaliwa Stephen Demetre Georgiou mnamo tarehe 21 Julai mwaka 1948 kwa baba mwenye asili ya Kigiriki na mama mzawa wa Sweden. Mwishoni mwa miaka ya 1960 alishatoa vibao kadhaa vya mtindo wa Pop nchini Uingereza ambazo zilimpa umaarufu mkubwa. Nyimbo kama "The First Cut is the Deepest" na "Tea for the Tillerman" zilitokea kupendwa sana. Mnamo mwaka 1977 Cat Steven aliamua kusilimu na kuwa Yusuf Islam. Inasimuliwa kwamba katikati ya miaka ya '70 Cat alisikia kwa mara ya kwanza kuhusu dini ya Kiislamu kwa kupitia kwa kaka yake aliyeitwa David Gordon ambaye alimpa nakala ya Qur'an Kitabu kitakatifu cha Waislamu. Cat mara moja akavutiwa na dini hii na hatimaye akaamua kuifuata. Baadaye akabadili jina na kuitwa Yusuf Islam. Aliamua kuacha muziki kwa sababu alihisi kwamba maisha ya nyota wa muziki wa Pop yasingekubaliana na maisha ya Muislamu wa kweli. Kwa kauli yake mwenyewe alisema: "Ulikuwa ni ukweli nilioupata toka katika sura inayoitwa 'Shu'ara' au 'Watunga Mashairi' iliyonifanya nijifanyie hesabu ya maisha yangu na hivyo kuamua kuacha shughuli za muziki niliposilimu yapata miaka 20 iliyopita. Mwisho wa sura hii Allah Mtukufu anasema:" Je nikuambieni ambao mashetani wanawateremkia? Wanateremka juu ya kila mzushi mkubwa, mwenye madhambi. Wanawapelekea (hao wanaowafuga) yale wanayoyasikia; (na wakaongezea yao ya uwongo mtupu). Na wengi katika hao ni waongo. Na watungaji mashairi (yasiyokuwa na faida) wanafuatwa na watu wapotofu. Je huoni kwamba wao (wanazuzuka) katika kila upande burebure. Na ya kwamba wao wanasema wasiyoyatenda? Ila wale (watunga mashairi) walioamini, na kufanya vitendo vizuri, na kumtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakalipiza kisasi baada ya kudhulumiwa. Na hivi karibuni wafanyao dhuluma watajua ni mgeuko (mpinduko) wa namna gani watakaogeukia. Qur'an Tukufu, Surah Shu'ara, aya 221-227 Tangu alipoacha muziki, Yusuf Islam ametoa albam kadhaa na baadhi yake akishirikiana na wasanii wengine. Mfano wa hizi ni The Life of the Last Prophet ambayo inasimulia maisha ya Mtume Muhammad (SAW) iliyotolewa mwaka 1995. Ndani ya albam hii kuna wimbo wa "Tala'a al-badr 'Alayna." Nyingine ni I have no Cannons That Roar ambayo ni mkusanyiko wa nyimbo za Bosnia. Yeye ameandika nyimbo mbili. Nyingine alizotoa ni "Prayers of The Last Prophet" au "Dua/Maombi ya Mtume wa Mwisho" na "A is for Allah" ambao ni maarufu katika mashule ya Kiislamu yenye kutumia lugha ya Kiingereza. Vilevile ameimba na kikundi cha Malaysia kiitwacho Raihan nyimbo za "God is Light" au "Mungu ni Nuru" na pia "Seal of the Prophets" au "Muhuri/Mwisho wa Manabii." Yusuf ameoa na ana watoto watano, mabinti wane na wa kiume mmoja (Muhammad). |
YALIYOMO
Tahariri
Cheyo kuendeleza ‘mfumo Kristo’ Rushwa katika kura za maoni: 'CCM isitafute mchawi' CUF yakanusha propaganda za waraka Wanachama wa CUF kortini Kilwa KINYANG’ANYIRO CHA UBUNGE: CCM Temeke wamtaka Bazaar 'Wanafunzi Lindi wamshughulikia Mkuu wa Shule aliyewazuia kuswali' Milioni moja zachangwa kujenga madrasa USHAURI NASAHA
MAKALA
MAKALA
MIPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
MAKALA
Burudani/Muziki
LISHE
|
|
|
|
|