|
Na. 057 Jumatano Julai 19 - 25, 2000 |
|
|
|
|
|
Mrema na Cheyo wajihadhari wasije wakatumiwa kuwavuruga wananchi GEORGE RAPHAEL UFORO HIVI karibuni mbunge wa Magu, naibu kiongozi
wa upinzani bungeni, na mwenyekiti wa chama cha UDP, mheshimiwa John Cheyo
ameelezea sababu za chama chake kujiengua katika ushirikiano na vyama vya
CUF na CHADEMA uliokuwa umelenga katika kumpata mgombea mmoja wa kiti cha
uraisi na kuachaniana majimbo katika kinyang'anyiro cha ubunge wakati wa
uchaguzi mkuu ujao. Kubwa katika sababu alizotoa mheshimiwa Cheyo ni tatu
nazo ni : moja , alichoashiria kuwa ni 'mwelekeo wa kiislamu wa chama cha
CUF'; mbili, alichokiita sera ya CUF ya 'jino kwa jino'; na tatu, ni tuhuma
kwamba chama cha CUF kinafanya hujuma kwa kuchukua wanachama wa UDP katika
kanda ya ziwa.
NI lazima nikiri kuwa nimeshtushwa sana na hoja hizi za mheshimiwa Cheyo kwa sababu siku zote nimekuwa nikiamini kwamba mheshimiwa Cheyo ni miongoni mwa watanzania wachache kabisa ambao wamekuwa makini katika kutambua na kuielezea hali halisi ya ya nchi yetu. Imani hii haikuzuka tu bali ni matokeo ya juhudi za mheshimiwa Cheyo tangu aingie bungeni katika kuibana serikali , si kwa kutumia ushabiki tu bali kwa hoja zinazoashiria kufanyiwa utafiti wa kutosha. Kutokana na imani yangu hii juu yake sikuamini kamwe kuwa itafikia siku mheshimiwa Cheyo akatujia na hoja ambazo siyo tu kwamba ni dhaifu, bali pia zimeonesha unafiki wa hali ya juu kabisa katika kuhalalisha maamuzi yake juu ya suala lolote lile. Hata hivyo naomba kabla ya kujadili hoja za Mheshimiwa Cheyo nitangulize kwanza ufafanuzi ufuatao ili mjadala wangu juu yake uwe wazi zaidi. Kuna sababu mbili ambazo kwa kawaida CCM na wapambe wake wamekuwa wakizitumia mara kwa mara kuonyesha kuwa CUF ni chama chenye udini wenye mlengo wa kiislamu. Sababu ya kwanza ni ile inayosema kwamba kwa kuwa viongozi wote wa juu wa CUF ni waislamu, basi hicho ni moja ya vielelezo kwamba chama hicho kina mwelekeo wa kiislamu. Hii ni hoja ya kipuuzi kweli kweli kwa maana -kama ambavyo waislamu wamekuwa wakihoji -udini unakuja kwenye chama cha siasa pale tu ambapo viongozi wa juu wa chama hicho ni waislamu na siyo vinginevyo? Waislamu wamekuwa wakiuliza kwa mantiki hiyo hiyo ni vipi mathalani CCM kisiitwe chama chenye mwelekeo wa kikristo ilhali nacho viongozi wake wote wa juu ni wakristo? Hivi karibuni mwenyekiti wa CHADEMA, mheshimiwa Bob Makani naye alihoji kwa mshangao undumilakuwili uliosheheni katika matumizi ya hoja hii pale alipohojiana na shirika la utangazaji la Uingereza, BBC. Sababu ya pili ni ile inayosema kuwa chama cha CUF kina udini kutokana na ukweli kwamba kinaungwa mkono na waislamu walio wengi. Sababu hii nayo inasambaratika inapoingizwa kwenye uchambuzi wa kina. Kwanza kabisa naamini hakuna mkristo yoyote anayeweza kujitokeza hadharani na kudai kuwa aliomba uanachama CUF akanyimwa kwa ajili ya dini yake, au alizuiwa kukishabikia chama hicho. Kutokana na sababu hii ndiyo maana CUF ina wanachama na wapenzi wengi tu ambao ni wakristo ( nikiwemo na mie pia ) tunaojiamini kuwa tuna uwezo wa kutosha kupima mambo na kujiamulia wenyewe hata kama ni kinyume na matakwa ya baadhi ya maaskofu na wachungaji wetu. Pili, waislamu kuiunga mkono CUF ni jambo ambalo linatarajiwa liwe wazi kwa yeyote yule mwenye akili hata ya wastani tu. Kumekuwa na tuhuma nyingi na hoja zilizo wazi toka kwa waislamu kwa muda mrefu sasa kuwa serikali ya CCM inawabagua. Serikali ya CCM haijawahi kuzifanyia kazi tuhuma na hoja hizi zaidi ya kujiuma uma midomo tu na kutoa vitisho. Hata pale waislamu walipofanikiwa kuwasilisha rasmi malalamiko yao kwa raisi Mkapa walipomwalika awe mgeni rasmi kwenye baraza lao la iddi miaka miwili iliyopita waliambulia kujibiwa kuwa malalamiko yao yatafanyiwa uchunguzi wa 'kisayansi' na majibu watapewa. Ni kweli majibu wamepewa lakini kutokana na mwelekeo wa majibu yaliyotolewa ni vigumu kuona kama sayansi yoyote ilitumika wakati wa kuchunguza malalamiko hayo. Katika vyama vya siasa nchini ni CUF ndiyo kimejitokeza hadharani kutangaza kuwa moja ya sera zake ni kuhakikisha kuwa HAKI SAWA KWA WOTE inapatikana nchini. Kwa mujibu wa CUF, hivi sasa haki sawa haipatikani kwa watanzania wote kwa sababu mbalimbali za kibaguzi kwa misingi ya kiuchumi, kidini, kijinsia, na pengine hata kikabila. Chama hiki kinasema kikishika uongozi wa nchi moja ya mambo kitakayoyasimamia kwa karibu kabisa itakuwa ni kuhakikisha kwamba haki inarejeshwa kwenye jamii kama njia pekee ya uhakika ya kudumisha amani na utulivu. Ni wazi basi kuwa mtanzania yoyote anayehisi hatendewi haki hivi sasa nchini mwetu na ambaye anajua fika kuwa utatuzi wa tatizo lake ni wa kisiasa, atavutiwa kwa kiasi kikubwa na chama hiki cha wananchi. Kwa mantiki hii sioni ni jinsi gani chama cha CUF kinaweza kikalaumiwa kwa kuwavutia waislamu kwa wingi ikizingatiwa kuwa kuwa siku zote jamii yao imekuwa na madai ya kutotendewa haki na serikali iliyoko madarakani na taasisi zake. Lakini pengine hoja kubwa na ya msingi kabisa inayoyapiga vita madai ya wale wanaoituhumu CUF kwa madai ya udini wenye mwelekeo wa kiislamu inajikita kwenye misingi ya kisheria. Sheria iliyorejesha siasa ya vyama vingi nchini haikuweka masharti kwamba ni lazima chama cha kisiasa kiwe na viongozi wa juu ambao ni wa mchanganyiko wa dini mbalimbali na wala kisiungwe mkono sana na watanzania wa dini fulani. Hii ina maana kwamba kukipa chama fulani sura ya udini kwa kutumia vigezo hivi viwili tu kwa mujibu wa sheria hii chama kinachohusika kina haki ya kufungua shauri la madai mahakamani kwa hoja ya kukashifiwa chenyewe binafsi, na pia kumkashifu msajili wa vyama kwa kuzembea kutimiza wajibu wake unaomtaka kukifutia usajili chama chochote ambacho kinaendeshwa kwa misingi ya udini. Mheshimiwa Cheyo ameituhumu CUF kwa udini wenye mwelekeo wa kiislamu kwa kuwa eti wagombea wote walioteuliwa na chama hicho kugombea nafasi za uraisi wa muungano na ule wa Zanzibar ni waislamu, na kwa sababu hiyo iwapo CUF itashinda basi viongozi wote wa serikali - kwa maana ya raisi wa jamhuri ya muungano, makamu wake, na raisi wa Zanzibar - wote watakuwa ni waislamu. Hii ni hoja ya kipuuzi kabisa kwa sababu wakati Cheyo na wenzake (Lipumba na Makani) wanatutangazia azma ya kuunganisha nguvu za vyama vyao kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao walituambia kwa pamoja kwamba njia watakayoitumia kumpata mgombea mmoja wa kiti cha uraisi ni kwa kila chama kumpata mgombea wake halafu kwa kutumia kigezo cha nani anakubalika zaidi kwa wananchi miongoni mwa hao wagombea waliopitishwa na vyama vyao, kamati ya pamoja ya vyama hivyo iliyopewa jukumu la kuratibu ushirikiano wao ingetangaza jina la huyo aliyefuzu. Hili la dini halikuwepo. Sasa kama halikuwepo, ghafla mheshimiwa Cheyo amelitoa wapi? Hivi mheshimiwa Cheyo anafahamu kuwa anachokisema kwa mujibu wa kanuni za kitakwimu ni sawa na kusema kuwa yeye hakubaliani asiliani na kuwepo kwa Raisi muisilamu ambaye anatokea Tanzania bara? Hii ni kutokana na ukweli kwamba uwezekano wa mgombea wa kiti cha uraisi wa Jamhuri ya Muungano anayetokea bara (bila kujali kuwa ni muislamu au ni mkristo) kumpata mgombea mwenza kutoka Zanzibar ambaye ni mkristo kitakwimu ni kama haupo. Vivo hivyo kwa mgombea uraisi wa serikali ya Zanzibar. Kujaribu kujenga hoja kwamba marehemu mwalimu Nyerere alipokuwa Rais alianzisha utamaduni wa kuhakikisha kuwa nafasi za juu kabisa za uongozi wa juu kabisa wa nchi zinashikwa na watu wa dini tofauti ni kumsingizia. Nyerere hata kama angetaka makamu wake wa kwanza awe mkristo, ingebidi ahakikishe kwanza kwamba Rais wa serikali ya mapinduzi Zanzibar ni mkristo kitu ambacho kwa kweli pamoja na umahiri wake wote kisiasa aliokuwa nao, kingemwia kigumu kwelikweli. Nina imani kabisa kuwa mheshimiwa Cheyo ana akili za kutosha kabisa kufahamu kuwa hoja aliyoleta siyo tu kwamba haina msingi, bali pia ni tangazo lisilo rasmi kuwa waislamu wa bara walio wanachama wa UDP ni wasindikizaji tu. Sasa kama mheshimiwa Cheyo anayafahamu yote haya ni nini basi kilimpelekea mwanzoni kukiingiza chama chake kwenye ushirikiano na vyama vya CUF na CHADEMA? Nina mashaka makubwa iwapo sababu iliyomplekea Cheyo kujaribu kushirikiana na wakina Lipumba na Makani kumpata mgombea mmoja wa kiti cha urais miongmwao ina uhusiano wowote na suala la nani miongoni mwao anakubalika zaidi kwa wananchi. Nadhani hili liko wazi na halihitaji mjadala mrefu. Ni wazi kabisa kuwa kwa kutumia kigezo cha kukubalika zaidi kwa wananchi hakuna shaka yoyote ile kuwa Lipumba ndiye anayekubalika zaidi. Siyo tu kwamba ni kijana zaidi na msomi zaidi, lakini pia kama mwanasiasa ameonyesha juhudi zaidi. Lipumba baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 alifukuzwa kazi yake ya uhadhiri katika chuo kikuu cha Dar es salaam akalazimika kwenda nchini Finland ambako aliingia mkataba na taasisi ya World Institute for Development Economics Research kuanzia 1996 hadi 1998 kama mtafiti mwandamizi. Baada ya kurejea nchini mwanzoni mwa mwaka 1999 hakudai chama chake kimpatie ofisi yenye kiyoyozi, gari zuri au marupurupu ndio aingie kazini kuchangia juhudi za kukiimarisha, bali ilhali hana wadhifa wowote kichama alianzisha harakati za nguvu kukipeleka chama kwa wananchi tena katika mazingira magumu sana ya ukata. Sitakuwa natia chumvi nikisema kuwa Lipumba kwa muda huo mfupi amefanikiwa kuifanya CUF iwe kweli ni Chama Cha Wananchi kama jina lake lilivyo. Wakati Lipumba yuko kwa wananchi akichakarika kutafuta kuungwa mkono mheshimiwa Cheyo naye alikuwa akichakarikia kama siyo bungeni, basi kwenye ukumbi wa habari MAELEZO. Pamoja na kwamba ni mambo mazuri mengi ambayo mheshimiwa Cheyo ameyaongea katika hadhara hizo, lakini alipaswa afahamu kuwa ni watu wachache tu ambao angeweza akawafikia kwa njia hiyo ya mawasiliano, na kwa hivyo kuelewa uzuri wa yale aliyoyasema. Mheshimiwa Cheyo pia alipaswa kutambua kuwa kukubalika kwa mwanasiasa yoyote ni jumlisho la mambo mengi na huenda dogo kabisa kati ya mambo hayo ni lile la kusikika redioni mara kwa mara, kuonekana kwenye TV, na kuandikwa na magazeti. Ni wazi kabisa kuwa hili lingekuwa na uzito wowote wa haja basi Rais Mkapa angekuwa ndiyo kipenzi cha watu ( anatajwa na kuandikwa na magazeti kuliko mwanasiasa mwingine yoyote hivi sasa) na Lipumba thamani yake mbele ya wananchi ingekuwa ni ndogo sana kuliko wanasiasa wote wanaowania uraisi hivi sasa ( ni nadra sana kusikia akitajwa kwenye radio na TV na ni nadra zaidi kusoma habari zake kwenye magazeti ukiondoa AN NUUR na NASAHA). Lakini kwa sababu kukubalika kisiasa kunachangiwa sana na jinsi mwanasiasa mhusika anavyojishughulisha na kuonana na watu, kuzungumzia matatizo yao, na kuwafundisha ufumbuzi haishangazi hata kidogo kuwa pamoja na vyombo vya habari kufanya mgomo usio rasmi wa kutoandika au kutangaza habari zake, Lipumba leo hii ndiyo kizingiti kikubwa kwa Mkapa kurejea kwenye uraisi baada ya uchaguzi mkuu ujao. Nadhani mheshimiwa Cheyo alijiunga na Lipumba na Makani akijua fika kuwa kwa kutumia kigezo cha kukubalika zaidi kwa wananchi asingekuwa na nafasi ya kuteuliwa. Pamoja na kulijua hili nadhani vilevile alijua fika kwamba hiki ndio kigezo pekee ambacho kisiasa kilikuwa kinaelezeka mbele za watu. Hata hivyo alijua ni wazi wananchi watataka kujua sababu za yeye kujiengua kwenye ushirikiano na akaona kuwa ni jambo rahisi kuurejea wimbo ule ule ambao watanzania tumeshausikia sana na umetukifu: CUF ina udini! Lakini pia inawezekana mheshimiwa Cheyo amejiengua kushirikiana na wenzake kutokana na shinikizo la viongozi wa dhehebu lake. Siyo siri kwamba viongozi wa dhehebu lake kutokana na uhusiano wa karibu ulioko kati ya dhehebu hilo na serikali ya CCM - hasa pale inapoongozwa na mkristo - wangependa sana Rais Mkapa ashinde uchaguzi mkuu ujao na kuendelea na kipindi kingine cha uongozi. Lakini pia viongozi hao wanajua kuwa hivi sasa watanzania wengi wameuchoka utawala wa CCM na wangependa kuona upinzani wenye nguvu ili waweze kuelekezea kura zao huko. Ni dhahiri ushirikiano wa Cheyo, Lipumba na Makani ulikuwa unatoa sura yenye upinzani wa aina hiyo. Kuwepo kwa upinzani huu bila shaka yoyote kungeiweka CCM mahala pagumu sana ifikapo Oktoba mwaka huu na hivyo kuhatarisha uwezekano wa Mkapa kuchaguliwa tena. Dawa ni nini? Kujaribu kuusambaratisha. Isingekuwa ni kazi kubwa kwa sababu kwa utamaduni wa dhehebu hili muumuni yeyote - bila kujali kuwa ana wadhifa gani katika jamii - hana budi kutii maagizo ya viongozi wake wa dhehebu. Mheshimiwa Cheyo asingeweza kuthubutu kukhalifu maagizo ya viongozi wake wa kiroho hata kama moyoni hakuridhika. Kwa mtizamo huu siyo tu kwamba imembidi muheshimiwa Cheyo awe kafara ili Mkapa ajiongezee uwezekano wa kurudi madarakani, lakini pia imempasa kukubali kubeba sifa ya unafiki, na huenda pia kukisambaratisha chama chake. Ama kuhusu sifa ya unafiki, hii sasa itakuwa inamwandama Mheshimiwa Cheyo kila atakapotia mguu wake. Bila shaka wananchi watakuwa wanajiuliza kila wamwonapo: Je, siye huyu huyu ambaye kwa kipindi cha miaka mitano sasa amekuwa na uswahiba mkubwa na CUF uliopelekea wakaunda serikali ya pamoja ya upinzani ndani ya bunge? Ni kwa nini kwake yeye udini wa CUF udhihiri sasa na siyo kabla ilhali siku zote huu ndio umekuwa wimbo wa CCM? Hoja nyingine alizokuja nazo mheshimiwa Cheyo juu ya kukiondoa chama chake kwenye ushirikiano na vyama vya CUF na CHADEMA, ni kuwa CUF inahatarisha usalama wa nchi kwa 'sera' yake ya jino kwa jino na kukihujumu chama chake. Kwanza kabisa sikubaliani naye kuwa CUF ina sera inayoitwa ya jino kwa jino. Ninachokijua mimi ni kwamba CUF imesema itauendea uchaguzi mkuu ujao ikiwa na msimamo wa jino kwa jino. Naamini kuna tofauti kubwa kati ya maana za maneno 'msimamo' na 'sera'.CCM na wapambe wake wanapotumia neno 'sera' mahala ambapo neno halisi lililokusudiwa ni 'msimamo' wakati wakiielezea CUF, hili linaeleweka. Hawa ni mahasimu wao wakubwa na hivyo kuwapindulia maneno ni jambo linalotarajiwa. Lakini UDP, TLP, NCCR, n.k., wanapoiangalia CUF kwa mtizamo wa CCM inatutia sana mashaka. Pili, sikubaliani na tafsiri ya mheshimiwa Cheyo kwamba kuwa na msimamo wa jino kwa jino ni kuhatarisha amani. Nadhani maana halisi ya kile kilichokusudiwa inaeleweka na kuikwepa ni kuleta upotoshaji wa makusudi. Upotoshaji huu wameuanza CCM na hii inaeleweka. Wao ndio waathirika iwapo CUF itaweza kweli kusimama kidete wakati wa uchaguzi mkuu na kuhakikisha kuwa vitendo vya wizi wa kura havifanyiki. Ni vipi basi UDP, TLP, NCCR, n.k., wawekewe maneno mdomoni na CCM na wao wayaimbe kama makasuku ? Mheshimiwa Cheyo na wenzake wangekuwa kweli wanapenda amani na utulivu bila shaka yoyote wangeuunga mkono kwa nguvu zao zote msimamo huu wa CUF. Toto onevu mtaani lenye tabia ya kuwapiga piga wenzake makonzi haliachi tabia hiyo mpaka pale watoto wote wanaoonewa wanapoamua kulifungia kazi. Si dhani kwamba iwapo siku ya uchaguzmaafisa wa tume ya uchaguzi, poilisi, mashushushu, na makada wa CCM hawatacheza rafu ili mgombea wa CCM, yeyote yule awaye ashinde wakati wananchi hawamtaki, kutakuwa na tatizo lolote. Lakini kuwaachia watu hawa wakiuke taratibu za uchaguzi kwa makusudi kabisa kwa sababu tu mkiwazuia kutakuwa na vurugu ni upumbavu ambao unaelekea kwenye uhayawani. Ni uendawazimu mtupu kuacha kuilinda kura yako, halafu kesho na kesho kutwa uwe mstari wa mbele kulalamika jinsi huduma za jamii zilivyo mbovu, jinsi rushwa ilivyo kithiri, jinsi wizi wa fedha za walipa kodi ulivyomkubwa serikalini nakadhalika. Hata hivyo wakati mheshimiwa Cheyo anaingia kwenye ushirikiano na CUF na CHADEMA, CUF ilikuwa zamani ishatangaza msimamo wake wa jino kwa jino kuhusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Ni unafiki mkubwa kwa Cheyo leo hii kututangazia kwamba amejiondoa kwenye ushirikiano kwa sababu ya msimamo huo. Ama kuhusu CUF kukihujumu chama chake, hapo napo kumejaa walakini. Bila shaka yoyote tungesikitika sana na mheshimiwa Cheyo iwapo angesema kwamba CUF mathalani inawahonga wanachama wa chama chake ili wakihame. Lakini kumbe ilichofanya CUF ni kufanya mikutano ya hadhara huko alikokuita ni ngome za UDP? Je, mheshimiwa Cheyo anaweza kuja na ushahidi wowote unaothibitisha kuwa kwenye mikutano hiyo waliisema vibaya UDP na yeye mwenyewe? Ni dhahiri kabisa kuwa ushahidi huo hana la sivyo angeutumia kukazia kesi yake alipoongea na vyombo vya habari. Tofauti na Cheyo, Mrema yeye tangu kipenga kinapulizwa alisema kuwa hana haja na kushirikiana na mtu na kuwa iwapo kuna mwenye haja ya kushirikiana naye, basi amfuate yeye kwa kuwa yeye ndiye mwenye mtaji mkubwa. Alisema vigezo vya kuthibitisha kwamba yeye ndiye mwenye mtaji mkubwa ni kura alizopata kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 pamoja na chama chake cha TLP kushika ushindi wa pili (?) katika uchaguzi wa serikali za mitaa mapema mwaka huu. Kwa maneno haya Mrema alikuwa anawambia watanzania kuwa kutoka katika kambi ya upinzani ni yeye pekee tu basi aliyestahili kuteuliwa na vyama vyote kupambana na Mkapa ifikapo Oktoba. Inashangaza kabisa kwamba kauli kama hizi zinatoka kwenye kinywa cha mtu ambaye anatarajia kabisa watanzania wampe kura zao ili awe kiongozi wa juu kabisa kwenye taifa. Inawezekana kabisa kuwa mwaka 1995 Mrema alipata kura nyingi kuliko wapinzani wenzake wote. Lakini atasahauje kwamba mwaka huu ni mwaka 2000, na hadithi za kina Chavda na wosia wa Nyerere n.k., zimepitwa na wakati? Lakini huenda kibaya zaidi alichokifanya kwenye hoja yake ya kukataa ushirikiano na wapinzania wengine ni kauli yake kwamba TLP ndiyo iliyokuwa ya pili nyuma ya CCM kwenye matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa. Kauli hii imekuja kudhihiri kuwa ni ya uongo mtupu kufuatia mheshimiwa Kingunge Ngombale Mwiru kutoa takwimu za matokeo hayo bungeni na kusema kuwa mshindi wa pili kilikuwa ni chama cha CUF. Ni kwa nini hasa Mrema aliamua kutudanganya? Ni vigumu kwa mtu kuamini kuwa Mrema ni mpinzani wa dhati kutokana na historia yake. Mwaka 1995 yeye na wenzake ndani ya NCCR mageuzi walimleta marehemu Abdulrahman Babu eti awe mgombea mwenza wa Mrema wakati wakijua fika kuwa Babu kwa mujibu wa sheria asingeruhusiwa kugombea. Ilikuwa ni kama bahati tu vyombo vya habari kustuka na kuhoji juu ya jambo hilo mapema la sivyo wote wawili wangezuiwa kisheria kugombea na tume ya uchaguzi na hivyo kuwatosa watu wote ambao kwa dhati walikuwa wamejitokeza kuiunga NCCR mkono. Pili, Mrema anakabiliwa na kesi nyingi za uchochezi. Vipi mwenzake Mtikila kwa kesi ya uchochezi iliyoibuka juzi juzi tu kesha hukumiwa siku nyingi kifungo lakini kesi za Mrema za siku nyingi hamna kinachoeleweka? Siyo kuwa nauliza maswali haya kwa nia ya kutaka Mrema afungwe, la hasha! Nayauliza tu katika hali ya kutaka kuwekana sawa. Kwa nini kwa mfano CCM ambao kinadharia ni mahasimu wa Mrema wakubwa hawajafikiria hata siku moja kuulizia ni vipi kodi za wafanyabiashara wa korosho miaka ile bado akiwa waziri wa mambo ya ndani zilikuja kulipiwa nyambani kwake Kiraracha, badala ya kwenye ofisi za serikali zilizohusika? Mbona haiulizwi hata siku moja ni vipi Mrema aliwachukua wale jamaa zetu waliokuwa wanatorosha dhahabu na fedha za kigeni kutoka DIA hadi ofisini kwake ambako baada ya mazungumzo aliwaachia na baadaye kulitangazia taifa kuwa aliwaachia kwa sababu eti walikuwa ni mawakala tu ? Vipi wakala aliyeshikwa na nyara za serikali asiwe mhalifu , ila yule anayeshikwa na gudulia la gongo au kiroba cha bangi atiwe hatiani? Bila maswali haya kupatiwa majibu ya kina kuna umuhimu wa wapinzani kumwangalia mheshimiwa huyu kwa tahadhari kubwa. Mwisho ningependa kuwaasa wakristo wenzangu kuwa hali mbaya ya nchi yetu nasi hali kadhalika tuna wajibu mkubwa wa kutafuta ufumbuzi wake kama walivyo watanzania wengine. Tukumbuke kuwa tunaoathirika ni wote bila kujali dini ya mtu. Ni muhimu tusikubali kabisa kuamuliwa watu wa kuwachagua wakati wa chaguzi bali tuchague wale tunaoona kwamba kwa kweli wana uwezo wa kuondoa kero katika nchi yetu. |
YALIYOMO
Tahariri
Cheyo kuendeleza ‘mfumo Kristo’ Rushwa katika kura za maoni: 'CCM isitafute mchawi' CUF yakanusha propaganda za waraka Wanachama wa CUF kortini Kilwa KINYANG’ANYIRO CHA UBUNGE: CCM Temeke wamtaka Bazaar 'Wanafunzi Lindi wamshughulikia Mkuu wa Shule aliyewazuia kuswali' Milioni moja zachangwa kujenga madrasa USHAURI NASAHA
MAKALA
MAKALA
MIPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
MAKALA
Burudani/Muziki
LISHE
|
|
|
|
|