NASAHA
Na. 057 Jumatano  Julai 19 - 25, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Cheyo kuendeleza 'mfumo Kristo' 
  • Bara 'hatakiwi' Rais Muislamu 
  • Mrema nae ajiegemesha kwa Pengo 
Na Mwandishi Wetu 

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha UDP, Bw. John Momose Cheyo, hana tofuati na viongozi wa serikali iliyoko madarakani ambao wamekuwa wakitoa upendeleo kwa Wakristo dhidi ya watu wa dini zingine, imedaiwa.

Madai hayo yametolewa na wananchi mbalimbali waliozungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki kufuatia kauli ya Bw. Cheyo kwamba muungano wa vyama vya CUF na CHADEMA katika kuwasimamisha wagombea urais wa Jamhuri na wa Zanzibar una harufu ya udini. Udini uliokusudiwa hapa ni Uislamu. 

Katika madai yake, Bw. Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha UDP, alisema ameamua kujitoa katika umoja uliokuwa ukihusisha chama chake na vyama vya CUF na CHADEMA kwa vile hali ya mambo ilielekea kuwa watu ambao wangeteuliwa kugombea nafasi za urais walikuwa ni Waislamu watupu. 

Bw. Cheyo alisema umoja huo uliamua kumuunga mkono mgombea urais wa Jamhuri kwa tiketi ya CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba ambaye ni Mwislamu hali ya kuwa mgombea mwenza wake, Bw.Nassoro Hamisi Mohamedi,ni Muislamu pia. 

Kwa mujibu wa madai ya Bw. Cheyo, iwapo kambi yao itafanikiwa kushinda katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu, nafasi za Urais wa Jamhuri, Makamu wa Rais wa Jamhuri na Rais wa Zanzibar zote zitakuwa zimeshikwa na Waislamu. 

Wananchi waliozungumza na gazeti hili wameeleza kwamba Bw. Cheyo ameonesha kuwa hana tofauti na viongozi wa serikali ya CCM ambao wanapohojiwa ni kwa nini nafasi nyingi serikalini zimeshikwa na Wakristo, hudai uteuzi wao haukuangalia dini za wahusika bali uwezo wao kitaaluma. 

Wananchi hao wameendelea kufafanua kuwa, ikitokea nafasi hizo kushikwa na Waislamu, viongozi hao hawachelewi kudai kuwa udini umetumika. 

"...tulidhani Cheyo hi tofauti na hao waliopo madarakani...wakiambiwa wafanye usawa katika uteuzi wao, wasiwapendelee Wakristo wanadai eti wao hawateui kwa kuangalia dini ya mtu, lakini wakiona Waislamu wameteuliwa wanafoka eti kuna udini", wameeleza wananchi hao. 

Aidha, wananchi hao wamedai kwamba kauli ya Bw. Cheyo inaashiria kwamba viongozi wa serikali walio madarakani wanatenda shughuli zao kwa kufuata zaidi matashi ya imani yao ya Kikristu kuliko maelekezo ya Katiba ya nchi. 

"Ikiwa mtu anatakiwa kutawala kwa kufuata taratibu za nchi, hii hofu ya mtu huyo kufuata matamanio ya dini yake yanatoka wapi?", alihoji mwananchi mmoja na kuongeza kuwa hofu ya Bw. Cheyo inatokana na jinsi Wakristo wenzake walivyozoea kuitawala nchi hii kwa kufuata imani ya dini yao. 

Wananchi hao pia wamedai kuwa kwa namna ya mambo anayoyataka Bw. Cheyo, haitatokea hata siku moja Tanzania Bara ikatoa kiongozi wa nchi Muislamu. 

Wamesema matakwa ya Cheyo ya kwamba ikiwa mgombea urais atakuwa ni Muislamu, basi mgombea mwenza awe ni Mkristo au kinyume chake. 

Wameendelea kueleza kuwa, kwa kuwa zaidi ya asilimia 99 ya wakazi wa Zanzibar ni Waislamu, na kwa vile katiba inataka mgombea urais akitoka Tanzania Bara basi mgombea mwenza wake atoke Zanzibar au kinyume chake, hivyo ni wazi hatapatikana mgombea Muislamu toka Tanzania Bara kwa vile kila uchaguzi Zanzbar itatoa mgombea Muislamu. 

...hivyo, kwa kauli ya Cheyo ni kwamba Waislamu toka Tanzania Bara hatuna haki ya kuwa Rais(wa Jamhuri) au Makamu, miaka yote nafasi hizo zitakuwa ni za Wakristu tu, ...vinginevyo ziletwe misheni kuwabatiza Wazanzibari au tuvunje muungano", alisema Bw. Athumani Kapongo wa Mwenge jijini Dar es Salaam. 

Aidha wananchi hao wameshangazwa na kimya cha serikali juu ya kauli hiyo ya Bw. Cheyo ambayo pia imemnasibisha Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Tanzania. Hayati Mwalimu Julius Nyerere na utamaduni wa "kuzingatia uwiano wa kidini" kwa watu wanaoshika nafasi za juu serikalini. 

Akiripotiwa na gazeti moja la Kiswahili litolewalo kila siku katika toleo lake la Jumanne Julai 11, mwaka huu, Bw.Cheyo alidaiwa kusema utamaduni wa kuweka usawa katika kushika nafasi za juu serikalini umekuwepo tangu enzi za Mwalimu Nyerere ingawa utaratibu huo haumo katika Katiba ya nchi. 

Wamesema wanashangaa ni kwa nini serikali haijatoa kauli yoyote kumkemea Bw.Cheyo kwa matamshi yake hayo yenye kuleta udini katika siasa au kumsafisha Hayati Mwalimu Nyerere kwamba hakuwa na hisia za udini katika jambo hilo. 

"(Rais)Mkapa, yeye ndiye mkuu wa nchi hii, kalihutubia Bunge (wiki iliyopita) lakini hajasema lolote juu ya Cheyo kana kwamba matamshi ya Cheyo hayana hatari hapa nchini", alisema mwananchi mmoja aliyefahamika kwa jina la moja la Mshindo na kuongeza kuwa Rais Mkapa ndiye anayefaa kuwa mstari wa mbele kumtetea Mwalimu Nyerere pale jina lake linapotaka kuchafuliwa. 

Hata hivyo, baadhi ya wananchi hao wamedai kuwa kimya cha serikali kimekuwepo kwa vile Bw. Cheyo alikuwa akitetea nafasi ya Wakristo. 

"Lakini yote haya tunayajua, viongozi serikalini wameamua 'kummezea' Cheyo kwa sababu ni mwenzao na anatetea mfumo Kristo", alidai Bi. Sauda Msumi wa Sokoni Kariakoo na kuongeza kuwa serikali isingekaa kimya kama maneno yale yangekuwa yamesemwa na mwanasiasa Muislamu kutetea nafasi ya Waislamu katika uongozi wa nchi. 

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Lyatonga Mrema alifanya mkutano wa hadhara Kidongo Chekundu mwanzoni mwa wiki ambapo katika hotuba yake alinukuu maneno ya Kadinali Pengo katika magazeti ya zamani yaliyodai kwamba CCM ni kichaka cha wahuni. 


Rushwa katika kura za maoni
'CCM isitafute mchawi' 

Na Mwandishi Wetu 

MADAI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba Chama Cha Wananchi (CUF) kilibajeti na kupenyeza jumla ya Shs. Milioni 800/- ili kuhujumu upigaji wa kura za maoni kuwapata wana-CCM wanaotaka kugombea udiwani zimepokewa kwa hisia tofauti miongoni mwa wananchi, ambapo wengi wao wamesema hayana msingi wowote.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa madai hayo yaliyotolewa na kiongozi mmoja mwandamizi wa chama hicho tawala umepelekea wapenzi na wakereketwa wa CCM kuona kuwa chama chao kinaudhaifu. 

Wakereketwa hao wa CCM wameeleza kuwa madai hayo ya chama chao yanaashiria kuwepo kwa idadi kubwa ya mapandikizi ndani ya chama chao ambacho ndicho chama cha siasa kikongwe nchini. 

Wakereketwa hao wamesema wameshangazwa na hali hiyo kwa vile chama chao kilikuwa kikijivunia kuwa na idadi kubwa ya wanachama, lakini kumbe 'walioikuza' idadi hiyo si wana-CCM. 

"Tuliowaona wakigawa pesa kwa wapiga kura ni Wana-CCM wenzetu, leo tunaambiwa pesa hizo zilitoka CUF... kwa kweli mambo hayo yanatukanganya na ni aibu kwetu", alisema Bw. Rogers Mashauri wa Manzese ambaye alidai ni mwanachama wa CCM. 

"Je hata Idd Simba ambaye tumesoma magazetini alikuwa akiwasaidia akinamama Mushi kukampeni huko Ilala naye ni CUF?", alihoji Bw. Mashauri. 

Mbunge wa Ilala (CCM) Mhe. Idd Simba, aliripotiwa na vyombo vya habari kutoa msaada wa hali na mali kuwasaidia wana-CCM wawili walioomba kugombea udiwani katika Kata za Ilala na Mchikichini. Mhe. Simba pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara katika serikali ya Muungano. 

Aidha, wana-CCM hao wamedai wanashangaa ni vipi viongozi wao wameweza kuifahamu mipango ya ndani ya chama kingine ya kuihujumu CCM lakini washindwe kuwanasa watu waliokuwa wakigawa pesa hizo. 

Akitolea mfano hali hiyo, Bw. Hassan Magongo pia wa Manzese jijini alisema, "ni jambo la kushangaza mtu ajipenyeze mpaka chumbani mwako na apate muda wa kuharibu haribu halafu ushindwe kumkamata". 

Wana-CCM hao wamesema ni jambo la busara kwa viongozi wao kusimama katika misingi ya ukweli na uwazi kuelezea hali halisi ya chama chao. 

"Ni lazima viongozi wawe wakweli na wawe wazi..... lazima tukubali kuwa rushwa imo katika chama (chetu) nawatu wanapendakung'ng'ania madaraka", alisema mwana-CCM aliyetambulika kwa jina moja tu la Makala, ambaye alongeza kusema kuwa viongozi wa CCM wasikimbilie kutafuta visingizio. 

Mwananchi mwingine, Mama Zaituni amedai kwamba anafahamu kuwa fedha ziligawanywa kwa wapiga kura lakini hajui fedha hizo zilitoka chama gani. 

Hata hivyo, amedai mama huyo mfanyabiashara wa Ilala, kura zao wamempa mgombea ambaye hakutoa rushwa. 

"Hela tumepata wanawake wote wa mtaa huu na kadi zetu (za uanachamam wa CCM) tumelipiwa, lakini kura hatukumpa", alieleza Mama Zaituni anayekadiriwa kuwa na umriwa miaka 50. 

Alipotakiwa kueleza ni kwa nini hawakuwapigia kura waliotoa pesa, Mama Zaituni alijibu bila kuchelewa, "hawa wenye pesa hawatujali sisi masikini, tukiwachagua wakawa madiwani ndio watakuja kuamrisha wanamgambo wao watumwagie vitumbua vyetu." 

Wananchi wengine wameonesha wasiwasi iwapo madai hayo ya CCM ni ya kweli. 

Wamedai kwamba si jambo rahisi kwa chama chochote cha upinzani kupata shilingi milioni 800 kwa ajili ya kukihujumu chama kingine. 

Vyama vya upinzani havina pesa, hao CUF wapate wapi hizo milioni 800, CUF haina akina Raza, CUF haina (wafanyabisahara) wenye vituo vya mafuta, wala haina wasagishaji ngano wala wamiliki meli", amedai mmoja wa wananchi hao. 

Hivi karibuni mfanyabiasha maarufu wa Zanzibar Mohamed Raza aliikabidhi CCM msaada wa thamani ya jumla ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya kampeni za chama hicho tawala. 

Aidha, taarifa zilizowahi kupatikana, jijini zilidai kwamba baadhi ya wafanyabiashara wakubwa, wakiwemo wanaomiliki viwanda vya kusagisha nafaka, vituo vya mafuta ya petroli, vituo vya TV na maduka makubwa (supermarkets) wamekuwa wakiisaidia CCM. 

Habari hizo ziliendelea kudai kuwa wafanyabiashara waliojaribu kuvisaidia baadhi ya vyama vya upinzani walisakamwa na biashara zao kutiwa msukosuko. 

Kadhalika wananchi waliozungumza na gazeti hili wamedai kuwa iwapo CCM itarejea madarakani, haitakuwa rahisi kwa chama hicho kupambana na rushwa kwa vile watendaji wengi watakuwa wamepata nafasi hizo kwa njia ya rushwa. 

"Wengi wa walioomba kugombea huo udiwani ni maafisa wa serikali na viongozi wa chama wenyewe, na hawa ndio waliotoa rushwa.... hawa wakichaguliwa wataweza vipi kuondoa rushwa hali ya kuwa wenyewe ametawaliwa na rushwa?",alihoji Bw. Amon Mrutu wa Muhimbili. 


CUF yakanusha propaganda za waraka 
  • Yadai ni mbinu za CCM 


Na Mwandishi Wetu 

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimekanusha waraka uliosambazwa Zanzibar unaodaiwa kuwa ni wa chama hicho.

Akihojiwa na Sauti ya Ujerumani juzi, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema waraka huo umesambazwa 'mashushu'wa serikali wakishirikiana na Chama Cha Mapinduzi(CCM). 

Mwanzoni mwa wiki hii iliripotiwa na vyombo vya habari kuwa CUF imesambaza waraka huo uliodaiwa kusainiwa na Maalim Seif, ambao unatoa ahadi 14 ambazo zinapaswa kutekelezwa na wagombea watakaposhika madaraka kwa kipindi cha siku 100. 

Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, ahadi hizo zimedaiwa kupitishwa na kikao cha kamati ya uongozi iliyokutana hivi karibuni jijini Dar es Salaam ni hizi zifuatazo:- 

Moja, Kuutangaza Mji Mkongwe kuwa ni Mji Mkuu wa Zanzibar, ambapo ukaazi na uingiaji wa watu katika mji huo utakuwa kwa masharti maalumu kwa lengo la kuzuia ongezeko la kuishi wageni wa kupandikizwa. 

Mbili, Kuwafungulia mashitaka viongozi na watendaji wote wa SMZ na CCM wanaotajwa kuhusika na vitendo vya wizi, ubadhirifu wa mali za umma na ukandamizaji wa kisiasa. 

Tatu, kuvunja uhusiano na Nigeria, nchi ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kuwawekea vikwazo viongozi wetu wanaodhalilishwa na kuonewa na madhalimu wa haki za binadamu. 

Nne, kujiunga na Umoja wa Kiislamu Duniani (OIC) na kuanzisha uhusiano mpya na ndugu zetu wa Brunei. 

Tano, kuivunja Tume ya Uchaguzi iliyopo sasa hivi kwa kuanza kuwaingiza wajumbe wapya wa Tume hiyo kutoka nje ya Zanzibar. 

Sita, kurejesha heshima na utukufu wa watu wa makabila mbalimbali ambao waliteremshwa utu wao tokea 1964. 

Saba, kuvidhibiti vyombo vyote vya habari vya Zanzibar (vya serikali na watu binafsi) ambavyo muda wote vimeonekana kupoteza maadili ya kazi zao kwa kutoa upendeleo kwa CCM. 

Nane, Vyombo vya ulinzi, Jeshi la Polisi, JKU na KMKM kuviunda upya kwa kuvibadilisha kuanzia ngazi ya uongozi wa juu hadi askari wakandamizaji wa kawaida. 

Tisa, kuyafuta na mengine kuyataifisha mahoteli ya kitalii ambayo hivi sasa yanaonekana kuwa ni chanzo kikuu cha kuongezeka umalaya nchini. 

Kumi, utawala wa Mahakama za Zanzibar utabadilishwa kwa kuweka watu wenye taaluma inayotakiwa ya sheria ya pamoja na kuwa na msimamo wa kuipenda nchi yao. 

Kumi na moja, masheha wote na hasa wale wa CUF wataongezewa nguvu za kuweza kutoa hukumu zenye maadili ya Kiislamu katika maeneo yao. 

Kumi na mbili, watumishi wote wa serikali watalipwa vizuri na wakati huo huo kutolewa adhabu kali ikiwemo ya kufukuzwa kazi mara moja kwa yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo vya ubadhirifu, utegeaji na uzembe. 

Kumi na tatu, kutoa uhuru kwa wanawake unaolingana na maagizo ya kitabu cha dini badala ya sasa kutegemea mkutano wa Beijing unaowafanya akina mama kuhemkwa ovyo na kufanya mambo watakavyo. 

Kumi na nne, kuangusha bei ya bidhaa kwa serikali kufidia bei halisi kwa kipindi cha miezi sita ya awali. 

Aidha, Maalim Seif alisema kuwa chama chake kina habari za uhakika kuwa CCM na serikali ina mpango wa kupeleka Zanzibar wapiga kura kutoka Bara. "......kama CCM inapinga mpango huo basi wakanushe", alisema Maalim Seif na kuongeza "mwaka huu hatutakubali kudhulumiwa". 

Wakati huo huo, Waislamu mbali mbali jijini Dar es Salaam wameulaani waraka uliodaiwa kusambazwa na BAKWATA Mkoa wa Dar es Salaam kwenda kwa watendaji wake unatoa maelekezo ya namna watakavyoipigia debe CCM. 

Waislamu walioongea na gazeti hili wamesema wamesikitishwa na kitendo hicho cha jumuiya ya kidini kukubali kutumika kwa manufaa ya wanasiasa badala ya waumini wa Kiislamu. 

Aidha, Waislamu hao wameitaka BAKWATA Makao makuu kuzungumzia suala hilo. 

Kwa mujibu wa waraka huo uliosainiwa na Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Dar es Salaam Ust. K. Mshindo, ambao NASAHA ina nakala yake viongozi wa BAKWATA mkoa, wilaya na kata wanatakiwa watoe taarifa kwa Maimam ili waisifie CCM na serikali yake mbele ya Waislamu. 

"Lengo letu halitatimia endapo tutachelewa kazi hii kuanzia sasa. Lazima Rais Mkapa arejee madarakani mwaka huu. Kama haturudi madarakani tena, eleweni hawa maadui zetu waliojitokeza lazima wataivunja BAKWATA", ilisomeka sehemu ya waraka huo wenye Kumbukumbu Na. BKT/DAR/048/VOL. II/2000/127 wa Julai 14, mwaka huu. 

Waraka huo umeendelea kueleza kuwa, "Bado tunaamini kuwa, Waislamu wengi hasa vijijini, bado masikio yao hayaja funguliwa na mawaidha ya akina Sheikh Mbukuzi, Bwana Ponda, na hawa watu wa mihadhara. Inabidi tuwahi mapema.... Madai ya Waislamu kuhusu mauaji ya Mwembechai ni ya kweli. Lakini endapo tutawasapoti Waislamu, tutakuwa tumeisaliti serikali tuendelee na msimamo wetu ule ule". 

Juhudi za gazeti hili kuwapata viongozi wa BAKWATA kuzungumzia juu ya waraka huo hazikufanikiwa mpaka tunakwenda mitamboni. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Tume, PCB na vyama vya siasa mmekiona mliochoandaliwa Oktoba?

Cheyo kuendeleza  ‘mfumo Kristo’

Rushwa katika kura za maoni: 'CCM isitafute mchawi'

CUF yakanusha propaganda za waraka

Wanachama wa  CUF kortini  Kilwa

Waumini waapa kulinda Msikiti

KINYANG’ANYIRO CHA UBUNGE: CCM Temeke wamtaka Bazaar

'Wanafunzi Lindi wamshughulikia Mkuu wa Shule aliyewazuia kuswali'

Milioni moja zachangwa kujenga madrasa

Hata na mimi sijala

USHAURI NASAHA
Jinamizi la ukewenza

MAKALA
Kushindwa kujitegemea ni laana

MAKALA
UDP, TLP wathibitisha hisia za Waislamu kuwa Uislamu ni kero Tanzania

MIPASHO NASAHA
Mwanasiasa wa kisasa

Kalamu ya Mwandishi
Mamluki wa mageuzi

MAKALA
Mrema na Cheyo wajihadhari wasije wakatumiwa kuwavuruga wananchi

MAKALA
Viongozi wa vyama vya siasa na udini nchini Tanzania

Mandela ni mfano wa kuigwa

Burudani/Muziki
Cat Stevens: Historia kwa Ufupi

Habari za Kimataifa

LISHE
Yanayoweza kumdhuru mtoto tumboni

MASHAIRI

MICHEZO

  • Jenerali Ulimwengu amgonga nyundo Mkapa
  • Hassan Affif aitabiria Simba Ubingwa

  •  



     
     

       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita