NASAHA
Na. 050 Jumatano Mei 31 - Juni 5, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
RIWAYA

Mapinduzi ya fikra - 4 

MTUNZI: ABU FIRDAUS 

WAKIWA wamefika Jangwani wakielekea hospitali Muhimbili, Mama Luqman alipepesa macho kulia na kushoto kisha alitoa shahada "Ash-hadu an Ilah ilaha illah ila wa ash-hadu anna Muhammad Rasurullah". Kisha alishusha pumzi kwa nguvu na kukata roho.Rahma alishtushwa na kutulia kwa mama yake, alijaribu kusikiliza mapigo ya moyo yaliyokuwa yakienda kasi, moyo ulikuwa umetulia huku joto lamwili likitoweka taratibu. Alimkumbatia marehemu mama yake katutangulia, alilalama kwa uchungu.

SIKU iliyofuata Luqman alimuandikia barua mjomba wake kumueleza yale waliyokusudia. Mjomba wake alipojibu, alikuwa yuko tayari kuendelea kumsomesha Omar pamoja na hali ngumu aliyokuwa nayo. Luqman kwa upande wake alianza kufanya pilikapilika huku na kule ili kutafuta fedha za ada ili amlipie Rahma na Lulu pindi muda wa kuanza masomo utakapowadia. Alikuwa tayari kufanya kazi ya aina yeyote ilimradi apate fedha za kuwasomesha wadogo zake. Haikuchukua muda mrefu akawa amepata kibarua cha kubeba zege katika kampuni moja ya ujenzi iliyokuwa inajenga majengo mawili makubwa katikati ya mji. Luqman alifurahi kwa fedha alizokuwa analipwa takriban elfu kumi na tano kwa wiki. Aliendelea na kazi hii kwa muda wa wiki tatu na siku nne. Siku hiyo alikuja mhandisi wa jengo ambaye alikuwa anapenda sana kuwa karibu na wafanyakazi na hata kufanya nao masihara hasa wakati wa chakula. Mhandisi aliagiza chakula na baada ya muda aliinuka na kumfuata Luqman ambaye alikuwa amekaa kwa kujitenga. Alinawa mikono na kuanza kula naye chakula huku akimuagiza muuzaji (mama ntilie)awaongezee chakula kingine. 

"Umejitenga kusudi nisile chakula chako." Alitania mhandisi. "Si hivyo basi, nina matatizo mengi ambayo yananifanya nikae pembeni."Unataka kuumba mtu?", aliendelea kudhihaki mhandisi. Luqman alikuwa kimya kwa dakika kadhaa. 

"Luqman una mawazo gani mbona mnyonge hivyo?", Aliuliza mhandisi. "Naomba unieleze shida yako na kama n`taweza kukusaidia niko tayari kufanya hivyo", Mhandisi alimbembeleza Luqman. "Ni habari ndefu inahitaji muda wa kutosha kukueleza", alijibu Luqman."Basi naomba tuonane ofisini saa tisa baada ya kumaliza kazi". "Sawa bosi", alijibu kwa kifupi Luqman. Bosi alinawa na kuondoka. Wafanyakazi walirejea kazini mpaka saa nane na nusu kisha walianza kunawa na wengine kuoga kisha kuondoka. 

Luqman alibisha hodi ofisini kwa bosi yapata saa tisa na dakika mbili. Bosi (Yusuph) alimkaribisha kwenye kiti. Bosi Yusuph aliacha kazi zote na kuanza kumsikiliza Luqman. Luqman alimueleza juu ya misiba ya wazazi wake, matatizo waliyokumbana nayo, majukumu yanayomkabili na kumwambia kuwa ni kutokana na majukumu hayo hakujali kuwa ana elimu ya FTC hivyo asibebe zege. "Umemaliza FTC?", aliuliza bosi Yusuph. "Ndio",alijibu Luqman. "Una cheti?". "Hapana. Vyeti bado havijatoka, ila nina result slip. Kweli Luqman ana majukumu mazito. "Sasa mimi n'takusaidia vitu viwili, kwanza n'takusaidia kumsomesha mdogo wako mmoja na wewe utamsomesha aliyesalia. Ili uweze kumudu kumsomesha huyo mmoja aliyesalia, ntakubadilishia kitengo. Kesho asubuhi ukifika njoo moja kwa moja ofisini saa mbili asubuhi na karatasi yako ya matokeo ya mitihani yako ya FTC". "Ntashukuru sana bosi", alishukuru Luqman. "Usiwe na wasiwasi Luqman, wewe ni ndugu yangu", alifariji bosi Yusuph. Waliagana na Luqman akaondoka huku akiwa na furaha tele. 

Alifika nyumbani na jioni ileile aliwaita wadogo zake na kuwaeleza yale aliyoongea na bosi. Wote walifurahi na kuomba dua. 

Siku iliyofuata, Luqman alifika ofisini kwa bosi Yusuph yapata saa moja na nusu asubuhi, muda ambao huwasili vibarua. Aliendelea kumsubiri bosi mpaka yapata saa mbili na robo, ndipo bosi aliwasili. Walisalimiana na bosi Yusuph alifungua mlango na kumkaribisha ndani Luqman. Baada ya kufanya mazungumzo na kukabidhi kivuli cha matokeo ya F.T.C, bosi Yusuph alimwambia kwamba angempeleka katika maabara ya udongo, na kwamba mshahara wake utakuwa shilingi efu tisini na nauli shilingi elfu kumikwa mwezi. Hivyo atapata shilingi laki moja kila mwezi. Luqman alimshukuru sana bosi. Bosi Yusuph alisimama na kuongozana naye mpaka maabara na kumtambulisha kwa wenzake. Luqman alianza kuchapa kazi kwa moyo wote hata wenzake walimsifia kwa juhudi zake. Kadri miezi ilivyokwenda ndivyo Luqman alizidi kujiwekea akiba, alitumia shilingi elfu moja tu kila siku. Hivyo alikuwa na akiba ya shilingi elfu sabini kila mwezi. 

Baada ya miezi mitatu tangu Luqman aanze kazi, muda wa Rahman kuanza masomo ya kidato cha tano uliwadia. Luqman alimpeleka dada yake shuleni na kumlipia ada ya shule ya nusu muhula, shilingi laki moja na elfu ishirini. Luqman aliendelea kumsomesha dada yake huku Lulu akilipiwa ada na matumizi mbalimbali ya shule na bosi Yusuph. Omar aliendelea kupokea ada ya shule kutoka kwa mjomba wao. Mbali na kumlipia ada Rahma, Luqman alikuwa na jukumu pia la kuihudumia familia kwa chakula na mahitaji mengine. Alimthamini sana mama Suleiman kwa mchango alioutoa mpaka kufikia wakati ule. 

Matokeo ya mtihani yalipotoka, Omar alipata daraja la pili katika mtihani wake wa Kidato cha Nne akachaguliwa kujiunga kidato cha tano katika shule ya sekondari ya Tambaza jijini. 

Rahama kwa upande wake alisoma kwa bidii, japo alikumbana na vishawishi vingi ambavyo vilitosha kuwa chachu ya kumfanya apoteze muelekeo, lakini Rahma aliendelea kuzingatia masomo. Hakutamani kupata kitu kilicho nje ya uwezo wake. 

Muda uliwadia wa Rahma kufanya mtihani wa kumaliza Kidato cha sita. Alimaliza masomo yake na kumuacha Omari nae akiingia kidato cha sita. Kwa upande wa Lulu ambaye alikuwa kidato cha tatu, yeye alikuwa ni Lulu kwelikweli. Alikuwa nyota wa kutumainiwa shuleni kwao. 

Baada ya matokeo kutangazwa, Rahma ambaye alikua anasoma mchepuo wa masomo ya uchumi, jiografia na hesabu alifaulu kwa kupata alama za daraja la kwanza pointi nane, na hivyo kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu kusomea shahada ya kwanza ya uchumi. Kutokana na posho walizokuwa wanalipwa pale chuoni, Rahma sasa aliweza kujikimu bila kuhitaji fedha kutoka kwa kaka yake. 

Mwaka mmoja baadae, Omar naye alifanya mtihani wa kidato cha sita. Omar yeye alisoma masomo ya fizikia, kemia na hesabu. Matokeo yalipotoka, Omar nae alifaulu kwa kupata daraja la kwanza pointi nne. Akiwa ameomba kujinga na Chuo Kikuu cha Dar es Saaam, Omar alipata nafasi ya kwenda nchini Marekani kusomea digirii ya kompyuta. Hivyo Omari alishauriana na nduguze na kufikia uamuzi wa kutokwenda Marekani Kwa kuwa mosi; anahitajika kumsaidia Lulu kitaaluma pamoja na vijana wengine na pili waliona si vizuri yeye kwenda huko kwa kuwa vijana walio wengi waendapo huko hupoteza maadili mema ya dini zao walizolelewa. Hivyo Omar alijiunga hapa hapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea digirii ya kompyuta. 

Baada ya kuona mzigo aliokuwa nao umepungua, Luqman naye alijiandikisha kusomea shahada ya kwanza ya sayansi na elimu, katika Chuo Kikuu huria. Hivyo kila atokapo kazini aliwahi nyumbani kujisomea. 

Rahma alimaliza shahada ya kwanza na ya pili katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, na Omar alisoma shahada ya kwanza tu ya kompyuta. 

Baada ya kumaliza masomo yao, Rahma aliajiriwa na kampuni ya uuzaji vyombo vya nyumbani kutoka Saudia Arabia kama meneja mauzo. Na Omari aliajiriwa katika kampuni moja iitwayo "Yasir Computer system management' ya hapa jijini. Lulu kwa upande mwingine aliamua kusomea udaktari baada ya kupata daraja la pili pointi kumi na mbili katika mtihani wake wa kidato cha sita. Akiwa kidato cha tano na sita, Lulu aliendelea kuwa nyota katika masomo ya kemia na Bailojia. 

Baada ya kuwa wote wamehitimu isipokuwa Lulu tu ambaye alikuwa mwaka wa nne pale Chuo Kikuu cha Muhimbili, Luqman aliandaa chai ya jioni nyumbani kwake Sinza. Walikutana baada ya sala ya Magharibi. Walizungumza mengi sana ya kufurahisha siku hiyo, lakini kubwa katika mazungumzo yao walikumbushana safari yao kuanzia kufiwa na wazazi, Rahma kumwagiwa chakula chake, Luqman kuvunjiwa kibanda pale Magomeni na kuporwa biashara pale Kariakoo na kikao chao kilichotoa maamuzi waliyoyaita "maamuzi ya busara" ya kuamua kusoma katika mazingira magumu na kuwa na subira. Lakini leo wanazungumza kila mtu akiwa na elimu ya kutosha, maisha mazuri na anamuabudu Mola wake bila mawazo ya kulala njaa. Baada ya historia hiyo iliyochangiwa na kila mmoja kadri alivyokumbuka, "kweli usia aliotupa Mama kuwa tuishi kimapinduzi ulikuwa nao ni usia wa kimapinduzi. Alisema Lulu, na wote wakamuunga mkono. Walimaliza kunywa chai, wakaomba dua kwa pamoja na kisha wakatawanyika majumbani mwao. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Tahadhari ya Warioba juu ya rushwa isipuuzwe

Mkapa afanya ziara Pwani

CCM ‘inaweweseka’ - Sheikh

Zanzibar wadai kuyumbishwa na Bara

Serikali yatoa muelekeo wa Bajeti na kutangaza njaa

Habari za ndani
Wapinzani kusimamisha mgombea Urais mmoja 

SMZ haishughulikii mikarafuu -Maalim Seif

Mwalimu Mkuu Msimbazi Mseto atishia kujiuzulu 

Hizi ni 'arobaini' za mapandikizi

Waislamu Mbeya wamsusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA 

Masheikh wa BAKWATA waongoza sherehe za kuwasimika makamanda wa vijana wa CCM 

Wakristo waishitukia CCM

MAKALA
Dini na siasa haviwezi kutenganishwa

Makala 
Mikutano ya Prof. Lipumba 'yaendelea' baada ya kuondoka 

MPASHO NASAHA
MATATA! MATATA!

Kalamu ya Mwandishi 
Wapinzani epukeni patupu 

MAKALA
CCM na sera za maendeleo (6)

Habari za Kimataifaza Kimataifa

Lishe 
Supu na umuhimu wake mwilini

BARUA

MASHAIRI

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra - 4 

MICHEZO

  • Uchaguzi Yanga Julai
  • BATA yahimiza usajili michezo
  • 'Simba SC, Singida United baba mmoja mama mbali mbali' 
  • Tarimba akalia Kuti Kavu Yanga

  • Ambari, Mwakipesile wajitosa kugombea DRFA



       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita