|
Na. 050 Jumatano Mei 31 - Juni 5, 2000 |
|
|
|
|
|
Sheikh Mkuu wa BAKWATA: Kafiri ni kafiri ukitaka ni hivyo hutaki ni hivyo Ndugu Mhariri, KATIKA moja ya radio binafsi nchini ilitangazwa wiki iliyopita kuwa Sheikh Mkuu wa BAKWATA amekemea Waislamu kuwaita wasiokuwa Waislamu makafiri na kuongeza kuwa kufanya hivyo ni "dhambi." Katika matangazo hayo ilielezwa pia kuwa Sheikh huyo amesema kuwa Idi Amin wa Uganda hakuwa kiongozi mzuri wa Kiislamu. Ni vyema Sheikh huyu wa BAKWATA akaelewa kuwa sifa ya mtu kuitwa kafiri iwazi na iliisha fafanuliwa katika Qur'an. Yaani anae kufuru ni kafiri. Na miongoni mwa waliokufuru ni wale wanaosema miungu ni watatu na kwamba Mwenyezi Mungu amezaa na kuzaliwa. Ama kuhusu Idi Amin, sidhani kama Sheikh huyu wa BAKWATA ambaye ni mwenyeji wa barabara ya tatu, mjini Tanga anauwezo wa kujua historia ya Uganda, siasa zake na fani ya kuchambua uongozi wa Al Hajj Iddi Amin Dada aliyekuwa rais wa Uganda. Hata hivyo ningelifurahi sana endapo Sheikh huyo wa BAKWATA angelikuwa na uwezo wa kufanya uchambuzi wa aina hiyo. Maana angalitambua ni kipi kilichofanyika katika nyanja za siasa za nchi hii kuufisadi mkoa wa Tanza toka katika nafasi ya juu iliyokuwemo wakati wa kupata uhuru hadi kuwa moja ya mikoa iliyo chini na masikini sana nchini. Je, Sheikh huyu anajua kuwa Tanga ni mji wa pili Tanzania kupata hadhi ya Manispaa baada ya Dar es Salaam? Anajua ni nini kilichoifanya ipitwe na miji mingine iliyokuwa nyuma yake ambayo sasa imepewa hadhi ya jiji (city)? Angelikuwa na uwezo huo angelijua ni vipi Tanga sasa haina viwanda hata vile vya kilimo. Ni vipi vijana wa Tanga sasa hawana hata ajira ya u-seaman kwasababu siyo tu ya wazee wao kukoseshwa nauli, bali hata pasi za kusafria (passport) ni kero kwa wale wenye nauli. Angalijua ni vipi wananchi wa Tanga wanabugudhiwa na kunyimwa hata fursa ya kujiendeleza kwa kutegemea ajira asilia ya uvuvi. Angelijua kwa nini kilio cha wananchi wa Tanga cha kunyimwa maendeleo ya jamii kinapuuzwa. Angelijua kwa nini shughuli za kibiashara katika Bandari ya Tanga zimefifia kuliko zamani. Angelijua kwa nini kituo cha karakana ya reli Tanga kilihamishwa na kuwanyima ajira watu wa Tanga. Angelijua kwa nini kina mama wa Tanga hivi sasa ni wanyonge sana kimaisha ukilinganisha na miaka ya zamani, hata enzi za ukoloni. Angelijua kwa nini hata sanaa ya taarab na michezo ya mpira wa miguu na ngumi imeanguka Tanga. Angelijua kuwa chimbuko la akina Matumla ni mzazi wao kucheza ngumu katika ujana wake akiwa Tanga. Angelijua kwa nini hivi leo Tanga haina akina Shaaban Robert, Maalim Kihere na kwa nini inashindwa kusomesha na kuhifadhi masheikh watukufu miongoni mwa watukufu waliopata kuwepo Tanga. Mwisho, angeliweza kutambua ni nani aliyehusika kisiasa kuifisadi Tanga na kuidhalilisha kimaendeleo kiasi hicho. Atambue kuwa kiongozi huyo hakuwa Muislam. Salim Haji,
Vumbua pombe ya kibo Gold na BAKWATA Ndugu Mhariri, NATANGULIZA shukrani zangu za dhati kwako kwa kupokea na kuchapisha barua hii. Madhumuni ya barua hii nikutafuta ukweli juu ya POMBE. Pombe ni haramu kwa Waislamu, na Uislamu unafundisha kuwa dhambi ya pombe iko kwa wale wote watakaohusika nayo ikiwa ni pamoja na mpishi wake, mbebaji, muuzaji; mnywaji na hata yule atakaye mmiminia mnywaji katika chombo cha kunywea. Kosa la pombe linamfika hata yule atakayemuelekeza mtu kunako uzwa pombe. Kutangaza pombe na kumpangisha (kwa kufanya biashara) muuza pombe ndani ya nyumba ni kosa kubwa zaidi. Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) likiwa linatazamiwa kusimamia sheria za Uislamu na kuhakikisha zinatekelezwa, likataze maovu na kuamrisha mema na pia kuwa mfano wa kuigwa, leo hii BAKWATA limekuwa msitari wa mbele kutangaza pombe kwani mbele ya jengo lake kubwa lilillopo katika makutano ya barabara za Bibi Titi Mohammed na Morogoro hapa jijini Dar es Salaam kumewekwa bango KUUBWA. Linalotangaza pombe aina "Kibo Gold". Juu ya bango hilo kuna motokari inayoshindaniwa na wanywaji wa pombe hiyo. Hivi MUFTI wa Bakwata na uongozi wake, hususan Ulamaa wanataka kutueleza nini juu ya pombe? Kuwa si haramu kuitanga ili izidi kunywewa na kwamba sasa kwa FATWA ya Bakwata pombe ni halali? Jee ni ujumbe gani ambao Bakwata linausambaza kwa umma, hivi haiingii akilini kuwa sasa kuweka au kuruhusu kuwekwa kwa bango hilo katika eneo linalomilikiwa kisheria na Waislamu ni kuudhalilisha na kuutukanisha Uislamu na pia ni kuwapa nafasi wasiokuwa Waislamu au wasioujua Uislamu kuona kuwa pombe si haramu katika Uislamu na pengine kuiga na kutolea mifano kuwa "mbona Bakwata watangaza pombe sasa kuna uharamu gani?" Ndugu Mhariri napenda kumalizia kwa kutoa ushauri kwa Waislamu wenzangu kuwa katika gazeti la NASAHA toleo Na. 048 la MEI 17-23, 2000 ukurasa wa sita, kuna habari za ziara ya Sheikh Mkuu wa Bakwata kuzua mtafaruku huko Iringa. Wito wangu kwa Waislamu ni kwamba huyu Sheikh Mkuu wa Bakwata tayari ameshafanya udhalimu mkubwa kwa Waislamu na Uislamu wenyewe, sasa kuna maana gani kumkaribisha ndani ya Misikiti au kwenda na kukaa kumsikiliza juu ya hayo aliyotumwa na mabwana zake? Kwa Waislamu wote kote linakosomwa gazeti hili, kuweni makini na Sheikh huyu anayeipinda Qur'an kwa manufaa yake, asiyewatakia heri Waislamu na anayeiamuru Serikali kuwakamata na kuwafunga Waislamu. Dawa yake ni kumfungia milango asiingie hata ndani ya Misikiti na ikibidi afukuzwe yeye na vibaraka wake. Afanyiwe kweli sasa. Asisikilizwe. Ibrahim Kitelezo,
Pongezi Sheikh Mbukuzi
Ndugu Mhariri, NAOMBA kwa idhini yako unipe nafasi nitoe machache katika gazeti lako tukufu la NASAHA. Hili ni gazeti ambalo linaandika habari zinazolenga kulinda na kutetea hali za wale tuliofanywa kuwa wanyonge au walalahoi. Napenda kumpongeza Amir wa Shura ya Maimamu Sheikh Juma Mbukuzi kwa kuonesha msimamo thatibi katika suala la kuwakomboa wanyonge wa Tanzania kutoka katika makucha ya utawala mbaya uliojaa rushwa, dhuluma, chuki,ubinafsi, ukristo(udini), ubadhirifu wa rasilimali za nchi na mengineyo mengi yenye kukera. Huu si utawala mwingine bali ni utawala wa CCM. Sisi Waislam tunafahamu kuwa dunia ni shamba la akhera na kuwa hatutoweza kuifaidi akhera yetu kama hatutolinda dunia yetu na maangamizo yanayoletwa na viongozi wabaya. Huwezi kuwa mcha Mungu katika mazingira ya rushwa, dhuluma, umaskini,kuzidi watoto yatima na wale wa mitaani wasio na huduma na kukosekana elimu bora. Mwisho katika kutetea haki hizi za Watanzania ujitahidi wewe binafsi na wale unaowatetea kujipamba na kila tabia njema. Tujilinde na tabia zote mbaya ambazo tunamtuhumu dhalimu kwazo. Abdullah Aziz Sompo, S.L.B. 555,Ujiji Kigoma.
Mufti unagawa ruzuku mikoani lakini wafanyakazi wako hatujalipwa mishahara
Ndugu Mhariri, Naomba nafasi unichapishie barua yangu ili Mufti wetu ajue taabu tuliyonayo wafanyakazi wa BAKWATA Makao Makuu. Tunasikia minong'ononong'ono hapa ofisini kuwa Mufti wetu anatembea na mamilioni ya pesa ambayo wanagawiwa ruzuku baadhi ya Masheikh wa BAKWATA. Kama hiyo ni kweli basi tunaomba Mufti wetu ajue kuwa wafanyakazi wake hapa Makao Makuu hatujalipwa mishahara na wahusika wanasema BAKWATA haina pesa. Hivyo tuna muomba Mufti wetu au Masheikh wowote wa BAKWATA mikoani watakao soma habari hizi watuonee huruma na kufikiria hali zetu. Sisi wengine tuna familia kubwa zinazotutegemea. Tunaomba hata kama mamilioni hayo yametolewa na wafadhili, basi nasi tufikiriwe japo mgao kiasi tu. Mtumishi Mtiifu,
Mahita (I.G.P.) tukueleweje? Ndugu Mhariri, TAARIFA alizotoa Mhe. Mahita wakati alipokuwa akitunukia nishani askari Polisi mkoani Mara aliwaonya kuwa askari polisi yeyote atakayejihusisha na maswala ya siasa, au kuegemea katika chama fulani cha siasa atakuwa amefanya kosa litakalompelekea kufukuzwa kazi, alionya kuwa hali hiyo, isijitokeze kama ilivyokuwa mwaka 1995 katika uchaguzi mkuu, baadhi ya askari walifukuzwa kazi kwa makosa kama hayo. Ni sawa kabisa Afande. Lakini la kushangaza sana pale alipoonya wananchi wajiepushe na wanasiasa ambao wanatumia matatizo ya askari Polisi kutaka kupendeka kwa wananchi, kwani matatizo ya Polisi yatamalizwa na jeshi la Polisi lenyewe, amesema hayo akiwa amesahau kuwa pia yeye mwenyewe ni askari Polisi vipi tena anapoingilia maswala ya wanasiasa na kuwaonya wananchi wajiepushe nao? Kwani hilo ni kosa linalompelekea askari kufukuzwa kazi. Hivyo tunasubiri sheria ifanye kazi yake juu yako kwa sababu sheria ni msumeno. Saidi M. Buweta,
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Zanzibar wadai kuyumbishwa na Bara Serikali yatoa muelekeo wa Bajeti na kutangaza njaa Habari za ndani
SMZ haishughulikii mikarafuu -Maalim Seif Mwalimu Mkuu Msimbazi Mseto atishia kujiuzulu Hizi ni 'arobaini' za mapandikizi Waislamu Mbeya wamsusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA Masheikh wa BAKWATA waongoza sherehe za kuwasimika makamanda wa vijana wa CCM MAKALA
Makala
MPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
Ambari, Mwakipesile wajitosa kugombea DRFA |
|
|
|
|