|
Na. 050 Jumatano Mei 31 - Juni 5, 2000 |
|
|
|
|
|
Uchaguzi Yanga Julai Na Badru Kimwaga UCHAGUZI Mkuu wa Klabu ya soka ya Yanga ambao ulipangwa na uongozi wa kamati ya muda ya klabu hiyo kufanyika mapema mwezi ujao umesogezwa mbele hadi mwishoni mwa Julai mwaka huu kutokana na ucheleweshwaji wa utolewaji wa hati ya usajili ya kampuni kwa klabu hiyo. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki kwenye ofisi zake mjini Dares Salaam, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo yenye makao makuu mitaa ya Jangwani na Twiga, Isack Shikihondo alisema kuwa uchaguzi wa kalbu hiyo sasa utafanyika Julai mwishoni badala ya Juni kama ilivyotangazwa awali. Makamu Mwenyekiti huyo alisema kuwa sababu za kusogezwa mbele kwa uchaguzi huo ni kutokana na kucheleweshwa kwa hati ya usajili kutoka msajili wa makampuni nchini, jambo ambalo litakwamisha uchaguzi huo na utaratibu mwingine kama ule wa kuandikisha majina mapya ya wanachama katika mfumo mpya wa klabu hiyo wa kampuni. "Si kweli kama uchaguzi mkuu wa Yanga umefutwa kama habari zinazosambazwa lakini ukweli ni baada ya kukwamishwa na upatikanaji wa hati ya usajili wa kampuni kwa klabu yetu, kama unavyojua kuwa timu yetu sasa ipo chini ya mfumo wa kampuni badala ya klabu kama ilivyokuwa hapo awali. Na mara baada ya kupatikana kwa hati hiyo tarehe ya uchaguzi huo itatajwa kwenye mkutano wa wanachama utakaoitishwa", alisema Shikihondo. Aliongeza kuwa Katibu Mipango wa klabu hiyo Abdul Sauko ndiye anayeshughulikia na kufuatilia hati hiyo ya usajili wa klabu yao. Lakini hadi sasa bado hajafanikiwa kupata usajili huo, hivyo hata zoezi la kuwandikisha wanachama wapya kwa mfumo wa kampuni nao kushindikana. Kutokana na mfumo mpya wa klabu hiyo ya Yanga wanachama watalipa ada ya shilingi 20,000 kwa wale wa daraja B na wale wa kundi A watalipa shilingi 200,000 ikiwa ni ada ya mwaka mzima na wataingia kwenye baraza la Seneti la klabu hiyo. Wakati huo huo Shekihondo alisema kuwa anashangazwa na timu za Kajumulo na Simba zote za jijini kutaka kuchukua nafasi ya klabu ya Yanga kwenye mashindano la klabu bingwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati yanayofanyika Kigali Rwanda wakati timu hizo hazikushiriki kwenye michuano hiyo au kushika nafasi za juu za ligi ya Tanzania Bara. Timu hizo zilitoa ombi la kuchukua nafasi hiyo ya Yanga baada ya timu hiyo kugoma kwenda kwenye michuano hiyo kutokana na kutolipwa dola 10,000 ikiwa ni zawadi kwa kunyakua ubingwa wa michuano hiyo kwa mwaka jana iliyofanyika nchini Uganda. Shekihondo alisema kuwa timu hizo pengine zimeshindwa kuelewa kuwa wao wanaenda huko kama bingwa mtetezi na sio bingwa wa nchi. Akasema kuwa Mtibwa ndiyo wawakilishi wetu kama bingwa wa nchi na kuongeza kuwa timu hizo zimekosa la kusema na kukimbilia mambo wasiyoyajua.
Na Mwandishi Wetu CHAMA cha mchezo wa Mpira wa Kikapu nchini (BATA) kimevihimiza vyama vya mikoa ambavyo havijajisajili kwao kufanya hivyo mapema kabla ya kufanyika mkutano maalum wa rasimu ya katiba mpya ya chama hicho utakaofanyika mwezi ujao. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi mjini Dar es Salaam, mjumbe wa kamati ya utendaji ya BATA, Ahmedi Simba alisema kuwa ni vyama vya mikoa saba tu ambavyo hadi sasa ndio wanachama halali wa chama hicho ambavyo vitaruhusiwa kuipitisha katiba mpya kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wake utakaofanyika kati ya Agosti na Septemba mwaka huu. Simba alisema kuwa mikoa ambayo bado haijasajiliwa ndani ya BATA inatakiwa kufanya hivyo mapema ili kuweza kupata fursa ya kushiriki kwenye mkutano huo maalum wa katiba mpya ya chama hicho vinginevyo vitakosa haki zao kimsingi na kuwa wasindikizaji tu. "Hadi sasa tuna wanachama hai saba tu, ambao wanahaki ya kupiga kura na kupitisha kila lenye maslahi na BATA, sasa tunatoa wito kwa vyama vya mikoa mingine ambayo bado haijasajiliwa kwetu kufanya hivyo mapema ili kusije kukatokea malalamiko huko mbele kuwa katiba mpya imepitishwa na idadi ndogo ya wanachama wakati wao hawataki kufanya usajili mapema kwa kipindi cha miaka zaidi ya mitatu", alisema mjumbe huyo. Aliitaja mikoa ambayo ina usajili ndani ya BATA kuwa ni Dar es Salaam, Arusha, Mara, Morogoro, Mwanza, Shinyanga na Dodoma na kuitaja isiyo na usajili kuwa ni Kilimanaro, Kigoma, Singida,Tabora, Iringa, Mbeya, Kagera, Ruvuma, Rukwa, Mtwara, Lindi, Pwani na Tanga. Mjumbe huyo alisema kuwa hivi karibuni kamati yao ya utendaji pamoja na ile ya kuratibu rasimu ya katiba mpya itakutana pamoja ili kuijadili katiba mpya na kuipitisha kabla ya kuiwasilisha kwa mikoa wanachama wao ambayo nayo itaipitia na kuipitisha na kutumika kwenye uchaguzi mkuu wa chama hicho. Alisema kuwa kamati hiyo ya kufanyia marekebisho katiba ya BATA iliundwa mapema mwaka uliopita na ilipokuwa inakaribia kumaliza kazi zake iliwabidi kufanyia tena kazi kutokana ana agizo la msajili wa vyama na klabu wa Taifa Leonard Thadeo alilolitoa kwa vyama na klabu nchini kufanyia marekebisho katiba zao kabla ya kuelekea kwenye chaguzi zao kuanzia ngazi za wilaya hadi Taifa. Agizo hilo la Thadeo lilikuja siku chache baada ya Waziri wa Elimu na Utamaduni, Alhaji Juma Othman Kapuya kusimamisha uchaguzi mkuu wa chama cha soka nchini FAT uliokuwa ufanyike Desemba 31 mjini Iringa na kuagiza kwamba vyama vyote kuanzia wilayani kufanya kwanza chaguzi zao baada ya kugundua kuwa vyama vingi haviko halali. Kama vilivyo vyama vingine vya michezo mbalimbali
BATA nacho muda wa viongozi wake umemalizika muda mrefu lakini kilikuwa
hakijafanya uchaguzi wa aina yoyote mpaka agizo hilo la Msajili ndilo lililowasukuma
kufanya hivyo.
'Simba SC, Singida United baba mmoja mama mbali mbali'
Na Hamis Kasabe
KOCHA Mkuu wa klabu ya Singida United ya Mkoani Singida, Selemani Mthew Luwongo, ameliambia NASAHA kwamba klabu yake inachangia baba na klabu ya Simba ya Dar es Salaam lakini mama mbalimbali. Mathew aliyanena hayo mwishoni mwa wiki alipotakiwa kuzungumzia uhusiano uliopo baina ya timu yake na Simba kufuatia timu hizo kudhaminiwa na kufadhiliwa na kampuni moja ya Mohammed Enterprises. Singida United na Simba baba yao ni mmoja, Mohamedi Dewji wa Muhammed Enterprises ambaye anazifadhili hizi timu lakini mama zao ni tofauti ambapo kwa upande wa Simba ni wanachama wakati kwa Singida United ni wakazi wa mkoa wa Singida. Pamoja na kwamba baba yao ni mmoja amesema Mathew hakuna uwezekano wa 'kubebana' katika ligi ya nane bora nchini itakayoanza Juni 17 mwaka huu.
Tarimba akalia Kuti Kavu Yanga
MWENYEKITI wa Kamati ya muda yaYanga, Abbasi Tarimba amezidi kujiongezea maadui ndani ya klabu hiyok wa kushikilia msimamo wake wa kutopeleka timu yake nchini Rwanda kushiriki katika mashindano ya klabu bingwa ya Afrika mashariki na Kati. Yanga kama bingwa mtetezi ilitakiwa icheze mechi yake ya kwanza Jumapili iliyopita dhidi ya St. Georges ya Ethiopia ambayo nayo imejitoa siku za mwisho kabla ya mashindano hayo kuanza. Tarimba amegoma kupeleka timu Kigali mpaka hapo klabu yake itakapolipwa sh. Milioni 8 ilizoahidiwa na shirikisho la soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kama bingwa wa michuano hiyo mapema mwaka jana nchini Uganda. Msimamo mkali wa Tarimba umepingwa vikali na baadhi ya wanachama waandamizi wa Yanga waliosajiliwa katika matawi ya Mwembe-Yanga, Buguruni Shule na Kariakoo. Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofuati jijini hivi karibuni wanachama hao wamesema, kwa kuizuia Yanga isishiriki michuano hiyo hali ya kuwa na fedha na timu nzuri Tarimba amefanya kosa la karne. "Hata kama tungekuwa (Yanga) tunaidai CECAFA milioni 100 na haijatulipa, bado Yanga tunagetakiwa kushiriki tu, sembuse hizo milioni 8 bwana milioni nane kitu gani.... Kwani Yanga tumepoteza vingapi toka 1926 amehoji", mwanachama kutoka tawi la Mwembe-Yanga. "Kama wachezaji wetu watakwenda Kigali, basi kuna uwezekano mkubwa wa kupata mechi nyingi za kimataifa ambazo zingewafanya wawe "fit" tayari kwa ligi ya nyumbani na hata ligi zinazoandaliwa na CAF, Shirikisho la Soka Afrika. "Na kwa kweli mazoezi ambayo wangeyapata huko yanathamani kubwa kwa klabu kuliko hata hizo milioni 8 anazozing'angang'ania Tarimba" ameongeza mkereketwa wa tawi la Buguruni Shule. Kwa upande wao,baadhi ya wanachama wa Yanga Kariakoo,wamemshangaa Mwenyekiti wao kwa kung'ang'ania kombe la thamani ya shilingi laki 4 wakati klabu inadai milioni 8. Licha ya kumuomba Tarimba abadili msimamo wake
lakini pia wanachama hao wameonyesha wasi wasi kwamba kiongozi wao amelewa
madaraka kutokana na kupendwa mno na Wanayanga kiasi cha kufanya maamuzi
makubwa kama hayo bila kuwashirikisha.
Ambari, Mwakipesile wajitosa kugombea DRFA Na Badru Kimwaga BAADA ya kushindwa vibaya kwenye chaguzi za vyama vyao vya wilaya aliyekuwa katibu wa IDFA Hamis Ambari na Mwenyekiti wa KIFA Erasto Mwakipesile wamejitosa kuwania uongozi katika chama cha soka mkoa wa Dar es Salaam DRFA utakaofanyika Jumapili ijayo. Ambari na Mwakipesile ni miongoni mwa wagombea 25 walijitokeza kuwania uongozi wa chama hicho wakiwemo hadhi ya viongozi wa sasa wa DRFA. Viongozi wa sasa ambao wamejitokeza katika nafasi zao ni Mwenyekiti Abushir Kilungo, Katibu Mkuu Kanali Ally Hassan Mwanakatwe, Katibu Msaidizi Hamis Kissiwa na mjumbe wa FAT, Azzan Mangushi. Kwa mujibu wa katibu wa kamati ya michezo wilaya ya Ilala, Mwamvita Fumba wagombea wengine ambao wamejitokeza kugombea nafasi mbalimbali za chama hicho ni Haji Nkuhi, Azzan Mangushi, Peter Mushi, Musin Said, Khamis Mattaka na Msafiri Mohamed wanaowania ujumbe wa mkoa -Taifa. Nafasi ya Mwenyekiti mbali na kutakiwa na Kilungo pia wapo James Mwakamele, Mohamed Missanga na Kafuku Ramadhani. Wengine ni Erasto Mwakipesile, Azzan Mangushi na Khamis Mattaka ambao wanaogombea umakamu mwenyekiti. Wanaopambana na Kanali Mwanakatwe katika nafasi ya Katibu Mkuu ni Amin Bakhressa, Hamis Ambari na Peter Mhinzi wakati nafasi ya katibu msaidizi mtetezi wa kiti hicho Hamis Kisiwa atawania nafasi hiyo na wagombea wengine ambao ni Athuman Nyamlani, Hamis Ambari, Msafiri Mohamed na Ramadhani Kafuku. Nafasi ya uweka hazina inawaniwa na wagombea wawili ambao ni Haroub Hassani na Gwakisa Mwambalaswa huku uweka hazina msaidizi unawaniwa na mgombea mmoja tu, Ally Hassani. Wagombea wengine ambao watafanyiwa usaili na kamati ya michezo mkoa wa Dar es Salaam (KMMD) siku ya Alhamis na nafasi wanazogombea zikiwa kwenye mabano ni Nurdin Hozza (ujumbe kamati ya utendaji), Juma Pinto (ujumbe), Salum Chaurembo, Abeid Mziba na Mlanzi Shadidu ambao wote wanawania ujumbe wa kamati ya utendaji Uchaguzi huo wa DRFA utafanyika Jumapili ijayo na mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu za wagombea ilikuwa jana saa 9.30. Wakati huo huo, uchaguzi wa chama cha Makocha Mkoa wa Dar es Salaam DAFCA ambao ulishindwa kufanyika wiki iliyopita sasa utafanyika Juni 4 na hadi sasa jumla ya wagombea sita wamejitokeza kuwania nafasi za uongozi wa chama hicho. Wagombea hao ni Shaaban Marijani na Tito Mwaluvunda
wanaotetea nafasi zao za Uenyekiti na ukatibu mkuu wa chama hicho. Wengine
ni Daud Kamti(katibu Msaidizi), Kennedy Mwaisabulo (Makamu Mwenyekiti),
Tamim Zavalla (ujumbe wa kamati ya utendaji) na Saidi Mpigi anayewania
ujumbe wa mkoa -Taifa.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Zanzibar wadai kuyumbishwa na Bara Serikali yatoa muelekeo wa Bajeti na kutangaza njaa Habari za ndani
SMZ haishughulikii mikarafuu -Maalim Seif Mwalimu Mkuu Msimbazi Mseto atishia kujiuzulu Hizi ni 'arobaini' za mapandikizi Waislamu Mbeya wamsusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA Masheikh wa BAKWATA waongoza sherehe za kuwasimika makamanda wa vijana wa CCM MAKALA
Makala
MPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
Ambari, Mwakipesile wajitosa kugombea DRFA |
|
|
|
|