|
Na. 050 Jumatano Mei 31 - Juni 5, 2000 |
|
|
|
|
|
Na Mwandishi Wetu IMEELEZWA kuwa kauli za tuhuma zinatolewa na baadhi ya viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na habari za propaganda zinazoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari vikiwemo vile vya chama hicho dhidi ya Waislamu ni "muweweseko" utokanao na madhambi ya chama hicho waliyowafanyia Waislamu nchini. Moja ya madhambi hayo yametajwa kuwa ni mauaji ya Mwembechai ambayo chama hicho kimedaiwa kuwa kiliitisha kikao cha juu na kuipongeza serikali yake kwa kuvamia Msikiti, kudhalilisha waumini wengi wao akinamama, kupiga risasi na kuua Waislamu kadhaa mwanzoni mwa mwaka 1998, katika Msikiti wa Mwembechai Jijini Dar es Salaam. Hayo yameelezwa na Sheikh Mussa Yusuf wakati akiongea na mwandishi wa NASAHA mara baada ya swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Kichangani Magomeni Mapipa Mei 26, mwaka huu. Awali, katika khutba yake ya Ijumaa, Sheikh Mussa aliwakumbusha Waislamu juu ya wajibu wao wa kutekeleza yake yaliyo mema na kukataza maovu. Akifafanua mada hiyo, Sheikh huyo alikhutubu kuwa utekelezaji wa hayo unatokana na amri ya Mwenyezi Mungu kwa hivyo ni ibada. Aliendelea kufafanua kuwa kama ilivyo kwa ibada zote, mwanadamu anahitaji kuongozwa kinafsi, ili maisha yake ya kimwili na mazingira yanayotawala maisha haya yapate kuongoka pia. Katika khutba yake hiyo aliwaeleza waumini waliohudhuria sala hiyo ya Ijumaa kuwa mafundisho ya dini yanakwenda sambamba na maisha yake, kwa sababu, alisema, Uislamu ni njia na mfumo kamili wa maisha ya mwanadamu hapa duniani. Sheikh Mussa alikazia nukta hiyo katika khotuba yake kwa kueleza kwa mantiki ya muongozo wa Qur'an, Muislamu anatakiwa ajishughulishe kikamilifu na masuala yote yanayohusu maisha ya kila siku ya mwanadamu ili kuwepo na mustkabali mwema kati ya maisha hayo na muongozo wa Mwenyezi Mungu ambao pia umejenga mwanadamu katika imani ya maisha mema ya amani na salama kati yake na mwenzie na jamii nzima ya wanadamu hapa duniani. Hivyo, alielimisha Sheikh huyo kwa kusema, kwa maana hiyo, ni jambo muhimu tena ni jambo la ibada kwa kila Muislamu kushiriki kikamilifu katika shughuli zote za kisiasa katika jamii aliyomo ili kuchangia haja ya kujenga mfumo wa utawala utakaongozwa na watu waadilifu wanaotambua haki na usawa kwa wanadamu wote. Viongozi ambao hawatodhulumu haki za binadamu wenzao kutokana na chuki zao za kidini dhidi ya wengine na kujipendelea wao kwa misingi hiyo. Hivyo aliwahimiza Waislamu walio waadilifu kujitokeza kwa wingi ili kugombea nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu ujao Oktoba mwaka huu. Aidha, aliwahimiza pia Waislamu kuhamasishana wao na wananchi wenzao kwa ujumla kujitokeza katika kujiandikisha na pia kuhakikisha kuwa wanapiga kura kuwachagua viongozi wawatakao miongoni mwa wale wenye sifa za uadilifu. Mara baada ya swala ya Ijumaa mwandishi wa habari hizi alimuuliza Sheikh huyo endapo Khutba yake haikuwa ni yenye kuchanganya dini na siasa tena Msikitini jambo ambalo limekuwa likishutumiwa na baadhi ya viongozi wa serikali na chama tawala. Sheikh huyo alijibu kuwa yeye kama Muislamu hajaona popote palipochorwa mstari wa katazo ndani ya Qur'an au katika muongozo wa Mtume (s.a.w.) unaotenganisha dini na siasa. "Hayo Bwana ni makatazo ya Biblia. Humo ndimo ilimoandikwa, ya Kaizari mpe Kaizari na ya Mungu mpe Mungu", alisema Sheikh huyo. Mbali na viongozi wa serikali kukemea 'kuchanganya dini na siasa', Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikiwatuhumu Waislamu kwa kuendesha siasa misikitini. Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Philip Mangula inadaiwa kuwa aliwatuhumu Waislamu kwa kuhongwa kanzu na kofia ili kuunga mkono vyama vya upinzani. Wakati Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho John Samwel Malecela amenukuliwa akiwaamrisha vijana wa chama hicho "kuwashughulikia" wale watakaochanganya dini na siasa Misikitini. Kuhusu tuhuma hizo, Sheikh Mussa alisema kuwa, maimamu walishakutana Dar es Salaam chini ya Shura inayoongozwa na Sheikh Mbukuzi kujadili kauli hizo za Katibu Mkuu wa CCM na za viongozi wengine wa chama hicho na kwamba Shura hiyo ya Maimamu ililaani kauli hizo na kukitaka chama hicho kiwaombe radhi Waislamu. Sheikh huyo alisema pia kwamba kuhusu kauli za hivi karibuni za Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Malecela, na zile alizodai kuwa ni propaganda zinazoendeshwa na baadhi ya vyombo ya habari pamoja na vile vya vinavyomilikiwa na CCM, ni kauli za kupuuzwa. "Hizi ni kauli za kupuuzwa tu, ni kauli za wanaoweweseka", alisema Sheikh huyo na kuongeza "hawa CCM walikutana kushangilia mauaji ya Mwembechai na kuipongeza serikali yao ... ukimwaga damu ya mwanadamu lazima ikusumbue kichwani na hivyo kukufanya uweweseke kwa madhambi ya kudhulumu uhai wa mtu". Hata hivyo, Sheikh Mussa alisema, pamoja na kuzipuuza kauli zao, Waislamu wanazifanyia kazi kauli za vitisho zinazotolewa na viongozi hao wa CCM. "Baada ya unyama wa kuvamia Msikiti wa Mwembechai na mauaji waliyoyafanya, Waislamu wote wamezipokea kauli zao za vitisho na kuzifanyia kazi... wanasubiriwa kwa hamu misitini, waje tu. Ulimwengu utashuhudia nguvu za wanyonge wa silaha lakini "ngangali" wa imani, kama ilivyokuwa katika vita vya Badri ambako makafiri wenye silaha kali waliangamia," alisema Sheikh huyo pasipo hamaki na kukataa kuongeza neno. Wakati huo huo, Imamu wa Msikiti wa Ubungo Darajani amewataka Waislamu kupuuza propaganda za CCM dhidi ya Waislamu na Uislamu. Aliyasema hayo katika hotuba yake ya Ijumaa ya Mei 26, mwaka huu ambapo aligusia habari iliyoandikwa kwenye gazeti moja linalomilikiwa na CCM eti kikundi cha Waislamu kutoka Mwanza kimo Moshi kwa ajili ya k uendesha ibada nchi nzima ili kuwahamasisha Waislamu kuwapigia kura Waislamu kwenye uchaguzi mkuu ujao. "Waislamu wanalazimika kuhamasishana nyumba hadi nyumba ili wapige kura kumwondoa madarakani yule aliyewadhulumu haki zao", alisema Sheikh huyo. Aliendelea kusema, Waislamu hawana tabia ya ubaguzi wa dini ndiyo maana wakati wa uhuru, walimwachia madaraka Mkristo akatawala. "Tunachotaka sisi Waislamu ni kiongozi muadilifu. Kama leo tunaikataa CCM siyo kwa sababu nyingine ila ni kushindwa kwa chama hicho kufanya uadilifu", alisisitiza Sheikh huyo. Alimalizia hotuba yake kwa kuwataka Waislamu kujiandikisha
kwa wingi wakati utakapofika na kisha kujitokeza kupiga kura ili kuiondoa
CCM madarakani na kuuweka utawala utakaojali haki sawa kwa wote.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Zanzibar wadai kuyumbishwa na Bara Serikali yatoa muelekeo wa Bajeti na kutangaza njaa Habari za ndani
SMZ haishughulikii mikarafuu -Maalim Seif Mwalimu Mkuu Msimbazi Mseto atishia kujiuzulu Hizi ni 'arobaini' za mapandikizi Waislamu Mbeya wamsusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA Masheikh wa BAKWATA waongoza sherehe za kuwasimika makamanda wa vijana wa CCM MAKALA
Makala
MPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
Ambari, Mwakipesile wajitosa kugombea DRFA |
|
|
|
|