NASAHA
Na. 050 Jumatano Mei 31 - Juni 5, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Zanzibar wadai kuyumbishwa na Bara 

Na Mwandishi wetu, Zanzibar 

WAKEREKETWA na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi upande wa Zanzibar wamelalamika kwamba mwenendo wa viongozi wa chama hicho toka Bara kutaka wagombea "wanaokubalika Bara bila kujali matashi ya Wazanzbar" unawayumbisha hali ambayo wamedai inaathiri nafasi ya chama hicho kushinda katika uchaguzi ujao na pia itauzorotesha muungano wa nchi mbili hizi uliodumu kwa miaka 36 sasa.

Aidha wana CCM hao wa Visiwani wamevishutumu vyombo vya habari nchini kwa madai kwamba vimekuwa vikitumika kupotosha demokrasia visiwani humo kwa kuyapuuza matashi ya Wazanzibar na badala yake "kuyanadi matashi ya viongozi wa CCM toka Bara". 

Wakereketwa hao wa CCM waliozungumza na gazeti hili mjini hapa wamesema uteuzi wa mgombea urais wa Zanzibar kwa tikiti ya chama hicho tawala unaelekea kutaka kutawaliwa na wanaCCM toka Bara. 

"Tumekwisha baini kwamba huko Bara wanamtaka Karume na wanayatumia magazeti yao yote kuonesha azma yao" alisema mmoja wa wakereketwa hao. 

Hivi karibuni magazeti kadhaa yanayochapishwa jijini Dar es Salaam yamekuwa yakiandika habari zenye kuonesha kwamba Bw. Amani Karume ndiye anayefaa kugombea urais wa Zanzibar na, kwa upande mwingine, magazeti hayo yamekuwa yakidai kwamba Dk. Mohamed Ghalib Bilal ambaye ni Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hafai kumrithi Dk. Salmin. Bw. Karume ni Waziri wa Mawasiliano katika serikali hiyo. 

Wakiongea katika maskani yao ambayo waliomba isitajwe gazetini kwa kile walichokidai kuwa "CCM Bara imejishikisha mpini" wana CCM hao wamesema wanafahamu kuwa kwa mujibu wa taratibu za chama chao Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar haina kauli ya mwisho juu ya nani agombee urais wa Zanzibar kwa tikiti ya CCM lakini wamedai itakuwa ni upuuzi wasiposikilizwa maoni yao. 

"Mwana CCM atakayefanikiwa kuchukua urais wa Zanzibar atafanya kazi zake za kila siku na sisi huku huku Visiwani, sasa kwa nini wang'ang'anie kutuletea mtu ambaye si ridhaa yetu... kama sio kutaka kutugonganisha na kuikwamisha Zanzibar ni nini basi?", alishangaa na kuhoji mmoja wa wanamaskani hao. 

Aidha, wameonya kuwa Wazanzibar siku moja watachoshwa na mtindo huu ambapo kila kinachotakiwa na Tanzania Bara lazima kitekelezwe Zanzibar. 

"Mambo haya yakiendelea na sisi tukasema sasa basi maana yake muungano haupo tena...", alitahadharisha mwana maskani mmoja ambaye wakati wote wa mazungumzo wenzake walikuwa wakimwita Mwalimu. 

"Tatizo la wenzetu Bara ni kuiona Zanzibar kama 'kijimkoa' tu cha Bara... lakini safari hii sisi wenyewe, vijana na wanawake tumeamua tutatembea nyumba hadi nyumba kuthibitisha (kwamba) Zanzibar sio mkoa", alitamba Mwalimu huyo. 

Tayari zipo habari mjini hapa kwamba kamati ya kuhamasisha kupitishwa kwa jina la Bw. Karume kugombea urais wa Visiwani imeundwa na wanaCCM wasio wazanzibar walioko Bara jambo amblo limewashitua wanaCCM Visiwani. 

"Kama ni kweli huyo (Bw. Karume) wanadai ndiye anayetakiwa na wananchi kuliko Bilal, iweje kamati yake ya uhamsishaji iundwe Bara", alihoji mwanamaskani mwingine. 

Mwalimu aliendelea kuonesha wasiwasi ni lazima upo mpango madhubuti wa kumpata mgombea wa CCM anayekubalika Bara kwanza bila kujali Wazanzibari wanamtaka nani. 

"Bila shaka lipo kundi kubwa zaidi nyuma ya hao wanaopiga kelele na nia yake ni kuona Zanzibar hakuna umoja, na Unguja na Pemba zinatenganishwa, alisema Mwalimu huyo wa maskani. 

"Wakiendelea hivi ni bora tuchague mpinzani ambaye amepitishwa huku huku kwetu (Zanzibar)", alisikitika mwana maskini mwingine. 

Wakizungumzia sababu za kumtaka Bilal, mmoja wa wanaCCM hao alisema: "...tulikuwa na Dokta (Salmin) na sasa tunataka Dokta tena (Dk. Bilal)...la kama sivyo basi tupewe Abdisalaam mwenye digrii mbili...". 

MwanaCCM huyo alisema kwamba Wazanzibar hawayataki maoni yaliyotolewa na Kanisa moja Tanzania Bara kwamba si lazima rais awe msomi wa chuo kikuu. 

"...sisi huku tumezoea madokta bwana, wao (Bara) hawajawahi kuongozwa na Profesa wala Dokta", alitamba mwanaCCM huyo. 

WanaCCM hao ambao wameonesha kupea katika siasa za hapa nchini wameyashutumu magazeti yanayochapishwa Dar es Salaam kwa kutaka kuonesha kuwa huenda Zanzibar ikampata mgombea wake nje ya taratibu za kidemokrasia na wakahoji kwamba ni kwanini magazeti hayo yasiandike kitu juu ya CCM Bara ambayo haikuruhusu wanaCCM wengine zaidi ya Rais Benjamin Mkapa wa kuchukua fomu ya kugombea urais muungano kwa tikiti ya chama hicho tawala. 

"Waandishi hawa wangejifunza demokrasia toka kwetu...watu wetu wote walikuwa huru kuchukua fomu na ndio sababu leo hii wapo wanaCCM watano wanaotaka kugombea urais, lakini kwao yupo (Rais) Mkapa peke yake...wanaCCM wa huko walikuwa wanatishwa na vijana", alisema mmoja wa wana CCM hao wakereketwa. 

"Watu wa magazeti wangefanya jambo la maana sana kama wangehoji ni vipi akina Kikwete, Malecela, na Bibi Mongela hawakujitokeza kuchuana na Mkapa", alisema mkereketwa huyo. 

Bw. Mrisho Kikwete na Bw. John Malecela mwaka 1995 walichukua fomu kuomba kugombea urais kwa tikiti ya CCM. Bw. Malecela alitolewa katika mchujo wa awali wakati Bw. Kikwete alishindwa na Rais Mkapa katika hatua ya mwisho. 

Mama Getrude Mongela, baaada ya kukamilisha kazi za kamati ya Umoja wa Mataifa iliyoandaa na kuendesha Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Wanawake uliofanyika Beijing China, 1995, alipata kunukuliwa na vyombo vya habari vya hapa nchini akisema kwamba yupo tayari kugombea urais. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Tahadhari ya Warioba juu ya rushwa isipuuzwe

Mkapa afanya ziara Pwani

CCM ‘inaweweseka’ - Sheikh

Zanzibar wadai kuyumbishwa na Bara

Serikali yatoa muelekeo wa Bajeti na kutangaza njaa

Habari za ndani
Wapinzani kusimamisha mgombea Urais mmoja 

SMZ haishughulikii mikarafuu -Maalim Seif

Mwalimu Mkuu Msimbazi Mseto atishia kujiuzulu 

Hizi ni 'arobaini' za mapandikizi

Waislamu Mbeya wamsusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA 

Masheikh wa BAKWATA waongoza sherehe za kuwasimika makamanda wa vijana wa CCM 

Wakristo waishitukia CCM

MAKALA
Dini na siasa haviwezi kutenganishwa

Makala 
Mikutano ya Prof. Lipumba 'yaendelea' baada ya kuondoka 

MPASHO NASAHA
MATATA! MATATA!

Kalamu ya Mwandishi 
Wapinzani epukeni patupu 

MAKALA
CCM na sera za maendeleo (6)

Habari za Kimataifaza Kimataifa

Lishe 
Supu na umuhimu wake mwilini

BARUA

MASHAIRI

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra - 4 

MICHEZO

  • Uchaguzi Yanga Julai
  • BATA yahimiza usajili michezo
  • 'Simba SC, Singida United baba mmoja mama mbali mbali' 
  • Tarimba akalia Kuti Kavu Yanga

  • Ambari, Mwakipesile wajitosa kugombea DRFA
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita