|
Mashairi
Siku ya kupiga kura...
Chagua chama cha haki, chenye mwelekeo bora,
Usikichague hiki, kiletacho ufukara,
Fahamuni halaiki, twaeni ninayochora,
Siku ya kupiga kura...........
Chama chao simurua kwa sasa kinadorora,
Cha nini kukichagua, wengi watu chatukera,
Mimi nimeshaamua, wallah sikipi kura,
Siku ya kupiga kura...........
Chama ni cha-wananchi, waliojaa subira,
Umoja hawauachi, na hawana masihara,
Fanya kije shika nchi, Tanzania ije ng’ara,
Siku ya kupig akura............
Chanyanyasa dini yetu, kila mara kila mara,
Chabugudhi watu wetu, hawapatiwi ajira,
Mwembechai ndugu zetu, wengine wapo akhera,
Siku ya kupiga kura............
Chagua haki ni yako, nchi ije tia for a,
Ulete mabadiliko, tuje pata mpya sera,
Fukuza masumbuko, tuwe nawatu imara,
Siku ya kupiga kura.........
Chama chao kile chama, kwa sasa hakina dira,
Chatetea udhuluma ndanimwe kina madhara,
Maamuzi ni yaumma, wa Visiwanina Bara,
Siku ya kupiga kura..........
Chukua yako shahada, ukiacha ni hasara,
Uwe kakaau dada, tumia yako busara,
Fanya usijali muda, itambe yetu bendera,
Siku ya kupiga kura............
Ustadh: Hassan Habibu Shindo,
S.L.P. 25100,
Kipawa, Dar es Salaam.
Hongera Ibrahim
Nakuombea kwa Mungu, akupege afya njema,
Akulipe lako fungu, leo na kesho kiama,
Asije kupa machungu, duniani kulalama,
Hongera baba hongera, Mema tunakuombea.
Hongera kwa kuchukua, bila mtu kukukera,
Fomu ya chama sikia, hivyo ndiyo barabara,
Na sisi tunakwambia, kwa hakika unang‘ara,
Hongera baba hongera, mema tunakuombea.
Hongera twakupa heko, kukubali kugombea,
Kwetu sisi ni kicheko, daima twakuombea,
Na hatuna mshituko, ushindi tajibebea,
Hongera baba hongera, mema tunakuombea.
Lipumba baba sikia, twakuombea Rabuka,
Hilo tunakuambia, usijekuwa na shaka,
Kura tutakutilia, Ikulu tutakuweka,
Hongera baba hongera, mema tunakuombea.
Ikulu inanukia, kwa hilo tuna hakika,
Dua tunaitikia, usijeingia shaka,
Uende huko kwa nia, Ikulu upate fika,
Hongera baba hongera, mema tunakuombea.
Na sera za chama chako, ni nzuri twakuambia,
Haki sawa ikiweko, wanyonge twafurahia,
Tutakuwa na kicheko, katika hii dunia,
Hongera baba hongera, mema tunakuombea.
Dhuluma ikiondoka, hapa kwetu Tanzania,
Amani itapofika, wote watafurahia,
Taishi kwa uhakika, mazao tajivunia,
Hongera baba hongera, mema tunakuombea.
Uhasama utaisha, kwa wananchi sikia,
Kwa furaha na bashasha, mashambani taingia,
Nasi tutaimarisha, uchumi taendelea,
Hongera baba hongera, mema tunakuombea.
Wewe mkombozi wetu, wanyonge tatutetea,
Wewe ndiye ngao yetu, hapa petu Tanzania,
Wewe ndo kioo chetu, tunachojiangalia,
Hongera baba hongera, mema tunakuombea.
Naweka kalamu chini, hapa ninaishilia,
Imeningia huzuni, tungo hizi kuishia,
Sijui nifanye nini, hamu haijanishia,
Hongera baba hongera, mema tunakuombea.
H.S.B.
Ummul Jamilah
(Safarini- Ngara Kagera).
Eti na yeye ngangari!!
Kawaida ya kichaa, hajui alifanyalo,
Kelele hujipigia, silo na lile liwalo,
Na watu wakisikia, humdharau kwa hilo,
Kwa vile wameshajua, hana mamlaka nalo.
Husubiri kwa wengine, waanzishwe mambo yao,
Kisha ye ajilingane, kama vile ni mwenzao,
Haanzi kitu chengine, ajifananisha nao,
Akili yake si nene, imeshavikwa pumbao.
Anajiona hodari, kuiga visivyo vyake,
Anajifanya ngangari, wakati si hadhi yake,
Hadhi yake chorichori, kulikojaa makeke,
Kama ni mporipori,asojua hali zake.
Lipojifanya ni wani,wengine hawakuiga,
Kajitapa uwanjani, hakuna alojimwaga,
Kawaona hawa nani, bure wanajikoroga,
Sasa hivi taabani, amevaliwa na woga.
Sasa amekuwa sawa, na aliye mfa maji,
Mno huchanganyikiwa, huweka kando ugwiji,
Apate kujiokowa, Roho bado ataraji,
Ili asijeuwawa, maisha ayahitaji.
Woga umeshamvaa, abaki kutapatapa,
Hana pa kushikilia,wengine anaogopa,
Ushindi wasijetwaa, na yeye wakamtupa,
Amebaki kuduwaa,akili zimemgwaya.
Akili zimemduru, sawa sawa na kichaa,
Hata kufanya kufuru, haoni kizaazaa,
Amegeuka kunguru, kazi nyakuanyakua,
Na sasa kawa ngumbaru, kuiga asoyajua.
Eti aona fahari, kujigamba hadharani,
Kwamba na yeye ngangari, namba wani kahaini,
Ameshaona hatari, iliyokaa mbeleni,
Atakikosa kiriri, aingie hamkani.
Matokeo mpya hana, amebaki uchakavu,
Na hali anavyoona, hanao tena ubavu,
Hatoweza kushindana, katoa macho makavu,
Hata mchozi hayana, sawa na ya kipumbavu.
Kila pembe kitazama, wenzake metamalaki,
Hayamkalii vyema, moyo unataharuki,
Aona sasa kiyama, karibu kumhiliki,
Na kuachia mchuma, hapo ndipo hapataki.
Kuuachia mchuma, ndiyo kunampa joto,
Wadudu wanamchoma, wanamuwashia moto,
Yu ovyo mtu mzima!, kakaa kama mtoto,
Kiona watu wavuma, hajui wana mvuto
Alianza kisonono,eti ameshitukia,
Sera ya jino kwa jino, kelele kaipigia,
Na sasa na yeye yumo, kwa mbali aitumia,
Ameshaona mchomo, dira imempotea.
Dira imemgeuka, hajui muelekeo,
Bure anahangaika, haoni mafanikio,
Kisunzi kimemshika, aona maruoruo,
Ajihisi kuanguka, akiangue kilio.
Ungangari wa wenyewe, si kila anotamani,
Kisikupate kiwewe,cha kujitia kundini,
Haufanani na wewe, katulie maskani,
Subiri uenguliwe, mwenyewe ukasaini.
Na pia twasisitiza, mara hii nasi tumo,
Uovu ataefanza, atakipata kibano,
Akome kutuchokoza, huo ndio msimamo,
Hatujui bembeleza, sera ni jino kwa jino.
KIGONGO WA KIGONGO,
DAR ES SALAAM.
Ua letu mechanua
Kwa jina lake azizi, utungo ninaanzia,
Namuomba anienzi, mazuri kusimulia,
Nisipate makerezi, lengo kutolifikia,
Ua letu mechanaua.
Mepita mingi miezi, tuko twalisubiria,
Tungekuwa na majonzi, kama letu lingevia,
Tunamuomba Mwenyezi, aweze kutulindia,
Ua letu mechanua.
Uzuriwe kichochezi, kwa rangi zilotulia,
Huhitaji mliwazi, unapoliangalia,
Waweza lifanya vazi, ukawa wajipambia,
Ua letu mechanua.
Hili kwetu changilizi, muhimu kulitumia,
Yawe kwetu mazoezi, maji kulimwagilia,
Ziwe kwetu simulizi, uzuri kulisifia,
Ua letu mechanua.
Nzuri sana harufuzi, na rangi zake sawia,
Haihitaji kurunzi, usiku kulangalia,
Sio kubwa kama nazi, wala so la kijinsia,
Ua letu mechanua.
Tuvibane vikohozi, silifanyie udhia,
Tutafute wapgazi, weweze kutuchumia,
Tuwatafutie ngazi, darini tutundikia,
Ua letu mechanua.
Ni lazima tulienzi, mazuri kulifanyia,
Naapa kamwe siwezi, ubaya kulirushia,
Hizi saba zangu beti, maneno namalizia,
Ua letu mechanua.
Na: Abu Maryama wa Mfaki,
S.L.P. 2700,
Dar es Salaam.
Dini na siasa
Fisadi imeshamiri, naja humu niwaonye,
Mashehe wakihubiri, chama kile tukisonye,
Hovyo wayatafusiri, ya siasa yasipenye,
Kwanini tusichanganye, dini yetu ni siasa?
Dini yetu na siasa, kwanini tusichanganye,
Qur’ani yatuasa, mafisadi tuwabinye,
Ibrahimu na Mussa, walilani mabwenyenye,
Kwanini tusichanganye, dini yetu na siasa?
Kitabu cha Qur’ani, kimekuja kituonye,
Twatakiwa Duniani, amani nzuri tufanye,
Na siasa imo ndani, wapotevu truwaonye,
Kwanini tusichanganye, dini yetu nasiasa?
Hizo ni propaganda, njama zao tuziminye,
Wasipende wakipenda, hila yao tuifinye,
Tusiache kuiponda, hadharanituwaonye,
Kwanini tusichanganye, dini yetu na siasa.
Dini yetu ina HOJA, imekuja ituponye,
Mwenyezi Mungu mmoja, hana mwana karikenye,
Na MUHAMADI ni mja, sio Mungu tumfanye,
Kwanini tusichanganye, dini yetu nasiasa?
Tumesha kuwagundua, njama zao kina Mwenye,
Nchini watubagua, elimu tusiifanye,
Mwembe Chai wameua, na CHUKI wasimponye,
Kwanini tusichanganye, dini yetu na siasa?
Ustadh: Hassan Habibu Shindo,
S.L.P. 25100,
Kipawa,
Dar es Salaam.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Tahadhari ya Warioba
juu ya rushwa isipuuzwe
Mkapa
afanya ziara Pwani
CCM
‘inaweweseka’ - Sheikh
Zanzibar
wadai kuyumbishwa na Bara
Serikali
yatoa muelekeo wa Bajeti na kutangaza njaa
Habari za ndani
Wapinzani
kusimamisha mgombea Urais mmoja
SMZ
haishughulikii mikarafuu -Maalim Seif
Mwalimu
Mkuu Msimbazi Mseto atishia kujiuzulu
Hizi
ni 'arobaini' za mapandikizi
Waislamu
Mbeya wamsusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA
Masheikh
wa BAKWATA waongoza sherehe za kuwasimika makamanda wa vijana wa CCM
Wakristo
waishitukia CCM
MAKALA
Dini
na siasa haviwezi kutenganishwa
Makala
Mikutano
ya Prof. Lipumba 'yaendelea' baada ya kuondoka
MPASHO NASAHA
MATATA!
MATATA!
Kalamu ya Mwandishi
Wapinzani
epukeni patupu
MAKALA
CCM
na sera za maendeleo (6)
Habari
za Kimataifaza Kimataifa
Lishe
Supu
na umuhimu wake mwilini
BARUA
MASHAIRI
RIWAYA
Mapinduzi
ya fikra - 4
MICHEZO
Uchaguzi Yanga Julai
BATA yahimiza usajili michezo
'Simba SC, Singida United
baba mmoja mama mbali mbali'
Tarimba akalia Kuti Kavu
Yanga
Ambari, Mwakipesile wajitosa
kugombea DRFA
|