|
Na. 050 Jumatano Mei 31 - Juni 5, 2000 |
|
|
|
|
|
Mikutano ya Prof. Lipumba 'yaendelea' baada ya kuondoka MIKUTANO isiyokuwa rasmi ya vigenge vya wananchi yenye kuzungumzia ziara na hotuba za Mwenyekiti wa chama cha wananchi (CUF) Mhe.Prof. Ibrahim Lipumba imekuwa inafanyika katika sehemu mbalimbali alizotembelea na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara hata baada ya yeye kuondoka katika maeneo hayo. Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa katika maeneo ya mkoa wa Pwani, Morogoro, Tabora na hapa jijini umebaini kuwepo kwa mikutano hiyo ya vigenge vya wananchi, yenye kuzitathmini na kuzitafakari hotunba hizo za Prof. Lipumba na kupanga mikakati ya kutekeleza yale yaliyomo ndani yake ambyo yalikuwa ni maagizo aliyowaachia. Hotuba ya Mwenyekiti huyo wa CUF ambaye ndiye mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba, zimekuwa zikiwavuta sana wananchi wa rika na jinsia tofauti kutokana na uchambuzi wake wa kina wa masuala mbalimbali yanayowagusa wananchi hao kulingana na hali ha nchi ilivyo hivi sasa. Uchambuzi huo ambao huambatana na takwimu zenye kuonesha wapi makosa yametendeka na namna gani wao (CUF) watarekebisha wakiingia madarakani umekuwa mwangaza na matumaini mema kwa wananchi wengi, na pia umekuwa msumali NGANGALI unaoonekana ngumu kung'olewa na hoja za kambi ya chama tawala. Akiongea na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina lake gazetini kigogo mmoja wa CCM Wilayani Kilombero alisema ilibidi wao waahirishe mkutano wao ili kumsikiliza Prof. Lipumba na baadaye waangalie kama wanaweza kuzikanusha hoja zake watakapofanya mkutano wao. "Lakini hoja za huyu Bwana hazijibiki. Kwa kweli kwa haraka haraka hamna kiongozi (wa CCM) anayeweza kujibu hoja hizi", alisema. "Zile takwimu za afya alizotoa kuwa wakati wa Mwinyi alitenga bilioni 27 kwa kununulia madawa kwenye hospitali zetu na kwamba zilikuwa hazitoshi, lakini Mkapa kashusha mpaka bilioni 4, hata mimi binafsi zimenichoma. Je, itakuwaje kwa wananchi wa kawaida ambao hali zao kiafya ni duni, hospitali hazina dawa na hapo hapo wanaona viongozi wa CCM na serikali wakitibiwa nje ya nchi", alisema kigogo huyo wa CCM kisha akamalizia, "ndio maana Bwana huyu amekomba matawi yetu mengi mazima mazima hapa Ifakara." Katika soko kuu la Ifakara NASAHA iliwakuta wauza mitumba wakiwa kwenye 'mkutano' mzito wakiijadili hotuba ya Prof. Lipumba aliyoitoa kwenye viwanja ya Kiungani mjini hapo, ambapo aliwaeleza wakazi hao kuwa umasikini wa vilaya hiyo unatokana na uongozi mbovu katika nchi. Kwani wilaya hiyo ina kila hazina ya maliasili pamoja na mito mikubwa ifaayo kwa kilimo cha umwagiliaji maji. "Sikiliza mwanangu, mimi nakubaliana na Lipumba moja kwa moja. Wewe angalia badala ya maji ya mito kutumika kwa ajili ya kilimo na kutoa nguvu za umeme, yanatuua wakati wa mafuriko", alisema kijana aliyejitambulisha kwa jinamoja tu lamkato la Sele. "Hawa mwisho wao mwezi wa kumi tu? Lazima tuwang'oe bwana. Inakuwaje tuteseke ilihali nchi yetu inaneema mradi wasituibie kura zetu. Hata hivyo tutazilinda kingangali", alisema kijana mwingine aitwaye Dagan. Mjini Morogoro katika barabara iendayo Bomani (maarufu kama Boma Road) NASAHA iliwakuta wazee waliokuwa wanazungumzia hotuba ya Lipumba na hamasa za vijana wa CUF katika mji huo. Wazee hao walisema kuwa kweli historia ya Morogoro kuwa ndio nguzo ya harakati za ukombozi inajirudia. Walisema kuwa wakati wa kupiginia uhuru Wakoloni waliweka mapandikizi wao mkoani humo lakini walishindwa. Walisema kuwa sasa wanafurahi kuona vijana wao wako mstari wa mbele kupigania kile kilichopiganiwa na wazee wao ambacho ni uhuru na maendeleo. "Tulipigania uhuru na maendeleo lakini CCM wamevurunda.Vijana wetu wameamua kuweka mambo sawa", alisema Mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Salum. Mzee mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Baba Koba alisema kuwa yeye alishangazwa na mkoa huo uliojaa rutuba kuingia njaa kiasi cha watu zaidi ya 50 kufa kwa njaa katika Wilaya ya Ulanga mwaka jana. "Uongozi gani bora unaosababisha uduni wa maendeleo mpaka watu wnakufa kwa njaa katika mkoa ambao una rutuba nyingi kama huu, alisema kwa kuhoji Mzee huyo huku uso wake ukijaa huzuni. Mazungumzo ya aina hiyo yametanda pia katika maeneo mengi ya mji wa Morogoro. Soko Kuu, Soko la Saba Saba, Mji mpya, Stendi ya Msamvu kote huko mjadala ilipamba moto. Huko Tabora wanafunzi wa shule mbalimbali za mjini hapo walisema kuwa wamefarijika sana na ziara ya Lipumba katika mkoa wao na kwamba wamemuelewa barabara. Wakaongeza kuwa watakapokwenda likizo kwenye maeneo yao wataufikisha ujumbe wake ili aweze kupigiwa kura na kuchaguliwa kuwa rais wa nchi hii. Nao wazee na wananchi wa maeneo mbalimbali ya mji huo walimueleza mwandishi wa NASAHA kuwa kipindi cha kupumbazwa wananchi wa Tabora kimepita. Walisema kuwa mara baada ya ziara ya Prof. Lipumba kumekuwepo ujumbe wa kila aina uliotembela mikoa huo kwa nia ya kupiga propaganda za kuwapumbaza wananchi dhidi ya ukweli wa yale aliyoyasema Prof. Lipumba lakini wamekwama. "Tabora ni mkoa mama wa mapambano na sasa utakuwa chimbuko la kufagia vumbi lililokuja kuvuruga matunda yetu ya uhuru", alisema Mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Jabu. Hapa jijini NASAHA ilitembelea huko Mbagala siku chache baada ya CUF kufanya mkutano mkubwa uliohutubiwa na Prof. Lipumba kwenye maeneo ya Kichemchemu. Nje ya kibanda cha kunyolea nywele kiitwacho "Classic Hair Cutting Salon" kilichopo Zakhem iliwakuta vijana kadhaa wakiendeleza 'mkutano' wa Mwenyekiti huyo wa CUF. Vijana hao walikuwa wamebarizi katika eneo hilo. Katika maongezi yao walimwelezea Lipumba kama mtu ambaye ameifanya siasa kuwa ukweli kwani huko nyuma wanasiasa waliopita muda mwingi wawapp majukwaani walikuwa hawaelezi sera na mikakati ya wazi ya kuwakomboa wananchi na hasa vijana. Mbali ya kuvutiwa na ufasaha wa Prof. Lipumba katika hotuba zake, vijana hao walisema kuwa wao walitiwa moya sana na jinsi Prof. Lipumba kuonesha kuwa anayajua matatizo yao. Kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Beka alisema kuwa yeye 1995 hakupiga kura kwa kuwa alikuwa na umri wa miaka 16, na kuahidi kuwa mwaka huu atapiga kura na anajua nani wa kumpa. "Sisi tuko hapa jobless kuanzia saa 6 tunapiga stori tu, utadhani nchi yetu maskini kiasi cha sisi kukosa ajira.Tukiwaomba passport tukabangaiza nje ya nchi hawataki.watu gani hawa wasio kuwa na huruma?" alihoji kijana huyo, akitiikiwa na wenzie waliosema,"Lipumba chukua nchi tupone, mwanangu." Nao wananchi kadhaa wa Mbagala wamesema kuwa Wilaya yao ina uzoefu wa kutembelewa na wanasiasa wengi. Hivyo walidai kuwa wanauzoefu wa kuchambua hotuba za kweli na zile za propaganda za hovyo. "Wananchi wa Wilaya ya Temeke tunauzoefu mkubwa na mwamko wa kutosha kuwatambua wanasiasa walio bora", alisemaMzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Msham. "Mzee Mwinyi aliposhika madaraka aliikuta nchi katika hali ngumu kuichumi, kiasi cha wananchi kutumia majani ya mapapai kama sabuni. Baada ya miaka michache ya utawala wake chini ya ushauri wa uchumi wa Prof. Ibrahim Lipumba mambo yalikuwa mazuri hadi kuwepo kwa Supermarket za magari wakati huko nyuma hata unga ulikuwa bidhaa adimu", alisema mkazi mwingine wa Mbagala Bw. Mbonde Hashim. Naye Juliwa Semili akaelezea matatizo wanayopata vijana kutoka kwa polisi mara kwa mara wakidaiwa kuwa ni wazuralaji na kwamba hawana vitambulisho. "Viongozi wenyewe wa serikali wanajua nchi hii maskini ajira hakuna sasa watoto wetu tuwapeleke wapi", alisema Bw. Juliwa na kuongeza," Sisi hata mtaji wa biashara au kilimo hatuna". Tatizo la ajira kwa vijana lilikuwa mada kuu ya mazungumzo mengi katika "vijiwe' mbalimbali maeneo ya Ilala kuhusu hotuba ya Prof. Lipumba aliyoitoa Bungoni wakati wa ziara yake Wilayani Ilala. Prof. Lipumba alionesha kusikitishwa na tabia ya kuwa kamata Vijana na kuwafungulia mashtaka ya "uzururaji". Prof. Lipumba alihoji "vipi kijana azaliwe Ilala, akulie Ilala, kisha akamatwe kwa kuzurura Ilala?" Prof. Lipumba alisema kuwa tatizo la vijana siyo uzururaji bali ni ukosefu wa ajira. Na kwamba wao wasiadhibiwe kwa kukosa ajira bali serikali ilaumuwe kwa kutotoa ajira kwa vijana. Wakati huo huo wananchi kadhaa kutoka maeneo ya Rufiji, Kibaha, Mlandizi, Chalinze, Kisarawe na Mkuranga ambao huja mjini kila wiki kwa shughuli za kibiashara, wamedai kuwa katika myao "wamevamiwa" na vikundi vya kuendesha propaganda dhdi ya Prof. Lipumba. Wananchi hao waliozungumza na NASAHA nyakati mbalimbali wamedai kuwa Prof. Lipumba ni "mdini" na hivyo hafai kuongoza nchi. Wananchi hao hata hivyo wameeleza kwamba propaganda hizo "zimeshtukiwa" na wakazi wengi wa maeneo hayo ambao ni Waislamu. Wananchi hao wamesema kuwa wao wanajua maana ya udini katika siasa za nchi hii. Wameeleza kuwa anaetaka kujua zaidi asome kitabu cha Padri Sivalon kinachozungumzia jinsi Kanisa Katoliki lilivyoingia kwenye siasa za Tanzania Bara na hivyo kuwahujumu walio wengi kwa manufaa yao wakatoliki na kanisa lao. Mmoja wa wananchi hao ambaye alikuwa na kitabu hicho kiitwacho: Kanisa Katoliki na Siasa za Tanzania Bara 1953-1985, alidai kuwa katika kitabu hicho kumeandikwa kuwa Muislamu na Uislamu ni adui mkubwa. "Hivyo, propaganda hizi za kumponda Lipumba ambaye ni Muislamu tunazijua chimbuko lake", alisema Bwana huyo, ambaye alidai kuwa anatoka Kisarawe. Mwananchi mwingine aliyesema kuwa yeye ni mfanya biashara ndogo ndogo kutoka Rufiji alisema kuwa wao wanazitambua sana propaganda hizo na kwamba hata asili ya vikundi hivyo pia wanaijua. "Sisi bwana vikundi hivyo tunavijua, na hata jina lao tunalijua, kule kwetu Rufiji wanaitwa 'Uwawaru' na baadhi ya wafadhili wao tunadhani ni hao aliowataja Padre Sivalon", alisema bwana huyo aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Ali. Nao vijana kadhaa wafanyabiashara kutoka maeneo ya Kibaha na Mlandizi ambao walizungumza na NASAHA katika maeneo ya soko la Tandale walikiri kuwepo kwa vikundi hivyo katika maeneo yao. Walidai kuwa baadhi ya vikundi hivyo vina baiskeli walizo fadhiliwa na watu wa 'dini' ambayo siyo Islam. Vijana hao ambao hawakupenda kutaja majina yao, walikataa kutoa ufafanuzi zaidi juu ya madai yao na kumtaka mwandishi aende "akajionee mwenyewe", huko Pwani. Huko Mafia nako mazungumzo na mijadala ilitanda kila sehemu. Majumbani, vibarazani, magengeni na pwani hususan Kilindoni. Katika maneo mengi watu wa Mafia walikuwa wakihoji kipi kilichofanywa na CCM katika Wilaya hiyo ya Kisiwa tangu nchi hii ipate uhuru miaka 40 sasa. Walitaja matatizo chungu nzima ambayo bado yanawakabili, ikiwemo afya usafiri na elimu. "Mafia hatuna hospitali kama ilivyo wilaya nyingine. Usafiri wa kwenda Tumbi au Muhumbili haupo . Wao wenzetu wanatibiwa Ulaya wanategemea mtu na mgonjwa wake waaogelee hadi Dar es Salaam au Kibaha?", alisema Bwana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Hashim. Bwana mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Shahame alisema kuwa yeye alishangazwa na ujasiri wa baadhi ya viongozi wa serikali kuwa na "USO" wa kuwatazama wananchi wa Mafia na kutamba kuwa wamewapelekea maendeleo wakati si kweli. Mwananchi huyo mkazi wa Bweni alisema kuwa Mafia kama Wilaya ina rutuba ya kutosha na mali asili nyingi ya baharini. Wananchi wake si wavivu, na alidai kuwa wamekuwa wakichangia hazina ya serikali kwa kodi na michango ya kila aina. Lakini, alilalamika mwananchi huyo kwamba serikali imewatupa. "Wilaya mzima kwa miaka zaidi ya 30 serikali imeshindwa kutujengea hata shule moja ya sekondari wakati Wilaya nyigine zina shule hadi 10", alisema Bwana huyo na kuongeza, "leo Mafia tuna shule moja ya sekondari iliyotokana na sisi wenyewe wananchi kujitolea, ipi ya serikali?" alisema kuwa amesikitishwa na hali ya kisiwa hicho kuachwa nyuma kielimu. Alidai kuwa hali hiyo ni mbinu ya kuwakandamiza wananchi hao ambao wengi wao ni Waislamu, akimaanisha kuwa ukandamizaji ni wa kiudini. Tunasikia uliletwa msaada kwa wananchi wa Mafia toka Falme za Kiarabu kutujengea shule kubwa mbili, ya wasichana na wavulana lakini, serikali imekataa kuupokea", alisema Bwana huyo. Wiki ijayo tutawaletea wasemavyo wananchi wa
Turiani, Dodoma, Kondoa na Singida.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Zanzibar wadai kuyumbishwa na Bara Serikali yatoa muelekeo wa Bajeti na kutangaza njaa Habari za ndani
SMZ haishughulikii mikarafuu -Maalim Seif Mwalimu Mkuu Msimbazi Mseto atishia kujiuzulu Hizi ni 'arobaini' za mapandikizi Waislamu Mbeya wamsusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA Masheikh wa BAKWATA waongoza sherehe za kuwasimika makamanda wa vijana wa CCM MAKALA
Makala
MPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
Ambari, Mwakipesile wajitosa kugombea DRFA |
|
|
|
|