|
Na. 050 Jumatano Mei 31 - Juni 5, 2000 |
|
|
|
|
|
Wapinzani epukeni patupu NA MAALIM BASSALEH WACHUNGUZI wa mambo ya siasa wanaona kuwa bila ya kambi ya upinzani kuungana na kusimamisha mgombea mmoja wa kiti cha urais, uwezekano wa kuishinda CCM, katika uchaguzi mkuu ujao, wa mwaka 2000, ni mdogo sana. Na karibu viongozi wote, wa vyamavya upinzani wanakiri hilo. Kwa nini basi wapinzani hawakubali, kuungana na kusimamisha mgombea mmoja tu? Jawabu la mkato kwa swali hilo ni kuwa, katika kambi ya upinzani, kuna baadhi ya viongozi waliotawaliwa na ubinafsi. Utamkuta kiongozi ameshupaa hataki kusikia jina la kiongozi mwingine wa kambi ya upinzani anatajwa kuwa anafaa kugombania nafasi hiyo. Anajiona ni yeye tu peke yake ndiye anayefaa. Kwa mfano kuna Mheshimiwa mmoja anaunga mkono wazo la kusimamisha mgombea mmoja wa kiti cha urais, kwa kambi ya upinzani. Amekwisha tamka mara mbili tatu kuwa bila ya kuungana ni ndoto kwa chama cho chote cha upinzani, katika hali hii ya sasa, kuweza kushinda kama kitasimamisha mgombea wake wenyewe. Na hilo ni kweli. Lakini, mheshimiwa huyo kila akizungumzia juu ya jambo hilo amekuwa akilihitimisha kwa kudai kuwa hakuna anayefaa kugombea kiti hicho, katika kambi ya upinzani, isipokuwa yeye tu. Kwa kauli yake hiyo ni dhahiri kuwa mheshimiwa huyo hataki wapinzani waungane, ili wasimamishe mgombea mmoja wa kiti cha Urais, bali inaonekana achokitaka yeye ni wapinzani waungane kumuunga mkono yeye awe ndiye mgombea pekee wa kiti hicho, kwa upande wa upizani! Jee! Kama huo si ubinafsi ni nini? Anayetaka kweli wapinzani waungane, hawezi kukimbilia kuanza kujipigia debe, yeye mwenyewe, bila ya kwanza, kufanya juu chini,kuvihamasisha vyama vya upinzani kuunda umoja baina yao. Waswahili hawakukosea waliposema, "chema chajiuza, kibaya chajitembeza!" Mtu anapopita huku na kule, akijigamba na kujisifu, kuwa yeye ndiye mwema, amefanya hili na lile anadhani Waswahili watamwelewaje? Niwazi kuwa watamdharau na kumwona ni mpuuzi. Kiongozi mmoja wa kambi ya upinzani, ambaye kiutendaji, alikuwa karibu sana na mheshimiwa huyo mwenye ubinafsi, na ambaye hivi karibuni amerudi CCM, amesema baadhi ya viongozi wa upinzani hawana cho chote wanachokitaka isipokuwa ni kulilia kuingia Ikulu tu, bila ya kuelewa wanachotaka kukifanya huko Ikulu. Ni wazi kuwa kiongozi huyo alikuwa akizungumzia juu ya yule mheshimiwa mbinafsi.Kwa sababu Mheshimiwa huyo hana lo lote analolitaka isipokuwa kuingia Ikulu na kuwa rais wa "inji" hii. Ni hivi juzi tu mheshimiwa huyo amekaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa yeye hatarudi CCM labda mpaka aahidiwe kuwa atapewa urais wa inji hii. Kumbe yeye tatizo lake siyo CCM na sera zake, bali ni kutaka kuwa Rais, kwa hali yo yote ile. Kama kweli wapinzani wanataka kuiondoa madarakani CCM, hawana budi kuunganisha nguvu zao na kusimamisha mgombea mmoja tu wa kiti cha Urais. Vinginevyo wataambulia patupu. Chama kitakachong'ang'ania kusimamisha mgombea wake, peke yake ijue kuwa kitaziharibu tu kura za Watanzania. Penye umoja pana ushindi. Baniani alisema, "Dogo dogo mingi nashinda kuba moja!", na wahenga walikwisha tamka, "umoja ni nguvu, na utengano ni udhaifu!" Jambo la kustaajabisha ni kuwa juu ya kwamba wapinzani wanatakiwa waungane, lakini anachomoza kiongozi kutoka katika kambi hiyo hiyo ya upinzani na kukishutumu chama cha kambi hiyo hiyo. Jambo hilo linavunja moyo sana. Kwa mujibu wa habari zilizoandikwa kwenye gazeti moja kongwe,linalotoka kila Jumapili, zimemkariri kiongozi mmoja wa chama kimoja cha upinzani akidai kuwa chama chake hicho hakiwezi kushirikiana na vyama vingine vya upinzani kusimamisha mgombea mmoja wa urais, eti kwa sababu baadhi ya vyama kama CUF vina udini. Gazeti hilo limesema kuwa kiongozi huyo amedai kuwa watu wanakishutumu chama cha CUF kuwa kina udini, na kwa vile chama chake kinapinga udini na ukabila basi chama chake hicho kikishirikiana na CUF watu wao watachukia. Ingawa kiongozi huyo amedai kuwa kuna watu wanaotoa shutuma za udini dhidi ya CUF lakini hakuwataja hao wanaotoa shutuma hizo, wala hakutoa ushahidi wo wote unaothibitisha madai yake hayo. Inaonekana kuwa huo ni mkakati maalumu ulioandaliwa ili kukipakazia tu chama hicho cha CUF. Na ilivyoelekea ni kuwa kila chama kinachoonekana kinapata kasi ya kukubalika na watu, basi, upesi upesi kuna watu waliokabidhiwa jukumu la kukipaka matope chama kama hicho. NCCR-Mageuzi ilipoundwa mwanzo tuliambiwa kuwa ni chama cha Wajaluo. Lakini baadaye Mheshimiwa Augustine Lyatonga Mrema alipotoka CCM na kujiunga na chama hicho watu wengi nao walitoka CCM na kumfuata Mrema. Na Wachaga wengi nao wakamfuata. Lakini katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 1995 NCCR-Mageuzi ilipoonekana imekuwa tishio kwa CCM basi watu hao hao walianza kukipakazia chama hicho eti kilikuwa ni chama cha Wachaga! Basi na CUF ilipoanzishwa Wapemba wengi na baadhi ya Waunguja wachache ndio waliokiunga mkono, tukaambiwa chama hicho ni cha Wapemba. Ingawa CUF ni chama cha kisiasa si cha kidini, na kinaungwa mkono na Watanzania wa dini na rangi mbalimbali, lakini kwa vile safari hii kimeanza kukubalika na kuungwa mkono na Watanzania wengi wa Bara, na kuonekana kimekwisha kuwa ni tishio kwa CCM katika uchaguzi mkuu ujao wa 2000, basi tayari wale watu wenye kazi yao wameanza kazi yao ya kukipakazia chama hicho eti ni chama cha Waislamu! Lakini ni kweli chama cha CUF cha Waislamu? Baniani kasema, "Domo jumba ya maneno!" Hiyo ina maana kuwa binadamu, kwa kutumia mdomo wake anaweza kutamka mengi, yanayofaa na yasiyofaa. Na Washihiri wakasema, "kama mwenye kusema ana wazimu, basi mwenye kusikiliza huwa ana akili!" Maana ya msemo huo ni kuwa mtu asiamini kila analoambiwa au kulisikia. Ni wajibu wa msikilizaji kupima lile analoambiwa au kulisikia kabla ya kuliamini. Basi kama kuna watu wanaodai kuwa CUF ni chama cha Waislamu ni wajibu wa wale wanaoambiwa hivyo wachunguze madai hayo kabla ya kuyaamini. Wale wanaokipakazia udini chama cha CUF wanadai kuwa chama hicho ni cha Waislamu eti kwa sababu viongozi wake wengi wa kitaifa ni Waislamu. Lakini kama hicho ndicho kigezo kinachokifanya chama cha CUF kiwe ni chama cha Waislamu, basi tutaona kuwa karibu vyama vingine vyote vilivyobaki, pamoja na chama tawala, CCM, navyo ni vyama vya Wakristo, kwa sababu ile ile, ya kuwa viongozi wake wengi wa kitaifa ni Wakristo. Hivi karibuni Amiri wa Shura ya Maimamu wa Dar es Salaam, Sheikh Juma Mbukuzi ametoa malalamiko kuwa zaidi ya asilimia themanini ya walioteuliwa kusimamia uchaguzi mkuu ujao ni Wakristo. Basi kama itasemwa kuwa CUF ni chama cha Waislamu kwa sababu wafuasi wake wengi ni Waislamu, na CCM nayo haitaepuka kuitwa ni chama cha Wakristo kwa sababu serikali inayoongozwa na chama hicho imekuwa mara kwa mara ikiwapa nafasi ya uongozi Wakristo wengi kuliko Waislamu. Huenda ikawa ni kwa sababu wafuasi wake wengi ni Wakristo au inawapendelea zaidi Wakristo kuliko Waislamu. Na kweli waanzilishi na wafuasi wengi wa chama cha TANU ambacho ndicho kilichozaa CCM walikuwa ni Waislamu. Lakini baada ya kupata uhuru na kuona nafasi za uongozi wanapewa zaidi Wakristo waliokuwa wamejitenga na mapambano ya kupigania uhuru, Waislamu wakaona wajitoe katika CCM kwa vile wanapunjwa. Maoni haya ndiyo yanayoelezwa na Dk. John C. Sivalon, katika kitabu chake alichokiita, "KANISA KATOLIKI NA SIASA YA TANZANIA BARA -1953 HADI 1985." Kwenye ukurasa wa 10, Dk. Sivalon anasema, nami namnukuu, "....Lakini kwa upande mwingine idadi kubwa ya Wakristo wenye elimu walishindwa kushiriki wazi katika TANU kwani aidha walikuwa waalimu au watumishi wa serikali. Serikali ya Wakoloni iliwakataza kisheria kushiriki kwenye vyama vya siasa. Hata hivyo wakati wa uhuru wengi kati ya Wakristo hao wenye elimu na waliokuwa wakifanya kazi serikalini walikuwa na nafasi nzuri zaidi kushika madaraka ya uongozi. Kwa hali hiyo walionekana hasa na Waislamu kama watu waliofaidi matunda ya uhuru bila kushiriki katika mapambano." Mwisho wa kunukuu. Na kilichowakasirisha zaidi Waislamu hata katika siku za hivi karibuni, wakatoka katika CCM na kujiunga kwa wingi katika chama cha CUF, ni kile kitendo cha serikali ya CCM kupuuzia kutatua kero za Waislamu walizomweleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa William Benjamin Mkapa. Na kilichowauma zaidi ni ile kauli ya kiongozi huyo ya kuwaambia Waislamu kuwa yeye hawezi kupuuzia maoni ya wasiokuwa Waislamu. Kwa kauli hiyo Waislamu wametafsiri kuwa wao wanabezwa lakini wenzao ndio wenye haki ya kusikilizwa. Kwa vyo vyote vile madai ya udini ndani ya CUF ni propaganda tu za kujaribu kukipaka matope chama hicho ili wasiokuwa Waislamu wasite kujiunga. Lakini jambo litakalowaondeshea hofu Watanzania ni kule kuona Ndugu Kamara Kusupa, ambaye ni Mwinjilisti ndiye mpiga debe mkubwa wa chama hicho. Inabidi wapinzani, kwa hivi sasa, watahadhari sana na hizi propaganda zinazolenga katika kuisambaratisha kambi yao. Ni wazi kuwa CCM yenyewe imekwisha ingiwa hofu na kasi ya ukuaji wa upinzani. Ndiyo maana safari hii wakapitisha bungeni sheria inayotaka mshindi wa kiti cha urais si lazima apate zaidi ya asilimia hamsini ya kura zilizopigwa. Kwa nini wafanye hivyo? Ni kwa sababu wana wasiwasi kuwa huenda katika uchaguzi mkuu ujao mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama hicho asifikie asilimia hamsini! Basi kama CCM inaona mgombea wake hawezi kufikia asilimia hamsini kwa nini kambi ya upinzani haiungani ikasimamisha mgombea mmoja tu? Kura za wapinzani wote zikiunganishwa pamoja zitapindukia asilimia hamsini. Tusisahau yale maneno ya Baniani, "Dodo dogo mingi nashinda kuba moja!" Kwa hivyo wapinzani wasipokubali kuungana wajue
watasababisha nchi hii ipate Rais asiyeungwa mkono na wengi.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Zanzibar wadai kuyumbishwa na Bara Serikali yatoa muelekeo wa Bajeti na kutangaza njaa Habari za ndani
SMZ haishughulikii mikarafuu -Maalim Seif Mwalimu Mkuu Msimbazi Mseto atishia kujiuzulu Hizi ni 'arobaini' za mapandikizi Waislamu Mbeya wamsusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA Masheikh wa BAKWATA waongoza sherehe za kuwasimika makamanda wa vijana wa CCM MAKALA
Makala
MPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
|
|
|
|
|