|
Na. 050 Jumatano Mei 31 - Juni 5, 2000 |
|
|
|
|
|
MATATA! MATATA! Na Abu Halima Sa Changwa MATATA alikuwa akifikiria kuhusu sherehe ya siku yake ya kuzaliwa. Alikuwa anafikisha miaka sita. Alikuwa haamini kama mama yake atamfanyia sherehe nzuri kama siku za nyuma, kwa sababu walikuwa wakikwaruzana kidogo katika mambo ya kitabia. Alipoona siku yake inakaribia, akaamua aende kumkumbushia mama yake. Akamwambia: "Mama, birthday yangu inakaribia. Katika birthday hii naomba uninunulie baskeli nyekundu". Mama yake akamwambia: "Siku hizi umekuwa mbishi sana, hata husikii. Huna adabu, hata Mungu humheshimu. Kwa hiyo mimi nimeamua kuwa safari hii sikununulii chochote, kwani hata Mungu atanikasirikia kwa kumshughulikia mtoto asiyesikia". Matata alijaribu saana kumsihi mama yake aamini kwamba sasa hivi amejirekebisha. Mama yake akamwambia: "Sasa ni lazima umhakikishie Mungu kwamba umejirekebisha, Umuandikie barua na uahidi kwamba hutarudia mambo yako ya ukaidi, kisha uilete hapa nimpelekee. Nakwambia hivyo kwa sababu kila kitu anatoa yeye, Hata hiyo baiskeli huwezi kuipata mpaka yeye atake". Matata akaona hii ni kasheshe. Hata hivyo akakubali. Akaenda zake chumbani kwake na kuanza kumuandikia Mungu barua. Barua yake ilikuwa kama hivi: Dear Mungu. Napenda kukujulisha kwamba mimi sasa hivi nimeacha ukorofi kabisa. Kwa hiyo naomba unisaidie safari hii nipate zawadi ya birthday. Ningependelea zaidi baiskeli nyekundu, tafadhali. Ni mimi kiumbe wako mtiifu, Matata. Matata akaisoma barua yake, akafikiria jinsi Mungu alivyo Kufuatana na mafundisho aliyopewa, akagundua kwamba amemdanganya Mungu na kwamba hatapata kitu, kwani Mungu hadanganyiki. Akaichana barua ile. Akajaribu kufikiria jinsi ya kuweka maneno kumfanya Mungu amuamini, lakini akaona itakuwa ni uongo na Mungu atajua kuwa ni uongo. Akapata akili. Akarusha ngumi hewani, akisema: "Yes, nimegundua la kufanya. Lazima nipate baiskeli". Matata akanyata akaenda ukumbini. Mama yake alikuwa ni mtu wa dini sana. Alikuwa na kasanamu kake anakapenda na kukaheshimu, na mara nyingi anapofanya maombi yake hukachukua kasanamu kale na kuwa kama anaongea nako, Siku moja Matata alimuuliza mama yake kale kasanamu kalikuwa ni ka nini, mama yake akamwambia, kale ni kasanamu ka Maria Mtakatifu, ambaye ni "mama wa Mungu". Kwa hiyo hapa Matata akawa amepata ujanja. Alipofika pale kasanamu kanapowekwa, akakachukua, akakaweka mfukoni, akaenda nako chumbani kwake. Halafu akaanza kumuandikia Mungu barua. "Mungu. Birthday yangu inakaribia. Kama nilivyotaka kukuambia saa ile, nahitaji zawadi ya baiskeli. Uilete hiyo zawadi, mama yangu aipate haraka, maana siku zinaenda mbio. Usipofanya haraka shauri yako. Hapa ninaye mama yako, naweza kumfanyia lolote nikikasirika. Naweza kumvunja au kumtupa chooni, au . Hakikisha kwamba baiskeli yenyewe inakuwa nyekundu, kama ya David. Ni mimi unijuaye". Sasa hivi katika jamii yetu kuna akina Matata, wanaotegemea kushereheka hivi karibuni. Hawa ni wale ambao walikuwa madarakani na kipindi cha madaraka kinakaribia kwisha. Wanarudi sasa kuomba zawadi za birthday, yaani wachaguliwe tena. Kabla ya hapo, walipopewa madaraka, walileta kibri, walijifanya wababe, wakawa hawana nidhamu. Sasa hivi wanarudi mikono nyuma. Wanataka kutushawishi tuamini kwamba wameshakuwa watoto wazuri. Matata wangu alijaribu kumueleza mama yake kwamba kaacha ukorofi, kwa hiyo apewe zawadi. Akina matata wa siasa nao wanakuja wakisema kwamba pamoja na matatizo na ukorofi walioufanya, kuwakurupusha watu, kuwavunjia vibanda vyao, kuwamwagia vyakula vyao walivyokuwa wakiuza, kuwakejeli, kuwanyanyasa, kuwajeruhi na wengine kuwaua, sasa hivi wanajionyesha wamekuwa watoto wazuri, na kwa heshima na taadhima wanataka wapewe tena "zawadi". Matata wangu alikubali kumuandikia barua "Mungu", lakini ana nafuu, maana alijua uwezo wa Mungu, na akajua kwamba hawezi kumdanganya. Akina Matata wa kisiasa wao hawaangalii Mungu. Hofu ya Mungu hawana. Baada ya ukorofi mwingi wameanza kuingia misikitini. Wanawatanguliza mashehe mbele ili mashehe hawa wawanadi kwa waumini wao. Maaskofu nao nasikia wameshaanza kutembelewa, kasoro akina Kakobe, waliokizima kitimoto. Vyombo vya habari vyatwambia mamufti na masharifu wameshapewa tenda kuwapigia debe akina Matata wa kisiasa, maana wao wenyewe akina Matata maji yako kwenye pua. Matata wangu alikuwa na akili sana, maana alijua dawa ya ushindi ni moja tu, kumkamata mama wa mtoa zawadi, akijua kwamba kwa mapenzi ya watoto kwa mama zao, "Mungu" angetoa zawadi tu. Akina Matata wa Kisiasa nao wanatafuta kila waliwezalo kuhakikisha kwamba wanapata wanachokitaka. Akili yao inawatuma kwenye kuwapora mashehe na masharifu, labda na maaskofu. Kwa mapenzi ya waumini kwa viongozi wao hawa, basi kura zitatoka tu. Kama Matata wangu alivyomdhania "Mungu", kwamba baada ya kuporwa mama yake angetoa baskeli, ndivyo akina Matata wa kisiasa walivyokuwa na mawazo kama hayo. Sasa hivi wanapanga kupora utu wa watu kwa kuwanunua. Kuwafanya bidhaa. Nafuu Matata wangu alimfanya Maria mateka, Matata wa Kisiasa hawapati mateka, wanapata mbuzi, maana mbuzi ndio hununuliwa. Na wao wakitaka kukufanya mbuzi hawaangalii kama wewe ni Shehe au Askofu, au Imamu, au maamuma, au Paroko au mlei. Wanakununua tu. Nasikia tayari akina Matata wa kisiasa wameshapata mbuzi mapema, na ndevu zao, wamewanunua kuwatumikia. Hili ndilo linalonisumbua sana kuhusu siasa za
Afrika. Siasa za Afrika hazionyeshi kama wapo waliojitoa kuisaidia Afrika
na waafrika. Nikionacho mimi ni wanaobahatika kutawala, muda wao wa kutawala
ukiisha, wanatafuta mbinu za kuendelea kutawala, na watatawala tena hata
kama nchi zao zinapiga rivasi, sio kwamba wanaotawaliwa wanapenda, bali
ni kwa sababu ya rafu, na katikati ya watawala na watawaliwa kuna mabuzi,
yako tayari kununuliwa ili wengine wote waje waswagwe na akina Matata.
Mabuzi haya ni yale yanayoheshimiwa na wananchi, lakini yanatumia heshima
na dhamana walio nazo kuwawekea njia akina Matata wa Kisiasa, katika jina
la Mungu. Nilifurahi sana niliposoma kwenye gazeti moja kwamba Mheshimiwa
Mzee Malecela amewaagiza vijana wawashughulikie wanaoingiza siasa misikitini.
Hili mimi naliunga mkono mia kwa mia. Ila ningependa kufahamu, ndugu vijana,
wale mashehe niliowasoma kwenye gazeti wakiwapigia kampeni akina Matata
wa siasa wameshughulikiwa? Sijasikia kama agizo la Mheshimiwa limetekelezwa.
Mimi nadhani neno "kushughulikia" halikueleweka. Sidhani kama Mheshimiwa
alimaanisha kushughulikia ni kuwapa hawa mashehe futari, au pilau. Kushughulikia
maana yake mkong'oto, yakhe, dhwaahir eeeh??? Je, wale mamufti mliwakong'ota?
Tena Mzee Malecela nilisoma amesisitiza kwamba kwenye siasa hakuna kugeuza
shavu, kwa hiyo anakubaliana na sera ya "shavu kwa shavu" kama wale wanaosema
"pua kwa pua", "jino kwa jino". Jingine niliotaka kufahamu kutoka kwa Mheshimiwa
ni hili. Je, kushughulikia ni msikitini tu, au hata Mahekaluni na Makanisani?
Maana unapoongea unatakiwa uweke mizani, la sivyo matata! matata! Matata!
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Zanzibar wadai kuyumbishwa na Bara Serikali yatoa muelekeo wa Bajeti na kutangaza njaa Habari za ndani
SMZ haishughulikii mikarafuu -Maalim Seif Mwalimu Mkuu Msimbazi Mseto atishia kujiuzulu Hizi ni 'arobaini' za mapandikizi Waislamu Mbeya wamsusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA Masheikh wa BAKWATA waongoza sherehe za kuwasimika makamanda wa vijana wa CCM MAKALA
Makala
MPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
|
|
|
|
|