|
Na. 050 Jumatano Mei 31 - Juni 5, 2000 |
|
|
|
|
|
VIONGOZI wa vyama vitatu vya upinzani wamekutana Mei 29, mwaka huu, Jijini, ili kukamilisha hatua za kusimamisha mgombea mmoja wa Urais. Taarifa iliyosainiwa na Mwenyekiti wa kikao hicho Prof.Ibrahim Haruna Lipumba na kusambazwa kwenye vyombo vya habari, vyama vilivyokubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa kiti cha Urais ni CHADEMA, CUF na UDP. Viongozi waliohudhuria katika makubaliano hayo ni Prof. Ibrahimu Lipumba, Mwenyekiti wa CUF, Mhe. Bob Makani, Mwenyekiti wa CHADEMA na Dk. Lwanyautika Masha, Makamu Mwenyekiti wa UDP aliemwakilisha Mhe.Joyn Cheyo aliye safarini. Wengine waliohudhuria katika kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za CUF zilizoko Buguruni, Jijini, ni Dk. Medard Matungi, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA na Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF. Taarifa hiyo ilisema kwamba wenyeviti wa vyama hivyo watakutana Julai 1, mwaka huu ili kupanga tarehe ya kumteua mgombea mmoja wa Urais wa Jamhuri na Mwenza wake, na mgombea Urais Zanzibar miongoni mwa wagombea waliopendekezwa na kila chama. Nafasi nyingine walizokubaliana kuwa na mgombea mmoja mmoja viongozi hao ni pamoja na ubunge na udiwani. Sambamba na hatua hiyo, vyama hivyo vya CHADEMA, CUF na UDP vimekubaliana kuvikaribisha katika muungano wao vyama vingine kama vile NCCR na TLP.
Na Suleiman Akilimali, Zanzibar KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi [CUF] Maalim Seif Shariff Hamad ameilaumu serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutoishughulikia Mikarafuu ingawa fedha nyingi hupatikana kutokana na zao hilo. Maalim Seif ameyasema hayo alipokuwa akizunmgumza na NASAHA huko nyumbani kwake Mtoni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Akitoa lawama hizo Maalim Seif amesema kuwa hivi sasa bei ya karafuu imepanda kutoka dola 1000 za Kimarekani kwa tani hadi dola 4000,lakini hata hivyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikificha ukweli huo na kutaja bei za chini kila wanapokutana na wananchi. Aidha alifahamisha kwamba hivi sasa miti hiyo ya mikarafuu imekuwa ikiugua kwa wingi na menginekufa kabisa lakini Serikali ya CCM hata haijali. Akizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar Maalim Seif amesema hali ya kisiasa ni vigumu kutulia hadi pale Zanzibar itapokuwa na maamuzi huru kuhusu mambo yake yenyewe. "Hivi sasa Zanzibar hakuna uhuru wowote wa maamuzi kwani mambo mengi yamefilisiwa na Serikali ya Muungano", Maalim Seif alilaumu. Amezidi kufahamisha iwapo chama chake cha CUF kitaingia madarakani kitu cha kwanza kabisa ni kuirudisha hadhi ya Zanzibar kwa kurekebisha mambo mbali mbali ya Muungano na kuwepo kwa Serikali tatu(3). Kuhusu tume ya uchaguzi kupanga uchaguzi kufanyika nchini kote Oktoba 29, Mwaka huu, amesema hilo ni kosa na chama chake hakijaondoa msimamo wa kuishitaki tume hiyo ya uchaguzi Zanzibar. Hata hivyo, Maalim Seif amesemea chama cha wananchi CUF hakitosusia uchaguzi Mkuu ujao bali kitaingia katika uchaguzi bila wasi wasi wowote kikiwa na mategemeo makubwa ya kushinda. Akizungumzia, kutopitishwa muswada wa marekebisho ya nane (8) ya Katiba ya Zanzibar, Katibu Mkuu huyo wa chama cha upizani amesema wawakilishi wa chama chake wametoa maamuzi hayo kwa kulinda muafaka na sio jambo jengine. "Mambo yote yaliowasilishwa katika muswada ule ni tofauti kabisa na yale yaliyopelekwa Serikalini na Kamati ya muafaka (IPC), ndio sababu ya Wawakilishi wetu wa (CUF)kuukataa muswada wote", Maalim Seif alifafanua. Katika kuifanya Kamati ya (IPC) iwe bado inaendelea kuwepo Maalim Seif Shariff Hamad amesema, ni vyema Kamati hiyo ikawa na mtazamo wa kijumuiya ya madola moja kwa moja ili iweze kusimamia hali ya kisiasa kikamilifu Zanzibar ambayo matatizo yake yanawezekana kabisa kutatuliwa kwa mazungumzo.
Na Badru Kimwaga MWALIMU Mkuu wa shule ya msingi ya Msimbazi Mseto, Mama Sanga ametishia kuachia ngazi kwenye shule hiyo iwapo wazazi wa shule hiyo wataendelea kusuasua kulipa michango na ada inayotozwa na shule hiyo kwa vile ameonekana mzembe mbele ya mwajiri wake. Tishio hilo lilitolewa na Mwalimu huyo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akizungumza na wazazi wenye watoto shuleni hapo kwenye mkutano wa pamoja ambao ulifanyika shuleni hapo ili kujadili maendeleo ya shule hiyo. Mama Sanga alisema, kutokana na wazazi kushindwa kulipa michango ya shule hiyo amekuwa akipata shinikizo na tishio la kutimuliwa kazi kwa vile ameonekana mzembe, naye ana budi kuachia ngazi iwapo wazazi hao watashindwa kumpa ushirikiano katika suala hilo la michango ambayo ndiyo inayoendesha miradi ya maendeleo ya shule nyingi nchini. "Wazazi nawafahamisha kabisa kuwa iwapo mtaendelea kukwepa kulipa michango ya shule mimi nitaiacha kwenye mataa shule yenu ingawa naipenda kwa vile shinikizo kubwa ambalo ninalipata kutoka kwa mwajiri wangu itaniwia vigumu kuendelea kukaa kwenye shule isiyotoa mshikamano", alisema Mwalimu Mkuu huyo. Aliongeza, anashangazwa na wazazi hao kushindwa kulipa shilingi 8,000 tu ilhali hao hao wako tayari kutoa hata laki moja itumike kwenye sherehe za kipaimara na ubatizo kwa watoto wao jambo ambalo linavunja moyo na ufanisi wa kazi zake. Mama Sanga alisema, kwa mfano hadi sasa anadaiwa na mwajiri wake Tume ya Jiji zaidi ya shilingi laki mbili za michango ya UMITASHUMTA zitokanazo na shilingi 1,000 ambayo inapaswa kulipwa na kila mwanafunzi wa shule hiyo ambayo ina zaidi ya wanafunzi 2000. Mwalimu huyo alisema, dhana ya huduma na maendeleo ya shule kutegemea serikali ni potofu kwa vile serikali ni wazazi wenyewe na sio kundi fulani la watu wenye kupaswa kutoa misaada na kusema kama suala la ujenzi wa choo cha shule hiyo unashindwa kukamilika kutokana na wazazi kuwa wagumu kuchangia fedha za ujenzi wake. Alisema, jumla ya fedha zinazotakiwa katika ujenzi wa choo hicho ni zaidi ya shilingi milioni 6 , lakini hadi sasa ni shilingi milioni 4 tu ndizo zilizotolewa na hivyo kushindwa kukamisha umaliziaji wa ujenzi huo ambao alisema kati ya shilingi 8,000 za ada ya shule hiyo ni shilingi 5,000 tu ndizo zinazotumika katika ujenzi huo baada ya kutoa shilingi 2,000 za UPE na 1,000 za UMITASHUMTA.
IMEDAIWA kuwa miongoni mwa wale wanachama wa vyama vya upinzani kurudi CCM wamo waliokwenda kwenye vyama vya upinzani kama majasusi waliopandikizwa ili kuvuruga nguvu za upinzani dhidi ya chama tawala. Hayo yamesemwa na wananchi mbalimbali waliozungumza na NASAHA na kutoa maoni yao kuhusu watu wanaohama vyama walivyokuwemo na kujiunga na vyama vingine. Idadi kubwa ya watu hao ambao waliohojiwa katika maeneo mbalimbali jijini walisema, ingawa suala la kujiunga, kutoka au kutojiunga na chama chochote ni haki ya kila mwananchi, lakini walidai pia kuwa baadhi ya watu hao wamo wanaokwenda au waliokuwemo katika vyama hivyo hutumiwa kwa madhumuni ya kuchunguza mwenendo wa vyama hivyo ili kuvidhoofisha kiftna kwa manufaa ya vyama vyao halisi. Baadhi ya wale waliodai hivyo walieleza kuwa wamo miongoni mwa hao wale waliokitumikia chama tawala na kwamba siyo wote wanaorudi au kuhama vyama hivyo wamemaliza kazi walizotumwa. "Wengine wanakimbia baada ya kuona wamegundulika kuwa ni mapandikizi", alisema Bwana mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Steven, mkazi wa Kimara Baruti. Mkazi mwingine wa Kimara Baruti ambaye pia alitaja jina lake moja tu la Michael alisema, baadhi ya wanaohama vyama hivyo wamo katika kutafuta manufaa ya uongozi wa kuchaguliwa au kuteuliwa baada ya uchaguzi mkuu ujao. Mkazi wa Magomeni Mapipa aliyejitambulisha kwa jina la Abdul alisema, kuhama kwa watu katika vyama ni dalili kuwa demokrasia imeanza kuonekana. Hivyo watu wanatumia haki yao ya kupima wapi kwenye ukweli na kwenda kwenye ukweli pasipo woga. Hata hivyo alisema kuwa yeye anawaamini sana wale wanaotoka chama tawala kwenda upinzani kwa sababu huko hakuna maslahi ya kiutawala ila "kazi tu" za kusimamisha utawala wa haki nchini". Mama mmoja wa Tandika Sokoni aliyejitambulisha kwa jina la Mama Ali alisema, siasa za upinzani sasa hivi zimepamba moto na kwamba yeyote aliyejiunga huko kwa nia mbaya atagundulika tu. "Hizi ni siku za mapindikizi kufikia arobaini zao. Hawawezi tena kuwaongopea wananchi, wamesha gundulika, kilichobaki wakimbie au wafukuzwe", alisema mama huyo bila ya kutaka kufafanua zaidi. Nae mkazi mmoja wa Mbagala ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini, alisema, yeye anachukizwa na kauli za baadhi ya wanasiasa wenye sera za kujipigia debe pasipo kujali maslahi na matakwa ya wananchi. Bwana huyo wa Makamo kidogo alisema, "mapandikizi" halisi ni hawa wanasiasa wanaopita huko na huko wakijitangaza kuwa wao ndio wanaofaa kuongoza nchi. "Wahenga walisema, chema chajiuza na kibaya chajitembeza", alisema Bwana huyo na kufafanua kuwa wale wanaojinadi kuwa wao wanafaa kuliko wenzao ni wabovu kwa sababu wanataka kuingilia uwezo wa wananchi wa kuwatambua na kuwachagua viongozi wanaofaa. Alisema, kiongozi mwenye uwezo hawezi kupita huku na huko kujitangaza. Wananchi watamtambua tu na kumchagua. Mtoa maoni mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Uledi ambaye alidai kuwa anatoka Magomeni "Saratoga" alisema wapo watu wanaopenda madaraka ya juu kama vile Urais wa nchi. Watu wa aina hii wanapokuwa hawana elimu ya kutosha kuwapatia ajira ya vyeo vya juu ni hatari sana. Kimbilio lao huwa vyama vya siasa, tena kutafuta Urais. "Hii ni karne ya sayansi na teknolojia. Tunataka watu waliojitosheleza kielimu. Kwanza watu wa aina hii wana uwezo wa kupata madaraka ya juu hata kwenye ajira za kimataifa", alisema Bw. Uledi na kumalizia kwa kusema, hawa si sawa na "wale wenye elimu ndogo ambao uwezo wa kuajiriwa katika nafasi za juu hawana, ila kuingia siasa za kugombea Urais". |
YALIYOMO
TAHARIRI
Zanzibar wadai kuyumbishwa na Bara Serikali yatoa muelekeo wa Bajeti na kutangaza njaa Habari za ndani
SMZ haishughulikii mikarafuu -Maalim Seif Mwalimu Mkuu Msimbazi Mseto atishia kujiuzulu Hizi ni 'arobaini' za mapandikizi Waislamu Mbeya wamsusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA Masheikh wa BAKWATA waongoza sherehe za kuwasimika makamanda wa vijana wa CCM MAKALA
Makala
MPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
Ambari, Mwakipesile wajitosa kugombea DRFA |
|
|
|
|