NASAHA
Na. 049 Jumatano Mei 24 - 30, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MICHEZO

Raza kufungua mashindano ya Wavu Zanzibar

Na Asma Mohammed -Zanzibar

Mshauri wa michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mohammedi Hassanali Raza anatarajiwa kufungua rasmi mashindano ya Klabu Bingwa ya Mpira wa Wavu kanda ya Unguja Jumamosi ijayo.

Katibu Mkuu wa mchezo huo Kisiwani Zanzibar Mwalimu Yustice Mwakanjuki amesema kwamba ufunguzi huo utafanyika katika uwanja wa polisi Bomani mjini Unguja.

Mwakanjuki amezitaja timu zitakazoshiriki katika mashindano hayo kuwa ni Polisi, Mafunzo, Chuoni, Amani, Daraja, Calipso na Fuoni.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Chama cha mpira wa mikono mjini hapa ameelezea masikitiko yake kutokana na kuendelea kunywea kwa mchezo huo kisiwani Zanzibar.

Katibu Mkuu huyo, Bwana Omari Nassor amesema kwamba kunywea huko kunatokana na Baraza la Michezo Zanzibar (BMZ) kushindwa kutoa misaada ya kutosha kuendeleza mchezo huo.


FAINALI KLABU BINGWA ULAYA
Real Madrid yaota Ubingwa leo

UFARANSA

TIMU ya mpira wa miguu ya Real Madrid ya Hispania ina matumaini makubwa ya kutwaa Ubingwa wa Ulaya kwa mara ya nane itakapopambana na Valencia pia ya Hispania katika fainali ya Kombe la Ubingwa barani Ulaya itakayochezwa nchini Ufaransa leo.

Matumaini ya timu hiyo yanatokana na historia yake katika mashindano hayo ambapo ilishatwaa taji hilo kwa mara nne mfululizo kuanzia 1957, 1958, 1959 na 1960.

Pia ina rekodi ya kuvitoa vigogo vya soka barani Ulaya wakiwemo Mabingwa watetezi wa kombe hilo, Manchester United ya Uingereza na washindi wa pili wa taji hilo Bayern Munich ya Ujerumani.

Hata hivyo, timu hiyo itatelemka dimbani leo ikiwa na majeruhi ya wachezaji wake nyoka wanne ambao imeripotiwa kuumwa na wengine kuwa majeruhi.

Wachezaji hao ni pamoja na mshambuliaji mwenye matata Nicolas Anelka na mlinzi mahiri Machael Salgado ambao wote wawili wameumia vifundo vya miguu.

Daktari wa timu hiyo Juan Carlos Haanandez aliwataja wengine walioumia kuwa ni pamoja na kiungo machachari Salvio ambaye ameumia mguu wa kushoto.

Aidha, matumaini hayo ya Real Madrid yana uwezekano mkubwa kutoka kapa kufuatia ukali wa timu ya Valencia uliuonesha katika mashindano hayo mwaka huu.

Timu hiyo ya Valencia ina wachezaji hatari ambao wanaweza kufanya matokeo kuwa kinyume na matumaini ya Real na hivyo kuweza kutwaa ubingwa huo.

Wachezaji hao ni pamoja na Claudio Lopez, Gaizka Mendieta, Juan Sanchez na Miguel Angel Angulo ambao wameonesha vipaji vikubwa vya kumiliki mpira na kupenya ngome za maadui watakavyo na kupachika mabao.

Hata hivyo, mashabiki wa soka wanatarajiwa kuona mafahari wawili, Claudio Lopezi wa Valencia ambaye amekuwa ni mwiba mchungu kwa timu pinzani kutokana na uwezo wake wa kwenda kasi na kupiga chenga za mwili akikabiliana na kisiki cha Real Madrid, Roberto Carlos na hivyo kuwa burudani nyingine ya aina yake katika pambano la leo.


Kajumulo asema Yanga timu ya Wananchi

Na Hamis Kasabe

Alex Kajumulo mmiliki wa timu ya Kajumulo World Soccer ya Dares Salaam ameibeza Klabu ya Yanga pia ya Dar es Salaam kwamba ni Klabu ya wananchi kutokana na kile alichodai kuwa ni kupendelewa na watendaji mbalimbali katika medani ya soka hapa nchini.

Kajumulo alidai hayo Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Taifa jijini kufuatia mwamuzi Emanuel Chaula kutoka Rukwa kukubali bao la utata la Yanga dhidi ya timu yake.

"Kwa kweli leo (Jumapili) nimeamini kwamba Yanga ni timu ya wananchi ambapo kila raia anatumia nafasi (kazi) yake kupindisha sheria katika kuhakikisha Yanga inashinda mchezo", alidai.

Bao hilo ambalo Chaula baadaye alilikataa baada ya kuhakikishiwa na aliyekuwa refa wa akiba Abdul Kadir katika mchezo huo lilitokana na shuti kali la umbali wa meta kama 30 hivi lililokung’utwa na beki Patrice Tambwe wa Yanga.

Katika kile kilichoonekana kumchanganya mwamuzi na washika vibendera wake ukiachilia mbali watazamaji waliogawanyika, shuti la Tambwe liligonga nguzo ya nyuma ya goli la Kajumulo inayoshikilia nyavu na watazamaji wakastukia mpira ukiwa umebarizi kimiani.

Baada ya mwamuzi kuashiria kuwa ni goli, wachezaji wa Kajumulo walimzonga na kumtia msukosuko huku tajiri wao Alex Kajumulo akiwataka wagomee mchezo kama Chaula atashikilia msimamo wake.

"Haya ni mapenzi ya wazi ya refa kwa Yanga, kwa sababu anataka kuwapa goli ambalo si goli na sisi hatuwezi kukubali kamwe", alisema na kuongeza kwa masikitiko kwamba Yanga "timu ya wananchi".

Hatimaye pambano liliendelea na kumalizika kwa suluhu licha ya Kajumulo kucheza wakiwa pungufu ya mwanandinga mmoja kwa dakika 65 kufuatia Abdalah Msamba kupewa kadi nyekundu.

Katika tukio jingine, wapenzi kadhaa wa soka jijini wamempongeza Alex Kajumulo kwa kukataa kuitwa Mheshimiwa kama ambavyo viongozi wa CCM hupenda. Kajumulo alitoa msimamo huo mwishoni mwa wiki uwanja wa Taifa baada ya shabiki mmoja kumwita kwa jina hilo.

Wakiongea na NASAHA kuhusu tukio hilo washabiki hao wamesema kwamba ni viongozi wa CCM pekee wenye maradhi ya ukubwa na "umamluki" sifa ambayo wamedai Kajumulo hana.
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
KERO katika Elimu ziondolewe haraka

Chuo Kikuu Dar wafanya mitihani katika Bwalo la chakula

Udini wa CCM utaisambaratisha nchi -Tambwe

‘Kutoweka’ kanda ya Kakobe: CCM yatuhumiwa

Maalim Seif awaambia Wazanzibari: Wenye mamlaka ya kumuweka mtu Ikulu ni wananchi

Mkapa afurahia maendeleo Pwani

Wapinzani wajiimarisha Moro

‘Zawadi’ ya Uchaguzi yatishia kusambaratisha taasisi ya Kiislam Tanga

Serikali yakemea mwanamke kudhalilishwa

Ushauri Nasaha
Umuhimu wa kushirikiana na majirani katika malezi ya watoto

MAKALA
Afande Mahita, wananchi hatutaki Dola ya kipolisi

Makala
CCM hawawezi kuondoa umasikini, ndio tegemeo lao

Kalamu ya Mwandishi
Makubaliano kwa vitendo Z'bar

MAKALA
CCM na sera za maendeleo (5)

Makala
Wanawake na maendeleo: Je ni wimbo wa kuchaguliwa?

Makala
CCM inatawala badala ya kuongoza

Habari za Kimataifa

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra -4

Lishe
Unachotakiwa kufanya kabla ya kuweka chakula kwenye jokofu

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Raza kufungua mashindano ya Wavu Zanzibar
  • Real Madrid yaota Ubingwa  leo
  • Kajumulo asema Yanga timu ya Wananchi

  •  


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita