NASAHA
Na. 049 Jumatano Mei 24 - 30, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA

CCM na sera za maendeleo (5)
Yanayosemwa na yanayotendwa ni tofauti

Tangu tupate uhuru karibu miaka arobaini iliyopita, imekuwa ni utamaduni wa viongozi wa serikali ya chama tawala, kuhimiza wananchi, wakati mwingine kwa sauti za kejeli kupalia mashamba, wakati mwingine kuwahimza kulima zao fulani, na wakati mwingine kuwatolea lawama eti hawafuati maagizo ya wataalamu, kama vile wanancbi ni punguani.Mwandishi Rajab Kanyama anaendelea...

Katika utawala wa Serikali ya awamu ya kwanza, serikali ilikuwa kama mnyampara kasuku.

Tulikuwa tukiimbishwa "Ujamaa na Kujitegemea", mpaka tukawiva, maskini hatukuelewa kwamba, ule ulikuwa ni mchezo wa kuigiza.

Kila kona ambayo ungepita ungesikia "usiwe kupe, jitegemee" aliyekuwa akiambiwa maneno hayo, wakati huo hakujulikana.

Sasa ndio tumeanza kupata mwanga, kumbe aliyekuwa akiambiwa maneno hayo ni mwananchi.

Kujitegemea kwa serikali, mpaka leo hii ni kukopa mabilioni ya mapesa kutoka katika mashirika ya fedha ya kimataifa na nchi binafsi kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya kikundi cha watu ambao wamejibatiza majina na kujiita serikali.

Au tuseme ni siri-kali, maana ni juzi tu ndio siri imefichuka na mfichuaji akiwa Waziri wa Maji, Mheshimiwa Nkhangaa.

Tarehe 18 Mei, mwaka 1999, Waziri Nkhangaa aliwaeleza waandishi wa habari kwamba serikali haiwezi kuwapatia wananchi maji safi na salama, kama ambavyo sera ya chama cha mapinduzi ilivyoeleza katika ilani yake ya uchaguzi kwamba ingewapatia wananchi wote wa Tanzania, maji safi, ifikapo mwaka 2002.

Kwa bahati nzuri, hakubakisha neno, maana katika maelezo yake, kunawakati alieleza kwamba, kuitegemea serikali kuwapatia wananchi wote maji, bila ya mipango thabiti, hasa ukizingatia uchumi duni na ufinyu wa bajeti ilikuwa ni sera mbovu. 

Hapa angalau waziri alikuwa mkweli na hakuwa mlaghai kwani ulaghai ni tabia ya viongozi wa serikali ya Chama tawala cha CCM tangu awamu ya kwanza.

Wakati wa ujamaa na kujitegemea, tulikuwa tunaambiwa tukusanyike katika vijiji vya ujamaa ili tuweze kupatiwa huduma za maji, elimu na afya kwa urahisi.

Waliokataa walikusanywa kwa nguvu za dola, bila ya kusikilizwa hoja zao.

Amri ya Mwenyekiti, ilikuwa ni sawa na amri ya Askofu kwa waumini wake, hakuna hoja wala maswali, ni kutekeleza tu.

Tukaimbishwa, adui ni umaskini, ujinga na maradhi; kumbe wajanja walikuwa wanatuzuga ili tusije tukamfahamu adui yetu wa kweli.

Umaskini, ujinga na maradhi ni hali ya uhitaji, ambayo kwa kawaida husababishwa na mazingira ya kiuchumi, kielimu na kiafya.

Kwa mantiki hiyo, adui ni kundi la watu (serikali) au taasisi (chama) kinachochangia kuwepo kwa hali ya uhitaji, kwa sababu ya kutokuwa na sera na mipango mizuri ya maendeleo.

Kila kukicha, wananchi wanalundikiwa lawama, eti wanachelewesha maendeleo yao kwa kutofanya hili au lile.

Wakati wote, tangu awamu ya kwanza ukweli ni kinyime chake kwani maendeleo yamekuwa yakicheleweshwa na viongozi wa chama tawala na serikali yake kwa kutoandaa mazingira muafaka, kama vile mtandao mzuri wa barabara, ugavi wa umeme, maji na huduma za afya, kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya watu, na kwa maana hiyo ya taifa.

Uwezo wa kutoa huduma na nguvu ya Serikali hupatikana kutoka kwa wananchi kupitia kodi wanazolipa, na wananchi wa nchi hii wanaongoza katika bara la Afrika kwa kutozwa kodi nyingi na kubwa. Kulikoni, leo waambiwe kuwa Serikali haina uwezo wa kuwapatia huduma?

Chanzo kingine cha uwezo wa Serikali ni maliasili za taifa kama vile madini, wanyama pori, misitu na mashirika ya umma.

Kwa bahati mbaya, serikali ya Chama Cha Mapinduzi imeamua kuwapa wageni vyanzo vyote hivyo tena kwa bei karibu na bure.

Wananchi wanataka kujua, kwa nini hao wanaopewa rasilimali hizo, hawapewi na majukumu ya kutoa huduma hizo? Na kama haiwezekani kwa nini wananchi wanaendelea kutozwa kodi kubwa, ambazo hazina manufaa kwa vile sasa huduma zote inabidi wazinunue?

Mfumo wa kodi hapa nchini unaathari mbaya sana kwa jamii, kwanza ni kwa sababu unawatisha wawekezaji kuwekeza katika miradi mikubwa ambayo ingetoa ajira kwa wananchi, na pili unalazimisha hata wale ambao wanafanya shughuli hapa kuzifunga.

Kutokana na mfumo mbaya wa kodi nchini, kiwanda cha General Tyre kinachotengeneza matairi ya magari kilichopo mjini Arusha, kimesitisha uzalishaji, na kwa hivyo watumishi karibu 2000 wamekosa ajira.

Sasa katika hali kama hiyo, watu hawa watawezaje kulipia gharama za maji, matibabu na elimu kwa watoto wao?

Vigogo wamebana kila kona, na wananchi sasa hawana pa kupumzikia.

Siku za hivi karibuni, Tanzania imepewa shilingi bilioni 59 na Benki ya Dunia, kwa lengo la kuwapatia wananchi uwezo wa kujiendeleza. Fedha hizo zimo katika mfuko wa kuongeza nguvu za wananchi ili kujiendeleza na kujitegemea (TASAF).

Wananchi wanatakiwa kuchangia asilimia 13.6 na serikali asilimia 5, inashangaza ni vipi mwananchi anayetakiwa kusaidwa, anatakiwa achangie ndipo apate msaada?

Wanaotakiwa kuchangia ni wananchi akiwa yakhe, lakini viongozi wa chama cha mapinduzi wana njia yao ya kujipa mgawo.

Mpaka hivi sasa tayari kiasi cha shilingi milioni 300,000,000 zimekiwsha tumika kwa ajili ya kuendeshea semina za kuandaa mikakati ya kupambana na umaskini nchini.

Kioja kikubwa!, aliyewaambia kwamba wananchi wanaridhika na umaskini huu mpaka waandaliwe mkakati na vigogo kwa kuwaendeshea semina ni nani?
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
KERO katika Elimu ziondolewe haraka

Chuo Kikuu Dar wafanya mitihani katika Bwalo la chakula

Udini wa CCM utaisambaratisha nchi -Tambwe

‘Kutoweka’ kanda ya Kakobe: CCM yatuhumiwa

Maalim Seif awaambia Wazanzibari: Wenye mamlaka ya kumuweka mtu Ikulu ni wananchi

Mkapa afurahia maendeleo Pwani

Wapinzani wajiimarisha Moro

‘Zawadi’ ya Uchaguzi yatishia kusambaratisha taasisi ya Kiislam Tanga

Serikali yakemea mwanamke kudhalilishwa

Ushauri Nasaha
Umuhimu wa kushirikiana na majirani katika malezi ya watoto

MAKALA
Afande Mahita, wananchi hatutaki Dola ya kipolisi

Makala
CCM hawawezi kuondoa umasikini, ndio tegemeo lao

Kalamu ya Mwandishi
Makubaliano kwa vitendo Z'bar

MAKALA
CCM na sera za maendeleo (5)

Makala
Wanawake na maendeleo: Je ni wimbo wa kuchaguliwa?

Makala
CCM inatawala badala ya kuongoza

Habari za Kimataifa

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra -4

Lishe
Unachotakiwa kufanya kabla ya kuweka chakula kwenye jokofu

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Raza kufungua mashindano ya Wavu Zanzibar
  • Real Madrid yaota Ubingwa  leo
  • Kajumulo asema Yanga timu ya Wananchi

  •  


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita