|
Mashairi
Uchaguzi unakuja
Uchaguzi unakuja, raia kaa tayari,
Tuache kujikongoja, tuwemo na nyingi ari,
Tusije tukaufuja, tufanye kwa uhodari,
Tumchague wa haja, atoleta hali shwari.
Tuchague wa kufaa, imara atasimama,
Uchumi atafufua, na kuondoa dhuluma,
Haki atasimamia, na ataleta salama,
Amani kufuarahia, na kuepa uhasama.
Tumchagueni huyo, asiejipendelea,
Kasujependa makuu, haki sawa atatoa,
Mwenye elimu ya juu, hekima alobobea,
Ni lazima mwaka huu, nafasi kumuachia.
Atakaepinga hayo, hafai kupiga kura,
Hatotupa tegemea, kupata alie bora,
Ni bora atoke mbio, nafasi asijepora.
Akaweka ambao, watajaleta hasara.
Huyo hafai kabisa, atatuendesha puta,
Na tuangalie sasa, tunavyoipatapata,
Wachache wanaotesa, wengi wanakula kwata,
Wengine wana anasa, wengine wajiburuta.
Anasa wakumbatia, hazina waikung’uta,
Wengi wetu waumia, wao bora wanapata,
Wamefanya mazoea, raha kwao kufumbata,
Lakini tukiamua, watakoma usalata.
Tusiwapeni nafasi, watu wa aina hiyo,
Wanahusudu ukwasi, wanadhani haki yao,
Hata kitupa fulusi, zisitutie pumbao,
Bali tuondoe nuksi, kando tuwapige bao.
Na tuwapigeni pande, kabisa sicheke nao,
Kama kukonda wakonde, hatuna habari nao,
Wakituona mashonde, hatujenda omba kwao,
Na yanini tuwagande, nema hawatupi wao.
Riziki atoa Mungu, kwake na tutegemee,
Aloumba Ulimwengu, kaweka wao na sie,
Wasikiweke kiwingu, ili haki waitwae,
Mara hii kwa mapingu, ngazi waziachilie.
Waziachilie ngazi, ili mchuma upete,
Tuweke wachapakazi, si wao masulupwete,
Walojaa ubazazi, nahadaa ketekete,
Tumechoka kwalowezi, kupe na chuma ulete.
Tusiziharibu kura, na tuwe na msimamo,
Tuchague kwa busara, tuzingatie vipimo,
Tusijefanya papara, tukajaenda mchomo,
Na watu wakatuchora, tukajakosa msemo.
Naomba tuwe makini, mwanya wasijeupata,
Wakakamata mpini, kisha wakaja uvuta,
Wakatupa hamklani, tukabakia kujuta,
Hapo isaidieni, hata kama tatateta.
Budi na tuhakikishe, kura hatutapoteza,
Mwaka huu tuonyeshe, tumechoka kuburuzwa,
Katu wasitupotoshe, ahadi kutupumbaza,
Kibidi tuwahenyeshe, wasipate kujikweza.
Tamati nasisitiza, kura tusiziharibu,
Tuchague bila chonza, tufanye ustarabu,
Tusiwape maliwazo, wale walotupa tabu.
Bali na wawe wa kwanza, hali mbaya watotibu.
“Sihaba” Mbagala,
Dar es Salaam.
Haki
Jamani haki jamani,
Imeingia mitini,
Imepotea nchini,
Wanyonge wanaumia,
Haki sawa ni lazima,
Tuidai kwa hekima,
Wala tusikae nyuma,
Haki imedidimia.
Haki yako ukidai,
Waonekana adui,
Waandamwa kama chui,
Bila kosa kulijua.
Kuidai ni muhimu,
Katika hii awamu,
Tusije kujilaumu,
Machungu yakitujia.
Haki isipotendeka,
Amani inatoweka,
Wachache hunufaika,
Na wengi kuteketea.
Ni vizuri ukumbuke,
Haki sawa uitake,
Tena usitetereke,
Haki kuipigania.
Tutakuwa mashughuli,
Mbele ya wetu Rasuli,
Ikiwa tutakubali,
Dhulma kuiachia.
Lazima tupiganie,
Haki nchini itue,
Dhulma tuiondoe,
Wa visiwani sikia.
Wanawake amkeni,
Nchi haina amani,
Imeingia gizani,
Hamna cha kuringia.
Haki tunapoitaka,
Viongozi huchafuka,
Mikononi hutuweka,
Tubaki kujitetea.
Haki ni kitu muhimu,
Kwetu sisi wanadamu,
Amani haitadumu,
Hilo wazi zingatia.
Kaditama nabaini,
Nimefika kituoni,
Kalamu naweka chini,
Haki nabaki lilia.
Umnul Jamilah,
Safarini Pemba, Wete.
Polisi gani hawa?
Kwa huzuni nasogea, Mhariri NASAHANI,
Hawa kuwaongelea, hawatufai nchini,
Wapo kutuonelea, ulinzi kwao sioni,
Hawa ni polisi gani? ”Hawatufai nchini”.
Moyoni mimi nalia, machungu yamenizidi,
Mabaya nawatakia, si wema ni wakaidi,
Awaadhibu Jalia, wote ili tuwanadi,
Hawa ni Polisi gani? ”Hawatufai nchini.”
Mengi nikifikiria, kwao machungu huzidi,
Mengi watuzuia, nyuma nyuma tunazidi,
Kazi kutushupalia, roho wataka zaidi,
Hawa ni Polisi gani? “Hawatufai nchini.
Mfano nikichambua, kwao rushwa imezidi,
Mfano kutubutua, wanyonge watufaidi,
Mfano kwa kutanua, matajiri ni zaidi,
Hawa ni Polisi gani? “Hawatufai nchini.
Mfano kutubagua, Islamu wamezidi,
Mfano kwa kutuua, Mwembechai ni zaidi,
Mfano kwa kutojua, moto wachuma zaidi,
Hawa ni polisi gani? “Hawatufai nchini.”
Mfano kwenye siasa, wanatumiwa zaidi,
Zanziba hivi sasa, wamekua ”magaidi”,
Mfano MAFUSO sasa, kwa CUF mwiko wanadi,
Hawa ni Polisi gani? “Hawatufai nchini.
Mfano SERONI sasa, vijana wengi zaidi,
Mfano KIDUMU sasa, kinathamani zaidi,
Mfano CHAGUZI sasa, wanatumiwa zaidi,
Hawa ni polisi gani? “Hawatufai nchini.”
Yote tisa kumi jama, roho yauma zaidi,
Hawa sio watu wema, ni adui mahasidi,
Ole wao tukisema, tumewachoka zaidi,
Hawa ni polisi gani?”Hawatufai nchini.
Natoa ombi mbinguni, Rabi kwako nakujia,
Ututoe dhulmani, polisi kuwazuia,
Rabi twatakaamani, naupendo Tanzania,
Hawa ni Polisi gani? “Hawatufai nchini.
Tasa beti ninagota, jama mwisho nimefika,
Mkome kutukong’ota, bila haki twauzika,
Jahanam kyafokota, mauti yakiwafika,
Hawa ni Polisi gani? “Hawatufai nchini.
Almasi H. Shemdoe,
“Tunda laMatumaini”,
Dar es Salaam.
Chapwaga kijungu gani? (JIBU)
Bismilahi anzia, kwa jina lake Manani,
Akili toa pazia, yaje mpaka moyoni,
Swali uloulizia, jibu laja Mtauni,
Kijungu hicho CCM, chapwaga mali ya Umma.
Umeuliza maswali, na swali juu ya swali,
Wenyewe ni nani kweli, na chungu nini kamili,
Mimi kwangu mswahili, yapo maswali mawili,
Kijungu hicho CCM, chapwaga mali ya umma.
Swali la kwanza kijungu, CCM namba wani,
Fedha toka kwa Wazungu, zafujwa kama vitani,
Kweli yatia uchungu, uliza utiwe ndani,
Kijungu hicho CCM, chapwaga mali ya umma.
Swali la pili wenyewe, hao akina vingunge,
Na hujazaliwa wewe, wao wapo na Bunge,
Mi, si, mtoto ka, wewe, hapo bora tu nifunge,
Kijungu hicho CCM, chapwaga mali yaumma.
Saidi M. Buweta,
S.L.P. 22010,
Dar es Salaam.
Ukweli
Ukweli kitu adimu, katika hii dunia,
Ukweli japo muhimu, watu wanauchukia,
Ukweli watia hamu, kutaka kuusemea,
Ukweli waleta hofu, sababu unaumiza.
Ukweli taona kiza, ukitaka kuusema,
Ukweli utaumiza, utabebeshwa na dhima,
Ukweli utakimbiza, mamboyo yende mrama,
Ukweli taleta kifo, sababu unaumiza.
Ukweli unaachisha, kazizenye manufaa,
Ukweli unahamisha, uende usikojua,
Ukweli unafupisha, maisha yaliyotua,
Ukweli unaadui, sababu unaumiza.
Ukweli waleta chuki, jamaa takuhaini,
Ukweli tapata dhiki, uishipo duniani,
Ukweli ingawa haki, waja hawauthamini,
Ukweli una machungu, sababu unaumiza.
Ukweli ukishiriki, mpweke utabakia,
Ukweli una mikiki, wenzako takukimbia,
Ukweli hata rafiki, khiyana takufanyia,
Ukweli warusharoho, sababu unaumiza.
Ukweli utapuuzwa, uonwe usiefaa,
Ukweli utaburuzwa, khofu itakufikia,
Ukweli utakatizwa, furaha ulozoea,
Ukweli taadhibiwa, sababu unaumiza.
Ukweli ukiushika, watachukia nduguzo,
Ukweli watakuweka, mnyonge bila liwazo,
Ukweli watakucheka, kwa dharau na mabezo,
Ukweli utateseka, sababu unaumiza.
Ukweli mesisitizwa, na Allah Mola Jalia,
Ukweli umehimizwa, waja watu wajibia,
Ukweli umetukuzwa, kila mtu kuuvaa,
Ukweli ulete haki, ijapo unaumiza.
Ukweli usidanganye, haki ikatokomea,
Ukweli haki ufanye, japo wengine talia,
Ukweli uutawanye, watu wapate zoea,
Ukweli ulete tija, ijapo unaumiza.
Ukweli ukizoea, raha yake ya pekee,
Ukweli utazindua, wanyonge wasinyongee,
Ukweli tasimamia, haki kote isambae,
Ukweli sio dhuluma, ingawa unaumiza.
Ukweli na tuuvae, tuishi kwa usalama,
Ukweli tukumbatie, tuziepuke naqama,
Ukweli tuujengee, hima udumu daima,
Ukweli ulete nema, ingawa unaumiza.
Ukweli kitamalaki, neema zitajazana,
Ukweli tandoa dhiki, ufisadi na fitina,
Ukweli utadiriki, kusimamia amana,
Ukweli taleta kheri, ijapo unaumiza.
Ukweli pia amani, tajaa na kufurika,
Ukweli si kisirani, uhasidi tatoweka,
Ukweli si uhaini, bali haki kuiweka,
Ukweli iwe ibada, ingawa unaumiza.
Mwanoti A. Abdullah
Safarini Chake-Chake,Pemba.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
KERO katika Elimu ziondolewe
haraka
Chuo
Kikuu Dar wafanya mitihani katika Bwalo la chakula
Udini
wa CCM utaisambaratisha nchi -Tambwe
‘Kutoweka’
kanda ya Kakobe: CCM yatuhumiwa
Maalim
Seif awaambia Wazanzibari: Wenye mamlaka ya kumuweka mtu Ikulu ni wananchi
Mkapa
afurahia maendeleo Pwani
Wapinzani
wajiimarisha Moro
‘Zawadi’
ya Uchaguzi yatishia kusambaratisha taasisi ya Kiislam Tanga
Serikali
yakemea mwanamke kudhalilishwa
Ushauri Nasaha
Umuhimu
wa kushirikiana na majirani katika malezi ya watoto
MAKALA
Afande
Mahita, wananchi hatutaki Dola ya kipolisi
Makala
CCM
hawawezi kuondoa umasikini, ndio tegemeo lao
Kalamu ya Mwandishi
Makubaliano
kwa vitendo Z'bar
MAKALA
CCM
na sera za maendeleo (5)
Makala
Wanawake
na maendeleo: Je ni wimbo wa kuchaguliwa?
Makala
CCM
inatawala badala ya kuongoza
Habari
za Kimataifa
RIWAYA
Mapinduzi
ya fikra -4
Lishe
Unachotakiwa
kufanya kabla ya kuweka chakula kwenye jokofu
BARUA
MASHAIRI
MICHEZO
Raza kufungua mashindano
ya Wavu Zanzibar
Real Madrid yaota Ubingwa
leo
Kajumulo asema Yanga timu
ya Wananchi
|