|
Na. 049 Jumatano Mei 24 - 30, 2000 |
|
|
|
|
|
Wanawake na maendeleo: Je ni wimbo wa kuchaguliwa? Na Mwandishi Wetu Ni muda kiasi tokea kujitokeza kwa harakati za kijinsia na ukombozi wa mwanamke. Wengi wamekuwa na shauku ya kutaka kufahamu chanzo au asili ya harakati hizo. Huenda inawezekana ikawa ni zaidi ya pale watu walio wengi wanayafikiria kuwa ndio chanzo cha harakati za ukombozi wa wanawake duniani na waanzilishi wakawa ama wanawake wengine au hata wanaume. HATA hivyo, wapo baadhi ya wanawake ambao wanaonekana wakiipamba historia ya harakati za ukombozi wa maendeleo ya wanawake juu ya jukwaa la juhudi zao. Wamo akina Bibi Indira Gandi, Margareth Sanger, Hanan Ashrawi, Benazir Butho, Barbara Mikulowski, Margareth Thatcher na wamo pia akina Rudo Gaidzanwa Winnie Mandela, Marry Robinson na hata Hillary Clinton. Kwa hapa kwetu Tanzania wapo Getrude Mongela, Anna Mkapa, Dr. Ruth Meena, Leila Sheikh, bi Asha Bakari na hata Ummy Alley ingawa kila mmoja na historia yake, asili yake, mila zake au hata maslahi yake. Duniani kote kila ambapo pamewahi au kutakuwepo na dhulma, mateso, vita, maafa, uonevu, mapambano na kila aina ya fujo na ukatili, basi wanawake huwa ndio wanaathirikaau tuseme wahanga. Labda inaingia akilini kusema ni kwa sababu ya udhaifu, unaoambatana na maumbile yao. Pengine ni kwa sababu ya usemi wa Kiswahili usemao "wapambanapo mafahali wawili nyasi ndio ziumiazo." Bila ya shaka, mafanikio yamepatikana sana kwani hayo yote ni mapambano, na"hakuna mapambano yasiyokuwa na mafanikio" ingawa pia" hakuna mapambano yasiyokuwa na usaliti" ushahidi wa hayo ni pale ambapo wanawake wamepata sauti na vyombo vya Kimataifa. Pia mikataba na sheria mbali mbali zipo ambazo zinalinda hali na maslahi ya wanawake kama vile nafasi za uongozi, kumiliki mali na hata njia zote za udhalilishaji wa kujinsia kama kubakwa n.k. Lakini sasa mambo muhimu ya kujitathmini wao wanawake wenyewe, ni jee wamefikia au watafikia pale walipotaka kwenda au wajiulize ni wapi hasa wanakwenda au wanajipeleka wenyewe? Jee, wanataka kufikia pale Mcheza Tennis maarufu aliyesumbua sana akili za viongozi wa mchezo huo kwamba ashindane na wanawake au wanaume? Huyo ni "Rennee Rich" ambaye kimaumbile ya misuli na haiba alikuwa mwanamme, lakini baadaye aliweza kubadilisha jinsia na hata jina na akawa mwanamke. Jee, haionekani kuwa watu wengi na hata wanawake wenyewe wamekuwa na wasiwasi wa wengi katika wanawake hao wanaharakati kwamba wanawapeleka kusikoendeka? Wengi kati ya hao hawakubaliki, hasa pale ambapo mila na desturi huzipa mgongo na kuonekana kama "wake si waume." Jee, si wengi tu wanaojiuliza kwamba, kuishi na kuonekana kama wazungu au Wamagharibi, nusu Uchi, kukosa adabu na nidhamu, staha, na heshima ya ubinaadamu "ndio maendeleo wanayo -yalilia dada zetu na mama zetu hawa? Jee, si wao wanamiliki, soko la ukahaba chini ya kivuli cha haki na ukombozi wa mwanamke. Jee, hao Wamagharibi sio hao ambao wanaipendelea na kuikodolea macho zabibu zilizo juu ya mti wake ndani ya mila na desturi nzuriza Kitanzania, ili zidondoke wazitie mikononi. Yaani si wao ambao wanashiriki kuporomosha maadili yetu na kukosa kupambanua mke na mume au mzazi na watoto. Hao sio ambao wanaipa nguvu na kuitangaza biashara ya Umalaya? Ni karibuni pia zilipojadiliwa rasimu na sera za wanawake na watoto Bwawani Zanzibar ambapo Bw. Bakari Abeid, msanii maarufu aliwatahadharisha wanawake na mambo ya kuiga na kuwaambia "huko mnakotaka ni wapi na bado mnapendwa katika jamii yetu." Hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Salmin Amour alikuwa ni mgeni rasmi katika Mkutano maalumu wa wanawake wa kutekeleza azimio la Beijing la wanawake na uongozi, uliofanyika katika Uwanja wa Amani Asubuhi ya Jumamosi, tarehe Mei 13, mwaka huu mkutano ambao ulihudhuriwa naviongozi mbali mbali wa kitaifa na wa wanawake. Rais aliwapongeza na kuwaarifu wanawake kwa umoja wao hasa kutokana na kuwepo kwa sauti maalumu ya wanawake kimataifa kufuatia mikutano yao mbali mbali kama vile Mexico, Copenhagen, Cairo, Nairobi na Beijing, mikutano ambayo imetoa sura mpya ya harakati za wanawake duniani. Rais alisisitiza umuhimu wa wanawake kupatiwa elimu kama msingi wa maendeleo yote pamoja na jukumu lao kubwa la malezi hasa katika familia. Kama ilivyokuwa kawaida kwa viongozi wa wanawake katika Mkutano huo, rais alilipongeza bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha marekebisho ya katiba na pia kushtumu vikali viongozi wa upinzani katika baraza la Wawakilishi kwa kutokuukubali muswada wa marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ambao unawapa wanawake nafasi zaidi ya Uwakilishi ndani ya Baraza hilo. Wakati huo huo kwa mujibu wa kauli ya Kiongozi wa Upinzani ndani ya baraza la wawakilishi ambaye pia ni Mwakilishi wa CUF jimbo la Mgogoni Bw. Abubakar Khamis Bakari kuwa, hizo lawama hazina faida au msingi wowote. Kwani aliongezea kuwa, wanawake kama wanamsimamo wa kauli kweli, kwanza wangelikomboa nafasi yao moja ndani ya Baraza na pia kumtaka Rais Salmin angalau kuwapa kiti katika nafasi zake maalum. Kwa mujibu wa sheria wanawake wanazo nafasi kumi ndani ya Baraza la Wawakilishi ambapo hivi sasa wapo tisa na inahofiwa nafasi hiyo ya kumi ingelikuwa ya CUF. Rais pia aliwaambia wanawake kuwa wajue nafasi yao muhimu hasa kwa Uchaguzi Mkuu ujao "Naomba muonyeshe ushirikiano, msimamo imara wa kutetea haki na maslahi yenu, bila ya kuingilia misingi y adini", alisema Rais. Ili kufanikisha zaidi maendeleo yao, Rais aliwambia wanawake kuwa wakati umefika wa kuanzisha kamisheni maalum ya wanawake. Dosari kubwa zaidi ilionekana pale wanawake hao waliposhindwa kabisa kutoa kauli ya kumuunga mkono mwanamke mwezao, Bi. Amina Salum Ally ambaye amejitosa kugombea urais wa Zanzibar. Hali hii inaleta wasiwasi kuwa huenda
hata hizo agenda za huo mkutano na hizo lawama juu ya CUF siyo za wanawake
hao bali wao wanatumiwa tu ili kufikia malengo ya kisiasa ya chama tawala.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Chuo Kikuu Dar wafanya mitihani katika Bwalo la chakula Udini wa CCM utaisambaratisha nchi -Tambwe ‘Kutoweka’ kanda ya Kakobe: CCM yatuhumiwa Maalim Seif awaambia Wazanzibari: Wenye mamlaka ya kumuweka mtu Ikulu ni wananchi Mkapa afurahia maendeleo Pwani ‘Zawadi’ ya Uchaguzi yatishia kusambaratisha taasisi ya Kiislam Tanga Serikali yakemea mwanamke kudhalilishwa Ushauri Nasaha
MAKALA
Makala
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Makala
Makala
RIWAYA
Lishe
|
|
|
|
|