NASAHA
Na. 049 Jumatano Mei 24 - 30, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Makala

CCM inatawala badala ya kuongoza

Na Mussa Tamim

CCM wanatawala badala ya kuongoza, ndio maana pamoja na kujigamba kwa maneno mengi na proganda majukwaani bado hali halisi inawasuta. Kwani, ili waendelee kubaki madarakani hivi sasa wanatumia vitisho, rushwa, na wizi wa kura. Wapo madarakani kutetea maslahi yao tu na matumbo yao pekee kiasi kwamba mwananchi ameachwa na umaskini wa kutisha.

Pamoja na Tanzania kuwa ni nchi inayotambulika kama moja ya nchi maskini sana ulimwenguni, bado viongozi wake wanaishi maisha ya kifahari ambapo kila kukicha utawaona wakiwa na mashangingi, mabenzi na magari mengine ya kifahari. Wakati huohuo bajeti ya Wizara ya Afya ya kununulia madawa ikiwa ni kama tone moja la maji lidondokalo kwenye sindano kuingia ndani ya tangi kubwa tupu bila shaka halitoonekana. Hii ndio hali halisi.

Hata hivyo kwa mtu yeyote mwenye akili timamu akifika Tanzania leo atashangaa kuona hali ya wananchi na utajiri wa nchi, kuwa ni vitu visivyo shabihiana. Pamoja na nchi kujaaliwa ardhi pana ifaayo kwa kilimo, maliasili, madini lukuki ya kila aina na hali nzuri ya hewa, mtu atashangaa akiambiwa nchi hii ni miongoni mwa masikini wakutupwa duniani. Atashangaa zaidi akiambiwa kwamba kuna watu, tena ni wazaliwa na wazalendo wa nchi hii hii, ambao waliaminiwa na kukabidhiwa kuiongoza nchi hii kwa miaka ipatayo 40 ndiyo walio ifikisha nchi hapa ilipo. Ni lazima ashangae kwani nchi imekaa kana kwamba haina viongozi. 

Mbaya zaidi ni pale ambapo demokrasia inapominywa makusudi ili kuzuia upinzani dhidi ya chama cha tawala. Chama ambacho serikali yake inawakamua wananchi kwa kodi ‘milioni kidogo’ kisha inawakebehi kuwa ni "wavivu wa kufikiri" ndio maana hawaoni kwamba maisha yao ni bora zaidi leo kuliko miaka ya nyuma, ambapo hata kama ingekuwa ni kweli bado ulikuwa ni utawal wa chama kilekile na wala si kingine. Jamani hii ni jeuri ya watawala. Wangekuwa ni viongozi bila shaka wasingethubutu kuyanena hayo. 

Hata hivyo siwezi kushangaa wakisema kwamba kwao wao hali nzuri ni kutokuwa na madawa hospitali, kutokuwa na madawati mashuleni ambapo watoto wanasomea sakafuni, walimu kutolipwa mishahara yao kwa wakati, kukosa vitabu, kukosa vifaa vya kufundishia, kukosa barabara, umeme kuwa ghali, simu kuwa ghali, mwananchi kulimbikiziwa kodi, magereza kuwa nusu ya kaburi, nk. 

Pamoja na hali kuonekana kama ilivyo hivi sasa, bado watawala haiwashtui na badala yake wanakuja na nyuso zao zisiokuwa na haya wakinadi kuwa CCM ndio chama pekee kitakachotuletea maendeleo. Kama mmeshindwa kuyaleta miaka 40 iliyopita mtaweza miaka mitano tu?!!

Ajabu ya watu hawa wanatugeuza sisi wote wajinga na wapumbavu. Bila shaka hivi sasa umefika wakati wa kukubali ukweli uliopo mbele ya macho yetu kwamba CCM imeshindwa kuongoza nchi badala yake inatawala.

Ushauri wa bure nilionao kwa viongozi wa CCM na wanachama walalahoi wa CCM waliojaa umaskini ni kwamba kwa amani kabisa wasaidie kukipa chama kingine cha siasa nafasi ya kuongoza nchi kwa kuichia demokrasia ichukue mkondo wake. Kwa amani kabisa watoke kwenye hicho kiti walichokalia kwa miaka 40 na kuteremka chini ili wananchi wengine wenye uchungu na roho za Watanzania washike madaraka ya kuongoza. Ni kweli nyuki kuacha asali ni muhali, lakini ndugu zetu ‘CCM’ kazi tuliyowapa kwa miaka 40 imewashinda sasa tokeni tuwape wengine.
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
KERO katika Elimu ziondolewe haraka

Chuo Kikuu Dar wafanya mitihani katika Bwalo la chakula

Udini wa CCM utaisambaratisha nchi -Tambwe

‘Kutoweka’ kanda ya Kakobe: CCM yatuhumiwa

Maalim Seif awaambia Wazanzibari: Wenye mamlaka ya kumuweka mtu Ikulu ni wananchi

Mkapa afurahia maendeleo Pwani

Wapinzani wajiimarisha Moro

‘Zawadi’ ya Uchaguzi yatishia kusambaratisha taasisi ya Kiislam Tanga

Serikali yakemea mwanamke kudhalilishwa

Ushauri Nasaha
Umuhimu wa kushirikiana na majirani katika malezi ya watoto

MAKALA
Afande Mahita, wananchi hatutaki Dola ya kipolisi

Makala
CCM hawawezi kuondoa umasikini, ndio tegemeo lao

Kalamu ya Mwandishi
Makubaliano kwa vitendo Z'bar

MAKALA
CCM na sera za maendeleo (5)

Makala
Wanawake na maendeleo: Je ni wimbo wa kuchaguliwa?

Makala
CCM inatawala badala ya kuongoza

Habari za Kimataifa

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra -4

Lishe
Unachotakiwa kufanya kabla ya kuweka chakula kwenye jokofu

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Raza kufungua mashindano ya Wavu Zanzibar
  • Real Madrid yaota Ubingwa  leo
  • Kajumulo asema Yanga timu ya Wananchi

  •  


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita