NASAHA
Na. 049 Jumatano Mei 24 - 30, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Habari

Mkapa afurahia maendeleo Pwani

Na Y. Kijukuu

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti waCCM Taifa, Mhe. Benjamin William Mkapa ameridhishwa na Taarifa ya maendeleo ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Lugoba tarafa ya Msoga maili chache kutoka Chalinze jana, Mhe. Mkapa aliwaambia wanakijiji hao kuwa maendeleo yaliyopatikana wilayani humo yametoka na utekelezaji mzuri wa sera za chama chake.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo akisoma taarifa ya maendeleo ya Wilaya hiyo mbele ya Rais Mkapa, alisema wilaya yake imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya elimu na uzalishaji wa zao la mahindi.

Mhe. Mkapa anaendelea na ziara yake mkoani Pwani ambapo tayari amekwisha tembelea wilaya ya Kibaha. 


Wapinzani wajiimarisha Moro

  • CUF yafungua matawi zaidi
  • Tawi la CCM lafungwa
  • TLP, Chadema, UDP watoa salaam
Na Mwandishi Wetu

Nguvu ya vyama upinzani dhidi ya chama tawala katika wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro imezidi kuimarika na hivyo kuongeza kitisho kwa chama tawala cha CCM katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Oktoba, mwaka huu, uchunguzi wa gazeti hili umebaini.

Kuimarika kwa nguvu hiyo kunafuatia ziara ya Mwenyekiti waTaifa wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba aliyoifanya hivi karibuni wilayani hapo ambapo pamoja na kufanya mikutano mikubwa ya hadhara na kuongea na wananchi alifungua matawi mapya ya chama hicho na kutoa kadi kwa wanachama wapya.

Miongoni mwa matawi yaliyofunguliwa ni pamoja na Tawi la Wenyemaguta ambalo awali palikuwa na tawi la CCM. Zaidi ya wanachama 60 wa CCM wameripotiwa kukihama chama hicho tawala na kujiunga na CUF hali ambayo imepelekea tawi la CCM Wenyemaguta kufungwa na bendera ya chama hicho kukabidhiwa kwa Profesa Lipumba.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa CUF wa Wilaya ya Kilombero Bw. Lihema imesema mpaka wakati Profesa Lipumba anaondoka Ifakara zaidi ya wana-CCM 250 walikuwa wamerudisha kadi zao na kujiunga na CUF. Aidha, jumla ya matawi 20 yalikuwa yamefunguliwa.

Akizungumza na wananchi katika viwanja vya Kiungani, Ifakara, Profesa Lipumba ambaye anatarajiwa kugombea urais kwa tikiti ya chama chake alisema dhiki ya maisha inayowakabili wananchi wa eneo hilo imetokana na nipango mibovu ya kiuchumi ya chama tawala na serikali yake kwa vile Ifakara inao utajiri mkubwa wa rasilimali.

Alisema zao la mpunga limekuwa likikauka kutokana na jua kali wakati Ifakara inavyo vyanzo vya maji vya kutosha ambavyo vingeweza kutumika kwa umwagiliaji.

Profesa Lipumba ambaye anatarajiwa kuchuana na mgombea urais kwa tikiti ya CCm katika uchaguzi wa mwaka huu aliwahimiza wananchi hao kujitokeza kwa wingi muda wa kujiandikisha utakapofika na kisha kupiga kura ili "kuchagua chama kitakachoandaa mipango madhubuti ya kuinua hali za wananchi".

"...CUF ni chama chenu wananchi... kipo (kwa ajili ya) kumkomboa mwananchi na kauli yetu ni ‘Haki sawa kwa wote’..."

Aliwaomba wawe wamejiandikisha katika muda wa siku kumi za mwanzo za uandikishaji wapiga kura ili kuhakikisha kuwa mtu hachelewi kujiandikisha japo kwa bahati mbaya.

Aidha, aliwataka wanachi hao wajiandae kuzilinda kura zao "zisiibiwe na ving’ang’anizi wa madaralka."

Awali, akizungumza na wazee wa Ifakara, Profesa Lipumba alisema Ifakara ni moja tu ya sehemu za kadhaa za Tanzania ambazo hazinufaiki na rasilimali zilizomo katika sehemu hizo kutokana na "mipango mibovu ya uchumi" ya chama tawala cha CCM.

"mabadiliko hayataletwa na wageni bali ninyi wenyewe ... na mwaka huu ndio wa kuibadili hali hii mbovu" alisema Profesa Lipumba. Mikutano hiyo pia ilihidhiriwa na viongozi wa wilaya wa vyama vya siasa vya UDP, Chadema na TLP.


‘Zawadi’ ya Uchaguzi yatishia kusambaratisha taasisi ya Kiislam Tanga

Na Mwandishi Wetu

Kuna habari kwamba Taasisi kongwe ya Kiislam iliyopo mjini Tanga imo hatarini kusambaratika kutokana na ‘zawadi’zilizokwishaanza kutolewa za maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini kote Octoba 29 mwaka huu.

Taasisi hiyo maarufu ambayo ina miaka zaidi ya 30 na miongoni mwa wanafunzi wake sasa ni masheikh katika mikoa mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa mpashaji habari wetu, viongozi wa taasisi hiyo tayari wameshafuatwa na kupatiwa ‘kitita’ ili kukipigia debe chama tawala katika uchaguzi mkuu ujao.

Wakazi wengi wa Tanga hususan Waislam wamekuwa wakiilaumu Taasisi hiyo kwa kujiweka katika hali na sura kama ya BAKWATA. BAKWATA imekuwa ikilalamikiwa na Waislam kuwa imekuwa ni chombo cha kuitumikia serikali na chama chake badala ya kuwatumikia Waislam. Uthibitisho unaotolewa kuonyesha kuwa BAKWATA ni chombo cha serikali ni ile kauli ambayo ilitolewa na Sheikh Mkuu wa BAKWATA wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa BAKWATA imeundwa na serikali. Kwa sasa hivi Sheikh Mkuu wa BAKWATA amefanya ziara mikoani na vyombo vya habari vimeripoti kuwa msafara wake umekuwa ukimpigia debe Rais Mkapa.

‘Kitita’ambacho kimetolewa kwa taasisi hiyo ya mkoani Tanga ndicho kilichosababisha mgogoro ambao unahatarisha kuisambaratisha. Inasemekana kuwa mgao wa kitita kilichodaiwa kutolewa umefanywa kiukoo hivyo kuwafanya wale masheikh wa mikoani (ambao ni wanafunzi wa taasisi hiyo) walioko nje ya mkoa wa Tanga kutaka kujua kwa nini wao wamekosa mgao huo wakati wao pia hutumika kueneza kampeni za chama tawala kinachotoa tenda na mgawo huo. Hali hii ya kutoelewana juu ya mgao huenda ikapelekea kupanguka kwa safu ya viongozi wa taasisi hiyo waliopo Tanga na nje ya mkoa huo. Habari hizo zinaendelea kupasha kuwa suala la taasisi hiyo kupewa ‘zawadi’ katika kipindi cha uchaguzi sio geni kwani mwaka 1995 baada ya ‘kitita’ kutolewa ,taasisi hiyo ilifanya kampeni kubwa ya kuwajenga baadhi ya viongozi wa kisiasa wa ngazi za juu nchini.

Tofauti na mwaka 1995, kipindi hiki kitita kimetolewa wakati kuna mabadiliko ya uongozi wa ngazi za juu katika taasisi hiyo. Kiongozi aliyekuwepo mwaka 1995 alikuwa na hadhi ya kuaminika, hakuulizwa kwa chochote alichokifanya. Kiongozi huyo alikuwa na uwezo wa kufanya chochote bila kuulizwa. Katika kipindi hiki kiongozi aliyekuwapo inaelekea hakukubalika wala kuaminika kusimamia mgao hususan na ndugu wa kiongozi wa zamani, ambao wanaona wao ndio waliostahili kushika wadhifa wa juu katika taasisi hiyo.

Habari zimesemwa kuwa ndugu hao ili kumdhibiti kiongozi ‘aliyerithi’ waliunda cheo ambacho kina hadhi ya juu zaidi na kushikwa na mmoja wa ndugu hao wa familia moja. Hatua hii ilipekea kiongozi aliyerithi madaraka kuamua kujitoa. Wako wanaosema kujitoa huku ni kwa shinikizo na wengine wanasema ni kutaka kulinda hadhi yake.

Baada ya kujitoa kwa kiongozi huyo nafasi yake sasa amepewa Sheikh mwingine. Habari zinasema kuwa Sheikh huyo haaminiki na chama kinachodaiwa kutoa zawadi hizo. Kutokana na msimamo wake wa kutotaka Waislam kuwa ngazi ya kuwapandishia vyeo madhalimu,habari za kuwepo kwa kiongozi huyo asiyependa dhulma dhidi ya Waislam zimepelekwa kwa viongozi wa juu wa chama kilichotoa tenda ya kupigiwa debe uchaguzi na inasemekana tayari viongozi wa chama hicho wameishatoa kitita kingine ili sheikh huyo aondolewe madarakani. Kutokana na hali hii waislam wengi mkoani Tanga wameitaka Taasisi kuacha kabisa kupigia debe chama kinachodhulumu waislam na kwamba endapo haitaacha imedaiwa kuwa waislam wataipiga pande. Mkoa wa Tanga ni moja ya mikoa ambayo ina hali ngumu kimaisha kutokana na kutokuwepo kwa ajira na maendeleo mazuri kwa wananchi wake. Ni kutokana na hali hiyo ambayo imekithiri zaidi wilaya ya Tanga, vijana wengi wamejitokeza kutaka mabadiliko ya uongozi ili waondokane na umaskini uliopo mkoani humo.


Serikali yakemea mwanamke kudhalilishwa

Na Tinker Mdimu

Vyombo vya habari hasa vituo vya televisheni vimetakiwa kulinda maadili ya jamii ya Kitanzania ili kilinda heshima ya mwanamke.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Athumani Mdoe, wakati akifunga semina juu ya tathmini ya maazimio ya mkutano wa Copenhagen, iliyofanyika katika jumba la sanaa jijini wiki hii.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa televisheni ni chombo muhimu cha kuelimisha na kuburudisha jamii, hatahivyo alitahadharisha kuwa ni muhimu maadili ya Kitanzania yakazingatiwa na heshima ya mwanamke ilindwe.

Alifafanua Mhe. Mdoe kuwa kuonesha picha za wanawake walio nusu uchi katika matangazo ya televisheni ni kinyume cha maadili ya Mtanzania na kwamba kufanya hivyo ni kuwadhalilisha wanawake ambao ni mama, shangazi na dada zetu.

Semina hiyo iliyofanyika katika jumba la sanaa jijini ilifanyika kwa siku mbili, Mei 19 na 20 mwaka huu, ikiwa na lengo la kufanya tathamini ya maazimio ya Copenhagen.

Katika mojawapo ya maazimio ya Copenhagen yaliyofikiwa mwaka 1995 ilikuwa ni kuweka mazingira mazuri kisiasa, kichumi, kijamii na kiutamaduni ili kuwawezesha wananchi kuendelea kijamii katika sekta zote.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya alitoa changamoto kwa wanasemina kuufikisha ujumbe waliopata katika semina kwa wanawake walioko majumbani, makazini na katika vikundi mbali mbali.
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
KERO katika Elimu ziondolewe haraka

Chuo Kikuu Dar wafanya mitihani katika Bwalo la chakula

Udini wa CCM utaisambaratisha nchi -Tambwe

‘Kutoweka’ kanda ya Kakobe: CCM yatuhumiwa

Maalim Seif awaambia Wazanzibari: Wenye mamlaka ya kumuweka mtu Ikulu ni wananchi

Mkapa afurahia maendeleo Pwani

Wapinzani wajiimarisha Moro

‘Zawadi’ ya Uchaguzi yatishia kusambaratisha taasisi ya Kiislam Tanga

Serikali yakemea mwanamke kudhalilishwa

Ushauri Nasaha
Umuhimu wa kushirikiana na majirani katika malezi ya watoto

MAKALA
Afande Mahita, wananchi hatutaki Dola ya kipolisi

Makala
CCM hawawezi kuondoa umasikini, ndio tegemeo lao

Kalamu ya Mwandishi
Makubaliano kwa vitendo Z'bar

MAKALA
CCM na sera za maendeleo (5)

Makala
Wanawake na maendeleo: Je ni wimbo wa kuchaguliwa?

Makala
CCM inatawala badala ya kuongoza

Habari za Kimataifa

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra -4

Lishe
Unachotakiwa kufanya kabla ya kuweka chakula kwenye jokofu

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Raza kufungua mashindano ya Wavu Zanzibar
  • Real Madrid yaota Ubingwa  leo
  • Kajumulo asema Yanga timu ya Wananchi

  •  


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita