NASAHA
Na. 049 Jumatano Mei 24 - 30, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Makala

CCM hawawezi kuondoa umasikini, ndio tegemeo lao

Na Rajab Nkawa

Propaganda na kelele zinazopigwa na viongozi wa CCM juu ya jitihada zao za kuutokomeza umasikini mkubwa unaowakabili Watanzania kwa asilimia hamsini ifikapo mwaka 2010 ni porojo tupu na kamwe sio kusudio lao.

Ukiangalia kwa uchambuzi wa kina matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwaka 1995, utagundua kuwa CCM ilipata ushindi mkubwa katika mikoa ya Tanga na Kusini, mikoa ambayo inaongoza kwa umasikini hapa nchini. Hii ni kwakuwa ni rahisi zaidi kuinyang’anya haki ya maskini hata kama anajua kuwa hapa hatendewei haki.

Katika safari zangu za mikoani nilifika Handeni, katika jimbo la uchaguzi la Handeni Mashariki ambalo wakati huo lilikuwa ni nguzo kubwa ya CCM, kwani ndilo lililoongoza kwa kumpa kura nyingi Mgombea wa urais wa chama hicho. Hali ya umasikini katika jimbo hilo ni ya kutisha ambapo nilimshuhudia msichana mwenye umri takriban wa miaka 16 akiwa amejifunga upande mmoja wa kanga akielekea shuleni. Unaweza kupata picha ya jinsi gani alivyo.

Sasa mama wa msichana huyu ambaye ameshindwa kummnulia sare ya shule bint yake huyo, ukampa kanga vipande viwili (doti moja); moja ya kwake na nyingine ampe mwanaye kwa ajili ya kwendea shule kama sare si tayari umeshapata kura yake! Au kijana wa kijijini katika maeneo yaliyoshambuliwa na umasikini umpe shilingi elfu tano si tayari umeshampa mahari ya kuolea ataacha kweli kukupigia kura! Mifano kama hii ipo mingi ambayo mingi wasomaji mnailewa nyema.

Hoja yangu hapa ni kuwa kelele wanazopiga CCM kuwa wao wananguvu zaidi vijijini si kweli isipokuwa ule umaskini wa wananchi katika maeneo hayo ndio unaowalazimisha kuikumbatia. Na kwa kweli watu hawa hawana huruma hata kidogo. Hawana huruma kwa sababu wale wanaowapandia migongoni ili kupata madaraka hawataki kuwasaidia, kwani wakisaidia wanajua kuwa hawatapata tena kura zao. Hivyo ni lazima waendelee kuwa masikini. Ndio maana maeneo yale ambayo yameshtadi kwa umaskini ndio CCM inanguvu zaidi, lakini ambayo watu wake wananafuu kidogo ya maisha CCM imepoteza wanachama na wafuasi.

Baada ya utangulizi huo sasa navunja hoja za serikali zilizotolewa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Edward Lowasa katika warsha iliyozungumzia namna ya kupambana na umasikini. Warsha hiyo ilitayarishwa na taasisi ya utafiti wa kupambana na umaskini (REPOA).

Lowasa alisema kuwa serikali imedhamiria kutokomeza umasikini kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2010, na kwamba ili kufikia lengo hilo uchumi ni lazima uwe unakuwa kwa asilimia 6-7 kwa mwaka, ambapo kwa sasa kiwango cha kukua kwa uchumi cha asilimia 4 kinaridhisha.

Akitaja mikakati ambayo serikali imeipanga alisema serikali kwanza itaboresha kilimo kwa kuwa asilimia 80 ya Wantanzania wanategemea kilimo na kwamba robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje zinatokana na kilimo.

Kwanza nianze na sekta ya kilimo. TANU ambayo iliizaa CCM ilipochukua uongozi wa nchi hii baada ya kuvisambaratisha vyama vingine vya siasa ilifahamika wazi kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa hili. CCM ilipokuja nayo ilikuwa inalijua hili. Sasa baada ya miaka 40 ya utawala wanakuja na nyimbo zilezile kuwa eti wataboresha kilimo kwa sababu asilimia 80 ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea kilimo.

Inabidi watueleze wanaposema wataboresha kilimo wanakusudia nini hasa; wakati wakulima katika baadhi ya maeneo hapa nchini wamekata na kung’oa mikahawa yao kwa kukosa soko, embe katika mikoa ya Pwani na Kusini zinaoza wakati juisi ya embe inaagizwa kutoka Arabuni. Bei ya mpunga Ifakara hailipi gharama za uzalishaji wake wakati bei ya mchele huo huo hapa Dar es Salaam ni shilingi 500 kwa kilo.

Hapa tatizo kubwa linaloonekana sio kuwa wakulima eti wanashindwa kulima la hasha, tatizo ni wapi watauzia bidhaa zao. Tatizo ni uchakavu na kukosekana kwa mawasiliano ya barabara, reli na ndege kutoka maeneo ya uzalishaji mpaka maeneo ya walaji. Kwa kifupi ni kuwa soko la ndani japokuwa ni kubwa na pana bado wakulima wanashindwa kulifikia na hivyo kukosa morali na tija katika kilimo.

Aidha Mhe. Lowassa alisime kuwa serikali itajitahidi kupunguza tatizo la ajira kwa kuwasaidia Watanzania wajiajiri wenyewe katika biashara ndogondogo na viwanda vidogovidogo.

Hapa ndipo serikali ya CCM inapofanya kampeni za kujipatia kura kupitia mgongo wa masikini ambao ni asilimia kati ya 70-80 ya Watanzania wote. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Bw. Helson Mahimbo, aliyesema kuwa tatizo la umasikini halitaondoka hadi hapo serikali itakapoweka SERA madhubuti za kukabiliana na tatizo hilo zinazowalenga watu masikini waishio mashambani.

Lazima ifahamika kuwa Watanzania sio wavivu, ni wahangaikaji wanapenda kujituma katika kujitafutia riziki zao za kila siku, tatizo lipo kwenye uongozi wa nchi. 

Jaalia kijana kapewa mkopo ili afanye mathalan biashara ya vyakula. Anajua wazi kuwa bei ya ndizi za kukopa bei yake hapa jijini ni kubwa, lakini hana namna ya kuzifikisha ndizi hizo hapa jijini halafu auze kwa bei ya faida, kutokana na gharama kubwa ya usafirishaji. Kwasababu ndizi zitatoka Tanzania, kwenda Uganda, Kenya na kurudi tena Tanzania. Kisa hakuna barabara ya kuaminika kati ya Dar es Salaam na Bukoba. Sasa biashara gani huyu kijana atakayofanya.

Lakini pia lazima tujuwe kuwa viwanda vidogo vya kuchonga fenicha (samani), kutengeneza koroboi, mikeka na nguo za batiki vitakuwepo tu ikiwa wanajamii wengine wanakazi za kuajiriwa. Kwa kifupi ni kuwa mtu ataweza kijijini tu ikiwa wangine wamejiriwa.

Jaalia kuna viwanda vikubwa ambavyo bidhaa zake zinauzwa nje ambavyo viko ndani ya mji mmoja mathalan Dar es Salaam ambavyo vina uwezo wa kuajiri watu laki mbili na kila mtu alipwe mshahara wa shilingi elfu hamsini tu. Ina maana kila mwisho wa mwezi kutakuwa na shilingi bilioni 10 katika mikono ya watu katika mji huo. Hivyo basi wapo watakaohitaji fenicha, batiki n.k. Hapo viwanda vidogo navyo vitashamiri. Lakini bila ya kuwa na viwanda vikubwa na sekta nyinginezo zitakazotoa ajira kwa watu wengi ni ndoto kuimarika kwa biashara na viwanda vidogovidogo.

Sasa ukiangalia yale yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tatu toka iingie madarakani utakuta zaidi ni kuiporomoshaajira kwa kiwango cha kutisha. Viwanda vingi vilivyouzwa, mfano kiwanda cha kutengenezea taa za umeme, light source manufacturers, havifanyikazi tena ya uzalishaji. Vimekuwa ni maghala ya kuhifadhia bidhaa zinazotengenezwa katikka nchi ambazo makampuni hayo yanatoka.

Sasa utasemaje kuwa unapambana na umasikini bila ya kwanza kuongeza ajira. Na utasemeje unataka kuimarisha biashara ndogondogo na viwanda vidogovidogo wakati huna watu wa kuwauzia. Huo ni udanganyifu mkubwa kwa wananchi hasa wale ambao bongo zao zimelala kutokana na propaganda hizo.

Bila kuwa na mipango madhubuti ya kuongeza ajira itakayokwenda sambamba na sera ya kutumia vizuri maliasili yetu katika kuweka misingi mizuri ya miundo mbinu kama vile barabara, reli, simu, maji n.k. na vyote hivyo vikawa vinapatikana kwa bei nafuu, ni ndoto kuondoa umasikini. Pamoja na kuwepo mpango maalum wa misaada (TAS) na mpango maalum wa kupambana na umasikini (PRSP) ambayo inandaliwa na serikali hatutegemei lolot kubadilika.

Lakini turudi palepale kuwa hizo zote ni geresha tu, lengo liko palepale; wananchi waendelee kuwa masikini ili waweze kutawalika na ndio maana haistaajishi kuwa kiwango cha elimu ya msingi kwa mwananchi wa Tanzania ni darasa lasaba. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
KERO katika Elimu ziondolewe haraka

Chuo Kikuu Dar wafanya mitihani katika Bwalo la chakula

Udini wa CCM utaisambaratisha nchi -Tambwe

‘Kutoweka’ kanda ya Kakobe: CCM yatuhumiwa

Maalim Seif awaambia Wazanzibari: Wenye mamlaka ya kumuweka mtu Ikulu ni wananchi

Mkapa afurahia maendeleo Pwani

Wapinzani wajiimarisha Moro

‘Zawadi’ ya Uchaguzi yatishia kusambaratisha taasisi ya Kiislam Tanga

Serikali yakemea mwanamke kudhalilishwa

Ushauri Nasaha
Umuhimu wa kushirikiana na majirani katika malezi ya watoto

MAKALA
Afande Mahita, wananchi hatutaki Dola ya kipolisi

Makala
CCM hawawezi kuondoa umasikini, ndio tegemeo lao

Kalamu ya Mwandishi
Makubaliano kwa vitendo Z'bar

MAKALA
CCM na sera za maendeleo (5)

Makala
Wanawake na maendeleo: Je ni wimbo wa kuchaguliwa?

Makala
CCM inatawala badala ya kuongoza

Habari za Kimataifa

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra -4

Lishe
Unachotakiwa kufanya kabla ya kuweka chakula kwenye jokofu

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Raza kufungua mashindano ya Wavu Zanzibar
  • Real Madrid yaota Ubingwa  leo
  • Kajumulo asema Yanga timu ya Wananchi

  •  


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita