|
Na. 049 Jumatano Mei 24 - 30, 2000 |
|
|
|
|
|
Umuhimu wa kushirikiana na majirani katika malezi ya watoto NA KHADIJA IDD Kwa mzazi anayemfahamu mtoto wake, anajua vyema tabia yake na iwapo kuna mabadiliko yoyote mara moja anagundua. Mzazi huyu atajua pia kuwa tabia hiyo anaweza kuwa ameipata wapi. Kutokana na ukweli huu, utasikia mara nyingi sana mzazi akilalamika kwamba, "mtoto wa fulani amemfundisha mwanangu kutukana", au tabia hii ya mwanangu ameiiga kwa fulani." Hali hii si bahati mbaya au balaa lakini ni jambo la kawaida na ni sehemu ya maisha ya watoto ambao hujifunza mambo yanayowazunguka kwa kuiga na kujaribu. Mzazi huweza kukasirishwa sana na hali hii na pengine akachukua uamuzi wa kumpiga au kumfungia mwanawe asiende kwa jirani, lakini je tabia hiyo mbaya itaondoka katika mazingira yanayomzunguka mtoto? Kukasirika huku hakuna maana yoyote kwani chanzo cha tabia mbaya ya mtoto bado kiko palepale. Vile vile tatizo si mtoto kumuambukiza mwingine tabia fulani bali ni ile tabia mbaya. Na je mzazi umechangia nini au umefanya nini ulipoiona tabia hii ya mtoto wa jirani yako? Katika mazingira tunayoishi, mzazi humfundisha, vizuri mtoto wake kuhusu mambo mbalimbali pamoja na maadili yanayotakiwa katika nyumba na jamii. Mtoto hukua katika maisha ya namna ambayo mzazi wake amemfundisha na hutenda vyema kadiri alivyoelekezwa. Lakini pamoja na hali hii, mtoto huyu haishi peke yake hapa ulimwenguni, ulimwengu unaomzunguka una mchango wake kwa mtoto huyu. Watu na vyombo vya habari huweza kumpa maelekezo ambayo hakufundishwa na wazazi wake . Na hapa ndipo ushirikiano na majirani unapohitajika. Mazingira ya nje yanapomuathiri mtoto na kuharibu malezi mazuri aliyopata, mambo mbalimbali huweza kutokea. Mtoto mwenyewe huweza kuficha tabia hizo na hivyo wazazi wakawa hawazijui. Lakini mara waondokapo huzidhihirisha na watu wanaoweza kugundua mabadiliko haya ni majirani, majirani hawa hufahamu mtoto ana marafiki gani na huweza kufahamu pia wanafanya vitu gani wanapokuwa pamoja, kwa mfano kuvuta sigara au bangi, kwenda disko n.k. Pamoja na kugundua mabadiliko ya tabia mtoto, majirani pia (baadhi) huwa ndio wanaowashawishi na kuwashauri watoto kutenda kinyume na maelekezo ya wazazi. Hawa wanaelewa maadili yanayofuatwa katika nyumba ya mtoto husika, lakini kwa sababu hakubaliani nayo huamua kumfundisha mtoto kutenda kinyume. Iwapo wazazi hawatachunguza wataona tu mabadiliko ya tabia ya mtoto na hawajui kwa nini, kwa vile jirani huyu hutumia ule muda ambao wazazi hawako nyumbani. Kutokana na uhusiano huu na maathiriano yaliyopo kuna umuhimu mkubwa kwa wazazi wanaoishi jirani kufanya kazi hii ya malezi kwa ushirikiano kwani kwa kufanya kazi pamoja watalea watoto vyema bila ya mzazi mmoja kufikiria mtoto wa mwingine anamuharibu wa kwake. Wazazi hawa watatoa maelekezo yasiyopingana na iwapo kuna tofauti wataeleweshana. Mtoto mmoja anapokuwa na tabia isiyostahiki atakanywa na mzazi yoyote na hivyo atakuwa (mtoto) hana sehemu ya kuficha uovu wake. Kukataza mtoto wako asicheze kwa jirani kwa sababu ya tabia fulani mbaya haisaidii sana, bali jambo la kwamba ni kwa mzazi kumuonya mtoto wa jirani yake kwa upole na kumueleza mwenendo mzuri. Unapofanya hivi utamsaidia yeye na mtoto wako pia. Kumfungia si dawa kwani wanaweza kukutana shule, dukani, bombani n.k. na mtoto wako atatumia muda mfupi alionao kujifunza mengi ambayo umeyakataza. Hata hivyo hili halitatokea iwapo utamuonya kama mwanao unayempenda, na mwanao asingeathirika. Wakati mwingine kunakuwa na uadui fulani baina ya majirani. Kwa ajili ya malezi bora ya watoto ni jambo muhimu kwa majirani hawa kusuluhisha mgogoro huo mapema kwani wasipofanya hivyo, hali hii itasababisha kuporomoka kwa maadili na kuharibika kwa tabia za watoto. Hata kama u-mchaMungu kiasi gani usipokuwa na ushirikiano na jirani zako ucha Mungu au Ulokole wako hautaonekana kwa watoto wako au ndugu unaoishi nao. Jirani hatakusaidia kukosoa tabia ya mtoto yako na wakati mwingine huishangilia tabia mbaya anayoifanya. Tatizo lolote likitokea kwako jirani huona "umepatikana" na husikika akisema kwa furaha "yako wapi basi, alijifanya mwenye imani kali", "tulijua yatamshinda......n.k." Hali hii isingetokea na haya yote yasingesemwa kama ungemaliza ugomvi mapema na kushirikiana na jirani yako. Jirani kama rafiki huona yale ambayo
wewe mwenyewe huyaoni. Kushirikiana nao kutasaidia kujua matatizo ya wanao
uliyokuwa huyajua na vile vile kufahamu njia bora ya kutatua yale ambayo
unayajua. Kulalamika hakusaidii, watoto kuigana na kufundishana ni hali
halisi ya maisha yao,bali tuwasaidie waige na kufundishana yaliyo mema.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Chuo Kikuu Dar wafanya mitihani katika Bwalo la chakula Udini wa CCM utaisambaratisha nchi -Tambwe ‘Kutoweka’ kanda ya Kakobe: CCM yatuhumiwa Maalim Seif awaambia Wazanzibari: Wenye mamlaka ya kumuweka mtu Ikulu ni wananchi Mkapa afurahia maendeleo Pwani ‘Zawadi’ ya Uchaguzi yatishia kusambaratisha taasisi ya Kiislam Tanga Serikali yakemea mwanamke kudhalilishwa Ushauri Nasaha
MAKALA
Makala
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Makala
Makala
RIWAYA
Lishe
|
|
|
|
|