AN-NUUR 
Na.177 Shaaban  1419, Novemba 27 - Desemba 3, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Mashairi
 

AN-NUUR  mjumbe mwema

AN-NUUR yako miali, baidi inafikia,
Wasomaji mbalimbali, nuru waifurahia,
Imekuwa ni muhali, ulivyo kukuchukia,
Ndugu umeniungia, An-Nuur mjumbe mwema.

Wewe ni mjumbe mwema, kwenye kheri waitia,
Wamekwitika kauma, kwako twakutanikia,
Mfano wa itiswama, tunapo pa kushikia,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

Umeutoa uwanja, nasi tukauingia,
Humo tunakuta hoja, fahamu zenye kutia,
Unajengeka umoja, na imani kutwingia,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

Awali sikuwajua, hata nao kwangu pia,
Kurasa tumefunua, ndani tukakutania,
Humo tukayavumbua, mengi ya kutufalia,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

Jicho halijawaona, wao wamenandikia,
Korogwe si mbali sana, bali sijapafikia,
Huko amepatikana, ndugu wa kunililia,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

Mwingine yuko Kigoma, na huko napasikia,
Nimepata ndugu mwema, dini ndio kaingia,
Baruaye nimesoma, An-Nuur kanikutia,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

Mpanda siachi kutaja, nimewahi kuingia,
Yuko kakangu wa haja, jichoni sijamtia,
Tumejuana pamoja, gazetini kupitia,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

Na Tabora pia wako, ndiko nilikoanzia,
Nawajua walioko, ndugu walojaa nia,
Huja kwangu maandiko, salamu kunitumia,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

Hata wa Darisalama, kuliko na Tanzania,
Gazeti wanolisoma, na nakishi kulitia,
Wapo wanipao hima, na tungo kuzipitia,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

Na Mwanza wamenijua, shule nilikopitia,
AN-NUUR meniinua, salamu nazipokea,
Na nasaha nachukua, na dua kuitikia,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

Bali na hapa jirani, si mbali kupafikia,
Ni Mwadui mgodini, Maganzo unapitia,
Nimepata ikhiwani, AN-NUUR likiwa “via”,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

AN-NUUR ifanye kazi, usije ukalegea,
Kazi zako twazienzi, na dua twakuombea,
Metutoa usingizi, mbele tunaelekea,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

AN-NUUR kama jahazi, mawimbi watukatia,
Hodari wako ujuzi, “kona” unazipatia,
Kukudhuru hawawezi, Mola atakukingia,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

AN-NUUR yaseme wazi, yakiukayo sharia,
Madhalimu uwakhizi, waipendao dunia,
Japo wanayo mavazi, uchi wapate bakia,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

AN-NUUR siyamalizi, hapa ninasimamia,
Ya kwako mambo azizi, thamani yamezidia,
Wa witiri mwenye enzi, azidi kukupa njia,
Ndugu umeniungia, AN-NUUR mjumbe mwema.

Jihad R. Saballa, 
S.L.P.  347, 
Shinyanga.


Ilaniwe Marekani
 

Laden anahimiza, “Sratwa” Mustaqima,
Ile inayo-ongoza, kwenye mwisho Akrama,
Iweje mwamgombeza, na kumvisha shutuma?
    Hastahiki lawama, ilaniwe Marekani.

Mtu akitetea haki, gaidi mnasema!
Wangapi mabaramaki, na mliwafata nyuma?
Walianzisha mikiki, dunia ikatetema,
 Laden hana lawama, ilaniwe Marekani.

Kutekeleza za Mungu, sheria ziwe za Toma!
Mwanzo wa huu ukungu, amanikuwa kilema,
Hayapungui majungu, kisha huzidi dhulma,
 Laden hana lawama, ilaniwe Marekani.

Mwapuuza maagizo, Mola aliyoyasema,
Mnafata makatazo, mfano watu wa zama,
Huu ukubwa uozo, mwatukosesha ghanima,
 Laden hana lawama, ilaniwe Marekani.

Wana hila Marekani, dunia wameiduma,
Nyote mko ujingani, kwa hizo zao ndarama,
Mjue huko mbeleni, adhabu yawaandama,
 Laden hana lawama, ilaniwe Marekani.

Siko nanyi mie aka, mi’kando nimesimama,
Maaluni Amerika, siwashiriki daima,
Mimi namcha Rabuka, natii anavyosema,
 Laden hana lawama, ilaaniwe Marekani.

Hapa nimegota tasa, namba yenye heshima,
Nafata mila ya Musa, na huyo Ibrahima,
Na Muhammadi hasa, Utume ndiye hatima,
 Laden hana lawama, ilaniwe Marekani.

Na Bin Laden,
Magori Chriss (Chifu Jaji)
S.L.P. 61402,
Dar es Salaam.
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri
Hii siyo Demokrasia ni fedheha

Urambo wamlilia Profesa Lipumba
Na Mwandishi Wetu

Sheikh aridhia Waislamu kubatizwa
Na Rajab Rajab, Morogoro

Zanaki kupiga marufuku Hijab?

Uongozi Masjid Qadiria waitwa Polisi kuhojiwa

Wakazi wa Mbagala Msalabani kuishitaki Tume ya Jiji

Wasemavyo wanaharakati

Akhera ipo, makafiri ni wakadhibishaji
Na Abubakar Marwilo

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo ni mgumu
Na Elia Batendi

Aina ya maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu

PAROLE:   Rais kasusa au hana ubavu?
Na Bisura Waziri Nyello

Serikali ikithamini kilimo
Na Abdallah Ahmad Seif

Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 3
Na Ustaadh Kupa Pazi Said

Madrasa Arrijalu Muswallin Damba

Ijue Madrasat Fauzia - Kibondo

Waislamu  Kondoa waanza kupokea misaada ya ujenzi wa Msikiti, Madrasa
Na Abu Zubeir, Dodoma

Waislamu Dodoma wasali sala ya Ghaib kwa marehemu Kilima na mkewe

Songea kujenga shule ya sekondari

Wanafunzi wa Bihawana Dodoma wamshukuru Alhaj Ismail Dawood

Mashindano ya kusoma Qur’an yafanyika Kondoa

Waislamu wautazame upya mfumo wao wa elimu

Ujenzi wa Chuo cha Kiislamu Shamsiya Bereko wakwama

Kesi ya kushambulia kituo yaahirishwa tena

Polisi waondolewa kimya kimya Mwembechai

Msikiti wa Kiwanja cha Ndege wapania kujenga shule

Sayansi na Teknolojia
[Kwenye Kompyuta RAM ni kitu gani?]

Mafundisho ya Quran

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Madini ya chuma]
 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita