|
|
|
Na Ustaadh Kupa Pazi Said Tulieleza huko nyuma kuwa, hatua za utoaji wa Elimu ya Awali kwa Watoto Wadogo ni nne. Hatua tatu za mwanzo, ambazo ni kabla ya Mimba, Wakati wa Mimba, na Baada ya Kuzaliwa, Mtoto hupewa Elimu ya Awali na Wazazi wake katika hatua zote hizo. Ndiyo maana tulisema kwamba, ndoa njema chini ya Misingi ya Sheria, ndiyo Msingi mkubwa wa kutoa Elimu ya Awali kwa watoto. Hatua ya Nne ya kutoa Elimu ya Awali kwa Watoto Wadogo, inatekelezwa na Mwalimu/Mlezi.Kwa kuwa jukumu hili kubwa amepewa Mwalimu/Mlezi, hapana budi kwake awe amepata mafunzo maalumu ya kumuandaa kwa ajili hiyo. Sifa za Mwalimu aliyeandaliwa na mwalimu asiyeandaliwa Mwalimu aliyeandaliwa kwa kupewa mafunzo maalumu ya kufundisha, hulazimika kufuata Muhtasari (syllabus) iliyotolewa katika somo lake bila ya kutoka nje ya mwongozo huo. Kwa sababu kufundisha si kuropoka chochote kile kinachokuja kichwani. Pia Mwalimu aliyeandaliwa, hufundisha kila maudhui (Topic) kwa wakati wake. Pia Mwalimu aliyeandaliwa husaidiwa kufundisha kwa kutumia vifaa vya kusomeshea (Teaching aids) ambavyo vina kazi kuu mbili:- (a) Kumsaidia Mwalimu kufundisha kwa urahisi. (b) Kumsaidia Mwanafunzi kujengeka kiakili katika yale anayofundishwa. Pia Mwalimu aliyeandaliwa, hutayarisha somo analotaka kufundisha kwa kupitia maudhui katika vitabu vilivyopangwa kwenye "scheme of work" na vingine vya maudhui hiyo hata kama havikupangwa ili afahamu barabara. Kisha hujaribu kujibu maswali yaliyopo katika mazoezi (Exercise), na hubuni maswali yake mwenyewe na kutafuta majibu yake. Hufundisha hatua kwa hatua; na amalizapo dondoo (point) fulani, hutoa fursa kwa wanafunzi kuuliza maswali ikiwa hapana budi kufanya hivyo. Hujaribu kujichunga sana kutoka nje ya maudhui, kwani anajua kuwa atawatoa wanafunzi nje kabisa ya somo kimawazo kwa kuzielekeza akili zao katika jambo jipya alilogusia. Vile vile Mwalimu huyu hatoki darasani ila lazima ajue kuwa somo limeeleweka au halikueleweka, iwe ni kwa kuwauliza maswali hapo hapo darasani, au hurudia kwa muhtasari dondoo muhimu. Huchunga sana wakati; hachelewi sana na kuacha kiporo, wala hawahi sana mpaka akawa hana la kusema darasani zaidi ya kufanya porojo, na darasa kuligeuza soko. Huwa hawabagui baadhi ya wanafunzi, kwani kufanya hivyo, hujenga chuki baina yao. Mwisho wa somo huandika maelezo (notes) juu ya somo alilofundisha na hutoa kazi ya nyumbani (Home Work) ikibidi kufanya hivyo. Kwa kuwa ana uhakika na kazi yake, huwa tayari kukaguliwa na wakaguzi wa elimu kwa kuulizwa maswali wanafunzi wake, au yeye mwenyewe kwa kutumia vitabu vyake anavyoandalia masomo. Kinyume chake, Mwalimu ambaye hakuandaliwa hufanywa tofauti na yule aliyeandaliwa. Yeye hatumii Muhtasari na wala hana mpango wa kujua hicho ni kitu gani na faida yake kwake ni ipi. Huwa hatayarishi somo, kwa kuwa hujiona anajua. Hutoka nje ya maudhuuisha baadaye. Matokeo yake huwa hawezi kuchunga muda. Huwabagua wanafunzi kwa kuwapenda wale mahodari na kuwachukia wenye akili za wastani na dhaifu. Mara nyingi hubakiza viporo, na kwa kuwa hakujitayarisha, hufundisha kwa kukwamakwama, na huwa anajibu maswali kwa mkato, tena bila ya uhakika. Hali hii huwafanya wanafunzi wasiwe na hamu ya kumsikiliza Mwalimu, na hivyo huanza kuzungumza porojo na kusababisha fujo darasani. Pia huwafanya wajenge khofu katika nyoyo zao, na kushindwa kumuuliza Mwalimu hata kama hawakulielewa somo. Mwalimu huyu huwa hana hamu ya kujiendeleza yeye mwenyewe kielimu, na hajui kujikosoa. Pia ni mwingi wa porojo akiwa darasani ambazo ziko nje ya mada. Mwalimu ni mfano mwema kwa wanafunzi Mwalimu hutakiwa awe mfano mwema kwa wanafunzi wake katika yote anayowafundisha. Kwa sababu wanafunzi huamini kuwa Mwalimu ni Mtu mwenye heshima na maarifa makubwa zaidi pengine kuliko wazazi wao kwa kupinga kutekeleza amri fulani kwa kuwa hawakufundishwa na Mwalimu au amewafundisha kuliacha jambo hilo. Hivyo Mwalimu ajichunge kufanya mambo yatakayomvunjia heshima na hadhi yake, kwa kuwa ataigwa. Kumuandaa mwalimu ni sunnah Waalimu wengi hasa wale wa Madrasa, hufikiria kuwa kuandaliwa kwa kupewa mbinu za kufundishia ni mambo ya Kizungu na wao kama wafundishaji wa dini hawawajibiki kuhudhuria kozi, semina na masomo mbalimbali yaliyoandaliwa kwa madhumuni hayo. Matokeo yake, ni kutofikia malengo katika ufundishaji wao; pia hushindwa hata kubadilisha vitabu vya kufundishia hata kama havileti athari, eti kwa kuwa hiyvo ndivyo walivyosomeshwa Ndugu zangu walimu! Fahamuni kuwa jambo hili ni Sunnah ya Mitume wote khususan Mtume wetu Muhammad (s.a.w.). Allah (s.w.) amesema: "Sema: Hii ndiyo njia yangu ninaita kwa Allah kwa ujuzi wa kweli, mimi (nafanya hivyo) na (kila) wanaonifuata. Na Allah ametakasika na kila upungufu, wala mimi simo miongoni mwa washirikina." (Qur...........). Pia amesema: "Bila shaka mnao mfano mwema wa kuiga kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu." (Qur.33:21). Kwa kuwa yeye ni kiigizo chetu, basi tunatakiwa tusome elimu za ufikishaji (ufundishaji) kama yeye alivyofundishwa na Allah (s.w.). Allah (s.w.) alimuandaa Mtume (s.a.w.) tangu akiwa mdogo kwa kumpeleka "safari za usomaji" (study tours) ili aje kuwa Mwalimu wa kufundisha kila fani inayohitajiwa na Ummah huu. Wakati akiwa mtoto, alisafiri mara mbili kwenda kusoma nje ya Mji Mtukufu wa Makkah. Alisafiri na Mama yake mpaka Madina ili kuzuru kaburi la Baba yake. Walipokuwa wanarudi, mama yake akafariki na kubaki bila Baba na Mama. Lengo la Allah (s.w.) kwa mja wake huyu, lilikuwa ni kumuandaa awe na subira kwa yote yatakayomkuta, na awe tayari kupoteza ndugu na jamaa kwa ajili yake. Allah (s.w.) amesema: "Je! hakukukuta Yatima akakulea? "(QUR.93:6). Ya pili alisafiri na ‘Ami yake Abu Talib mpaka Shamu. Katika safari hii, Allah (s.w.) alikuwa na malengo makuu mawili:- (a) Kumfahamisha Abi Talib kuwa mwanae atakuwa Mtume wa Allah (s.w.) (b) Kumfahamisha Mtume (s.a.w.) namana ya kutafuta masoko na kufanya biashara (study marketing).. Kutokana na kozi hiyo, alikuwa mfanya biashara bora, mkweli na mwaminifu na mwenye kupata faida kwa kuwa alisoma kabla. Alikuwa akipishana na wafanya biashara wengine (yaani alikuwa haandamani na misafara yao), hivyo akifika Shamu huuza kwa faida kubwa bidhaa zake, na akifika Makkha huuza kwa faida kubwa bidhaa zake, kwa kuwa hakuwa na mpinzani. Ndio maana akatuusia tusome masoko kabla hatujafanya biashara. Alikuwa akichunga mbuzi. Lengo la Allah (s.w.) kwa Mja wake ni kumuandaa awe Mchungaji wa Waja wake katika kuwaongoza kwenye kheri, na kuwatoa kwenye maovu. Allah (s.w.) alimtayarisha aje kuwa Hakimu kwa kuweza kuwahukumu Makureshi waliogombania kuweko jiwe jeusi (Hajar As-wad) katika Al Ka’abah baada ya kuifanyia ukarabati. Baada ya kuona uovu wa watu wake umezidi, aliamua kusafiri hadi Jabal Nuur akawa anakaa peke yake kwenye pango la Hiraa. Humo alifanya Ibada mbalimbali kama kufanya fikra juu ya Mungu wa Kweli na kuomba Dua ili aweze kuwatoa ndugu zake katika ujinga walionao. Ilipofika tarehe 17, Ramadhani, 611M, Malaika Jibril (a.s.) alimjia na kumbashiria kuwa yeye ni Mjumbe wa Allah (s.w.) kwa viumbe wote, na akamsomesha Aya hizi:- "Soma kwa Jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba mwanadamu kwa pande la damu. Soma na Mola wako ni Karimu mno. Ambaye amemfundisha (Binadamu elimu zote hizi) kwa wasita (msaada) wa kalamu (zilizoandika vitabu watu wakapata elimu). Amemfundisha mwanadamu (chungu ya) mambo aliyokuwa hayajui. (QUR. 96:1-5) Wahyi wa pili na wa tatu, ulikuwa ni kwa ajili ya kumuandaa Mtume (s.a.w.) kwa kazi ngumu ya kuulingania na kuusimamisha Uislamu katika jamii iliyozingirwa na ujahili. Allah (s.w.) amesema: "Ewe uliyejifunika maguo! Simama usiku (kucha kufanya Ibada) ila muda kidogo (tu hivi). Nusu yake au ipunguze kidogo. Au izidishe na soma Qur’an vilivyo. Hakika sisi tutakuteremshia kauli nzito. Hakika kuamka usiku (na kufanya Ibada) kunaafikiana zaidi na moyo, na maneno yanatuwa zaidi. Hakika mchana unashughuli nyingi. Na litaje jina la Mola wako na ujitupe kwake kwa kweli. Bwana wa Mashariki naMagharibi, hakuna Muabudiwa ila Yeye, basi Mfanye kuwa Mlinzi (wako)". (QUR.73:1-9). "Ewe uliyejifunika maguo! Simama auonye (viumbe) Na Mola wako umtukuze. Na nguo zako uzisafishe (uzitakase). Na mabaya yapuuze. Wala usiwafanyie (watu) ihsani ili upate kujikithirishia. Na kwa ajili ya Mola wako, fanya subira." (QUR.74:1-7). Ukaguzi Kumkagua Mwalimu katika kazi yake ni Sunnah. Kwani imesimuliwa na Umar bin Khattab (r.a) kuwa, siku moja wakiwa pamoja na Mtume (s.a.w.) aliwajia Malaika Jibril katika umbo la kibindamu na kuketi mbele ya Mtume (s.a.w.), na akaanza kumuuliza maswali kuhusu Islam, Imani, Ihsan, na Dalili za Kiyama. Kila alipomjibu, Yeye alikuwa akithibisha jibu hilo kuonyesha kuwa amepatia. Kisha akenda zake. Baadaye ndio Mtume (s.a.w.) akawafahamisha kuwa huyo ni Jibril (a.s.) amekuja kuwafunza dini (yaani amekuja kumkagua Mtume (s.a.w.) kama anafundisha vilivyo, au la). Hadithi hii kwa utaratibu wake ni ndefu, na imepokewa na Muslim. Tendo la kukaguliwa, linamfanya Mwalimu ajiamini na kuondokwa na wasiwasi, na kutosahausahau yale anayoyasomesha. Hivyo ndugu walimu tuwe tayari kwa hilo. Nadharia na vitendo Muda wote aliokuwa Makkah, Mtume (s.a.w.) alifundishwa Kinadharia (Theory), kisha akaamrishwa kwenda Madina kutekeleza kwa vitendo (Practical). Na kwa kuwa Allah (s.w.) alimuandaa vilivyo Mtume (s.a.w) awe Mwalimu wa Ummah huu, alimtangaza kwa kusema: "Ewe Mjumbe wa Allah! Kwa hakika sisi tumekupeleka uwe shahidi na Mtoaji wa khabari njema na Muonyaji. Na uwe Muitaji (wa watu) kwa Allah kwa idhini yake, na uwe Taa itoayo nuru." (QUR6:45-46). Na akamwamrisha Mtume (s.a.w.) haya: "Sema: Kwa hakika mimi, Mola wangu Ameniongoza kwenye njia iliyonyooka; kwenye dini iliyo sawa kabisa; ndiyo Mila ya Ibrahimu, Mnyofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina." (QUR.6:161). Nasaha kwa kwalimu/walezi Ndugu zangu Walimu/Walezi! zindukeni na kuikumbuka Ibara isemayo: "Mwalimu ni Mwanafunzi." Hivyo sote tujitahidi kila uchao kujifunza mambo mapya kulingana na wakati tulionao. Tusibaki na yale tuliyojifunza zamani na yale tunayofundisha tu, bali tujifunze hata mambo mengine mbalimbali ya maisha ya kila siku. Tujitahidi kusoma magazeti, Vitabu, vijarida, Makala n.k. Tusikilize Redio, T.V. (hasa vile vipindi vilivyo muhimu kwetu). Tuhudhurie kozi, semina, makongamano na Darsa mbalimbali za kielimu. Tunapofundisha, kuusimamisha Uislamu liwe ndiyo lengo la kila mmoja wetu. Nasaha kwa wanaomiliki madrasa/shule Kuweni makini mnapoajiri Walimu, kwa kuwaajiri walimu waliondaliwa ili lengo litimie. Kama mnao tayari walimu ambao hawajaandaliwa, basi wapeni mafunzo maalumu ya ufundishaji. Nasaha kwa wazazi Kumbukeni kuwa Firaun (L.A.) alikosa kwa kuwachinja watoto wa Kiisrail. Kwa hiyo kuwapeleka watoto wenu kwenye Madrasa au shule ambazo waalimu wake hawakuandaliwa, ni kuwadumaza kiakili/kielimu, na ni moja ya uchinjaji wa watoto hali wako hai, na kwa hilo mtaulizwa na Allah (s.w.), kwani mmewapotezea malengo yao tangu wakiwa wadogo. Kwa wale ambao watapenda kujiendeleza na kozi ya elimu ya awali kwa watoto wadogo, wawasiliane nasi kwa anuani ifuatayo: IRC - BUREAU,
|
YALIYOMO
Tahariri
Urambo wamlilia Profesa Lipumba
Sheikh aridhia Waislamu
kubatizwa
Uongozi Masjid Qadiria waitwa Polisi kuhojiwa Wakazi wa Mbagala Msalabani kuishitaki Tume ya Jiji Akhera ipo, makafiri ni wakadhibishaji
Mdahalo kati ya Waislamu na
Wakristo ni mgumu
Aina ya maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu PAROLE: Rais kasusa
au hana ubavu?
Serikali ikithamini kilimo
Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto
wadogo - 3
Madrasa Arrijalu Muswallin Damba Ijue Madrasat Fauzia - Kibondo Waislamu Kondoa waanza
kupokea misaada ya ujenzi wa Msikiti, Madrasa
Waislamu Dodoma wasali sala ya Ghaib kwa marehemu Kilima na mkewe Songea kujenga shule ya sekondari Wanafunzi wa Bihawana Dodoma wamshukuru Alhaj Ismail Dawood Mashindano ya kusoma Qur’an yafanyika Kondoa Waislamu wautazame upya mfumo wao wa elimu Ujenzi wa Chuo cha Kiislamu Shamsiya Bereko wakwama Kesi ya kushambulia kituo yaahirishwa tena Polisi waondolewa kimya kimya Mwembechai Msikiti wa Kiwanja cha Ndege wapania kujenga shule Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|