|
|
|
MAELFU ya Waislamu walikusanyika katika kijiji cha Dalai kutazama na kusikiliza wasomaji wa Qur’an wakishindana, kutoka vijiji mbalimbali wilayani Kondoa, mkoa wa Dodoma hivi karibuni. Mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Ustadh Rashid Ramadhani yaliwakusanya Waislamu elfu mbili na baadaye kuendelea na kisomo cha Maulidi kwa kuadhimisha kuwekwa kwa jiwe la msingi la Masjid Dalai na madrasa yake ambayo yanakaridiwa kugharimu shilingi milioni 11. Jumla ya washiriki wapatao 40 waliweza kushindana kusoma Qur’an kwa hifadhi na tajiwidi. Jumla ya majaji (Masheikh) watano wakiongozwa na Sheikh wa Wilaya Twalha Abdallah Ally na Sheikh Msafiri Mbwana wa Dodoma walishiriki kikamilifu kupatikana kwa washindi hao. Akikaribishwa mgeni rasmi katika kutoa zawadi, Shekh Ally Mzee Commorian kutoka Dar es Salaam, aliwapongeza Waislamu wa Dalai kwa kufanikisha shughuli hiyo nzito. Sheikh Commorian aliwasisitiza wazazi kuwapeleka watoto wao kusoma Qur’an na kuhifadhi, alisema maadui wa Uislamu wanatumia kila mbinu kuhakikisha Qur’an isithaminiwe na Waislamu. Alisema Qur’an ni mwongozo wa maisha, hivyo kila Muislamu aielewe Qur’an kuisoma na maana yake. Akiweka jiwe la msingi la Masjid Dalai na madrasati Dalai, Sheikh Commorian alisema elimu kwa Muislamu ni haki yake kwani ndiyo amri ya kwanza tuliyopewa na hivyo hivyo uimarishaji wa kujenga Misikiti iende sambamba na kusaliwa. Jumla ya shilingi 24,595 zilipatikana kama michango ya awali, tofali 10,000 na mifuko 10 ya sementi vilipatikana. Naye Sheikh Abdallah Ally na Mhisani Bw. Khalifa Abdallah (Hongera) kutoka Masjid Quba mjini Dodoma wameahidi kutoa bati 20 na mafundi wawili wamejitolea kujenga Msikiti bure. Aidha, jumla ya washindi kumi walipatikana na kuzawadiwa jumla ya shilingi 59,000 wakitangazwa washindi hao Sheikh Commorian aliwataja washindi wawili waliofungana Boki R. Boki na Hassan Juma walipata shilingi 15,000 kila mmoja. Washindi watano walifungamana nao walipata shilingi 4,000 kila mtu nao walikuwa Sharifu Iddi, Haruni Issa, Asnal Omar, Maulidi Kilindo na Abdul Jabal. Wengine watatu walipewa zawadi ya shilingi 3,000 kila mtu na saa za mkono. Hao walikuwa Ally Mohamed, Kinoji A. Kinoji na Alawi Mohamed. Haya ni mashindano ya tatu kufanywa mfululizo katika kijiji cha Dalai.
Dhana hii potofu iliumbuka katika miaka ya ’80 Waislamu nchini waliposimama imara na kutaka kuona kwamba watoto wao wanapata elimu ya sekondari na sio kukwamia katika elimu ya msingi tu. Baadhi ya wengi watakumbuka kuwa ni katika miaka ile Waislamu walipozozana na BAKWATA ilipokuwa inazifunga shule mbili pekee za Kiislamu nchini yaani shule za Kiislamu za Kinondoni (DSM) na Jumuia (Tanga) na kuzifanya shule za kawaida za kuchukua wanafunzi mkululo hata wale ambao tayari walikuwa na nafasi za peke yao mahali pengine, Wakristo walikuwa na shule za kwao 19 nchini. Kitendo kile ambacho kilikuwa cha kuufudikiza Uislamu kilichochea hamasa kwa Waislamu nchini kote mmoja mmoja au katika vikundi na kujenga shule za sekondari za Kiislamu katika sehemu zao. Hivi leo katika muda wa miaka isiyozidi 20 Waislamu wamekwisha jenga mashule yao 23 ambayo yangegawiwa kimikoa kila mkoa ungepata angalau sekondari moja. Na hii ni kasi kubwa ya wastani wa ujenzi wa shule moja kila mwaka. Wakati tunaendelea na juhudi za kuimarisha elimu katika shule ambazo tumekwisha zijenga kwa elimu bora za dini, na ekuyula pamoja na maadili mazuri na wakati tukiwa tunaongeza mashule mengi zaidi ya Kiislamu katika mikoa ambayo imekwisha jenga na tukihimiza mikoa ambayo bado kujenga nayo ijenge napenda nitoe wazo hapa ili lifanyiwe kazi sambamba na juhudi hizo na mafanikio hayo. Nalo ni kuwa kwa vile hatimaye kila mkoa utajitegemea kwa kuwa na shule zake na vijana wao kutosheka kupata elimu katika mikoa yao tu hali hiyo mwishowe itajenga nyigo zitakazo zaa jamii ya Waislamu Watanzania ambao wamejinyima nafasi ya kuchanganyika na hivyo kutofahamiana. Na kwamba Waislamu hao wapya wa makundi watakuwa hawayafahamu mazingira ya mikoa yao nchini na kuzijua tabia tofauti za Waislamu katika mikoa jambo ambalo linaweza likazua migogoro ndani ya Uislamu. Historia inatufundisha kwamba hapa nchini kwetu udugu wa Kiislamu na kufahamiana kwao vema asili yake ni watu kusafiri huko na huko nchini wakati mwingine kutoka upande mmoja wa nchi hadi upande mwingine kuitafuta na au kuifuata elimu (ya dini). Kwa mfano tu, watu kutoka Kigoma ambayo ni ukingo wa upande wa magharibi ya nchi walitoka na kupita miji ya Tabora, Dodoma, Morogoro na kufika Dar es Salaam ambayo ni ukingo wa nchi kwa upande wa mashariki na kwa wakati ule kuvuka hadi Unguja. Kule waliko kwenda vijana kutoka sehemu mbali mbali walikutana vyuoni, walichanganyika na kuishi pamoja, hali hii si tu kwamba ilivunja mipaka ya Kiutawala na ukabila, lakini vile vile ilijenga uelewano mkubwa miongoni mwa watu nchini na kujenga/kuimarisha udugu wa Kiislamu. Mwenendo huu wa Waislamu uliotumika nchini kwa karne nyingi umehusika sana kujenga misingi ya amani na utulivu tunajivunia katika taifa letu leo hapa nchini, japokuwa mchango huu wa Waislamu hili linawaudhi wengi kulisema. Mfumo wa elimu wa leo pamoja na usawa wake nidhahiri kwamba utabomoa na kuyaondoa kabisa mazuri yaliyowekwa na mfumo wa zamani na badala yake kuangua madhara yasiyoendesheka baadaye. Ili tusijenga Uislamu wa kimikoa na ili tujiepushe na migogoro itakayotokana na hali hiyo inapendekezwa kwamba shule zetu zisifundishe masomo yote kabisa kwa mfano kujaza michepuo yote katika shule moja kwa vidato vya V na VI. Badala yake shule ziteuliwe na kutengewa au kugawiwa masomo ya kufundisha; pili jukumu la kuwafunza na kuwaendeleza vijana wa Kiislamu wenye uwezo wa kuipokea elimu na kuifaidisha jamii lisiachiwe wazazi peke yao ila liwahusu jumuia ya Kiislamu kwa kutumia Taasisi zake, Misikiti na Mashirika yake visaidie kubeba gharama za kuelimisha Umma wa Kiislamu. Kwa kukutana wakuu wote wa mashule pamoja na wamiliki wake, kutawezesha kupata mfumo mzuri. Sidhani kama nitakuwa narudiarudia kwa kueleza hilo, lakini nahisi ufafanuzi unahitajika ili kukamilisha na kuwasilisha fikra katika usawa. Hadi hivi sasa tuna mashule zaidi ya 20 ya Kiislamu yenye kutoa taaluma mbalimbali, kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Kwa fikra zangu, nadhani huu ni wakati muafaka wa kuweka taratibu zitakazotuwezesha kuujenga Uislamu, wenye mueleko wa namna moja kitaaluma. Ni vyema kukiwa na mitaala ya aina moja kuanzia "Nursery School’ za Kiislamu hadi vyuo vikuu vyake. Kwa kuhitimisha, naona ni vizuri sana kwa wamiliki wa taasisi za Kiislamu za elimu kuwatumia vyema wasomi wa Kiislamu wenye taaluma mbalimbali, kuleta mapinduzi ya Kislamu nchini. Ningependekeza Waislamu wanaomiliki taasisi hizo wakutane pamoja na kuandaa mkakati mpya wa kuboresha elimu kwa vijana wa Kiislmu. Kwa mawazo yangu moja ya njia za kuboresha elimu katika jamii ya Kiislamu, ni pamoja na kuzigawanya shule katika makundi tofauti kitaaluma na kuzipa majukumu kwa mfano, shule ya Jabal hira inavifaa vingi vya sayansi na uwezo mkubwa wa masomo hayo na shule ya Ubungo ina uwezo mkubwa katika masomo ya biashara basi shule ya Ubungo ivunje mikondo yake ya sayansi na kuipa jukumu hilo Jabali Hira, halikadhalika Jabal Hira ivunje mikondo ya biashara na kuiachia jukumu hilo Ubungo. Tukizigawanya sekondari zote katika mafungu hayo tutajikuta tuna kitu cha kujivunia, hayo ni mawazo yangu binafsi. Mwisho ningewaomba Waislamu nchini washikamane vilivyo ili kupambana na adui aliyeko mbele yetu. Wajiimarishe kitaaluma na kiuchumi kwa kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo
iliyoko ndani ya uwezo wao, hii ni kuanzia ngazi ya misikiti hadi katika
taasisi zao.
UJENZI wa Chuo cha Kiislamu Shamsiya upo katika utata wa kutojengeka kwa sababu ya kukosa kuungwa mkono na baadhi ya Waislamu wa tarafa hiyo ya Bereko iliyopo wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma. Hayo yalisemwa na muasisi wa Chuo hicho Ustadh Shaaban Issa Nondi alipotembelewa na mwandishi wa AN-NUUR nyumbani kwake hivi karibuni. Chuo cha Kiislamu cha Shamsiya kiliwekwa jiwe la msingi na Sheikh Mkuu Mufti Hemed bin Jumaa bin Hemed Oktoba 7, 1997 lakini tokea hapo jitihada ya kuliendeleza zimekuwa za mtu binafsi tu Ustadh Nondi na wanafunzi wake. Ustadh Nondi amesema kwamba chuo kimekipa jina la Shamsiya ikiwa ni kumbukumbu kwani alipata elimu yake ya dini kwa Sheikh marhemu Mohamed Ayoub wa Madrasati Shamsiya Tanga. Ustadh Nondi alisema Chuo chake kimefungua matawi saba na kina wanafunzi 400 katika tarafa ya Bereko. Ustadh Nondi ameomba kuwa wale wote ambao wameshirikiana naye wakati akisoma Tanga wamsaidie wawasiliane katika kuimarisha Uislamu Bereko. |
YALIYOMO
Tahariri
Urambo wamlilia Profesa Lipumba
Sheikh aridhia Waislamu
kubatizwa
Uongozi Masjid Qadiria waitwa Polisi kuhojiwa Wakazi wa Mbagala Msalabani kuishitaki Tume ya Jiji Akhera ipo, makafiri ni wakadhibishaji
Mdahalo kati ya Waislamu na
Wakristo ni mgumu
Aina ya maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu PAROLE: Rais kasusa
au hana ubavu?
Serikali ikithamini kilimo
Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto
wadogo - 3
Madrasa Arrijalu Muswallin Damba Ijue Madrasat Fauzia - Kibondo Waislamu Kondoa waanza
kupokea misaada ya ujenzi wa Msikiti, Madrasa
Waislamu Dodoma wasali sala ya Ghaib kwa marehemu Kilima na mkewe Songea kujenga shule ya sekondari Wanafunzi wa Bihawana Dodoma wamshukuru Alhaj Ismail Dawood Mashindano ya kusoma Qur’an yafanyika Kondoa Waislamu wautazame upya mfumo wao wa elimu Ujenzi wa Chuo cha Kiislamu Shamsiya Bereko wakwama Kesi ya kushambulia kituo yaahirishwa tena Polisi waondolewa kimya kimya Mwembechai Msikiti wa Kiwanja cha Ndege wapania kujenga shule Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|