AN-NUUR 
Na.177 Shaaban  1419, Novemba 27 - Desemba 3, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Urambo wamlilia Profesa Lipumba
 
  • Wadai CCM imewatelekeza
  • Waislamu Tabora wakutana kujadili mwelekeo
Na Mwandishi Wetu 

HABARI kutoka Tabora zimeeleza kwamba wananchi wa Urambo wanatafuta taratibu za kuwasiliana na Profesa Ibrahim Lipumba ili awakwamue na hali inayowakabili sasa. 

Wananchi hao hasa wakulima wa tumbaku wamedai kwamba CCM na Serikali yake mkoani Tabora badala ya kuwatetea wamekuwa wakiyaunga mkono makampuni ya biashara ambayo mwelekeo wake ni wa kuwanyonya wananchi. 

Wamesema kwamba makampuni hayo, DIMON Ltd, TLTC na Stancom yameweka mkakati wa kununua tumbaku kupitia mwakilishi mmoja ili kuzuia ushindani katika biashara. 

Kwa utaratibu huo, wakulima hao wamesema kwamba makampuni hayo yatakuwa yananunua bila kujali maslahi ya mkulima. 

Aidha, wamesema kwamba kwa utaratibu huo mpya watakaoruhusiwa kuuza tumbaku yao kwa makampuni hayo ni wale wenye kilo zaidi ya 1000 hali ambayo itawakwamisha wakulima wadogo wadogo. 

Bw. mmoja 

aliyejitambulisha kwa jina moja la Wibonella alisema kwamba tarajio lao kubwa lilikuwa tumbaku, lakini kwa mwelekeo huu mpya watakuwa ni wenye kudhulumika. 

Amesema kwamba hakuna dalili zozote kwamba CCM na serikali yake zinachukua mwelekeo wa kuwatetea. 

Habari kutoka Urambo zimeeleza kwamba wananchi mbalimbali wamekuwa wakikutana na kutafakari ni vipi watapata ukombozi. Wengine wamekuwa wakijaribu kuwasiliana na uongozi wa CUF ili kumpata aliyekuwa mgombea Urais 1995 kupitia chama hicho Profesa Lipumba ili washauriane lipi la kufanya kwa siku za usoni. 

Juhudi za gazeti hili kuwasiliana na makampuni ya ununuzi wa tumbaku pamoja na serikali ya mkoa juu ya madai ya wananchi wa Urambo hazikuweza kufanikiwa. 

Wakati huo huo, Waislamu mjini Tabora wazee kwa vijana pamoja na Masheikh wao wamekutana ili kujadili mwelekeo wa umoja wao. 

Mkutano huo uliofanyika Jumanne Novemba 24, mwaka huu ukiwajumuisha watu maarufu kama Sheikh Hussein Ikunji, Sheikh Salala, Sheikh Issa Mzee na wengineo ulilenga kuondoa tofauti miongoni mwa Waislamu na kujenga umoja na mshikamano madhubuti kwa maslahi ya dini na dunia yao. 



Sheikh aridhia Waislamu kubatizwa 
 
  • Wamo wajukuu zake, watoto wa mdogo wake
  • Wabatizwa katika bwawa la Mindu
  • Akiri kushirikiana na Wasabato na kudai alighafirika
Na Rajab Rajab, Morogoro 

SHEIKH wa Kata ya Mlandizi Kijiji cha Melela mjini hapa, Maulidi Saidi Senzagale amedaiwa kushirikiana na Wasabato kwa kuwapa eneo la uwanja wa nyumba yake ambao una Msikiti na Madrasa ambapo Wasabato hao walitoa mahubiri na kuwabatiza watu wa madhehebu mbalimbali wakiwemo Waislamu. 

Mahubiri hayo ya Wasabato ambayo yalidumu katika eneo hilo kwa siku zisizopungua kumi na nane (18) ziliambatana na vivutio na vishawishi mbalimbali kama vile dawa za hospitali, fedha, mahindi pamoja na nguo za mitumba ambapo yule aliyeamua kuingia au mtu atakayepeleka watu katika dini hiyo hupewa zawadi hizo. 

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia mahubiri hayo ambao walihojiwa na gazeti hili mapema wiki hii, wamesema kuwa watu wengi waliobatizwa kwa upande wa Waislamu walivutika sana kuingia katika dini hiyo kwa kufuata maslahi pamoja na kuona Sheikh wao akisikiliza mahubiri hayo ambayo yalikuwa kero kwa wanafunzi waliokuwa wanasoma katika Madrasa iliyopo eneo hilo. 

"Kwa kweli ilikuwa kero kubwa sana katika Madrasa yetu, lakini nilikuwa sina uwezo wa kuzuia vipaza sauti vyao au kuwaondoa Wasabato hao kwa kuwa wamepata baraka za Sheikh wangu", amesema Mwalimu wa Madrasa ya Jabalkhan ambayo ipo nyumbani kwa Sheikh Shaaban Ramadhani Kibaragua wakati akiongea na gazeti hili nyumbani kwake Mlandizi Madukani. 

Ustadh Kibaragua ambaye ameshika nafasi ya Uimamu katika kata ya Mlandizi na kumsaidia Sheikh Senzagale amesema kuwa hakutegemea kama Sheikh wao kama angeweza kufanya vitu kama vile kwa kuwa mwaka jana aliweza kuzuia mahubiri ya 

Walokole yaliyotaka kufanyika karibu na Msikiti wa Ijumaa wa kata hiyo ya Mlandizi. 

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya waumini hawakuridhishwa na kitendo kilichofanywa na Sheikh wao, hivyo waliamua kumshitaki katika ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mlandizi. 

Inadaiwa Sheikh huyo alikiri kosa na kudai kuwa alikuwa ameghafirika katika maamuzi yake hayo. 

"Ni kweli hata sisi wazee tulikuwa hatukufurahia kitendo kilichofanywa na mzee mwenzetu na tulipanga tumwite Msikitini ili tumalize Kiislamu, lakini jazba za vijana wakampeleka katika ofisi ya Afisa Mtendaji na yaliyopatikana huko siyafahamu", alisema mzee Hassan Abdallah Msimbe wa kijiji cha Melela wakati akihojiwa na gazeti hili. 

Aidha, uchunguzi umeendelea kubaini kuwa Wasabato baada ya kuona wamefanikiwa kuungwa mkono na Sheikh Senzagale, wakamfuata ndugu mmoja na Sheikh huyo (jina halikupatikana mara moja) na kumshawishi awauzie kiwanja ambacho kinatazamana na nyumba ya Sheikh huyo yenye Msikiti mdogo na Madrasa. 

Wasabato hao wameweza kujenga Kanisa la miti na kuezeka manyasi na wakati huo huo wameamua kufyatua matofali ya kuchoma kwa ajili ya kuimarisha Kanisa lao hilo. 

Pia baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu walipohojiwa zaidi na gazeti hili wamesema kuwa wapo hata ndugu zake Sheikh Senzagale ambao inasemekana wamebatizwa ambapo yupo mtoto wa mdogo wake aitwaye Hassan maarufu kwa jina la "Pipa". 

Wengine wanaodaiwa kubatizwa na katoswa katika bwawa la Mindu ili wawe wasafi "kiroho" ni pamoja na Omary Shaaban Kidunda ambaye yeye imedaiwa amebadilisha na jina na kuitwa Ibrahimu. 

Mwingine anayedaiwa kukumbwa na zoezi hilo la Wasabato ni mjukuu wa Sheikh Senzagale aitwaye Mohammed Hassan Senzagale ambaye anasoma katika madrasa ya Jabalkhan ya Ustadh Kibaragua. 

Hata hivyo, Ustadh Kibaragua amesema kuwa hana uhakika kama kijana wake (mwanafunzi) huyo alibatizwa na ameongeza kusema kuwa alikuwa makini sana na vijana wa madrasa yake ili wasiweze kuingia katika dini hiyo ya Wasabato na ameahidi kumfuatilia kijana wake huyo ili kupata ukweli zaidi. 

Mwandishi wa habari hizi alijaribu kumtafuta Sheikh Maulid Said Senzagale nyumbani kwake, lakini hakuweza kupatikana kwa vile alikuwa amekwenda shambani. 

Hata hivyo, familia ya mzee huyo ilimthitibishia mwandishi wa habari hizi kuwa tukio la mahubiri na kubatizwa watu limefanyika eneo la uwanja wa nyumba yao, lakini wakakataa kuzungumzia suala hilo kiundani na kudai kuwa Sheikh ndiye anayejua zaidi habari hizo. 

Wakati huo huo, habari kutoka Mang’ula Kilosa zimesema kuwa hali ya Uislamu katika vijiji hivyo inazidi kuwa mbaya kutokana na waumini wa eneo hilo kutopata mafundisho ya dini yao na viongozi waliokuwepo kutofuatilia masuala ya dini yao na kuamua kuhodhi Misikiti. 

Akiongea na gazeti hili hivi karibuni, Ustadh Hassan Abdallah wa Mang’ula Kilosa amesema kuwa Misikiti mingi imefungwa na funguo ameondoka nazo Imam Shaban na hafungui Msikiti mpaka siku ya Ijumaa, hatua iliyopelekea waumini wengi kushuka imani zao za dini na kupelekea Misikiti kuwa magofu na vichaka vya kuhifadhia madudu na madanguro ya walevi. 

Hivi karibuni katika toleo lake Na. 175 Rajab 1419, Novemba 13-19, 1998 gazeti hili liliandika habari ya kupotea na kufa Uislamu Uluguruni ambapo matambiko na mizimu ya Dunale, Matotola, Kingalu, Lubandile, Korelo yamepewa uwezo wa kiungu na huku Waislamu wa mjini Morogoro wakiwa usingizini na Masheikh wao wakiwa katika mizozo ya kiitikadi na kugombania ukubwa Misikitini. 


Zanaki kupiga marufuku Hijab?

Shule ya Sekondari Wasichana ya Zanaki ya Jijini Dar es Salaam, huenda ikapiga marufuku uvaaji wa vazi la Hijab kwa wanafunzi wa shule hiyo, AN-NUUR imedokezwa. 

Taarifa ambazo gazeti hili imezipata zinafahamisha kwamba uongozi wa shule hiyo maarufu nchini, umetishia kuchukua hatua hiyo itakapofika Januari mwakani (1999). 

Akitangaza azma hiyo katika mkutano na wanafunzi wa vidato vya tano na sita hivi karibuni, mkuu wa shule hiyo Mama A. W. Mramba amedaiwa kujigamba kuwa hakuna mtu anayeweza kumzuia kuchukua hatua hiyo. 

Aidha, aliwataka wanafunzi kwa Kiislamu wanaotaka kuvaa sare inayozingatia masharti ya Hijab waende wakasome Al-Muntanzir, Alharamain au shule zingine za Kiislamu. 

Tishio hilo la Mkuu wa Shule lilifuatia taarifa iliyopelekwa kwake iliyodai kwamba kulikuwepo na wanafuzni wawili wa kidato cha tano (wavaa hijab) ambao walipigana darasani. 

Hata hivyo gazeti hili limefahamishwa kwamba hapakuwepo na ushahidi wa kupigana kwa wanafunzi hao. Uchunguzi zaidi umegundua kwamba wakati mkuu huyo anatishia kupiga marufuku vazi la stara, baadhi ya wanafunzi shuleni hapo huvaa sketi fupi na za kubana. 

Mwandishi wa habari hizi alipowasiliana na uongozi wa shule hiyo kwa njia ya simu jana (Alhamisi), mkuu wa shule Mama Mramba alikataa kukubali au kukanusha kuwepo kwa vitendo vyovyote vya kuwanyanyasa wanafunzi Waislamu wanaovaa Hijab. 

Mama Mramba alitaka mwandishi afike shuleni ili akaongee na mwalimu mlezi wa Waislamu. 

Alipotakiwa kujibu iwapo ametishia kupiga marufuku Hijab shuleni hapo, mkuu huyo hakuwa tayari kujibu swali hilo. 

Ingawa Wizara ya Elimu imesambaza waraka kuwataka wakuu wa shule kuwaruhusu wanaotaka kuvaa Hijab, kumekuwa na pingamizi na kero za mara kwa mara dhidi ya wanaojitokeza kutekeleza haki hiyo kwa mujibu wa dini zao. 

Taarifa kutoka shule mbalimbali nchini zinathibitisha kupuuzwa kwa waraka wa Serikali na wakuu wa vyuo au shule. 

Kufuatia kero hizo baadhi ya wanafunzi wameiomba Serikali itoe ufafanuzi zaidi. 

Juu 
 

YALIYOMO 
 

Tahariri
Hii siyo Demokrasia ni fedheha

Urambo wamlilia Profesa Lipumba
Na Mwandishi Wetu

Sheikh aridhia Waislamu kubatizwa
Na Rajab Rajab, Morogoro

Zanaki kupiga marufuku Hijab?

Uongozi Masjid Qadiria waitwa Polisi kuhojiwa

Wakazi wa Mbagala Msalabani kuishitaki Tume ya Jiji

Wasemavyo wanaharakati

Akhera ipo, makafiri ni wakadhibishaji
Na Abubakar Marwilo

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo ni mgumu
Na Elia Batendi

Aina ya maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu

PAROLE:   Rais kasusa au hana ubavu?
Na Bisura Waziri Nyello

Serikali ikithamini kilimo
Na Abdallah Ahmad Seif

Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 3
Na Ustaadh Kupa Pazi Said

Madrasa Arrijalu Muswallin Damba

Ijue Madrasat Fauzia - Kibondo

Waislamu  Kondoa waanza kupokea misaada ya ujenzi wa Msikiti, Madrasa
Na Abu Zubeir, Dodoma

Waislamu Dodoma wasali sala ya Ghaib kwa marehemu Kilima na mkewe

Songea kujenga shule ya sekondari

Wanafunzi wa Bihawana Dodoma wamshukuru Alhaj Ismail Dawood

Mashindano ya kusoma Qur’an yafanyika Kondoa

Waislamu wautazame upya mfumo wao wa elimu

Ujenzi wa Chuo cha Kiislamu Shamsiya Bereko wakwama

Kesi ya kushambulia kituo yaahirishwa tena

Polisi waondolewa kimya kimya Mwembechai

Msikiti wa Kiwanja cha Ndege wapania kujenga shule

Sayansi na Teknolojia
[Kwenye Kompyuta RAM ni kitu gani?]

Mafundisho ya Quran

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Madini ya chuma] 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita