|
|
|
Hukumu ya kusengenya: Sehemu hii inayofuatia tutazungumzia kusengenya na hukumu yake katika Uislamu. Kusengenya ni haramu kutoka katika kitabu na Sunnah (mafundisho ya Bwana wetu Muhammad s.a.w.) na pia makubaliano ya wanazuoni wa umma. Na tumekwisha zitangulia dalili za kuharamisha kusengenya katika toleo lililopita. Amesema Imamu AnNawawii ya kwamba: Kuitaja aibu ya mwanazuoni na ikawa kuitaja aibu hiyo ni kwa ajili ya kubainisha kosa lake ili asiigwe au kubainishwa udhaifu wake katika elimu ili wasidanganyike watu kutokana na udhaifu wa elimu aliokuwa nao mwanazuoni huyo na ili asikubalike mafundisho yake, basi kufanya hivyo siyo kusengenya, bali ni kupeana naswiha ambayo ni wajibu juu ya kila Muislamu kumpa naswiha nduguye aliyetereza na mwenye kufanya hiyo basi analipwa thawabu ni kama mtu au mwandishi akisema au kuandika kuna kundi fulani la watu wanasema kadhaa na kadhaa nahaya ni makosa au wanasema kwa kutofahamu au wanasema kwa kughafilika na mfano wa hayo si katika kusengenya, kwani nia yake hapa siyo kuzitaja kasoro zao kwa nia ya kuwadhalilisha la! Bali kwa nia ya kuuelimisha ummah yaliyo sawa na kuuepusha kufuata yale yaliyo baatil. Hukumu ya kusikiliza usengenyi Amesema Imam AN-Nawawii: Fahamu ya kwamba kusengenya kama ilivyokuwa ni haramu kwa mwenye kusengenya vile vile ni haramu kwa msikilizaji kuusikiliza usengenyi, kwa hiyo inawajibika juu ya yule mwenye kumsikia mtu anaanza kusengenya amkataze pindi asipoogopea madhara ya waziwazi na kama akiogopa basi anamuwajibikia juu yake kuchukia kuendelea kusikiliza usengenyi kwa moyo wake na akiepuke kikao kile pindi akiweza kukiepuka na kama akiweza kuuondoa mnukari ule kwa mdomo wke au kwa kuyakata mazungumzo yale kwa kuanzisha mazungumzo mengine, basi itakuwa ni wajibu juu yake kufanya hivyo, na pindi asipofanya hivyo basi atakuwa ameasi. Na kama akisema kwa mdomo wake kumwambia msengenyaji ‘nyamaza’ na hali ya kuwa yeye mwenyewe anatamani kwa moyo wake msengenyaji aendelee kusengenya, basi amesema Abuu Haamid Al-Ghazali kuwa huo ni unafiki, wala hakimuepushi kitendo hicho kutokana na dhambi ya kusikiliza usengenyaji, kwani ni lazima kuuchukia munkari huo kwa moyo na pindi atakapokuwa amelazimika kuwepo katika kikao ambacho ndani yake kuna usengenyi na ameshindwa kuuzuia munkari huo au amejaribu kuuzuia lakini hakukubaliwa basi itakuwa ni haraamu juu yake kuusikiliza na ni juu yake awe anamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa mdomo wake na kwa moyo wake au kwa moyo tu, au ajishughulishe na kufikiri juu ya mambo mengine ili asiweze kuusikiliza munkari ule na pindi atakapoweza kujiepusha na kikao kile ni wajibu juu yake kujiepusha kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu iliyosema: Na (wewe Muislamu kama kweli Muislamu si mnafiki) unapowaona wale wanaozungumza (kuzikadhibisha) aya zetu, basi jitenge nao (wende zako) mpaka wazungumze maneno mengine. Na kama shetani akikusahaulisha (ukakaa nao na hali wamo katika mazungumzo haya) basi badala ya kutanabahi usikae pamoja nao (hawa) watu madhalimu". (Suuratul An-am 68) Na imepokelewa kutoka kwa Ibrahim Ibn Ad-Ham Mwenyezi Mungu amuwie radhi ya kwamba hakika yeye (Ibrahim) aliitwa kwenye walima (karamu ya arusi) akaenda, pakatajwa mtu mwingine ambaye alikuwa hakuwahi kufika mahali pale, wakasema baadhi yao ‘yeye ni mzito’, akasema Ibrahim ‘mimi nimelifanya hili kwa nafsi yangu kwa kuwa nimehudhuria sehemu ambayo wanasengenywa watu ndani yake!’ Akaondoka na wala hakuweza kula chakula kwa muda wa siku tatu! Yaani anajutia kitendo alichokifanya cha kuhudhuria sehemu wanayosengenya watu. Na inaelezwa kuwa kutokana na kisa hiki ndipo ikateremka aya hii: "Na wanaposikia upuuzi hujitenga nao na husema (kuwaambia wapuuzi hao) sisi tuna vitendo vyetu (vitakuwa malipo kwa ajili yetu) na nyinyi mna vitendo vyenu (vitakuwa malipo kwa ajili yenu) amani juu yenu (inayotokana na sisi hamtasikia kwetu baya). Sisi hatutaki (kujibizana na) watu wajinga". (Suuratul Qasas 55) Na amesema pia Mwenyezi Mungu: "Hakika masikio na macho na moyo, hivyo
vyote vitaulizwa". (Suuratul Banii - Israil 36)
Na Bisura Waziri Nyello JUNI 6, 1998, Rais Benjamin Mkapa alizivunja Bodi za misamaha kwa wafungwa (PAROLE) zilizoundwa kwa misingi ya udini na akamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani aunde Bodi mpya akizingatia uwiano wa jamii. Yapata miezi mitano sasa bado Waziri hajatekeleza agizo la Rais na Rais hajachukua hatua yoyote ya maana kulinda uamuzi wake huo wa kuvunja ‘PAROLE - Udini’ na hivyo kuwacha mamia ya wafungwa waliojirudi waendelee kurundikwa magerezani, Kulikoni? Rais kasusa au hii mamlaka isiyo rasmi ya ‘udini’ ina nguvu na madaraka makubwa ya kutisha? Bodi ya misamaha kwa wafungwa (PAROLE) zilivunjwa na Mheshimiwa Rais kwa sababu ziliundwa kwa misingi ya ‘udini’. Haiwezekani Bodi hizo ziwe na wajumbe Wakristo watupu wakiwemo Maaskofu halafu zisiwe zao la ‘udini’. Kwa kuzingatia hoja hii na ukweli wa ushahidi wa Waislamu kuhusu muundo wa Bodi hizo ndipo Mhe. Rais alipotoa amri ya kuzivunja na kumuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani aziunde upya. Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw. Ali Ameir Mohamed bado anavunga kwamba Bodi zile hazikuwa kazi ya ‘udini’ lakini yaonysha anakwamishwa na ‘udini’ huo huo kuziunda upya. Kama siyo hii mamlaka ya ‘udini’ ndiyo iliyombana mbavu atueleze kwanini hataki kuunda Bodi mpya? Aliwahi kukaririwa na gazeti moja la kila wiki kushangazwa na "Waislamu kulalamikia uteuzi huo ambao wakati unafanywa haukuzingatia kigezo cha udini". Anashangazwa na malalamiko ya Waislamu lakini hashangazwi na kushindwa kwake kuziunda upya. Kwa mujibu wa sheria namba 25 ya 1994 iliyotiwa saini na Rais Januari 17, 1995 sehemu ya pili ukurasa 236 kifungu cha 3(a) kinazungumzia teuzi za Uenyeviti wa Bodi za mikoa: ‘Bodi ya PAROLE ya mkoa itajumuisha na Mwenyekiti ambaye atateuliwa na Waziri na ambaye atakuwa mtu mwenye ujuzi na uzoefu wa masuala ya sheria na usimamizi wa masuala ya jinai’. Kwa muda wa miaka 37 ya uhuru hakuna Waislamu wenye sifa za kuwemo katika Bodi za PAROLE! Labda hii mamlaka ya ‘udini’ inaweza kutoa jibu sahihi. Wao ndio wanaofahamu sifa gani Waislamu wanakosa; na sifa gani walizonazo Maaskofu hata wawe viongozi wa Bodi hizo. Lakini kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha kuundia Bodi hizo, kama kweli hakuna Muislamu mwenye sifa ya kuwa Mwenyekiti wa Bodi za PAROLE: Gazeti moja maarufu hapa nchini lilitufahamisha kwamba: "kuna ugumu katika uundaji wa Bodi za PAROLE kwa misingi ya uwiano wa kidini kwa sababu muundo wake unafuata sheria ya mwaka 1994 na wajumbe wake asilimia 50% wote wenye nyadhifa hizo ni Wakristo". Sheria ya mwaka 1994 ya kuundia Bodi hizo ndiyo hiyo tulioitaja hapo juu. Ina ugumu gani kwa Waislamu kuwemo katika Bodi hizo? Hakuna Waislamu wenye nyadhifa za kuingia kwenye Bodi hizo? Askofu Bruno Nyongani, Askofu Paul Ruzoka na Askofu Mario Mgulunde wanazidi nini hawa! Labda ‘Canoncial Law’ ambayo siyo muhimu kwa nchi isiyoendeshwa kidini. Tatizo siyo sheria wala nyadhifa za wajumbe bali ni ‘udini’. Huyu Bwana Mkubwa ‘udini’ hataki Waislamu katika vyombo na taasisi za serikali. Mbaya zaidi ana mamlaka makubwa. Sijui tutafanyaje? Kama hakuna uwezo wa kupambana na mamlaka hii isiyo rasmi, nani anayeweza kutia mguu. Tangu lini agizo la Rais likapuuzwa na Waziri na Rais mwenyewe asijuwe la kufanya kama hakuna kitu hapa! Mitihani ilipovuja tu Waziri kaitwa kwenda kutoa maelezo Ikulu, lakini agizo la Rais kuhusu PAROLE linapuuzwa. Inaelekea Mhe. Rais kilimtoka tu kuhusu kuvunjwa kwa PAROLE. Mbona kanyamaza! Bodi za PAROLE zilivunjwa kwa sababu ya ‘udini’ na hivi sasa zinashindikana kwa sababu hiyo hiyo ya ‘udini’. Huyu ‘udini’ ana nguvu kiasi gani? Hii mamlaka ya ‘udini’ inapoamua jambo lake hakuna wa kulipinga. Katika kipindi cha serikali ya awamu ya pili wanafunzi Waislamu waliruhusiwa na Rais kuvaa hijab kama wanataka na waraka wa kuthibitisha hilo upo. Lakini utekelezaji wa jambo hilo umekwamishwa na ‘udini’ mpaka leo hakuna wa kufanya lolote! Hii mamlaka ya ‘udini’ inafanana na gari moshi kiutendaji. Ukiingia kwenye njia yake ‘unakwenda na maji’ na hakuna wa kuuliza! Kwa hiyo kimya cha Waziri na Rais kuhusu PAROLE huenda siyo cha bure! Tuwaonee huruma Watanzania wenzetu walioko magerezani na mienendo yao
inaridhisha kuchanganyika na raia wengine. Kama PAROLE ingeundwa mapema
hivi sasa wangeshaanza kuwa huru. Lakini ‘udini’ siyo kosa letu. ‘Udini’
uko radhi binadamu wenzao wateseke magerezani lakini azma yao itimie tu.
Watanzania wote tujiulize kuna sababu gani ya msingi ya kutoundwa Bodi
za PAROLE mpaka leo? Hivi ni kweli kuna ugumu wa kuziunda upya Bodi hizo?
Kwanini Waziri haombi msaada kwa wenye maarifa hayo?
Na Abdallah Ahmad Seif INASHANGAZA mno katika nchi yetu ya Tanzania kuona suala la kilimo lisivyopewa kipaumbele na serikali yetu kama inavyopasa. Serikali yetu haina habari kabisa na upande huo muhimu ambao kwa hakika kama utatumiwa inavyotakikana, basi bila shaka nchi yetu itapiga hatua kubwa katika maendeleo na kujikwamua kutoka katika hali ngumu inayolikabili Taifa hili. Sekta ya kilimo ni muhimu sana, kwani ina uwezo mkubwa wa kuliingizia taifa fedha za kigeni kutokana na mazao yatakaouzwa nje. Kwa bahati nzuri Tanzania ni moja ya nchi chache zilizojaaliwa hali nzuri iliyokamilifu ya mazingira yanayofaa kwa kilimo. Inayo ardhi nzuri sana na yenye rutuba na uwezo wa kustawisha mazao ya aina mbalimbali, na isitoshe inavyo vyanzo vingi vya maji. Ipo mito, mabwawa, maziwa na hata bahari. Vitu ambavyo vinatosheleza kabisa kukiwezesha kilimo kuleta mafanikio mazuri na ya kujivunia katika nchi yetu. Cha kusikitisha serikali yetu haionyeshi kujali suala hilo muhimu la kilimo, pamoja na kuwa kimsingi ndilo hasa nguzo kuu ya uchumi. Pamoja na msemo kuwa ‘kilimo ni uti wa mgongo wa taifa hili’ lakini kutotoa msukumo unaofaa katika upande huo muhimu, msemo huo unapoteza maana yake halisi na kuligeuza suala hilo kuwa kitu ‘hewa’. Wakulima ambao kwa kweli wanastahili sifa kutokana na juhudi zao wanazozifanya katika kilimo, licha ya kukabiliwa na uhaba wa nyenzo za kisasa, lakini bado walikuwa wakikopwa mazao yao na kusababishiwa usumbufu mkubwa. Ilikuwa inafikia mahali inapita hadi misimu miwili wakulima bado hawajalipwa fedha zao. Hii ilikuwa ni dhuluma kubwa mno dhidi ya wakulima, na inaonyesha wazi jinsi serikali isivyotilia maanani suala zima la kilimo, mbali ya wakulima kuhenyeka kwa kufanya kazi katika mazingira magumu, bila ya kuwa na pembejeo bora za kisasa, jembe litumikalo la mkono, ukosefu wa mbolea, hakuna soko la kuaminika. Sasa wakati umefikia kwa serikali kuamka na kulizingatia sana suala hilo muhimu, kwani wanaweza kulipa mwelekeo mzuri na likaleta mafanikio katika nchi yetu. Nchi yetu hivi sasa iko hoi mahututi kiuchumi, na inatia huzuni kwa kutegemea wafadhili, hili linatia simanzi mno. Wakati sekta ya kilimo ingepewa kipaumbele tungeweza kwa kiasi kikubwa kuondokana na matatizo ambayo kwa sasa yanatukabili. Kilimo kinapaswa kipewe msukumo wa pekee ili kulikwamua taifa hili kutoka katika dimba la nchi omba omba. Zinahitajika juhudi za dhati ili kujiweka katika mustakabali wa kujitegemea, na sio tuwe wa kutegemea kila kitu kutoka kwa wahisani. Serikali inabidi itizame upya mazingira ya kilimo. Ijue kuwa lengo la kukienzi kilimo lazima liende sambamba na nyenzo bora za kisasa zinazofaa. Itumie vilivyo vyanzo vya maji ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji katika sehemu zenye uwezekano huo, hasa maeneo yenye mabwawa, mito na maziwa. Vile vile serikali ikae ikijua ukulima wa jembe la mkono umepitwa na wakati, na asilani nchi haiwezi kufuta umasikini kwa ukulima wa jembe la mkono, hizo ni ndoto, inaiwajibikia serikali ifanye jitihada hususan za kuwakopesha wakulima matrekta, majembe ya plau, mbolea na pembejeo zote muhimu kwa ajili ya kilimo. Kwani hilo ni jukumu lililo ndani ya uwezo wao. Namaana hasa ya serikali nikuweza kuwahudumia wananchi wake huduma muhimu kama hizo za kuwakopesha mikopo ili kuendesha miradi yao. Kinyume chake maana ya kuwepo serikali itakuwa hakuna iwapo itakuwa haiwasaidii wale walioipa dhamana ya kuwaongoza. Iwapo kilimo kitapewa kipaumbele basi Tanzania inaweza bila shaka kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada nje. Mazao ya biashara kama vile kahawa, chai, karafuu, tumbaku, korosho, na pamba. Iwapo yakizalishwa vilivyo na kupatiwa masoko nje, yana uwezo wa kuliingizia taifa fedha nyingi kigeni, kiasi cha sisi wenyewe kuweza kuwa na nguvu yetu ya kujiendesha. Kuliko hivi tulivyo sasa twaishi kwa kuwategemea wahisani, na hivyo kujikuta tunaburuzwa na hao "wenye kitu" kwa mambo mbalimbali kwani ndio wao wafadhili wetu. Hivyo chochote watachotaka itabidi turidhie kama masharti ya kupewa msaada. Hivyo kwa sasa serikali inabidi ijihimu katika suala hilo muhimu la
kukiinua kilimo ili kitukwamue. Izindukane na isifanye makosa tena kama
iliyotangulia kuyafanya huko nyuma.
|
YALIYOMO
Tahariri
Urambo wamlilia Profesa Lipumba
Sheikh aridhia Waislamu
kubatizwa
Uongozi Masjid Qadiria waitwa Polisi kuhojiwa Wakazi wa Mbagala Msalabani kuishitaki Tume ya Jiji Akhera ipo, makafiri ni wakadhibishaji
Mdahalo kati ya Waislamu na
Wakristo ni mgumu
Aina ya maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu PAROLE: Rais kasusa
au hana ubavu?
Serikali ikithamini kilimo
Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto
wadogo - 3
Madrasa Arrijalu Muswallin Damba Ijue Madrasat Fauzia - Kibondo Waislamu Kondoa waanza
kupokea misaada ya ujenzi wa Msikiti, Madrasa
Waislamu Dodoma wasali sala ya Ghaib kwa marehemu Kilima na mkewe Songea kujenga shule ya sekondari Wanafunzi wa Bihawana Dodoma wamshukuru Alhaj Ismail Dawood Mashindano ya kusoma Qur’an yafanyika Kondoa Waislamu wautazame upya mfumo wao wa elimu Ujenzi wa Chuo cha Kiislamu Shamsiya Bereko wakwama Kesi ya kushambulia kituo yaahirishwa tena Polisi waondolewa kimya kimya Mwembechai Msikiti wa Kiwanja cha Ndege wapania kujenga shule Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|