|
|
|
Mabadiliko ya Katiba Tanzania Ndugu Mhariri TAFADHALI sana niweke japo pembeni mwa gazeti lako ili nifikishe ujumbe wangu kwa wananchi wa Tanzania. Jambo ninalopenda kuwakumbusha ni kwamba hivi karibuni serikali ya CCM imetoa nafasi ya kutoa maoni yetu wananchi juu ya mabadiliko ya Katiba (kanuni ya nchi). Nawaasa Watanzania wenzangu kuwa Katiba iliyopo sasa hivi ni kweli imepitwa na wakati, lakini ni baadhi ya vipengele tu ambavyo vingehitajika marekebisho kidogo, lakini marekebisho zaidi yanatakiwa yafanywe kwa viongozi wenyewe wanaoshikilia katiba hiyo, vinginevyo kurekebisha katiba na kuwaacha vigogo hivyo vimeshikilia katiba hiyo kwapani na kutenda lile ambalo nafsi zao na dini zao (imani) zao zinavyotaka, hakuna maana yoyote ni usumbufu na tunapoteza wakati na fedha za kodi zetu bure. Kwani hakuna haja ya kubadili katiba, katiba iliyopo inamlinda mwananchi, lakini waloshikilia katiba ndiyo walioruhusu wananchi wapigwe risasi bila hatia, katiba iliyopo inaheshimu dini, lakini polisi (vyombo vya dola) ndiyo walokanyaga Misikiti kwa buti kule Morogoro na Dar es Salaam (Mwembechai) na kukataza mihadhara ya dini, kazi ambayo ilifanywa na Manabii wote walopita na dunia nzima hufanya hili kwa amani, lakini Tanzania ukifanya unaambiwa unaleta vurugu. Tafadhali, nashukuru jambo moja limetangulizwa suala la uboreshaji katiba, baada yake mwaka 2000 linafuata zoezi la uboreshaji "viongozi" hivyo nawaasa Waislamu (wananchi kijumla) tutumie fursa hii kwa mantiki zaidi, vinginevyo mabadiliko ya katiba hayana sababu. Ustadh Muhammad Ibn Hakika Machollah,
Wakubwa ‘wanapokopeshwa’ na walalahoi Ndugu Mhariri WIMBI la dhihaka ya aina yake linavuma kwa viongozi kuwabeza walalahoi kwa kuwahadaa kuwa wanatangaza mali zao, ambazo kwa yakini yao wanaona wamepata kwa njia zilizo halali. Watanzania wengi wanafikiria hatua ya kupata mali zilizotajwa na hao wachache waliojitokeza ni ndoto za mchana, na haiwezekani kutokana na mfumo mzima wa maisha tulionao. Ikizingatiwa mtumishi wa umma ambaye anaishi kwa kutegemea mshahara ni wazi kuwa mali zilizotangazwa na hao waheshimiwa zitakuwa zimepatikana kwa njia zenye utata. Hivyo hivi sasa ni wakati muafaka kwa taasisi ya kuzuia rushwa kutumia taaluma ya kazi yao ili kufanya linalotarajiwa na umma wa Watanzania. Hata hivyo, kitendo cha kupata mkopo wa kiasi kilichoelezwa na Mheshimiwa Sumaye unahitaji kufanyiwa kazi ili kuona kama hapa madaraka hayajatumika kujipatia mkopo huo. Bw. David Mattaka ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Mfuko wa Pensheni wa mashirika ya umma (PPF) anayo nafasi ya kujibu mashaka yanayojitokeza. Ni kweli mwanachama wa shirika la Akiba ya Wafanyakazi wa mashirika ya umma anaweza akapata kiasi angalau robo ya hicho alichopata Waziri Mkuu? Pia wananchi inafaa waangalie ni viongozi wa aina gani tulionao na kama wana uchungu nasi pamoja na nchi kwa ujuma, isiwe wana uchungu wa ubinafsi. Utawakuta baadhi ya viongozi wana nyumba, viwanja, mashamba, magari na vitu vingi vya anasa na bado anadai ana uchungu wa maendeleo ya nchi. Waheshimiwa wote waliotajwa hapo awali wanastahili kuchukuliwa hatua kama alivyochukuliwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Wanyapori Tanzania. Mkurugenzi huyu ambaye mali zake anazotuhumiwa kuzimiliki kwa kutumia mkondo wa rushwa hazikaribii hizi za hawa waheshimiwa, taasisi ya rushwa huu ni wakati muafaka wa kujiondoa katika lawama za utendaji wa kusukumwa. Na Jamillah N,
Waislamu tusiwe makondoo Ndugu Mhariri NAOMBA nafasi katika gazeti lako ili nitoe dukuduku langu kwani linanikera sana moyoni mwangu. Kwani ukimkamata kondoo katika zizi kisha ukamchinja mbele ya kondoo ukamchuna, kisha ukamkatakata, muda wote wa shughuli hiyo kondoo wenzake hawatokula majani watakuwa wameduwaa na kumsikitikia kondoa mwenzao. Ajabu ukimaliza kuondoa minofu na kufukia damu mchanga kondoo wale watasahau mkasa ule na kuanza kula majani kama kawaida. Sisi Waislamu tusiwe kama kondoo, mauaji ya Mwembechai yasipate nafasi ya kusahauliwa kiasi hicho tufungue kesi mahakamani. Paroko Lwambano, Mhe. Waziri Ameir, Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Makamba, polisi ‘piga yule’, ‘bado ongeza’ Nani alichochea na nani aliidhinisha amri hiyo wakaieleza mahakamani. Ramla Iddi Salum,
Tatizo la maji Newala halijapatiwa uvumbuzi Ndugu Mhariri, Kwa muda mrefu wananchi waishio Wilayani hapa Newala, mjini na vijijini wamekabiliwa na tatizo hilo la maji. Tatizo ambalo kwa vizazi vya miaka ya hivi karibuni tangu miaka ya 1980 hadi1998 wamezaliwa na kukulia katika tatizo hilo na kwamba ikitokea kuhadithiwa upatikanaji wa maji wakati wa Mkoloni na baada, miaka michache baada ya uhuru, bila kuwepo alama ya matanki ni jambo la kushangaza na kwamba anaweza kushindwa kuaminika mwenye kutowa habari hiyo, kwani hutokea mtoto huyo au (kijana) huyo hajaona hata kwa siku bomba zilizopo zinatoa maji, kinyume cha kupata maji katika mabwawa (visima) vilivyojengwa katika nyumba za mababu zao. Kutokana na adha hii, Serikali Wilayani hapa, iliamua kuchangisha mfuko wa maji kupitia zao la Korosho kila kilo moja kukatwa sh.7/- na kuweza kukusanya kiasi ambacho kingeweza kutatua tatizo hili. Kwa maelezo ya serikali katika ziara ya Waziri Mkuu mwaka huu ni kwamba "wananchi wamechanga fedha sio chini ya sh.50,000,000 ambazo zitawezesha kwa kiasi fulani kupunguza au kumaliza tatizo hilo, lakini jambo la kushangaza ni kwamba tangu mashine mpya yamefungwa" wananchi hupatiwa maji hayo kwa mgao, wiki mara moja -ambayo hupampu kwa dakika chache tu. Swali la kujiuliza ni kwamba (1) Mji wa Newala waweza kutosha maji kwa dakika 30? (2) Kama tatizo lilikuwa mashine, na wananchi kuchangishwa, mashine ikafungwa, vipi maji yasipatikane kama nyakati za nyuma? au Kwenye chanzo cha maji - maji yamepunguwa? Na kama yamepunguwa, yanayomwagiliwa bustani za wakubwa pale Makondeko na sehemu zingine ni yapi?" Tafuteni uvumbuzi!! Mohamed Ibn Hakika Machelah (Mkereketwa wa jamii).
Swadaka kwa wasomaji AN-NUUR Kanda ya Kusini Lindi na Mtwara Ndugu Mhariri, Awali ya yote nianze kumshukuru Mola Subhana wa Taghala aliyeniwezesha kushika kalamu na karatasi, baada ya fikra ambazo yeye ni mwenye kunibariki ili niweze kutafakari nasema :Alhamdulillah." Lengo langu ni kwamba, nimeona si busara kutowa shukrani zangu kinyemela, bali nitowe shukrani hizo kwa uwazi kwenu AN-NUUR kupitia katika gazeti letu tukufu la AN-NUUR baada ya kitendo cha ujasiri mlichokifanya baada ya ziara yenu katika Kanda ya Kusini. Mmeamua kwa makusudi kwa nia safi mbele ya Alwah, kutowa swadaka kwa wasomaji wa kanda ya kusini, kupunguziwa bei, badala ya sh.200/- na kutuuzia sh. 100/- ambayo ni sawa na asilimia 50 ya mauzo. Hii inathibitisha na kuonyesha jinsi kwa kina mlivyodhamilia kuuendeleza Uislamu haujakamilika na tatizo lililopo ni elimu kuwekwa nyuma - jambo ambalo linabidi litafutiwe uvumbuzi haraka iwezekanavyo - ikiwa ni pamoja na kutoa gazeti hili daima milele. Juhudi zenu Molla ndiye mjuzi wakuhesabu na kuhifadhi Inshallah Mtalipwa. (Mtazikuta). Mwisho napenda kuikumbusha jamii ya Kiislamu kuwa endapo mtakumbushwa jambo ambalo hamjawa na yakini nalo, au mlisahau kulitekeleza ukakumbushwa kwa dalili haswa, na ukaelewa au kukumbuka, basi hamna tena mjadala, kwani penye aya ya Mwenyezi Mungu au Hadithi ya Mtume (s.a.w.) hapatakiwi tena mjadala au fatuwa ya Sheikhe, la msingi ni kutekeleza tu endapo ma-waumini wa kweli. Muhammad Mkasheikh -Newala.
|
YALIYOMO
Tahariri
Urambo wamlilia Profesa Lipumba
Sheikh aridhia Waislamu
kubatizwa
Uongozi Masjid Qadiria waitwa Polisi kuhojiwa Wakazi wa Mbagala Msalabani kuishitaki Tume ya Jiji Akhera ipo, makafiri ni wakadhibishaji
Mdahalo kati ya Waislamu na
Wakristo ni mgumu
Aina ya maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu PAROLE: Rais kasusa
au hana ubavu?
Serikali ikithamini kilimo
Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto
wadogo - 3
Madrasa Arrijalu Muswallin Damba Ijue Madrasat Fauzia - Kibondo Waislamu Kondoa waanza
kupokea misaada ya ujenzi wa Msikiti, Madrasa
Waislamu Dodoma wasali sala ya Ghaib kwa marehemu Kilima na mkewe Songea kujenga shule ya sekondari Wanafunzi wa Bihawana Dodoma wamshukuru Alhaj Ismail Dawood Mashindano ya kusoma Qur’an yafanyika Kondoa Waislamu wautazame upya mfumo wao wa elimu Ujenzi wa Chuo cha Kiislamu Shamsiya Bereko wakwama Kesi ya kushambulia kituo yaahirishwa tena Polisi waondolewa kimya kimya Mwembechai Msikiti wa Kiwanja cha Ndege wapania kujenga shule Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|