|
|
|
UPO msemo wa wahenga kwamba kwa fundi seremala mzuri hakuna kiti. Hivi karibuni tumepata bahati ya kupata nasaha kutoka kwa Mwalimu Nyerere juu ya demokrasia na uongozi bora. Nasaha juu ya uongozi bora kama ilivyoripotiwa na gazeti la Sunday News (Nov. 22,1998) alizitolea huko Harare, wakati zile za demokrasia alizitoa wakati tulipotembelewa na Rais Nelson Mandela hivi karibuni. Mwalimu Nyerere katika nasaha zake aligusia umuhimu wa watu kuheshimu katiba, demokrasia pamoja na kuwa na utawala madhubuti wenye ridhaa ya watu na unaotekeleza majukumu yake kwa manufaa ya watu. Maneno kama haya kusemwa na mtu kama Mwalimu si jambo la kupuuzwa kwani ameona na kushuhudia mengi ndani ya kipindi cha miaka 25 aliyotawala. Mfano katiba ya muda ya Muungano ya Mwaka 1964 ambayo hadi leo makubaliano ya kuunda katiba mpya baada ya mwaka mmoja yanasubiri utekelezaji (Rejea Kitabu cha Aboud Jumbe 1994). Kuhusu suala la kukaa miaka mingi madarakani hili Mwalimu aliliona; kwamba mtu anaweza akakaa miaka tele na bado akachaguliwa kwa kura nyingi tu. Kimsingi mpiga kura angeweza kuamua nani akae na nani aondoke, lakini nguvu za kidemokrasia za wananchi kutumia kura hazitoshi kumwondoa mtu madarakani. Bahati mbaya nasaha hizi zinatolewa katika mtazamo wa kimataifa tena kwa lugha ya Kiingereza. Upo wasiwasi kwamba nasaha nzuri kama hizi zitawanufaisha zaidi watu wa nje kuliko wazawa ambao hawapati fursa yakuzielewa hotuba hizi zinazotolewa kwa lugha ya Kiingereza. Hali kama hii inaweza ikatoa picha isiyo sahihi, watu wakadhani kuwa sisi hapa petu hivi sasa hatuna matatizo yanayohitaji nasaha za namna hii. Kwa mfano matokeo ya uchaguzi wa 1995 katika baadhi ya majimbo hadi leo kesi zinaendelea mahakamani watu wanapinga matokeo. Katika mazingira ya kawaida mtu ungelitarajia mtu akubali kushindwa katika demokrasia ya watu kuchagua viongozi wanaowapenda. Kwa kutizama hukumu za mahakama kuhusu baadhi ya kesi, imebainika kwamba baadhi ya waliotangazwa kushinda hawakushinda katika misingi halali ya demokrasia. Inasikitisha kuwa miongoni mwa matokeo yaliyobatilishwa yaliwahusu mawaziri. Katika mazingira hayo kuheshimu demokrasia hakuishii tu kukubali kushindwa. Bali kukubali pia kuzingatia umuhimu wa kuheshimu na kufuata taratibu halali za kupata ushindi huo. Siku moja kabla ya uchaguzi wa 1995 wananchi walihakikishiwa kuwa maandalizi yote ya uchaguzi yalikuwa yamekamilika. Lakini siku ya uchaguzi baadhi ya vituo havikuwa na karatasi za kupigia kura. Baadhi havikuwa na orodha za wapiga kura, vingine havikupata vifaa kuanzia asubuhi mpaka jua lilipokimbia hatua. Ili mradi kila aina ya kasoro zilijitokeza. Ni katika hali kama hiyo mkoa wa Dar es Salaam ulilazimika kurudia uchaguzi. Baya zaidi wakati wa kurudiwa uchaguzi huo wapo waliochoshwa na usumbufu uliotokea hapo awali na hivyo kususa kurudia kura. Wengine vikaratasi vyao vilipotea na baadhi yao walipoteza imani juu ya namna uchaguzi mzima ulivyokuwa unaendeshwa. Kama alivyosema Mwalim hata hii nayo siyo demokrasia ni fedheha tupu. Neno hili Mwalim alilitumia katika hotuba zake hizo alizotolea nasaha. Lakini alilisema kwa Kiingereza "It is not democracy, it is a shame." Laiti Mwalim angelituandalia nasaha zake na kuzielekeza nyumbani katika matatizo mengi yanayotukabili, hakika tungelifaidika sana. Katika kadhia hiyo ya demokrasia aliyoizungumza kwa lugha ya Kiingereza, Mwalim pia alitilia mkazo umuhimu wa kuwa na utawala mzuri. Unaozingatia sheria za nchi na haki za binadamu. Mwaka huu wa 1998 Tanzania imejitia doa kubwa katika suala hili la utawala mzuri na haki za binadamu. Februari mwaka huu raia waliuliwa kwa kupigwa risasi na polisi mchana kweupe tena hadharani. Watu wameuliwa kwa kulengwa kwa amri na mashinikizo ya "piga yule, bado ongeza" mpaka hao waliokuwa wakipigwa wanakata roho mbele ya halaiki na mbele ya kamera za televisheni. Tukio hilo la kusikitisha limemhuzunisha karibu kila mwananchi. Katika mazingira ya utawala mzuri wa kidemokrasia unaojali haki za kibinadamu wafiwa wasingewahi kurejea toka makaburini kabla ya wahusika hawajatiwa mbaroni. Hapa tunapenda kumwambia Mwl. Nyerere Baba wa Taifa hatua hizo hazikuchukuliwa. Waliouliwa ni watoto wa taifa hili. Lakini hadi leo hatujasikia kutoa kauli juu ya tukio hilo ndani ya nchi wala si nje ya nchi. La kustaajabisha zaidi chama cha siasa alichokiasisi, CCM ambacho ndicho kilichounda na kinachoongoza serikali hii iliyopo madarakani kilionesha kuridhishwa na tukio hili. Na uongozi wa Jeshi la Polisi uliwapongeza askari wake kwa yale waliyoyafanya katika tukio lile la Mwembechai. Lakini hatujasikia kauli wala msimamo wa Mwenyekiti wa Chama (CCM) na Rais wetu hadi hivi leo. Katika mazingira kama haya tusingetegemea nasaha za kutounga mkono wale wanaotulaumu kuwa demokrasia yetu ina kasoro, hatuna utawala mzuri unaofuata sheria na haki za binadamu. Pengine mtu anaweza akashawishika kuamini kuwa Mwembechai ingekuwa Bujumbura, Kigali au Kinshasa na mauaji hayo yakafanyika huko Mwalimu asingekaa kimya. Wahenga walisema; kwa fundi seremala mzuri wanawe hawalalii vitanda. |
YALIYOMO
Tahariri
Urambo wamlilia Profesa Lipumba
Sheikh aridhia Waislamu
kubatizwa
Uongozi Masjid Qadiria waitwa Polisi kuhojiwa Wakazi wa Mbagala Msalabani kuishitaki Tume ya Jiji Akhera ipo, makafiri ni wakadhibishaji
Mdahalo kati ya Waislamu na
Wakristo ni mgumu
Aina ya maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu PAROLE: Rais kasusa
au hana ubavu?
Serikali ikithamini kilimo
Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto
wadogo - 3
Madrasa Arrijalu Muswallin Damba Ijue Madrasat Fauzia - Kibondo Waislamu Kondoa waanza
kupokea misaada ya ujenzi wa Msikiti, Madrasa
Waislamu Dodoma wasali sala ya Ghaib kwa marehemu Kilima na mkewe Songea kujenga shule ya sekondari Wanafunzi wa Bihawana Dodoma wamshukuru Alhaj Ismail Dawood Mashindano ya kusoma Qur’an yafanyika Kondoa Waislamu wautazame upya mfumo wao wa elimu Ujenzi wa Chuo cha Kiislamu Shamsiya Bereko wakwama Kesi ya kushambulia kituo yaahirishwa tena Polisi waondolewa kimya kimya Mwembechai Msikiti wa Kiwanja cha Ndege wapania kujenga shule Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|