|
Na.164 Jamada Awal 1419, Agosti 28 - Septemba 3, 1998 |
|
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 3
(a) Rais hatakuwa na mamlaka ya kuwakilisha kwa Waziri kwa mujibu wa masharti ya ibara hii ndogo kazi yoyote ya Rais aliyokabidhiwa na sheria yoyote inayotokana na masharti ya mkataba wowote uliotiwa sahihi na Shirikisho iwapo kisheria Rais haruhusiwi kuwakilisha kazi hiyo kwa mtu mwingine yeyote. (b) ifahamike kwamba maagizo yanayotolewa na Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara hii ndogo, ya kumwagiza Waziri yeyote kutekeleza kazi yoyote ya Rais , hayatahesabiwa kwamba yanamzuia Rais kutekeleza kazi hiyo yeye mwenyewe. (9) Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara hii mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanywa kwa ajili ya kuwasilisha kwa Rais wa Mahakama azimio kuhusu hali ya afya ya Rais utahesabiwa kuwa ni mkutano halali hata kama mjumbe yeyote wa Baraza hilo hayupo au kiti chake kiwazi, na itahesabiwa kuwa Baraza limepitisha azimio hilo ikiwa litaungwa mkono kwa kauli ya wajumbe walio wengi waliohudhuria mkutano na kupiga kura. (10) Bila ya kujali masharti yaliyoelezwa hapo awali katika ibara hii, mtu atakayetekeleza kazi na shughuli za rais kwa mujibu wa ibara hii hatakuwa na madaraka ya kulivunja Bunge , kumwondoa yeyote kati ya Mawaziri katika madaraka yake au kufuta uteuzi wowote uliofanywa na Rais. (ii) Mtu yeyote atakayetekeleza kazi na shughuli za Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara hii kama ni Mbunge hatapoteza kiti chake katika Bunge wala hatapoteza sifa zake za kuchaguliwa kuwa Mbunge kwa sababu tu ya kutekeleza kazi na shughuli za Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara hii. Uchaguzi wa Rais 38.(1) Rais atachaguliwa na wananchi kwa mujibu wa masharti ya katiba hii na kwa mujibu wa Sheria itakayowekwa masharti kuhusu uchaguzi wa Rais ambayo itatungwa na Bunge kwa kufuata masharti ya Katiba hii. (2) Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, kiti cha Rais kitakuwa kiwazi, na uchaguzi wa Rais utafanyika au nafasi hiyo itajazwa vinginevyo kwa mujibu wa Katiba hii, kadri itakayokuwa, kila mara litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo:- (a) baada ya Bunge kuvunjwa; (b) baada ya Rais kujiuzulu bila ya kulivunja Bunge kwanza; (c) baada ya Rais kupoteza sifa za kushika nafasi madaraka ya kuchaguliwa; (d) baada ya Rais kushtakiwa Bungeni kwa mujibu wa Katiba hii, na kuondolewa katika madaraka; (e) baada ya kuthibitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 36 ya Katiba hii kwamba Rais hawezi kumudu kazi na shughuli zake; (f) Kama Rais atavunja sheria ya maadili ya viongozi. (g) baada ya Rais kufariki (3) Kiti cha Rais hakitahesabiwa kuwa ki wazi kwa sababu ya Bunge kupitisha hoja ya kutokuwa na imani kwa makamo wa Rais. Sifa za mtu kuchaguliwa kuwa Rais 39. B (1) Mtu hatastahili kuchaguliwa kushika kiti cha Rais wa Shirikisho isipokuwa tu kama (a) ni raia wa kuzaliwa na Shirikisho kwa mujibu wa Sheria ya Uraia; (b) ametimiza umri wa miaka arobaini;
Haki ya kuchaguliwa tena 40. (1) Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote ambaye ni Rais anaweza kuchaguliwa tena kushika kiti hicho. (2) Hakuna mtu atakayechaguliwa zaidi ya mara mbili kushika kiti cha Rais. (3) Mtu aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika au wa Zanzibar hatapoteza sifa za kuweza kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho kwa sababu kwamba aliwahi kushika madaraka ya uwaziri mkuu wa Tanganyika au wa Zanzibar. Utaratibu wa uchaguzi wa Rais 41.(1) Baada ya Bunge kuvunjwa au kukitokea jambo jingine lolote lililotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara ya 37 na inalazimu uchaguzi wa Rais kufanyika, kila chama cha siasa kinachopenda kushiriki katika uchaguzi wa Rais kitawasilisha kwa Tume ya Uchaguzi, kwa mujibu wa sheria, jina la mwanachama wake mmoja kinayetaka asimame kama mgombea katika uchaguzi wa Rais wa Shirikisho na jina la mwanachama wake mwingine kinayempendekeza kwa nafasi ya Makamu wa Rais. (2)Ifahamike pia kwamba mtu yeyote atakayependa kugombea Kiti cha Rais bila kupitia chama chochote cha siasa atawasilisha jina lake kwa Tume ya Uchaguzi pamoja na jina la mtu mwingine atayegombea nafasi ya Makamu wa Rais. (3)Mgombea wa Kiti cha Makamu wa Rais atatoka sehemu tofauti na ile anayotoka Mgombea wa Kiti cha Rais katika Shirikisho. 94) Mapendekezo ya majina ya wagombea katika uchaguzi wa Rais yatawasilishwa kwa Tume ya Uchaguzi katika siku na saa itakayotungwa na Bunge, na mtu hatakuwa amependekezwa kwa halali isipokuwa tu kama kupendekezwa kwake kunaungwa mkono na wananchi wapiga kura kwa idadi na kwa namna itakayotajwa na Sheria iliyotungwa na Bunge. (5) Endapo inapofika saa na siku iliyotajwa kwa ajili ya kuwasilisha mapendekezo ya majina ya wagombea, ni mgombea mmoja tu ambaye anapendekezwa kwa halali, Tume itawasilisha jina lake kwa wananchi, nao watapiga kura ya kumkubali au kumkataa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii na ya Sheria iliyotungwa na Bunge. (6) Uchaguzi wa Rais wa Shirikisho utafanywa siku itakayoteuliwa na Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge. (7) Mambo mengine yote yahusuyo utaratibu wa uchaguzi wa Rais yatakuwa kama itakavyofafanuliwa katika Sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo. (8) Mgombea yeyote wa kiti cha Rais atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa Rais iwapo tu amepata zaidi ya nusu ya kura zote halali zilizopigwa au, kama uchaguzi umerudia kwa sababu ya kutopatikana mgombea mwenye zaidi ya nusu ya kura zote halali, iwapo amepata ama zaidi ya nusu kura zote halali zilizopigwa au kura nyingi zaidi kuliko wagombea wengine. (9) Mtu anayegombea kiti cha urais anaweza pia kugombea kiti cha Bunge. Wakati wa muda kushika madaraka ya Rais 42.(1) Rais mteule atashika madaraka ya Rais mapema iwezekanavyo baada ya kutangazwa kwamba amechaguliwa kuwa Rais , lakini kwa hali yoyote itabidi ashike madaraka kabla ya kupita siku saba. (2) Isipokuwa kama atajiuzulu au atafariki mapema zaidi mtu aliyechaguliwa kuwa Rais, bila ya kuathiri masharti yaliyo katika ibara ndogo ya (5), atashika kiti cha Rais kwa muda wa miaka mitano tangu siku alipochaguliwa kuwa Rais. (3) Mtu aliyechaguliwa kuwa Rais atashika kiti cha Rais hadi (a) Siku ambapo mtu atakayemfuata katika kushika kiti hicho atakula kiapo cha Rais; au (b) siku ambapo atafariki dunia akiwa katika madaraka ; au (c) siku atakapojiuzulu ; au (d) atakapoondolewa kushika kiti cha Rais kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii. (4) Iwapo Shirikisho linapigana vita dhidi ya adui na Rais anaona kuwa haiwezekani kufanya uchaguzi, Bunge laweza mara kwa mara kupitisha azimio la kuongeza muda wa miaka mitano uliotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara hii isipokuwa kwamba muda wowote utakaoongezwa kila mara hautazidi miezi sita, na kwamba nyongeza hiyo kwa ujumla isizidi miezi kumi na miwili. (5) Kila Rais mteule na kila mtu atakayeshikilia kiti cha Rais, kabla ya kushika madaraka ya Rais, ataapa mbele ya Rais wa Mahakama ya Shirikisho, kiapo cha uaminifu na kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge. Masharti ya kazi ya Rais 43. (1) Rais atalipwa mshahara na malipo mengineyo na atakapostaafu atapokea malipo ya uzeeni, kiinua mgongo au posho, kadri atakavyoamuliwa na Bunge, na mshahara, malipo hayo mengineyo, malipo ya uzeeni na kiinua mgongo hicho, vyote vitatokana na mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Shirikisho na vitatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii. (2) Mshahara na malipo mengine yote ya Rais havitapunguzwa bila ya ridhaa yake wakati Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii. Madaraka ya kutangaza vita 44. (1) Bila ya kuathiri Katiba hii, Rais aweza kutangaza kuwapo kwa hali ya vita kati ya Shirikisho na nchi yoyote. (2) Baada ya kutoa tangazo, Rais atapeleka mara moja nakala ya tangazo hilo kwa Spika wa Bunge ambaye, ndani ya siku kumi na nne kuanzia tarehe ya tangazo, ataitisha mkutano wa Bunge ili kuitafakari hali ya mambo na kufikiria kupitisha au kutopitisha azimio la kuunga mkono tangazo la vita lililotolewa na Rais litakaloungwa mkono wa kura za wabunge wasiopungua theluthi mbili ya wabunge wote. Uwezo wa kutoa msamaha 45. (1) Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika ibara hii , Rais anaweza baada ya kushauriana na chombo kitakachoundwa na sheria ya Bunge kwa ajili hiyo kutenda lolote kati ya mambo yafuatayo; (a) kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama kwa kosa lolote , na aweza kutoa msamaha huo ama bila ya masharti au kwa masharti kwa mujibu wa sheria, (b) kumwachilia kabisa au kwa muda maalum mtu yeyote aliyehukumiwa kuadhibiwa kwa ajili ya kosa lolote ili mtu huyo asitimize kabisa adhabu hiyo au asitimize adhabu hiyo wakati wa muda huo maalum; (c) kuibadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote iwe adhabu tahafifu; (d) kufuta adhabu yote au sehemu ya adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa ajili ya kosa lolote au kufuta adhabu yote au sehemu ya adhabu ya kutoza, au kuhozi (au kuchukua) kitu cha mtu mwenye hatia ambacho vinginevyo kingechukuliwa na Serikali ya Shirikisho. (2) Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka utaratibu utakaofuatwa na Rais katika utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa ibara hii. (3) Masharti ya ibara hii yatatumika kwa watu waliohukumiwa na kuadhibiwa na mahakama za Shirikisho. Kinga dhidi ya mashtaka na madai 46. (1) Bila ya kuathiri masharti yaliyomo kwenye Ibara ya 47 (2) aya ya (a), (b) na (c) ya Katiba hii. Itakuwa ni marufuku kwa sheria yoyote kutungwa ya kumkinga Rais asishitakiwe mahakamani kwa kosa lolote la jinai alilotenda yeye binafsi anapokuwa ameshika madaraka ya Urais na baada ya kushika madaraka ya Urais. (2) Wakati wote Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii, haitaruhusiwa kufungua mahakamani shauri kuhusu jambo lolote alilolitenda au alilokosa kulitenda yeye binafsi kama raia wa kawaida kabla ya kushika madaraka ya Rais, yenyewe, jina lake na anwani ya mahali anapoishi huyo mdai na jambo hasa analodai. (3) Isipokuwa kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na masharti ya ibara ya 47 (10), itakuwa ni marufuku kumshtaki aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo lolote alilofanya yeye kama Rais kwa nia njema wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya Rais kwa mujibu wa Katiba hii. Bunge laweza kumshtaki Rais 47. (1) Bila ya kujali masharti ya ibara ya 46 ya Katiba hii, Bunge linaweza kupitisha azimio la kumuondoa Rais madarakani endapo itatolewa hoja ya kumshtakiwa Rais na ikapitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii. (2)Bila ya kuathiri masharti mengine ya ibara hii, hoja yoyote ya kumshtaki Rais haitatolewa isipokuwa tu kama inadaiwa kwamba Rais- (a) ametenda vitendo ambavyo kwa jumla vinaivunja Katiba au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma; (b) ametenda vitendo ambavyo vinakiuka maadili yanayohusu uandikishwaji wa vyama vya siasa yaliyotajwa katika ibara ya 18 (2) ya Katiba , au (c) amekuwa na mwenendo unaodhalilisha kiti cha Rais wa Shirikisho, na haitatolewa hoja ya namna hiyo ndani ya miezi kumi na miwili tangu hoja kama hiyo ilipotolewa na ikakataliwa na Bunge. (3) Bunge halitapitisha hoja ya kumshtaki Rais isipokuwa tu kama (a) taarifa ya maandishi, iliyotiwa sahihi na kuungwa mkono na Wabunge wasiopungua asilimia ishirini ya Wabunge wote itawasilishwa kwa Spika siku thelathini kabla ya kikao ambapo hoja hiyo inakusudiwa kutolewa Bungeni, ikafafanua makosa aliyoyatenda Rais , na ikipendekeza kuwa Kamati Maalum ya Uchaguzi iundwe ili ichunguze mashtaka yaliyowasilishwa dhidi ya Rais; (b) wakati wowote baada ya Spika kupokea taarifa iliyotiwa sahihi na Wabunge na kujiridhisha kuwa masharti ya Katiba kwa ajili ya kuleta hoja yametimizwa Spika atamruhusu mtoa hoja kuiwasilisha hoja hiyo, na kisha ,Spika atalitaka Bunge, bila ya kufanya majadiliano, lipige kura juu ya hoja ya kuunda Kamati maalum ya Uchaguzi na kama ikiungwa mkono na Wabunge wasiopungua theluthi mbili ya Wabunge wote , atatangaza majina ya wajumbe wa Kamati Maalum ya Uchaguzi. (4) Kamati Maalum ya Uchaguzi , kwa madhumuni ya ibara hii, itakuwa na wajumbe wafuatao, yaani- (a) Rais wa Mahakama ya Rufaa, ambaye atakuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati, (b) Jaji Mkuu wa Tanganyika; (c) Jaji Mkuu wa Zanzibar; (d) Wajumbe wawili walioteuliwa na Spika kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. (5) Endapo Bunge litapitisha hoja ya kuunda Kamati Maalum ya Uchaguzi, Rais atahesabiwa kuwa hayupo kazini, kisha kazi na madaraka ya Rais yatatekelezwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 37 (3) ya Katiba hii hadi Spika atakapomfahamisha Rais juu ya azimio la Bunge kuhusiana na mashtaka yaliyotolewa dhidi yake. (6) Ndani ya siku saba baada ya Kamati Maalum ya Uchaguzi kuundwa, itakaa, ichunguze na kuchambua mashtaka dhidi ya Rais, pamoja na kumpatia Rais fursa ya kujieleza, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Kanuni za Bunge. (7) Mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile katika muda usiozidi siku tisini Kamati Maalum ya uchaguzi itatoa taarifa yake kwa Spika. (8) Baada ya Spika kupokea taarifa ya Kamati Maalum ya Uchaguzi, taarifa hiyo itawasilishwa Bungeni kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Kanuni za Bunge. Baada ya taarifa ya kamati Maalum ya Uchaguzi kuwasilishwa kwa mujibu wa ibara ndogo ya (8), Bunge litajadili taarifa hiyo na litampa Rais fursa ya kujieleza, na kisha kwa kura za Wabunge wasiopungua theluthi mbili ya Wabunge wote ,Bunge litapitisha azimio ama kuwa mashtaka dhidi ya Rais yamethibitika na kwamba hastahili kuendelea kushika kiti cha Rais, au kuwa mashtaka hayo hayakuthibitika. (10) Endapo Bunge litapitisha azimio kuwa mashtaka dhidi ya Rais yamethibitika na kwamba hatastahili kuendelea kushika kiti cha Rais Spika atawafahamisha Rais na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi juu ya azimio la Bunge, na hapo Rais atawajibika kujiuzulu kabla ya kuisha kwa siku ya tatu tangu Bunge lilipopitisha azimio hilo. (11) Endapo Rais ataacha kushika kiti cha Rais kutokana na mashtaka dhidi yake kuthibitika, hatakuwa na haki ya kupata malipo yoyote ya pensheni wala kupata haki au nafuu nyinginezo alizo nazo kwa mujibu wa Katiba au Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge. Wajibu wa Viongozi Wakuu wa Vyombo vya mamlaka ya utendaji kudumisha Muungano 48.(1) Bila ya kuathiri wajibu wa kila raia uliotajwa katika ibara ya 27 ya Katiba hii, viongozi wakuu wa vyombo vyenye mamlaka ya utendaji katika Shirikisho vilivyotajwa katika ibara ya 4 ya Katiba hii, watawajibika, kila mmoja wao katika kutekeleza madaraka aliyopewa kwa mujibu wa Katiba hii , kuhakikisha kuwa analinda Katiba hii na kuimarisha na kudumisha umoja wa Shirikisho. (2) Kwa madhumuni ya masharti ya ibara ndogo ya (1), kila mmoja wapo wa viongozi wakuu wa vyombo vyenye mamlaka ya utendaji katika Shirikisho kabla ya kushika madaraka yake kwa mujibu wa Katika hii, ataapa kuitetea na kudumisha Katiba hii pamoja na Umoja wa Shirikisho. (3) Viongozi Wakuu wanaohusika na masharti ya ibara hii- (a) Rais wa Shirikisho; (b) Makamu wa Rais wa Shirikisho; (c) Waziri Mkuu wa Tanganyika; (d) Waziri Mkuu wa Zanzibar. SEHEMU YA PILI MAKAMU WA RAIS Makamu mmoja wa Rais, kazi na mamlaka yake 49 (1) Kutakuwa na Makamu wa Rais ambaye atakuwa ndiye msaidizi mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Shirikisho kwa jumla , na hususan- (a) atamsaidia Rais katika kufuatilia utekelezaji wa siku hata siku wa Mambo ya Shirikisho. (b) atafanya kazi zote atakazoagizwa na Rais; (c) atafanya kazi zote za Rais kama Rais hayuko kazini au yuko nje ya nchi. (2) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ya 37 (5), Makamu wa Rais atapatikana kwa kuchaguliwa katika uchaguzi ule ule kwa pamoja na rais , na watapigiwa kura kwa pamoja. Mgombea kiti cha Rais akichaguliwa basi na Makamu wa Rais atakuwa amechaguliwa. (3) Mtu atateuliwa kugombea kiti cha Makamu wa Rais kwa kufuata kanuni kwamba endapo Rais wa Shirikisho atatoka sehemu moja ya pili ya Shirikisho. (4) Mtu hatateuliwa kugombea au kushika kiti cha Makamu wa Rais wa Shirikisho isipokuwa tu kama (a) ni raia wa kuzaliwa wa Shirikisho kwa mujibu wa sheria ya Uraia; (b) ametimiza umri wa miaka arobaini; (c) anazo sifa za kumwezesha kuwa Mbunge. (5) Mtu yeyote hatazuiwa kuwa mgombea kiti cha Makamu wa Rais kwa sababu tu kwamba mtu huyo kwa wakati huo ameshika kiti cha Waziri Mkuu wa Tanganyika au Waziri Mkuu wa Zanzibar. (6) Makamu wa Rais hatakuwa kwa wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Tanganyika , wala wa Zanzibar. (7)Makamu wa Rais atatekeleza madaraka yake chini ya uongozi na usimamizi wa Rais , na ataongoza na kuwajibika kwa Rais kuhusu mambo au shughuli zozote atakazokabidhiwa na Rais. Wakati wa Makamu wa Rais kushika madaraka 50 (1) Makamu wa Rais atashika madaraka ya Makamu wa Rais siku hiyo hiyo Rais anaposhika madaraka. (2) Makamu wa Rais aliyeteuliwa kwa mujibu wa Ibara ya 51 (3) ataapa na kushika madaraka yake baada ya uteuzi wake kuthibitishwa na Bunge. Kiapo cha Makamu wa Rais 51.Makamu wa Rais , kabla ya kushika madaraka yake ataapa mbele ya Rais wa Shirikisho na kuitetea Katiba hii, chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge. Muda wa Makamu wa Rais kushika madaraka 52. (1) Isipokuwa kama atajiuzulu au atafariki mapema zaidi, mtu aliyechaguliwa au kuteuliwa kwa mujibu wa ibara ya 37(5), kuwa Makamu wa Rais, bila ya kuathiri masharti mengine ya ibara hii, atashika kiti cha Makamu wa Rais kwa muda wa miaka mitano tangu alipohaguliwa kuwa Makamu wa Rais. (2) Makamu wa Rais atashika kiti hicho hadi- (a) muda wake utakapokwisha; (b) akifariki dunia akiwa katika madaraka; (c) atakapojiuzulu; (d) atakapoapishwa kuwa Rais baada ya kiti cha Rais kuwa wazi; (e) atakapotiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai linaloonyesha utovu wake wa uaminifu; (f) atakapoapishwa Rais mwingine kushika nafasi ya Rais pamoja na Makamu wake; (g) atakapoondolewa madarakani baada ya kushtakiwa Bungeni kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (3) ya Ibara hii. (h) atakapoacha kushika kiti cha Makamu wa Rais, vinginevyo kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii. (3) Bunge litakuwa na madarakani kama yale liliyonayo kuhusiana na Rais, isipokuwa kwamba hoja yoyote ya kumshtaki Makamu wa Rais itatolewa tu kama inadaiwa kwamba; (a) Rais amewasilisha hati kwa Spika inayoeleza kwamba Makamu wa Rais ameacha au ameshindwa kutekeleza kazi za Makamu wa Rais; (b) ametenda vitendo ambavyo kwa jumla vinaivunja Katiba au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma; (c) Ametenda vitendo ambavyo vinakiuka maadili yanayohusu uandikishwaji wa vyama vya siasa yaliyotajwa katika ibara ya 18 (2) ya Katiba; au (d) amekuwa na mwenendo unaodhalilisha kiti cha Rais wa Shirikisho au kiti cha Makamu wa Rais, na haitatolewa hoja ya namna hiyo ndani ya miezi kumi na miwili tangu hoja hiyo ilipotolewa na ikakataliwa na Bunge. (4) Ikitokea kwamba kiti cha Makamu wa Rais ki wazi kutokana na masharti yaliyomo katika Ibara ya 52 basi mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote ndani ya siku zisizozidi kumi na nne baada ya kushika madaraka yake, Rais atamteua mtu atakayekuwa Makamu wa Rais kulingana na ibara 49 ibara ndogo ya (3) na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura za Wabunge walio wengi. (5) Masharti mengine yote ya ibara ya 47 ya Katiba yatatumika pia kuhusiana na Makamu wa Rais isipokuwa mtu tu kwamba Makamu wa Rais aliyeondolewa tena madarakani chini ya ibara ndogo ya (3) hatakuwa na sifa za kushika nafasi ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wa Tanganyika au wa Zanzibar. Kazi mamlaka ya Makamu wa Rais 53 (1) Makamu wa Rais atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Shirikisho (2)Makamu wa Rais atakuwa Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni. (3) Makamu wa Rais atatekeleza maamuzi yote ya Baraza la Mawaziri na maamuzi yote ya Bunge. (4) Bila ya kuathiri Ibara hii, Makamu wa Rais atatekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo Rais ataagiza kwamba yatekelezwe. Uwajibikaji wa Serikali 54. Serikali ya Shirikisho , chini ya mamlaka ya Rais, ndiyo itakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi juu ya Sera ya Serikali kwa jumla , na Mawaziri, chini ya uongozi wa Makamu wa Rais, watawajibika kwa pamoja Bungeni kuhusu utekelezaji wa shughuli za Serikali ya Shirikisho. Baraza la Mawaziri Serikali Baraza la Mawaziri 55. (1) Kutakuwa na Baraza la Mawaziri ambalo Wajumbe wake watakuwa ni Makamu wa Rais na Mawaziri wote wa Shirikisho. (2) Rais ndiye atakayeongoza mikutano ya Baraza la Mawaziri na endapo hayupo basi mikutano itaongozwa na Makamu wa Rais. (3) Baraza la Mawaziri litakuwa ndicho chombo Kikuu cha kumshauri Rais juu ya mambo yote yanayohusika na utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, na litamsaidia na kumshauri Rais juu ya jambo lolote litakalowasilishwa kwenye Baraza hilo. Rais atawajibika kufuata ushauri wa Baraza la Mawaziri. (5) Mwanasheria Mkuu wa Serikali atahudhuria mikutano yote ya Baraza la Mawaziri na atakuwa na haki zote za mjumbe wa mikutano hiyo isipokuwa hatakuwa na haki ya kupiga kura katika mikutano hiyo. Uteuzi wa Mawaziri Sheria ya 56.(1) Mawaziri wote ambao ni wajumbe wa Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa ibara ya 54 watateuliwa na kuondolewa madarakani na Rais baada ya kushauriana na Makamu wa Rais. (2) Pamoja na Mawaziri waliotajwa katika ibara ndogo ya (1), Rais aweza, baada ya kushauriana na Makamu wa Rais, kuwateua au kuwaondoa Naibu Mawaziri. Naibu Mawaziri wote hawatakuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri. (3) Rais aweza kuteua idadi yoyote ya Naibu Mawaziri ambao watawasaidia Mawaziri katika utekelezaji wa kazi na shughuli zao. (4) Mawaziri na Naibu Mawaziri si lazima wote watateuliwa kutoka miongoni mwa Wabunge. (5) Bila ya kujali masharti ya ibara ndogo ya (1) ikitokea kwamba Rais anahitajiwa kumteua Waziri au Naibu Waziri baada ya Bunge kuvunjwa, basi aweza kumteua mtu yeyote ambaye alikuwa Mbunge kabla ya Bunge kuvunjwa. Kiapo cha Mawaziri na Naibu Mawaziri 57. Waziri au Naibu Waziri hatashika madaraka yake ila mpaka awe ameapa kwanza mbele ya Rais kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge. Mawaziri kushika madaraka 58. (1) Muda wa kushika madaraka ya Waziri na Naibu Waziri utaanza tarehe atakapoteuliwa kushika madaraka hayo. (2) Kiti cha Waziri au Naibu Waziri kitakuwa wazi litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo:- (a) endapo mwenye madaraka atajiuzulu au kufariki dunia (b) ikiwa mwenye madaraka hayo atakoma kuwa Mbunge kwa sababu yoyote isiyohusika na kuvunjwa kwa Bunge; (c) Ikiwa Rais atafuta uteuzi na kumuondoa kazini mwenye madaraka hayo; (d) iwapo atachaguliwa kuwa Spika; (e) ukiwadia wakati wa Rais mteule kushika madaraka ya Rais basi mara tu kabla Rais mteule hajashika madaraka hayo. (f) iwapo Baraza la Maadili linatoa uamuzi unaothibitisha kwamba amevunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma; Masharti ya kazi ya Mawaziri 59. Mawaziri na Naibu Mawaziri watalipwa mshahara, posho na malipo mengineyo kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge. Mwanasheria Mkuu wa Serikali 60. (1) Kutakuwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Shirikisho ambaye katika ibara zifuatazo za Katiba hii atatajwa tu kwa kifupi kama "Mwanasheria Mkuu" ambaye atateuliwa na kuondolewa na Rais baada ya kushauriana na Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge. (2) Mtu yeyote hatastahili kuteuliwa kushika madaraka ya Mwanasheria Mkuu isipokuwa tu kama kwa mujibu wa Katiba hii ana sifa maalum, kama ilivyofafanuliwa katika ibara ya 100(8) zinazomwezesha kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanganyika au Mahakama Kuu ya Zanzibar, na amekuwa na mojawapo ya hizo sifa maalum kwa muda usiopungua miaka kumi na mitano. (3) Mwanasheria Mkuu atakuwa ndiye mshauri wa Serikali ya Shirikisho juu ya mambo ya sheria na, kwa ajili hiyo, atawajibika kutoa ushauri kwa Serikali ya Shirikisho kuhusu mambo yote ya kisheria, na kutekeleza shughuli nyinginezo zozote zenye asili ya au kuhusiana na sheria zitakazopelekwa kwake au atakazoagizwa na Rais kuzitekeleza, na pia kutekeleza kazi au shughuli nyinginezo zilizokabidhiwa kwake na katiba hii au na sheria yoyote. (4) Katika kutekeleza kazi na shughuli zake kwa mujibu wa ibara hii, Mwanasheria Mkuu atakuwa na haki ya kuhudhuria na kusikilizwa katika mahakama zote katika Shirikisho na Mahakama ya Rufaa. (5)Mwanasheria Mkuu atashika madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii na atalipwa mshahara, posho na malipo mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge. Katibu wa Baraza la Mawaziri 61. Kutakuwa na Katibu wa Baraza la Mawaziri ambaye atakuwa ndiye mtendaji mkuu katika ofisi ya Baraza la Mawaziri, na atatekeleza shughuli zifuatazo kwa kufuata maagizo ya jumla au maalum atakayopewa na Rais, yaani; (a) kuandaa ratiba ya mikutano ya Baraza na kutayarisha orodha ya shughuli za kila mkutano; (b) Kuandika na kuweka kumbukumbu za mikutano ya Baraza; (c) kutoa taarifa na maelezo ya maamuzi ya Baraza kwa kila mtu au chombo cha umma kinachohusika na uamuzi wowote; na (d) kutekeleza kazi na shughuli nyingine zozote atakazoagizwa
mara kwa mara na Rais.
|
TAHARIRI: Dawa ya ugaidi si kufanya ugaidi ndani ya ugaidi Bakwata yalaani ubabe wa Marekani
Wanakijiji wawapiga Polisi
Olesiva
Waislamu washinda kesi Same
Wasafiri ATC wadai ndege ya Jeddah
inahujumiwa
Mahojiano kati ya CNN na Bwana Usama bin Ladin Historia ya damu za mashujaa Afghanistan Msikiti wa Wagoma Kigoma wapata
viongozi wapya
Muhadhara wanguruma Masjid
Hijaz
Waislamu waitumie Misikiti
ipasavyo
Mpango wa kudhibiti uzazi utawaangamiza
wengi
Hoja za kutofautisha Yesu na Issa
ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 3
Wanawake wa Kiislamu washiriki
maonyesho ya kilimo
Wanawake wa Kiislamu washauriwa
kupigania haki zao
Africa Muslims Agency: Inavyohudumia
jamii
Kitengo cha Zakkah chasafirisha wanafunzi
Kupinga kifo cha Yesu ni kumpinga
Mungu?
Zanzibar na biashara ya utumwa
Marekani ishitakiwe
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 3
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org