AN-NUUR
Na.164 Jamada Awal 1419, Agosti 28 - Septemba 3, 1998
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
Msikiti wa Wagoma Kigoma wapata viongozi wapya

Na Suleiman Simba, Kigoma

MSIKITI wa Wagoma mjini hapa umepata viongozi wapya baada ya kufanyika uchaguzi Jumapili ya Agosti 23, 1998.

Waliochaguliwa kushika uongozi wa Msikiti huo ni Bw. Isa aliyeshika nafasi ya Uenyekiti, Sheikh Ibrahim Misango (Imamu) na Sheikh Hemed Shaaban Babadudu ambaye anakuwa naibu Imamu.

Wajumbe wengine waliochaguliwa wametajwa kuwa ni Bw. Saliboko Abas Mrombo, Amrani Mrombo, Hemed Id pamoja na kuwa mjumbe pia ameshika nafasi ya unaibu Katibu.

Baadhi ya waumini walioshiriki uchaguzi huo wamesema wamefurahishwa na jinsi uchaguzi huo ulivyoendeshwa hadi matokeo na wanamatarajio makubwa kwa viongozi hao kuwa huenda wakawa chemchem ya maendeleo ya Msikiti huo na waumini wake.
 
 


Muhadhara wanguruma Masjid Hijaz


 


- Vitabu vinne vya Mungu vyahubiriwa
- Wanne waingia katika Uislamu
- Biblia zagawiwa shuleni Kibamba

Na Said Shariff

MUHADHARA wa kwanza wa Kiislamu umefanyika hivi karibuni baada ya mihadhara hiyo kukwama kufanyika kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita kufuatia Polisi kuvamia Msikiti wa Mwembechai ambapo Waislamu kadhaa waliuawa.

Muhadhara huo ambao ulifanyika Masjid Hijaz Kigogo Mwisho njia panda Jijini, kwa muda wa wiki mbili kuanzia Agosti 4, 1998 uliwajumuisha wahadhiri kutoka vikundi vya Khidamat Da’awaat Al-Islamiya na Al-Mallid International Propagation Centre.

Vitabu vinne vya Mwenyezi Mungu, Zaburi, Torati, Injili na Qur’an vilihubiriwa katika muhadhara huo ambapo wahadhiri walitoa mada mbalimbali. 

Kulikuwa na vipindi vya maswali na kujibiwa kwa kutumia maandiko (aya) matakatifu ya Allah (sw).

Wakristo wanne waripotiwa kuingia Uislamu kufuatia muhadhara huo.

Wakati huo huo, wazazi Waislamu wa Kibamba wamelalamika kwamba watoto wao katika shule za msingi wamekuwa wakigawiwa Biblia.

Wamedai kwamba wamewaona walimu wakuu wa shule husika hata hivyo wamedai kwamba hawajui lolote. 

Walimu hao wakuu wamesema kwamba wamegundua kwamba wapo waalimu binafsi ambao huwashawishi watoto na kuwapa Biblia wasome, kwani ni neno la Mungu.
 
 

Waislamu waitumie Misikiti ipasavyo


 


Na Ashraf Yusuph, Moshi

WAISLAMU mjini Moshi wamehimizwa kuitumia Misikiti katika kuendeleza na kuilinda jamii ya Kiislamu.

Hayo yamesemwa na Sheikh Ramadhani Hamza katika khutba ya sala ya Ijumaa katika ufunguzi wa Msikiti wa Al-Haramain Islamic Foundation hapo hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya khutba na shukrani kwa wale wote walioamini kweli kweli, na shukrani kwa wadhamini wa Msikiti huo Al-Haramain Islamic Foundation.

Akinukuu aya za Qur’an na tafsiri zake, Sheikh Ramadhani alisema, "hakika Misikiti ni mali ya Mwenyezi Mungu" (ingawa wajengaji na watu). Hivyo pasiwepo na dhana au fikra kuwa Misikiti ni mali ya mtu au watu fulani.

Aliendelea Sheikh huyo kuwa pamoja ardhi yote kuwa ni Msikiti bado Mtume (saw) alipohamia Madina kutoka Makka kitu cha kwanza kufanya alijenga Msikiti ili iwe ni kituo cha harakati za Kiislamu.

Sheikh Ramadhani alionya juu ya imani potofu kwa baadhi ya waumini kusema kuwa Misikiti ni mali ya watu au dhehebu fulani, hiyo inapelekea kuwafarakanisha Waislamu badala ya kuwaunganisha.

Sheikh Ramadhani alihitimisha khutba ya Ijumaa kwa kuwakaribisha waumini wote wa Kiislamu kuja kufanya ibada na kusoma katika Madrasa ya Al-Haramain bila woga wala kujali itikadi zao.

Msikiti huo wa Al-Haramain ni mmoja kati ya Misikiti mizuri na mikubwa katika mji wa Moshi, upo sehemu ya Njoro-Railways. Kutokana na ukubwa wa Msikiti huo pamoja na madrasa iliyojengwa baadhi ya waumini wa mji wa Moshi Majengo na Njoro wameonyesha matumaini yao kuwa Masjid Al-Haramain ni kituo cha elimu na maendeleo ya Waislamu wa Moshi mjini na nchi nzima kwa ujumla.

Sheikh Ramadhani ni muasisi wa Madrasa maarufu hapa Mji Mpya Njoro na Moshi mjini ambayo inaongoza kwa kutoa taaluma zote za dini, inayojulikana kama Madrasat Iyahudiin.

Msikiti wa Al-Haramain utatoa fursa kwa Waislamu wa Moshi Mjini, Majengo na Njoro wenye uchu wa elimu ya dini kuchota elimu kwa mwanazuoni Sheikh Ramadhani Hamza ambaye ndiye Imamu mkuu na Amir wa Msikiti huo.

Wakati huo huo, vijana wa Kiislamu Majengo Moshi wameanzisha jumuiya yao kwa lengo la kuleta umoja na mshikamano baina yao. 

Vijana hao wameazimia kufuata Qur’an na Sunna ya Mtume (saw) katika maisha yao ya kila siku.

Aidha, vijana hao wameazimia kushirkiana katika mambo ya harusi, maradhi pamoja na vifo ili kuondoa tofauti baina yao kiitikadi.

Vijana hao wamejiwekea mikakati kabambe kama vile michango maalum ya kila mwezi ili baadaye kuweza kutumika katika masuala mbalimbali ya Uislamu na umoja huo.

Wameazimia kuanzisha miradi mbalimbali ili kuweza kupata fedha za kuendesha umoja huo pale mipango itakapokamilika.

Mpango wa kudhibiti uzazi utawaangamiza wengi’

Na Mwandishi Wetu

WANAWAKE wametakiwa kuchukua hadhari kubwa dhidi ya kampeni zinazoendelea za kudhibiti uzazi kwani huenda zikawaletea maangamizi makubwa.

Imeelezwa kwamba madawa kemikali na njia mbalimbali zinazotumika kuzuia mwenendo wa kawaida (maumbile) wa mwili kibaolojia; imekuwa ndio sababu kubwa ya matatizo mengi yanayowasibu kina mama sasa hivi.

Matatizo hayo ni pamoja na kansa katika sehemu za uzazi, shinikizo la damu na matatizo mbalimbali yahusuyo hali za wanawake.

Akiwasilisha mada katika hafla ya kuwaaga wanachuo wa M.C.H Same hivi karibuni, mshiriki mmoja Mama Kiseto alisema kwamba mbali na matatizo hayo ya kiafya yapo matatizo makubwa ya kijamii ambapo huenda jamii ikafika mahali ikakosa nguvu kazi.

Aidha, kwa kutojua mambo ya ghaibu mara nyingi wazazi hujuta kwa ukiwa baada ya kukosa wa kuwalea au kuwafariji kwasababu mtoto mmoja au wawili waliowategemea waweza kufa au kuharibikiwa kimaisha.

Mama Kiseto ambaye ni Mwalimu wa shule ya msingi Chalao Mlimani, Same alisisitiza kwamba mbali ya kuwa kuacha kuzaa kwa kuchelea hali ya maisha ni kuingilia milki ya Mwenyezi Mungu, lakini pia ni mpango ambao hatima yake ni kumuangamiza mwanadamu mwenyewe.

Akizungumzia suala la mahari, Mama Kiseto alisema kwamba mahari ni zawadi na sio bei na hivyo sio lazima iwe fedha au ng’ombe, mbuzi n.k.

Aidha, amesema kwamba kwa mujibu wa Qur’an apewaye mahari ni yule anayeolewa na kwa hivyo basi yeye ndiye anayepanga kiwango cha mahari. Kwa hiyo akasema si haki na wala si katika sheria ya Allah wazazi kuwapangia mahari mabinti zao kulingana na rangi, sura au elimu.

Kwa upande mwingine, mama Kiseto ameyataka mashirika na taasisi zinazodai kupigania haki za wanawake ziangalie hali inayokubuhu ya kudhalilishwa wanawake kupitia matangazo ya biashara, uvaaji nguo fupi na kujichubua ngozi pamoja na kupungua kasi ya ndoa huku ufuska ukiongezeka.

Mama Kiseto alisisitiza kwamba haki na heshima ya wanawake hupatikana katika Uislamu na wala si mila, desturi na kampeni zilizo nje ya Uislamu.

Kati ya wahitimu 36 wa M.C.H. Same, kwa mwaka huu 1998, 9 tu ndio Waislamu. Pamoja na uchache wao wahitimu hao Waislamu waliandaa hafla kubwa ya kuagana na wenzao.

Katika hafla hiyo ilisomwa Maulid Nabii, ambapo mada mbalimbali zilitolewa
 

Juu

YALIYOMO

TAHARIRI: Dawa ya ugaidi si kufanya ugaidi ndani ya ugaidi

Bakwata yalaani ubabe wa Marekani
Na Mwandishi Wetu

Wanakijiji wawapiga Polisi Olesiva
Na Mwandishi wetu, Arusha

Waislamu washinda kesi Same
Na Mwandishi Wetu, Same

Wasafiri ATC wadai ndege ya Jeddah inahujumiwa 
Na Mwandishi Wetu

KOSOVA: Bosnia nyingine

Mahojiano kati ya CNN na Bwana Usama bin Ladin

Historia ya damu za mashujaa Afghanistan

Msikiti wa Wagoma Kigoma wapata viongozi wapya
Na Suleiman Simba, Kigoma

Muhadhara wanguruma Masjid Hijaz
Na Said Shariff

Waislamu waitumie Misikiti ipasavyo
Na Ashraf Yusuph, Moshi

Mpango wa kudhibiti uzazi utawaangamiza wengi
Na Mwandishi Wetu

Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu,  ni uzushi mtupu! - 3
Na Muhibu Said

Wanawake wa Kiislamu washiriki maonyesho ya kilimo
Na Habiba Swedi

Wanawake wa Kiislamu washauriwa kupigania haki zao
Na Habiba Swedi, Arusha

Africa Muslims Agency: Inavyohudumia jamii
Na Mwandishi Wetu

Kitengo cha Zakkah chasafirisha wanafunzi
Na Mwandishi Wetu

Kupinga kifo cha Yesu ni kumpinga Mungu?
Mahfudhi M. Mahfudhi

MAONI: Porojo za Ngatara -2

Zanzibar na  biashara ya utumwa
Na J. Hussein

Marekani ishitakiwe
Na Abubakar Msham

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 3

Mafundisho ya Quran

Barua za wasomaji

Mashairi

Masomo ya dini ya Kiislam

Chakula na Lishe
 
 
 
 
 
 
 

 

 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita