AN-NUUR
Na.164 Jamada Awal 1419, Agosti 28 - Septemba 3, 1998
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
Uovu usihusishwe na dini

Ndugu Mhariri

NAOMBA nisahihishe mawili yaliandikwa katika barua ya Bi. Getrude John na pia Uhariri wa gazeti litokalo kila siku ya Jumapili la dini (siyo Annuur) katika toleo Na. 023 la tarehe 16-22, Agosti, 1998 ukurasa wa 4.

Bi John, Qur’an 8:23 aliyenukuu haimaanishi kuwa Mungu anayo sifa ya kutojua, bali inathibitisha kuwa Mungu anajua kila kitu nyakati zote. Ili kuilewa aya hiyo vizuri, anzia aya ya 8:22 "Hakika vinyama (viumbe/creations) yaani watu (tazama pia sura 2:18) viovu ni hawa wanaojipa uziwi na ububu (wa kutosikia wala kukiri haki), ambao hawayatii akilini wanayoambiwa (bali wanayakataa tu bila ya kupima kwanza). 23: Na kama Mwenyezi Mungu angalijua (angaliona kuwa watu hao wanao) wema (usikivu wa haki) wowote kwao (hao watu viziwi, na mabubu) angeliwasikilizisha…"

Kwa bahati, maneno ya Kiarabu yenye tafsiri hii ni jirani na Kiswahili, nanukuu: ‘Walau alima Llahu Fiyhim Khayran = Lau Mungu angeijua kheri (usikivu haki) yeyote juu ya watu hao"" Yaani Mungu alijua fika kuwa watu wale ni wale ambao hata Biblia yawaita vipofu, viziwi na mabubu (Zaburi 115:4-8), hawaisikii, hawaoni wala hawaikiri haki kila waambiwapo, ndiyo maana Mungu hakuwasikilizisha.

Aliyetengeneza sanamu na kuiabudu, hata umwabieje juu ya Mungu asiyemwona hawezi kusikia, kuelewa, kuona wala kukiri. Anakuwa zuzu kama sanamu lake!

Sahihisho jingine lahusu katika ukurasa huo huo unaodai hivi: "… Wahusika (waliolipua mabomu kwenye Balozi za Marekani Dar na Nairobi) mnamo tarehe 7, Agosti, 1998 hao wanahisiwa ni makomandoo wa Mujahidina, ambao kwa mujibu wa imani yao kumuua kafiri tayari wamekata tikiti ya kuingia peponi…"

Semi za kijumla (generalization) namna hizi si kweli, hususani baadaye kidogo Agosti 15, 1998 huko Ireland watu wengine kabisa wameuwa kikatili Wairish 28, na vyombo vyote vya habari katu havitaji kuwa magaidi wale ni Wazungu (siyo Waarabu) tena Wakristu (siyo Waislamu).

Mwaka juzi pia jumba kubwa kule Oklahoma, Marekani lilipolipuliwa, vyombo vya habari vilishataja hata majina ya washukiwa kuwa ni Waarabu na Waislamu, kumbe ni Mzungu tena Mkristo!

Kila dini au taifa au kabila haikosi watu waovu miongoni mwake. Utambulikapo uovu wowote, kamwe usihusishwe na dini hiyo yote, bali ahusishwe yule mwovu peke yake.

Kila uovu upo katika kila dini au taifa, ufuska upo kwa viongozi wa kidini (Marais, marabi, Masheikh na hata Mapapa), uuwaji pia upo kila mahala, si kwa Waislamu tu.

Naomba nisahihishe dhana ya watu wengi kuhusu "Mujahidina" na neno lihusianalo nalo "Jihad".

Jihad yaani kwa maana ya Vita Vitakatifu (Qital) ina masharti mengi sana katika Uislamu, na kuu ni sharti vita hivyo vitetee Uislamu na siyo maslahi ya mtu au kundi moja la kisiasa au kiuchumi, n.k..

Endapo nchi inatawaliwa na wasio Waislamu na Uislamu utokee kuchokozwa kivita, hapo Waislamu wameruhusiwa kuutetea Uislamu ikibidi kivita pia, lakini mara uchokozi utakapokoma, basi Jihad pia ni lazima isitishwe.

Historia imeonyesha kuwa wapo viongozi wengine wameitisha Jihad kukidhi maslahi yao binafsi hasa ya kisiasa. Hiyo siyo Jihad (Qital), na Waislamu wana haki ya kuikataa.

Lakini watu wanaokufa katika Jihad ya kikweli kabisa, na sharia zitawalazo vita vya aina hii ni ngumu (complex) sana. Wafu hao huwa ni mashahidi halisi na hao huingia peponi moja kwa moja.

Qur’an imeruhusu kupiganwa vita pale tu dini ya mtu inapohujumiwa: 22:39-41 Wameruhusiwa kupigana wale wanaopigwa, kwa sababu wamedhulumiwa… 40" ambao wametolewa majumbani mwao pasina haki ila kwa sababu wamesema ‘Mola wetu ni Mwenyezi Mungu’. Na Kama Mwenyezi Mungu asingaliwakinga watu, baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangalivunjwa mahekalu, na Makanisa na nyumba zingine za ibada na Misikiti ambamo jina la Mwenyezi Mungu hutajwa kwa wingi. Na bila shaka Mungu humsaidia yule anayesaidia dini yake…"

Si kweli pia kwamba kila asiyekuwa Muislamu au kila anayekufuru (kafiri) ni sharti auawe hata asipochokoza mtu. Ndiyo maana mjomba wa Mtume Muhammad (saw), Abu Lahab alikuwa adui mkuu wa Uislamu hata alivyobakia kuwa mkuu wa Bani Hashim, ukoo wa Mtume (saw) na hatimaye alikufa huku akiwa adui na kafiri vile vile bila kusilimu.

Hata Qur’an ilimtabiri Abu Lahab akiwa yu hai kuwa hatowahi kuuacha ukafiri na asilimu, na mwishowe alikuja kufa na mkewe na wanawe bila kusilimu, na hakuna aliyejaribu kuitisha jihad ya kumuua Abu Lahab ili ajipatie pepo ya bure. Utabiri huo (wa Abu Lahab kufa bila kusilimu) pamoja na tabiri nyingi zingine za Qur’an zimebakia na zitabakia kweli hadi mwisho.

Dk. A. Juma,
S.L.P. 70511,
Dar es Salaam. 
 
 


Ujumbe kwa waandishi


 


Ndugu Mhariri

NAOMBA unifikishie ujumbe wangu kwa waandishi wako wawili, Bw. Muhibu Saidi na Bw. Abdul Gullam ambao waliandika makala zao kwenye gazeti hili la tarehe 14, Agosti, 1998.

Bw. Muhibu aliandika kuhusu Yesu au Isa na Bw. Gullam aliandika kuhusu Ukristo na Ujamaa vimeshindwa.

Mabwana hawa wawili wamejitahidi kunukuu aya mbalimbali za Biblia ili kutetea hoja zao, pia wote wawili wamemshambulia Mtume Paulo. Bw. Gullam anadai Ukristo uliasisiwa na Paulo, na Bw. Muhibu anadai Paulo ndiye aliyezua kuwa Yesu alikufa kisha kufufuka.

Tatizo kubwa lililopo kwa hawa mabwana pamoja na Waislamu wengine ni kule kuisoma Biblia kwa kuchagua aya mtu anayotaka aisikie, aya ambazo ni kali kwao hawathubutu kuzisoma.

Kwa mfano wao hupenda kunukuu Mathayo 15:24 Yesu anaposema sikutumwa ila kwa wana kondoo wa nyumba ya Israel, lakini hawanukuu aya inayoendeleza hapo Yoh. 10:16 Yesu anasema anao kondoo wengine ambao siyo wa zizi hili (siyo Waisrael) ambao aliazimia awaite nao watakuwa kundi moja. Watu hawa hawawezi kunukuu Isaya 9:6 Tumepewa mtoto mwanaume (Yesu) ataiwa Mshauri wa ajabu, MUNGU Mwenye Nguvu.

Aya kama hizi ambazo ni nyingi sana hawataki kuzisikia bali huzua uongo kuwa Wakristo ndio walioanza kumwita Yesu ni Mungu.

Usomaji wa kuchagua aya mtu anazotaka kuzisikia pia umelaaniwa vikali kwenye Qur’an Suratul Al-Aaraf 7:203 "Na usipowaletea aya wazitakazo husema "kwanini huzizuii mwenyewe? Qur’an pia imeendelea kuwalaani wanafiki wanaoziogopa sura zinazowataja wao Suratul Tawba 9:64.

Bw. Muhibu na mwenzake Gullam wanafanya unafiki wa kunukuu aya wanazotaka wasikie tu. Wanadai Paulo kaanzisha Ukristo wakati Yesu mwenyewe hana habari nao. Je, wataweza kujibu maswali yafuatayo?

Wakati Yesu anaagiza lianzishwe Kanisa Mathayo 16:18 alikuwa na maana waswali humo Waislamu? Wakati Yesu anawatuma wanafunzi wake waende duniani kote, wawafanye watu kuwa wanafunzi wa Yesu, wawabatize kwa jina la Baba la Mwana na la Roho Mtakatifu (Mathayo 28:19) alikuwa na maana Waislamu wabatizwe? Wakati Yesu anasema (Yoh. 3:18) wasiomwamini mwana PEKEE wa Mungu wamekwisha hukumiwa, aliagiza Waislamu waamini hivyo?

Au wakati Yesu alipotabiri kuwa wafuasi wake watafukuzwa kwenye Misikiti (Masinagogi) Yoh. 16:1-2 Je, utabiri huo ulitimia vipi? Ni kina nani waliobaki Misikitini? Kwa kuwa Yesu alijua wafuasi wake watatoka Misikitini, ni vipi sasa Yesu asiujue Ukristo?

Usomaji wa kuchagua ni upotoshaji. Ni sawa na Mkristo anukuu Qur’an Suratul An Nahl 16:81 kuwa Mwenyezi Mungu amekufanyieni kanzu zinazowakingeni na joto (na baridi) … na kisha Mkristo huyo atafsiri kuwa kumbe Mungu wa Waislamu ni fundi cherehani anawashonea Waislamu kanzu – ni vyema? Haya ndiyo wafanyayo akina Muhibu na wenzake – upotoshaji.

Paulo wala hajazua lolote, na Biblia inawaita wajinga na wasio na msimamo Petro 3:15-16. Mwisho, naamini Mhariri utafikisha ujumbe huu bila ubaguzi kama taaluma yako ilivyo.

Elia Batendi,
S.L.P. 538,
Dar es Salaam.
 
 

Tuomboleze na kutafakari pia


 


Ndugu Mhariri

HAPA kwetu Afrika Mashariki pametokea tukio baya sana. Watu wengi wamepoteza maisha yao, wengine vilema. Kitendo hicho si kizuri kwa watu wote wapendao amani.

Lakini chakushangaza kabla ya uchunguzi haujafanyika mara zimezuka tuhuma za Waislamu.

Na watu wakamatwe, eti kwa sababu katoka Sudan au Iraq. Eti kwa sababu hana viza au paspoti. Siwezi kusema kwamba ni sahihi mtu kuingia nchi ya watu bila sheria, lakini sasa tuangalie ni nani kazembea?

Wizara ipo, polisi wapo, mtu anaingia nchini kienyeji. Mimi naona kwanza ahojiwe Waziri wa Mambo ya Ndani na watu wa Idara ya Nje za usalama wa nchi.

Pamoja na yote hayo tujiulize huu uwezekano wa mtu kutoka huko atokako akaingia ubalozini sio wa Msumbiji au Congo lakini Amerika na bomu.

Katika ulimwengu huu wa siasa za kijambazi hakuna kisichowezekana.

Napenda kumalizia kwa kuwataka wapenda amani wote duniani walaani ugaidi wa Marekani walioufanya kule Sudan na Afghanistan.

Yasini Chikwawa, 
Vingunguti,
Dar es Salaam.
 
 


Upigaji mabomu Dar, Nairobi na... wapaswa kulaaniwa vikali


 


Ndugu Mhariri

NINAKUOMBA nafasi kidogo katika gazeti lako ili kuzungumzia somo lililotajwa hapo juu.

Kwanza kabisa ninapenda kuvilaani vitendo vya mauaji kwa mabomu yaliyotokea hivi karibuni katika miji ya Dar es Salaam, Nairobi, Sudan na Afghanistn. Waislamu wapenda amani wote tunapaswa kuvilaani vikali vitendo hivi vya kinyama.

Watu wanaohusika wapaswa kushutumiwa hata kama ni Waislamu au wababe wa mataifa.

Ninapenda kutoa salamu zangu za rambirambi kwa ndugu na jamaa wa waliokumbwa na mkasa huu.

Uislamu hauruhusu kamwe vitendo vya kikatili kama hivyo dhidi ya wanaume, wanawake pamoja na watoto wasio na hatia.

Waislamu wengi tumepokea habari hizi kwa mshangao pamoja na masikitiko mengi. 

Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza viongozi wa nchi zote kwa uongozi wao wa hali ya juu walioonyesha katika kipindi hiki kigumu.

Kwa kumalizia napenda kuwauliza Wahusika wa vyombo vya kimataifa kama vile OAU, UN na vitengo vyake mbona mnaweweseka kuiambia Marekani iache sera za mabavu.

Mohamed A. Saidi,
124-8051 Ryan Rd.
Richmond B.C.
V7A 2E4
Vancouver, Canada.
 
 


Kina Ngatara na wenzake ndio urithi tuliachiwa na wakoloni


 


Ndugu Mhariri

NAOMBA nafasi ili nimpongeze Ndugu J. Hussein katika maoni yake yenye kichwa cha habari "Kina Ngatara na wenzake ndio urithi tulioachiwa na wakoloni" katika gazeti hili la Agosti 14020, 1998.

Hakika Ndugu J. Hussein amedhihirisha Uislamu wake wa dhati, usomi (itelligence) na anamjibu Ludovick Ngatara kwa ujuzi wa hali ya juu (technically and intellectually).

Hivi ndivyo tunatakiwa Waislamu wote tuwe. Siyo kama wenzetu waliopokea na kuimeza dozi ya ganzi ya kukosa kufikiri, ambao thamani ya hoja na tunu ya utafiti havina maana yoyote kwao. (Kama alivyosema Ndg. J. Hussein).

Pamoja na hongera zangu, tunakuomba Ndg. J. Hussein uirudie kuiandika hiyo makala kwa kiingereza uwatumie Sunday Observer ili watu wengine wasiosoma AN-NUUR (hawajui kwamba wanapitwa na mengi na ni gazeti pekee lenye ujasiri na ukweli wa kusisimua – One in a million) waweze kuiona.

Ujumbe wangu: Hebu jamani jaribuni kuitumia akili mliyopewa na Muumba. Hivi kweli Mungu gani anaweza kutamka "Mungu wangu! Mungu wangu! Mbona umeniacha!"?? (Eloi!, Eloi! La Sabaktani!) mmehojiwa sana kuhusu hili suala, lakini mmeshindwa kujibu, (why) mnakimbilia kiupaka matope Islamic Club! Club ambayo haizungumzii siasa wala chuki bali Uislamu wetu na maendeleo yetu wenyewe, hii inawauma nini?

Mnaacha kupiga vita ufuska na waenda uchi madisko na kwenye macasino, mnaivalia njuga Islamic Club inayohimiza mema, stara na ucha Mungu.

Si kama shetani anawashawishi nini basi? Jamani iko siku mtalalamika kusikia mtu anaitwa Fatma ama Hussein, mtataka kusikia majina yasiyo ya Kiislamu! Kama ni hivyo, hiyo ni ndoto kwenu – sahauni!

Na Islamic Club itadumu na Mola atailinda kwani inahimiza kumtii na siyo kumuasi! Idumu Islamic Club.

Fatma al-Bulush,
Box 8738,
Dar es Salaam.
 

Juu

YALIYOMO

TAHARIRI: Dawa ya ugaidi si kufanya ugaidi ndani ya ugaidi

Bakwata yalaani ubabe wa Marekani
Na Mwandishi Wetu

Wanakijiji wawapiga Polisi Olesiva
Na Mwandishi wetu, Arusha

Waislamu washinda kesi Same
Na Mwandishi Wetu, Same

Wasafiri ATC wadai ndege ya Jeddah inahujumiwa 
Na Mwandishi Wetu

KOSOVA: Bosnia nyingine

Mahojiano kati ya CNN na Bwana Usama bin Ladin

Historia ya damu za mashujaa Afghanistan

Msikiti wa Wagoma Kigoma wapata viongozi wapya
Na Suleiman Simba, Kigoma

Muhadhara wanguruma Masjid Hijaz
Na Said Shariff

Waislamu waitumie Misikiti ipasavyo
Na Ashraf Yusuph, Moshi

Mpango wa kudhibiti uzazi utawaangamiza wengi
Na Mwandishi Wetu

Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu,  ni uzushi mtupu! - 3
Na Muhibu Said

Wanawake wa Kiislamu washiriki maonyesho ya kilimo
Na Habiba Swedi

Wanawake wa Kiislamu washauriwa kupigania haki zao
Na Habiba Swedi, Arusha

Africa Muslims Agency: Inavyohudumia jamii
Na Mwandishi Wetu

Kitengo cha Zakkah chasafirisha wanafunzi
Na Mwandishi Wetu

Kupinga kifo cha Yesu ni kumpinga Mungu?
Mahfudhi M. Mahfudhi

MAONI: Porojo za Ngatara -2

Zanzibar na  biashara ya utumwa
Na J. Hussein

Marekani ishitakiwe
Na Abubakar Msham

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 3

Mafundisho ya Quran

Barua za wasomaji

Mashairi

Masomo ya dini ya Kiislam

Chakula na Lishe
 
 
 
 
 
 
 
 

 

 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita