|
Na.164 Jamada Awal 1419, Agosti 28 - Septemba 3, 1998 |
|
Marekani ishitakiwe Na Abubakar Msham Milipuko iliyotokea Ijumaa, Agosti 7, 1998 kule jijini Nairobi na hapa Dar es Salaam katika ofisi za balozi za Marekani imeleta tafsiri za namna tofauti kwa Watanzania na duniani kote. Kwanza ninasikitishwa sana na tabia ya baadhi ya Watanzania na vyombo vya habari ya kutojenga tabia ya kuwa wachunguzi wa mambo na kupata uhakika ila kutanguliza hisia zao na kuhukumu waonavyo. Aidha, imeonyesha namna gani hata uongozi na vyombo vya Dola walivyo na mtazamo finyu katika kuelewa na kufuatilia mambo. Hapana shaka kwamba kumekuwa na udhaifu mkubwa katika kutafuta kweli iliyo nyuma ya milipuko iliyotokea. Kinachozingatiwa zaidi ni udini na utaifa yaani ni lazima walipuaji wawe ni Waislamu (siasa kali) au Waarabu na hivyo kuanza kazi bila ujuzi wowote ila kamatakamata na kupambiwa sana na vyombo vya habari vyote nchini ambavyo takribani vyote vinatenda kazi zao kwa kufuata itikadi za kisiasa na kidini. Hata kama itagunduliwa ni hao wanaoshukiwa lakini bado inapaswa sisi sote kujiuliza ni kwanini walipuaji wachukue hatua hiyo. Na kwanini iwe ni Marekani tu na hao ‘Waarabu’? Waislamu si wajinga kama inayodhaniwa bali ni watu mahir wanaoujua wajibu wao vilivyo kulingana na mazingira waliyomo. Walimwengu tungekuwa wakweli tungalifuatilia historia ya matukio kama hayo kisha tukaangalia sababu zinazowapelekea walipuaji kufanya hivyo; halafu tukaangalia pia historia inayotawala katika mahusiano ya serikali ya Marekani kimataifa ambayo ni mabaya kwa baadhi ya nchi au jumuiya za wananchi wa nchi kadha duniani. Hili liko wazi kwa wafuatiliaji wa mambo . Hivyo si rahisi kwa mtu kufanya madhara kwa mwema wake; bali kanuni iliyo wazi ni kudhuriana ima kwa kisasi au uonevu. Serikali ya Marekani ina sehemu yake katika vurugu zote na migogoro duniani na imekuwa wazi mno na kujiamini kuwa ni ‘mbabe’ wa dunia (Superpower) katika harahkati zake za kuegemea upande mmoja na kushinikiza au kuathiri mwingine kwa gharma zake na kwa malengo yasiyo ya kibinadamu. Hili limekuwa ni kero duniani na hata nchini Marekani wananchi wapenda haki wamekuwa wakilikemea sana na ndio maana baadhi ya milipuko imekuwa ikifanywa na Wamarekani wenyewe. Hivyo basi vita hiyo ipo na bila shaka ni kutoka sehemu zote duniani ambapo athari hizo zimefika. Alipokuwa akizungumzia mauaji ya kinyama pale Mwembechai, Makamu wa Rais, Dk. Omar Juma alitutaka wananchi tusiwalaumu polisi kwa kuua bali tuwalaumu wale waliwatuma wananchi wale marehemu kufanya vurugu iliyowalazimisha polisi kufyatua risasi! Basi kwa mantiki ya Mkuu wa pili wa nchi viongozi wetu Tanzania na ulimwenguni kote wasiwalaumu walipuaji wa mabomu tu, bali waulize pia kwanini? Aidha Marekani ni taifa kubwa lililoendelea katika sayansi na teknolojia na ni taifa lenye mbinu za hali ya juu za usalama. Inahitaji maandalizi makubwa mno kuweza kulihujumu kiasi kile tofauti na nchi nyingine changa. Na ndio sababu, kwa kulijua hilo, Rais wa Marekani Bw. Bill Clinton alisema "tutawatafuta [walipuaji hao wa mabomu] kwa gharama yoyote bila kujali itachukua muda mrefu kiasi gani ... tunajua kuwa wao ni maadui zetu na wana mitandao ya ugaidi wa kimataifa". Tukiyazingatia hayo, inatushangaza: eti katika siku tatu tu baada ya milipuko hiyo nguvu za dola za Tanzania zinadai zimekwisha watia mbaroni wahusika hao na wakuonewa siku zote ni waarabu na wasomali - ‘Mujahiddina’! Haya yote yanatoa tafsiri ya udini uliopo nchini na kutokuwa makini na mambo. Katika vita haizingatiwi raia mwema au asiye na hatia; na ndiyo sababu serikali ya Marekani iliwaua kwa makombora raia wasio na hatia huko Iraq, Libya na Lebanon na hapa kwetu ni Mwembechai. Ni Marekani hiyo hiyo inaendelea kusababisha mateso makubwa na hata vifo kwa raia wa Sudan kwa kumuunga mkono gaidi na muuaji mkubwa Bw. John Garang. Hali ni hiyo hiyo huko Palestina na Algeria. Inatusikitisha kwa viongozi wetu kutosema yaliyo ya haki. Makamu wa Rais Dk. Omar alipotembelea ubalozi wa Maerkani alisema kwamba "walipuaji hawa wanaua watu wasio na hatia"; lakin mbona serikali yetu haijawahi kuiambia Marekani kuwa inaua watu wasio na hatia huko Iraq na Libya kwa kulazimisha kuwepo kwa vikwazo dhidi ya nchi hizo. Yatupasa tuutambue ukweli kwamba wanaodhulumiwa na Marekani wanaweza kufikia ukomo wa uvumilivu na hii ni hali ya hatari sana kwa mwanadamu! Pengine niukumbushe umma duniani kote maneno aliyopata kusema Mwandishi mashuhuri wa riwaya Mtanzania Bw. Edi Ganzel, katika utangulizi wa riwaya yake ya Kitanzi kwamba mwanadamu ni mnyama kama wanyama wengine ila tu ni ustaarabu ndio unaomfanya adumishe amani, lakini akichokozwa na akachokozeka basi ukali na unyama wake ni zaidi hata wa yule mnyama wa porini, akimaanisha kuwa hapo mwanadamu huwa tayari kufanya lolote, hataogopa tena ‘virungu na risasi’ za poilisi wa Tanzania wala ‘maroketi’ ya Mmarekani! Wakati umefika sasa kwa jumuiya ya kimataifa kuimbia Marekani yafuatayo: 1. Marekani yenyewe ndiyo inayochochea ugaidi. Pole (kifuta machozi) alichotuletea Bi. Madeline Albright, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, si chochote si lolote kwani tayari kuna ‘dazeni’ ya watoto ambao wamefanywa yatima baada ya baba zao kuuliwa, wapo dada zetu ambao sasa ni wajane baada ya waume zao wapenzi kuuawa na mabomu hayo ‘ya Marekani’. Hawa wanahitaji kusoma kula kuvaa na mengi mengineyo kwa siku kadhaa zijazo! Na zaidi ya yote hayo sasa Marekani ishitakiwe kwa kusababisha vifo
vya watu wasio na hatia na pia hasara ya mali.
|
TAHARIRI: Dawa ya ugaidi si kufanya ugaidi ndani ya ugaidi Bakwata yalaani ubabe wa Marekani
Wanakijiji wawapiga Polisi
Olesiva
Waislamu washinda kesi Same
Wasafiri ATC wadai ndege ya Jeddah
inahujumiwa
Mahojiano kati ya CNN na Bwana Usama bin Ladin Historia ya damu za mashujaa Afghanistan Msikiti wa Wagoma Kigoma wapata
viongozi wapya
Muhadhara wanguruma Masjid
Hijaz
Waislamu waitumie Misikiti
ipasavyo
Mpango wa kudhibiti uzazi utawaangamiza
wengi
Hoja za kutofautisha Yesu na Issa
ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 3
Wanawake wa Kiislamu washiriki
maonyesho ya kilimo
Wanawake wa Kiislamu washauriwa
kupigania haki zao
Africa Muslims Agency: Inavyohudumia
jamii
Kitengo cha Zakkah chasafirisha wanafunzi
Kupinga kifo cha Yesu ni kumpinga
Mungu?
Zanzibar na biashara ya utumwa
Marekani ishitakiwe
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 3
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org