|
Na.164 Jamada Awal 1419, Agosti 28 - Septemba 3, 1998 |
|
Na Mwandishi wetu, Arusha Askari polisi wa kituo cha Ngaramtoni wilayani Arumeru mkoa wa Arusha, wameripotiwa kupigwa na wanakijiji wa Olesiva kata ya Kiranyi wilayani humo. Imedaiwa kuwa polisi hao wamepata kipigo hicho kufuatia hatua yao ya kutaka kumkamata mwanakijiji mmoja anayetuhumiwa kuhusika na jinai ya kufanya vurugu na kuhatarisha amani katika mhadhara wa kidini uliofanyika kijijini hapo siku ya jumatatu agosti 24,1998, ambao uliandaliwa na waumini wanaosemekana kuwa ni wa dhehebu la kilokole. Imeelezwa kuwa sababu iliyompelekea mwanakijiji huyo anayesemekana kuwa muumini wa kilutheri kufanya vurugu hizo, ni taarifa za kushawishiwa nduguye kuingia katika ulokole. Mmoja wa watu walioshuhudia kadhia hiyo ameidokeza AN-NUUR kwa njia ya simu kwamba kutokana na vurugu hiyo ambapo imeripotiwa taa na vifaa vingine kuvunjwa, Waumini waliokuwa wakifanya mhadhara huo walipeleka taarifa polisi kituo cha Ngaramtoni. Baada ya taarifa hiyo polisi wawili walikwenda kijijini hapo kutaka kumkamata mtuhumiwa huyo, lakini wakati wakiwa katika harakati hizo, walijikuta wakizingirwa na wanakijiji wote ambao walitoka na silaha mbalimbali baada ya kusikia wito wa"vita" na kuanza kuwashambulia polisi hao. Taarifa zinafahamisha kwamba mmoja wa askari hao alijeruhiwa vibaya kufuatia kipigo hicho na mwingine alisalimishwa na gari iliyoegeshwa jirani ambayo aliirukia na dereva aliyekuwemo kuiondoa kwa kasi kutoka mahali hapo. Hata hivyo imedaiwa kuwa Wananchi hao walilirushia mawe gari hilo na kulivunja vioo. Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni juhudi za kumpata
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha kuhusiana na kadhia hii hazikuweza
kufanikiwa.
Na Mwandishi Wetu, Same KESI ya madai Na. 63/98 iliyokuwa mbele ya Hakimu E. Ndeteyai imetolewa hukumu ambapo wadai wamepwa ushindi. Katika hukumu yake, Hakimu Ndeteyai amesema kwamba eneo lenye daawa ni haki ya Waislamu sio la R.C na kwamba Wakatoliki wameamriwa kuondoa majengo yao waliojenga katika eneo la Waislamu na kulipa fidia ya shilingi 20,000 ikiwa ni thamani ya miti ya miwati waliyokata na pia kulipa gharama za shauri. Awali, Waislamu wa Duma Mbaga kupitia kwa Sheikh wao Amir A. Mleli walifungua shauri mahakamani wakidai kwamba Wakatoliki walikuwa wamevamia na kupora eneo lao lenye ukubwa wa hatua 39 x 35 Novemba 24, 1997 wakakata miti yao na kuanza kuchimba kiwanja. Waislamu walidai kwamba eneo hilo lililovamiwa ni seheumu ya eneo lao ambalo walipewa na serikali mwaka 1953. Kwa upande wa Wakatoliki wakiwakilishwa na Padri Stephano Richard walidai kwamba eneo waliokata miti na kuanza kujenga sio la Waislamu bali ni lao walilopewa na serikali ya kijiji. Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili mahakama ilisema kwamba ushahidi unathibitisha kwamba Waislamu ndio waliotangulia kupatiwa eneo huko Duma na serikali ya wakoloni 1953 ambapo walipanda miti na kujenga shule ya Muslim iliyofunguliwa mwaka 1955. Mahakama ilibainisha kuwa hili Wakatoliki hawalipingi ila wanakataa kuwa miti waliyoikata ni ya Waislamu. Wao wanadai kwamba miti ilipandwa na wanakijiji wote 1940. Hata hivyo, mahakama hiyo ilisema kwamba hata kama wananchi wa Duma ndio waliopanda miti hiyo 1940 na Waislamu wakapewa eneo hilo 1953, miti iliyopo ndani ya eneo hilo inakuwa mali yao. Katika kuelezea hoja kwamba Wakatoliki walipewa eneo hilo na serikali ya kijiji mwaka 1980; makahama ilisema kwamba serikali ya kijiji ilifanya hiyo kwa makosa. Katika ufafanuzi wake, mahakama ilisema kwamba serikali ya kijiji kabla ya kutoa eneo hilo kwa R.C. ilipaswa kufanya upelelezi kujua kwamba eneo wanalotoa halina mwenyewe. Aidha, ilisema serikali hiyo ilipaswa kuwaita viongozi wa Waislamu waonyeshe mipaka yao kabla ya kuwapatia wengine. Mahakama ilisisitiza kwamba Mwenyekiti wa Kijiji hana haki ya kugeuza ugawaji wa serikali ya mwaka 1953 na kwa kufanya hivyo amefanya kosa la kuwachonganisha Waislamu na Wakatoliki. Kuhusu nyumba ya Wakatoliki iliyoanza kujengwa katika eneo hilo, mahakama ilisema kwamba nyumba hiyo ilijengwa wakati shauri hili linaendelea na kubwa zaidi ndani ya siku 60 za rufaa zilizotolewa na Baraza la Kata kwa aliyeshindwa. Awali katika kesi hii Baraza la Kata lilitoa haki kwa Wakatoliki ndipo Waislamu wakalipeleka mahakama ya mwanzo mjini Same. Kwa kujenga nyumba haraka haraka kabla
ya siku 60 za rufaa kumalizika, mahakama ilisema kwamba R.C. walijenga
nyumba hiyo kwa makusudi ili kutumia ujanja wa kunyang’anya eneo la Waislamu.
Na hivyo mahakama ikaamuru ivunjwe.
- Wadai upo udini
Na Mwandishi Wetu WANANCHI kadhaa ambao wamekuwa wakipata huduma ya usafiri kati ya Dar es Salaam na Jeddah kupitia Aden wamelalamika kwamba huduma hiyo imekuwa ikihujumiwa hali inayopelekea kutaka kufutwa kabisa kwa huduma hiyo. Wananchi hao ambao wametoa malalamiko yao kwa nyakati tofauti wamesema kwamba awali ndege ya Jeddah ilikuwa ikiondoka siku ya Alhamisi mchana na kurudi Jumamosi alfajiri. Wamesema kwa ratiba hiyo walikuwa wanapata muda wa kutosha kwenda Makka kufanya ibada zao siku ya Ijumaa na kuwahi ndege hiyo ambayo ilikuwa ikiondoka Jeddah Ijumaa saa 6.30 usiku. Aidha hata wale ambao walikuwa wanakwenda kwa lengo la biashara walikuwa wanapata fursa ya kutosha kumaliza shughuli zao na kuwahi ndege hiyo hiyo waliyokuja nayo. Hata hivyo walisema kwamba ratiba hiyo ilibadilishwa ikawekwa siku ya Jumatatu; kuondoka na kurudi Jumatano asubuhi. Ratiba hiyo mpya wamedai kwamba inawakwamisha wale ambao wanakusudia kufanya ibada zao Msikiti wa Makkah siku yote ya Ijumaa. Hiyo ni kwasababu wamesema inawabidi kukaa wiki nzima kusubiri ndege nyingine. Wasafari hao ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini wamedai kwamba ndege hiyo sasa imehamishiwa Jumapili tena kwa kupitia Nairobi. Wamesema kwa kuipitishia ndege hiyo Nairobi ndio kuihujumu na kuiua kabisa kwani kulikuwa na wasafiri wengi wa kwenda Aden au kutoka Aden kuja Dares Salaam ikilinganishwa na Nairobi. Wamedai kwamba huenda kuyumbishwa kwa kuduma hiyo ni kutokana na chuki za kidini za baadhi ya watu. AN-NUUR iliwasiliana na kitengo cha Biashara ATC Agosti 26, ambapo msemaji wake alikiri kuwepo kwa mabadiliko hayo ya ratiba toka Alhamisi kuja Jumatatu na sasa Jumapili hata hivyo alisisitiza kwamba wao (ATC) wanachojali ni biashara na kwamba walilazimika kubadili ratiba kutokana na matakwa ya wasafiri. Alisema kwamba siku ya Ijumaa sio siku ya kazi Jeddah na hivyo maofisi mengi huwa yamefungwa kwahiyo wasafiri hawapati mahitaji yao. Kwa hiyo kwa kukidhi mahitaji ya soko wakabadili ratiba. Hata hivyo baadhi ya wasafiri wamedaikwamba japo Ijumaa sio siku ya kazi kiserikali lakini maduka yanakuwa wazi isipokuwa zile saa za swala. Kubwa zaidi Afisa huyo wa kitengo cha biashara (jina tunalihifadhi) alidai kuwa kibiashara njia hiyo ya Dar-Aden-Jeddah-Aden -Dar, haifai kwani ilifikia wakati mwingine ndege ikawa inakwenda na abiria watano (5) na kurudi na abiria wawili (2). Hata hivyo uchunguzi wa gazeti hili katika kitengo cha mauzo umegundua kwamba kiwango cha chini cha abiria kwa ndege hiyo ilikuwa abiria 182 kwa mwezi (Oktoba 1997) sawa na abiria 45 kwa safari ya kwenda na kurudi.Kiwango hicho kilipanda kufikia abiria 675 (Machi, 1998) sawa abiria 169 kwa safari ya kwenda na kurudi. Habari zaidi kutoka kitengo cha mauzo zilionyesha kwamba abiria waliokuwa wamefanya mipango ya kusafiri (booking) Agosti 10, kwenda Aden na Jeddah walikuwa 85 wakati wale ambao ilikuwa waondoke Agosti 17 walikuwa 67. Mfanyakazi mmoja wa sehemu ya mauzo na ‘booking’ ambaye jina lake tumelihifadhi alisema kwamba hadi kufikia Agosti 8; abiria 6 wa kwenda Aden na 42 wa kwenda Jeddah walikuwa wameshafanya mipango (booking) kusafiri na ndege ya Agosti 31. Mfanyakazi huyo alidai kwamba ikilinganishwa njia ya Jeddah na ile ya Dubai; ya Jeddah inafanya vizuri zaidi japo huwa bado ni changa. Bila ya kufafanua akadai kwamba njia ya Dubai ina maslahi zaidi kwa watu binafsi ikilinganishwa na maslahi ya shirika hasa baada ya kuanza kwa huduma za ndege ya Falme za Kiarabu. AN-NUUR iliongea na kampuni tatu za uwakala wa safari za ndege ambazo zote zililaumu mabadiliko ya ratiba yaliyokuwa yakifanywa na ATC ambayo yamekuwa yakilalamikiwa sana na abiria. Habari zaidi zimeeleza kwamba yalitolewa maelekezo huduma hiyo ya Jeddah ifutwe rasmi Agosti 24. Kufuatia maelekezo hayo taarifa za huduma hiyo zilitolewa katika mtandao wa ‘Computer’; na tiketi zikasitishwa kupelekwa Jeddah. Habari kutoka ndani ya ATC zimedai kwamba mabadiliko yote hayo yamefanywa na Mkurugenzi wa biashara bila ya idhini ya uongozi wa Shirika (Management) na bodi. AN-NUUR ilitaka kuwasiliana na Bw. Peter Matumula, Mkurugenzi wa kitengo hicho hata hivyo ikaambiwa kwamba hayupo kazini. Juhudi zaidi za kuwasiliana na uongozi pamoja na Mwenyekiti wa Bodi zilikwama jana baada ya kuambiwa kwamba wapo kwenye kikao cha bodi. Aidha AN-NUUR iliwasiliana kwa simu na ofisi ya ATC Jeddah kutaka
kujua ukweli wa madai kwamba walitumiwa maelekezo ya kufunga ofisi na kwamba
hawakutumiwa tiketi. Hata hivyo haikumpata Bw. Mtambo ambaye ndiye muhusika
na aliyekuwepo ambaye hakutaka hata kutoa jina lake alikataa kusema chochote
|
TAHARIRI: Dawa ya ugaidi si kufanya ugaidi ndani ya ugaidi Bakwata yalaani ubabe wa Marekani
Wanakijiji wawapiga Polisi
Olesiva
Waislamu washinda kesi Same
Wasafiri ATC wadai ndege ya Jeddah
inahujumiwa
Mahojiano kati ya CNN na Bwana Usama bin Ladin Historia ya damu za mashujaa Afghanistan Msikiti wa Wagoma Kigoma wapata
viongozi wapya
Muhadhara wanguruma Masjid
Hijaz
Waislamu waitumie Misikiti
ipasavyo
Mpango wa kudhibiti uzazi utawaangamiza
wengi
Hoja za kutofautisha Yesu na Issa
ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 3
Wanawake wa Kiislamu washiriki
maonyesho ya kilimo
Wanawake wa Kiislamu washauriwa
kupigania haki zao
Africa Muslims Agency: Inavyohudumia
jamii
Kitengo cha Zakkah chasafirisha wanafunzi
Kupinga kifo cha Yesu ni kumpinga
Mungu?
Zanzibar na biashara ya utumwa
Marekani ishitakiwe
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 3
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org