AN-NUUR
Na.164 Jamada Awal 1419, Agosti 28 - Septemba 3, 1998
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
Wanawake wa Kiislamu washiriki maonyesho ya kilimo

Na Habiba Swedi

WANAWAKE wa Kiislamu mkoani hapa kwa mara ya kwanza mwaka huu wameshiriki katika maonyesho ya kilimo yaliyoandaliwa na TASO na kufanyika mapema mwezi huu hapa Arusha.

Nilipozungumza nao ili kujua nini hasa kilichowapeleka na wao mwaka huu kushiriki maonyesho hayo yaliyoanzishwa takriban miaka mitatu iliyopita,na kama kushiriki kwao kunalingana na mafundisho ya Uislamu, walinifahamisha kuwa Uislamu unamruhusu kabisa mwanamke kutoka, kufanyakazi na kwamba ndani ya Qur’an kazi ni faradhi na mwanamke kama kiumbe mwingine anastahili kufanyakazi hali ya kuwa ni mwenye kujisitiri na kujichunga na haramu, asitende yale yote aliyokatazwa na Mola wake.

Ama wao katika maonyesho hayo waliendea jambo moja tu ambalo ni kuonyesha na kutangaza biashara zao kwa wanawake wenzao na jamii kwa ujumla.

Maonyesho yalisimamiwa na umoja wa vikundi vya wanawake wa Kiislamu wa Manispaa ya Arusha, ambapo wanawake wa Misikiti yote mkoani hapa walitakiwa kutayarisha vitu na kuviwakilisha katika maonyesho.

Wakiwa katika banda lao maalum, katika uwanja wa Themi Njiro, walionyesha mavazi ya stara kwa wanawake, mapishi mbalimbali, usindikaji wa vyakula, mboga na matunda, ukaushaji wa mboga za majani, kazi za mikono, usafi wa mazingira bila kusahau urembo wa mwanamke kwa kutumia vitu vya asili.

Kadhalika, walionyesha namna ya kutumia udi kwa kufukiza khanga, baibui na hata usafi wa ndani ya nyumba kwa kufukiza na kacha hewa safi yenye harufu ya uturi wa udi.

Waamuzi wa maonyesho haya walitoa cheti cha ushindi wa nafasi ya pili kwa banda hili kwa mashindano yaliyovishirikisha vikundi vya wanawake.

Mbali na ushindi huo, wanawake wenyewe wanakiri pia kujipatia faida nzuri kutokana na mauzo ya vitu vyao, faida ambayo imegawanywa kati ya Misikiti husika na wasimamizi wa maonyesho hayo yaani umoja wa vikundi vya wanawake wa Kiislamu wa Manispaa ya Arusha.

Ijapokuwa ni mara yao ya kwanza kujitokeza katika maonyesho hayo, ushirikiano miongoni mwao ulikuwa ni wa kiwango cha juu na hivyo kuweza kufanikisha maonyesho haya.

Kwa hilo wanasema wamevutiwa na ari kubwa ya kutaka maendeleo walionyesha wanawake wa Kiislamu.

Imedhirika kwamba, mwanamke wa Kiislamu si yule wa kukaa tu ndani kama anavyodhaniwa na kwamba ana uwezo mkubwa wa kuamua kufanya jambo lake la kumletea maendeleo.

Wanajivunia kuundwa kwa umoja huu uliowawezesha mwaka huu kushiriki maonyesho haya na wameahidi kukuza mshikamano waliouanzisha bila kujali tofauti zao za kiitikadi.

Ama kwa tathmini ya maonyesho haya, wanawake wanasema "yamekuwa kama ni jukwaa, ambapo kila mwanamke amepanda na kuonekana na kufahamiana na wenzie, vipaji vyetu na kazi zetu zimeonekana na kufichua siri kuwa sisi wanawake wa Kiislamu ni watalaamu, ila tu hatupati nafasi ya kuonyesha utaalamu wetu na hivyo kuwaachia wengine wafaidike".

Bidhaa nyingi zimepata masoko nje na ndani ya nchi. Kikundi kimoja cha wanawake kutoka Kenya kimenunua bidhaa nyingi na kuonyesha niya yakutaka kuwepo kwa ushirikiano wa kibiashara baina ya vikundi hivyo viwili. Alimdokeza mwandishi wa habari hizi wanawake hawa.

Vile vile wanayatazama maonyesho haya kama ni changamoto kwa wanawake wenzao wa Kiislamu pote nchini, hivyo wanawataka wajitokeze kushiriki mwakani.

"Ni lengo letu kuyaandaa mapema na vizuri zaidi maonyesho yajayo ili tupate ushindi na kutwaa nfasi ya kwanza", walijigamba wanawake hao.

Hivi sasa wamo katika pilikapilika za kutayarisha vitalu vya mboga, miti na matunda ambapo kila madrasa imetakiwa kuwa na japo ekari moja ya kuotesha vitu vitakavyotolewa katika maonyesho siku za usoni, pamoja na kuandaa kazi mbalimbali za mikono ikiwemo ushonaji, ufumaji na ufinyanzi.

Kwa mujibu wa Bw. Ole Kisambu, Mwenyekiti wa TASO Kanda ya Kaskazini, jumla ya washiriki 100 walikuwepo katika maonyesho haya yajulikanayo kama Nane Nane.

Arusha ni mwenyeji wa kudumu wa maonyesho haya yaliyofikia kilele chake tarehe 8 mwezi wa Agosti, 1998.
 
 


Wanawake wa Kiislamu washauriwa kupigania haki zao


 


Na Habiba Swedi, Arusha

MWALIMU wa madrasa ya akina mama Masjid Quba Arusha, Ustadha Halima Saidi Yahya amewashauri wanawake wa Kiislamu kupigania na kudai haki zao kwa misingi ya dini yao na kwamba waisome barabara ili kuzielewa haki hizo.

Amewataka pia wanawake wa Kiislamu kuisoma elimu mbalimbali bila ya kujali umri au kujiona wanapoteza muda ama kuhisi elimu haina manufaa kwao.

Akifafanua zaidi, bibi Halima amesema, elimu zote ni muhimu ili mwanamke asiyumbe katika maisha yake kwa kuwa mjinga na kupoteza haki zake.

Aidha, amesema ukosefu wa elimu unaweza kumfanya mwanamke adai haki ambayo siyo ya kwake.

Ustadha Halima alitoa mfano kwa kusema kuwa, mwanamke ni haki yake kujisitiri kwa kufanya hivyo anakuwa katika ibada, lakini kutokana na ukosefu wa elimu, mwanamke aliyejisitiri anaonekana mshamba.

"Kwa mwanamke mwenye elimu ya dini yake, maneno hayo hayatomyumbisha na atakuwa mstari wa mbele kupigania na kudai haki ya yeye kujisitiri mahali popote anapokuwa", alisisitiza Ustadha Halima.

Akichambua zaidi alisema, haki ya kujisitiri kwa mwanamke iko katika sehemu tatu ambayo hata hivyo alizitaja kwa kifupi tu. 

Haki ya kwanza alisema ni kujisitiri mwili wote, ya pili ni kuacha uso na viganja viwili na ya tatu alisema ni haki inayomzuia mwanamke asikae faragha na mwanaume awezaye kumuoa.

Kwa mujibu wa Ustadha Halima, hizo ndizo haki za msingi za mwanamke wa Kiislamu anazostahili kuzidai na kuzipigania..
 

Juu

YALIYOMO

TAHARIRI: Dawa ya ugaidi si kufanya ugaidi ndani ya ugaidi

Bakwata yalaani ubabe wa Marekani
Na Mwandishi Wetu

Wanakijiji wawapiga Polisi Olesiva
Na Mwandishi wetu, Arusha

Waislamu washinda kesi Same
Na Mwandishi Wetu, Same

Wasafiri ATC wadai ndege ya Jeddah inahujumiwa 
Na Mwandishi Wetu

KOSOVA: Bosnia nyingine

Mahojiano kati ya CNN na Bwana Usama bin Ladin

Historia ya damu za mashujaa Afghanistan

Msikiti wa Wagoma Kigoma wapata viongozi wapya
Na Suleiman Simba, Kigoma

Muhadhara wanguruma Masjid Hijaz
Na Said Shariff

Waislamu waitumie Misikiti ipasavyo
Na Ashraf Yusuph, Moshi

Mpango wa kudhibiti uzazi utawaangamiza wengi
Na Mwandishi Wetu

Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu,  ni uzushi mtupu! - 3
Na Muhibu Said

Wanawake wa Kiislamu washiriki maonyesho ya kilimo
Na Habiba Swedi

Wanawake wa Kiislamu washauriwa kupigania haki zao
Na Habiba Swedi, Arusha

Africa Muslims Agency: Inavyohudumia jamii
Na Mwandishi Wetu

Kitengo cha Zakkah chasafirisha wanafunzi
Na Mwandishi Wetu

Kupinga kifo cha Yesu ni kumpinga Mungu?
Mahfudhi M. Mahfudhi

MAONI: Porojo za Ngatara -2

Zanzibar na  biashara ya utumwa
Na J. Hussein

Marekani ishitakiwe
Na Abubakar Msham

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 3

Mafundisho ya Quran

Barua za wasomaji

Mashairi

Masomo ya dini ya Kiislam

Chakula na Lishe
 
 
 
 
 
 

 

 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita